Prime
Exclusive Aziz KI afichua ishu yake Yanga na siri za Wydad
MASHABIKI wa Yanga, bado wanaendelea kumuota kiungo mshambuliaji, Stephanie Aziz KI, nyota aliyeitumikia timu hiyo kwa karibu misimu mitatu kwa mafanikio makubwa.
Aziz KI aliyekuwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu msimu wa 2023-24 aliondoka Yanga katika dirisha dogo la msimu uliopita na kutua Wydad Casablanca ya Morocco.
Nyota huyo raia wa Burkina Faso aliyezaliwa Ivory Coast, ambaye ni mume wa mwanamitindo na msanii maarufu nchini, Hamisa Mabetto, alirejea nchini hivi karibuni akiwa na Wydad kwa ajili ya mechi ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Azam FC na timu hiyo kushinda mabao 2-0 kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.
Mara baada ya mechi hiyo ambayo nyota huyo aliumia mwishoni kwa kugongana na Himid Mao 'Ninja' uwanjani katika dakika ya 78 na kuwahishwa hospitalini, aliachwa na wenzake walipoondoka akaungana na familia yake (yaani mkewe Hamisa) na Mwanaspoti likabahatika kufanya naye mahojiano maalumu na jamaa kufunguka mambo mengi.
Kiungo mshambuliaji huyo mwenye misuli na anayesifika kwa kupiga mashuti makali, licha ya kufichua dili zima la kutua Wydad lilivyompa ugumu kwake kuiacha Yanga, pia amezungumzia namna alivyomchimba mkwara kocha wa timu hiyo juu ya kucheza, huku akisimulia 'alivyozimika' New Amaan baada ya kugongana na Ninja na maisha yake kwa ujumla na mkewe, Hamisa. Endelea naye...!
ALIVYOZIMIA ZANZIBAR
Kwa wanaokumbuka katika mechi ya Azam na Wydad iliyopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar Aziz Ki alianzishwa katika kikosi cha kwanza wakati timu yake ikishinda kwa mabao 2-0, lakini hakumaliza dakika 90 baada ya kuumia katika dakika ya 78 na kutolewa uwanjani.
Aziz Ki alionekana kugongana na Himid Mao na ikaja kuelezwa aliumia eneo la kichwani na kupewa saa 24 kwa wakati huo baada ya kutibiwa hospitalini. Mwanaspoti lilitaka kujua kitu gani kilichomtokea naye anasema hakumbuki kilichomtokea zaidi ya pale alipogongana kisha kutaka mawasiliano.
“Kilichotokea kwa kweli sikumbuki, ila nilishtuka tu nimekaa chini baada ya kugongana na Himid kabla ya kupoteza nuru ya macho kwa kutoona vizuri na kutolewa uwanjani. Nilikuja kupata fahamu na kukaa vizuri baadaye kidogo baada ya matibabu hospitalini," anasema Aziz KI na kuongeza;
“Namshukuru Mungu naendelea vizuri hadi leo nikiwa salama, kitu ninachoshukuru pia ni kwamba timu yangu ilishinda ile mechi ambalo hilo lilikuwa muhimu sana kwetu tukiwa ugenini Tanzania. Ila ukweli niliogopa sana pale nilipopoteza uoni na kumbukumbu."
HAIKUWA RAHISI KWENDA WYDAD
Aziz anasema, dili lake la kwenda Morocco halikuwa rahisi kutokana na mapenzi makubwa aliyokuwa nayo kwa Yanga na Tanzania, kwani alishapazoea kama nyumbani, hivyo ilikuwa ngumu kutengana na familia na kwenda kuanza upya.
“Niwe mkweli haikuwa rahisi kufanya uamuzi ule, unajua Yanga ipo nafasi ya kwanza kwenye moyo wangu ndio kila kitu kwangu ni familia yangu," anasema Aziz KI na kuongeza;
“Haikuwa Yanga pekee niliyokuwa na furaha nayo hapa Tanzania, unafahamu maisha kuna wakati yanatufundisha hata kama unafanya kitu kizuri unatakiwa kujua wakati gani sahihi wa kuondoka, kwangu mimi ilikuwa ni uamuzi mgumu niliotakiwa kuufanya kwa kuondoka kwa ajili ya kipaji changu hasa kule nilipotakiwa kwenda, kwa hiyo ulikuwa ni uamuzi sahihi unaoumiza."
WYDAD KUBWA
Anasema, haisifii Wydad ila ni timu ambayo kwa hapa Afrika ni miongoni mwa vigogo hivyo kutoka Yanga mpaka Wydad ni hatua kubwa kwake.
"Nafikiri kila moja anafahamu kwamba hapa Afrika Wydad ni moja ya klabu kubwa, Kwa hiyo kuondoka kwangu Yanga na kwenda Wydad ni kupiga hatua kubwa kitu ambacho ni muhimu sana kwenye maisha, kwangu ilikuwa ni hatua nzuri kwenda sehemu kubwa ambayo nitaonyesha kupiga hatua kubwa ili nikafurahie mpira na kujifunza zaidi na ndicho kinachotokea kwa sasa."
MKATABA WYDAD
Anajibu kwa kusema, amesaini mkataba wa miaka miwili ila suala la kukaa kwenye mpira wa miguu sio la uhakika unaweza kusaini kandarasi ndefu na ukakaa muda mfupi sana.
"Mimi nimesaini mkataba wa miaka miwili na Wydad na huu ndio msimu wangu wa kwanza naanza kutumikia mkataba huu, unajua soka unaweza kusaini mkataba wa miaka mitano lakini baada ya miezi sita tu unaweza kupata ofa kubwa.
“Au inaweza kutokea baada ya muda mfupi ukajikuta hauna furaha ya kuendelea kuwa pale na ukataka kuondoka au timu ikakuacha. Kwa hiyo kwangu mimi kitu muhimu ni kuendelea kujituma, leo nipo Wydad lakini kiukweli nataka kwenda mbali zaidi, nafasi ikija naweza kwenda sehemu nyingine."
KUCHEZA KOMBE LA DUNIA LA KLABU
Baada ya Aziz KI kuondoka Yanga na kujiunga na Wydad ilihitajika usajili huo kufanyika haraka ili awahi kushiriki Fainali za Kombe la Dunia kwa Klabu zilizofanyika nchini Marekani na akacheza japo kwa muda mchache. Hapa anaeleza alivyoyapokea mashindano haya makubwa:
"Naweza kusema ilikuwa ni faraja kwangu kucheza mashindano makubwa kama yale, unajua unapocheza soka ndoto zako kubwa zinakuwa kucheza mashindano kama haya dhidi ya timu kubwa kama zile tulizokuwa tunakutana nazo.
"Kwangu mimi ilikuwa kubwa, lakini ni kama kufikia hatua ambayo ulikuwa unaisubiria na sasa imefika, kwanza nilimshukuru Mungu na baada ya hapo unafanya kile ambacho unaweza kuonyesha ili uongeze uzoefu, sikuwa peke yangu ambaye nilikuwa na ndoto za kucheza mashindano kama yale.
“Kila mchezaji ana ndoto ya kupata nafasi kama ile, kuwa kwenye timu kubwa kama Wydad au hata kucheza na timu kama zile, kwa hiyo ilikuwa nzuri kwangu kucheza mashindano yale na kufurahia mchezo."
MAISHA YAKE NA MASHABIKI WA WYDAD
Alipocheza Tanzania, Aziz KI alikuwa kivutio cha kila shabiki wa soka kutokana na kipaji chake, kisha akaenda kujiunga na Wydad ambayo nayo ina mashabiki vichaa wanaojua kuipenda timu yao. Hapa anaeleza walivyompokea:
“Walikuwa na furaha sana (mashabiki wa Wydad), unajua walikuwa wananisubiri kwa takribani mwaka mmoja, nilipofika nilianza kuhisi ile hali ya mashabiki kufurahi kuniona, ninapokuwa natembea na mke wangu walikuwa wanafurahia sana kuniona, hii ilikuwa muhimu kwani inakupa nguvu ya kuhakikisha unawafanyia makubwa na kuwarudishia upendo wanaokuonyesha.
"Upendo wa mashabiki wa Wydad ulikuwa una sura mbili kwangu kwanza ni kwamba wanakukubali kwa kukupa ukaribisho mzuri, pia sura nyingine ni mbaya na ngumu kwamba mapokezi wanayokupa ni kama deni kwako, wanatarajia utawafanyia makubwa unapojiunga na timu yao hasa wakiangalia yale uliyoyafanya kwenye timu uliyotoka lakini niliichukulia kwa njia nzuri."
ALISIKIA UVUMI HUU
Baada ya kuondoka kulikuwa na maneno ya kwamba ametolewa kwa mkopo Wydad, uvumi ambao anathibitisha aliusikia.
"Kweli nilisikia hayo maneno, unajua unavyokuwa mchezaji sio salama kuzingatia kila kitu wanachoongea huko nje, mtu anaweza kusimama na kusema Pacome Zouzoua hana furaha na anataka kuondoka, lakini sio kweli, hata kabla hata sijaondoka ilijulikana kwamba naondoka kwa kuuzwa kutoka Yanga na kwenda Wydad, hakukuwa na habari ya mambo ya kutolewa kwa mkopo, hao ni watu tu waliamua kusema wasiyoyajua, Kwa hiyo haikuwa sahihi kwangu kuanza kukanusha, niliona na nikaachana nayo.
“Unajua siku zote muda ni jibu zuri kwa kila kitu na kila mtu, wengine walisema kocha hana furaha na mimi na nitarudi Tanzania, lakini maneno hayo yote nani anaweza kuyasema tena, sikuwajibu, lakini walipata majibu kupitia wakati ambao waliniona nacheza na naendelea vizuri na nina furaha, muda ni kitu bora wakati wote.
KUANZA TARATIBU WYDAD
“Hapa niwe mkweli, unajua nilifika Wydad mwezi mmoja kabla ya mashindano ya Kombe la Dunia na nilipofika nilikuwa na majeraha, nikawa nacheza nikiwa na maumivu na wakati huo huo nilipofika nilifanya mazoezi mara mbili tu kisha nikaenda kujiunga na timu ya Taifa.
“Kwa hiyo hata ile kufika mwezi mmoja kabla ya Kombe la Dunia kumbuka nilipokwenda timu ya taifa nilitumia kama siku kumi kule, hata niliporudi Wydad nilielewa kwa nini kocha hakunipa nafasi ya kutosha kutokana na kwamba alikuwa hajaniona vyema.
“Unajua kocha anafanya kazi na wachezaji wengi kwenye timu, sikuwa na tatizo alipokuwa hanipi nafasi, lakini pia ndani ya moyo wangu nilijiapiza kwamba nitakaporudi na kuwa sawa sitaruhusu kocha aniweke benchi na hii siku zote imekuwa nguzo yangu.”
TOFAUTI YANGA VS WYDAD
“Unajua tofauti sio kuhusu Wydad na Yanga ni kuhusu utofauti wa nchi hizo mbili kwa sababu naweza kusema kama Tanzania wote tunafahamu kwamba watu wanapenda sana soka, lakini ukweli ni kwamba sio kila mmoja anauelewa mkubwa.
“Lakini pia maisha ya wachezaji na tusisahau kuhusu miundombinu bora. Kule Morocco ni tofauti kwanza unaweza kuangalia utofauti miundombinu, kule kila unapokwenda utaona maeneo mazuri hususan viwanja bora, maeneo mazuri ya kufanyia mazoezi, haraka utaona ni tofauti na yale ambayo utayapata hapa Tanzania.
“Nina furaha kwamba hata hapa Tanzania mambo yanazidi kubadilika kwa kasi kwenda kwenye ubora mkubwa, hapa sasa unaanza kuona viwanja vizuri na vitu vingine, unaweza kuangalia kule ni vigumu kuona kiwanja cha nyasi za bandia, lakini hapa Tanzania viko vingi .
“Unajua nyasi bandia kwa wachezaji wakati mwingine sio kitu kizuri na hata vile viwanja vya nyasi za kawaida kuna vingine haviko vizuri sana. Kwa hiyo unapokwenda kwenye timu nyingine ambako unaona wana karibu kila kitu, unafanya mazoezi vizuri, kuna maeneo mazuri ya kurudisha mwili sawa (recovery) utaona utofauti kwa hiyo kama nilivyosema sio kuhusu utofauti wa Yanga na Wydad ni kuhusu uwekezaji mkubwa kwenye nchi husika.”
HAJAFUATA FEDHA WYDAD
“Unajua kama ingekuwa ishu ya fedha, kusema ukweli ningeondoka Yanga kitambo sana na ningeondoka kabla ya msimu uliopita, unajua msimu mmoja nyuma nilikuwa nimeshinda kila kitu ambacho kilikuwa nakihitaji hapa Tanzania ilikuwa kasoro Kombe la Afrika tu.
“Hata kama Yanga inashiriki Ligi ya Mabingwa na Wydad inashiriki Kombe la Shirikisho lakini Wydad sio timu ndogo, mimi siku zote napenda kuwa eneo chanya hata kama Wydad inashiriki Kombe la Shirikisho nadhani ni Mungu ananipa nafasi ya kuchukua taji hili nikiwa na hii timu ambayo itakuwa nzuri kwangu.
URAHISI KUCHEZA NA ZIYECH, AMRABAT
Aziz KI sasa anacheza pamoja na mastaa kama winga wa zamani wa Chelsea, Hakim Ziyech, Nurdin Amrabat ambaye ni kaka wa kiungo wa zamani wa Manchester United, Sofiane Amrabat na Tembankosi Lorch, hapa anaeleza namna mambo yalivyokuwa rahisi.
“Ni rahisi sana hakuna ugumu, unacheza na wachezaji wa daraja la juu, wana uzoefu, unajua unapocheza na wachezaji wa daraja kubwa kama hilo ambao wamefanya makubwa, kwangu inakuwa kama wananiongezea morali ya kutamani kuonyesha kitu kikubwa ili niwe juu zaidi, kwahiyo kwangu nina furaha kuwa pamoja na wachezaji wa namna hiyo.”
AZIZ KI RAFIKI WA WOTE
“Mimi napenda kuwa karibu na wachezaji wote wazuri, najua mara nyingi mnaniona nipo na Lorch ni kweli ni rafiki yangu wa karibu pale, lakini mimi ni mtu wa wachezaji wote, kuwa karibu na Lorch hakunifanyi nisiwe karibu na wengine.
“Unapokuwa kwenye timu na wenzako mnakuwa familia moja, mimi ni mchezaji wa timu nzima kwa hiyo napenda kuwa sawa na kila mmoja kwenye timu kwa sababu hao wote ndio wataifanya kazi yangu kuwa rahisi uwanjani, mmoja kati yao atanipa pasi ya bao au mimi kumpa pasi ya bao, kwangu mimi ni muhimu kuwa na maelewano mazuri na kila mmoja.”
KOCHA AMEMPA MALENGO GANI
“Ukweli kocha hajaonyesha kuhitaji mengi kutoka kwangu, kitu pekee anachotaka ni kuwa na mchezaji ambaye wakati wote anatamani kushinda. Kwangu mimi kila ninapokuwa mazoezini uwanjani nataka kufanya kila ninaloweza kuisaidia timu, mimi nataka kila wakati niwe uwanjani nacheza.
“Hata wakati aliponiweka benchini kwenye Kombe la Dunia, tulipomaliza yale mashindano nilimfuata moja kwa moja nikamwambia kocha umeniweka benchini, lakini hautafanya hivi tena kwangu, akaniuliza kwa nini unasema hivi nikamwambia sikufurahia ila nilielewa kwa kuwa sikuwa sawa kutokana na maumivu, ile iliniumiza kwa kuwa nataka kucheza muda wote na nikamwambia hujanipa nafasi kwa kuwa sikufanya maandalizi ya timu, nikirudi nitafanya kila kitu kukuonyesha uwezo wangu, akanielewa na baadaye nikafanya kweli.
“Sasa unaona nacheza kwa kuwa ameona ambacho nilimwambia na hakuwa na shida kutokana na maneno niliyomwambia, nilimpa changamoto, mimi nipo hivyo wakati wote nilimwambia una wachezaji 25 hapa, lakini nitaingia katika kikosi cha kwanza na sasa nipo."