Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Elizabeth John: Anavyojigawa kwenye masomo na kucheza mpira

Eliza Pict

Muktasari:

  • Ukiachana na burudani hiyo wachezaji wa mpira ambao wamekuwa wakionyesha ufundi wao uwanjani kuna baadhi yao wamefanikiwa kuonyesha talanta zao na kitabuni pia wamo.

KWENYE ulimwengu wa michezo, soka umekuwa moja ya burudani kubwa inayovuta hisia za mamilioni ya watu kote duniani.

Ukiachana na burudani hiyo wachezaji wa mpira ambao wamekuwa wakionyesha ufundi wao uwanjani kuna baadhi yao wamefanikiwa kuonyesha talanta zao na kitabuni pia wamo.

Mfano mzuri ni nyota wa zamani wa Manchester United na Chelsea, raia wa Hispania, Juan Mata ambaye mbali na kusakata kabumbu lakini alipata shahada mbili, moja katika Masoko (Marketing) na nyingine katika Sayansi ya Michezo (Sports Science) kutoka Chuo Kikuu cha Camilo Jose Cela mjini Madrid.

Mata na nyota wengine wanatoa dhana potofu ya kwamba wachezaji hawawezi kufanikiwa nje ya michezo hususani kwenye elimu ikionekana wanapoteza muda.

Ishu hiyo inamgusa pia kiungo mshambuliaji wa Alliance Girls, Elizabeth John ambaye anaamini anaweza kutoboa kwenye kipaji chake na hata masomoni.

EL 04

Akifanya mahojiano na Mwanaspoti, mchezaji huyo anasema maisha ya soka ni mafupi kwani lolote linaweza kutokea na kama huna kitu cha ziada inakula kwako.

“Sina maana kama kama huna elimu huwezi kutoboa hapana lakini kuna muda shule inaingia kwa asilimia kubwa kwenye maisha yetu, ishu za mikataba na vitu vingine,” anasema.

Elizabeth alijiunga na Alliance msimu 2021 akiwa kidato cha kwanza wakati ambao hapo awali hakuwa na nafasi ya kuanza kwenye kikosi cha kwanza.

“Nilijiunga na shule ili niweze kupata nafasi ya kucheza kwenye timu, nashukuru mwaka jana nimemaliza masomo yangu ya kidato cha nne.”


EL 03

MASOMO NA KUCHEZA MPIRA

Kinda huyo anasema hakuna ugumu anaopata kuchanganya masomo na kucheza mpira kwa sababu vyote viwili anavipenda kutoka moyoni hivyo anafanya kwa moyo mmoja.

Anajigawaje kwenye masomo na soka, anasema: “Mimi nina ratiba ya kila siku ya vitu ninavyofanya, hivyo asubuhi naamka nafanya mazoezi kidogo najisomea na kuingia darasani kwa sababu nasoma shule ambayo ipo pamoja na timu, jioni ndio muda wangu mzuri wa kufanya mazoezi,” anasema.

Anapoulizwa pindi timu inaposafiri kutoka Mwanza kwenda mikoa mingine ama nchi nyingine huwa unafanyaje kama masomo yanaendelea, anasema: “Timu inaposafiri naondoka nayo na uzuri walimu wanafahamu kuhusu kipaji changu na ni kwa sababu ni Alliance, shule inayomilikiwa na timu, hivyo nikirudi naangalia wenzangu walichosoma napitia na kuwa nao sawa darasani.

“Hata wazazi ndio watu wa kwanza kunisapoti na wananishauri nihakikishe nasoma na kufaulu vizuri kisha mambo ya kipaji yatakuja tu na ndio maana niko vizuri darasani na uwanjani.”


EL 02

MALENGO YAKE

Elizabeth anasema malengo yake ni kuhakikisha anafika mbali kisoka kwa kuwa ni ndoto ya muda mrefu kucheza Ulaya na nchi nyingine zenye soka la kiushindani.

“Ukiachana na mpira nachukua kozi ya sanaa, natamani kuwa mwanasheria au mwanajeshi na naamini hazitaingilia na mambo yangu ya soka kwa kuwa unaweza kuwa jeshini na ukacheza soka,” anasema na kuongeza:

“Ukiwa una kipaji na umesoma utaweza kuendesha vitu vyako kwa ustadi wa hali ya juu, hivyo nikiwa mwanasheria nitaweza kufuatilia mikataba kwa umakini kuna fursa zinatokea zinahitaji msomi.

Anamtolea mfano mshambuliaji wa Zambia, Babra Banda anayekipiga Orlando Pride inayoshiriki Ligi ya Wanawake nchini Marekani.

“Banda anacheza Ligi Kubwa Marekani lakini kwao Zambia ana cheo kikubwa jeshini na anafanya vizuri uwanjani,” anasema.


EL 01

TIMU YA TAIFA

Anasema anatamani kuitumikia timu ya taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’ ingawa amewahi kuitwa kwenye kikosi hicho licha ya kutocheza michezo ya kirafiki.

“Unajua kila mchezaji mwenye malengo ya kufika mbali anatamani kuichezea timu yake ya taifa hivyo najivunia na natamani siku moja nicheze Twiga Stars ambayo ina wachezaji wengi wazuri.

“Nimecheza timu ya taifa ya vijana kwenye mashindano ya shule mwaka jana na juzi nimeitwa Twiga Stars kwenye mechi za kirafiki lakini natamani zaidi kucheza kwenye mashindano makubwa kama Olimpiki.”


AWATAMANI MASAKA, LUVANGA

Kila binti mwenye ndoto ya kufika mbali basi anakuwa na mtu wa kumtazama kama mfano wake ili awe kama yeye au afanye zaidi yake.

Kwa Elizabeth ni wachezaji watatu wa kike anaowafuatilia akiamini siku moja na yeye anaweza kufika walipo.

“Wachezaji kama Masaka, Clara Luvanga kina Opah Clement ni wachezaji ambao wamefanikiwa kiasi fulani hivyo nawatazama kama (role rodels) wangu na natamani siku moja nifanikiwe kama wao,” anasema.

“Huwa tunawasiliana na muda mwingine wananipa ushauri wa kufanya na ikitokea nimecheza mechi wananipongeza na kama kuna sehemu nimekosea wananiambia hivyo ni watu wanaonipa ushauri sana.” 


AMTAJA CHOBANKA

Licha ya aliyekuwa kocha wa Alliance Girls, Ezekiel Chobanka kutimka klabuni hapo na kuibukia Ceasiaa Queens lakini kwake anamtazama kama mzazi wake.

“Kocha Chobanka ndiye aliyenipandisha na kunisaidia hadi kucheza kikosi cha kwanza, naweza kusema ni kama mzazi kwetu licha ya kutufundisha lakini anatushauri kwa mengi.”


Anaongeza kuwa kocha huyo amekuwa na mchango mkubwa kwenye soka la wanawake kwani ametoa wachezaji wakubwa ambao ni muhimu kwenye vikosi vyao.

“Wapo kina Aisha Mnunka, Enekia Lunyamila na kadhalika. Kocha Chobanka amewafundisha na sasa ni nyota wakubwa nchini ana mchango mkubwa sana kwetu mabinti na mimi najivunia kuwa miongoni mwa wachezaji waliopita mikononi mwake.”


MVP UGANDA

Mwaka jana Alliance Girls na shule ya Bwire kutoka Tanzania zilishiriki mashindano ya shule FEASSA ambayo yalifanyika nchini Uganda, huku Elizabeth akiwa miongoni mwa wachezaji waliofanya vizuri.

“Pamoja na ubingwa tuliobeba lakini kama mchezaji kuchaguliwa mchezaji bora wa mashindano mbele ya wachezaji wengine kutoka Kenya, Uganda sio jambo dogo nilifurahi sana,” anasema na kuongeza:

“Sasa hivi pia tupo tunaendelea kupambania TDS Academy ifanye vizuri kwenye mashindano ya GIFT yanayoendelea Azam Complex, natamani pia nifanye vizuri na huko.”