Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

DTB FC yairejesha Singida United kiaina

USAJILI unaofanywa na DTB FC inayoshiriki Ligi ya Champonship (zamani Ligi Daraja la Kwanza) unairejesha Singida United kiaina kutokana na nyota wake kibao kujiunga na timu hiyo.

Singida United ni moja ya timu zilizokuja kwa kasi katika Ligi Kuu Bara misimu kadhaa iliyopita na kushuka daraja hadi Ligi ya Mkoa.

DTB ni moja ya timu inayotarajiwa kushiriki Championship kupambania nafasi ya kupanda Ligi Kuu msimu wa 2022/23, huku usajili wake ukizua gumzo kutokana uwepo wa mastaa wa ndani na nje ya nchi.


MAJEMBE SINGIDA NDANI

Baadhi ya wachezaji waliokuwa wakiitumikia Singida wameonekana katika usajili wa DTB - picha inayoonyesha dhahiri kuwa timu hiyo kuonekana kurejea katika anga ya soka baada ya kuporomoka.

Wachezaji hao waliwahi kucheza Singida ambao ni Tafadzwa Kutinyu, Shafiq Batambuzi, Owen Chaima na Miraji Athuman.

Mbali na wachezaji hao, pia aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Ramadhan Nsanzurwimo na katibu mkuu, Muhibu Kanu wako DTB.


MASTAA WENGINE USIPIME

Mbali na wakali hao kutoka Singida United, pia wapo Ramadhan Siame aliyewahi kukipiga Mbao FC na Njombe Mji - zote zilishuka daraja.

Pia imemsajili nyota kutoka TP Mazembe Yanik Bazola na Juma Abdul aliyewahi kucheza Yanga, David Mwantika aliwahi kukipiga Azam na Amisi Tambwe ambaye aliwika akiwa Simba na Yanga.


GUMZO KILA KONA

DTB kwa namna ambavyo inafanya usajili imekuwa gumzo kubwa katika vilinge mbalimbali vya soka mitaani mashabiki wakiizungumzia kutokana na mastaa waliosajiliwa.

Mdau wa soka katika majadiliano juu ya timu hiyo Kimara Suka jijini Dar es Salaam, Masha Mtumbo anasema timu hiyo inashtua kutokana na aina ya wachezaji ambao inawasajili wakati haichezi hata Ligi Kuu.

“Au kwa sababu ni timu ya benki kwa hiyo hela ziko njenje, maana timu ambayo haipo kwenye Ligi Kuu kusajili wachezaji kama hao si mchezo,” anasema.

Naye Alfred Casto anawataka wadau wengine ambao wana uwezo wa kumiliki timu waige mfano huo kwani utazidi kuongeza ushindani na kuleta chachu zaidi kwenye ligi husika.

“Wachezaji wa kigeni wapo wengi kwenye hiyo timu tunawasoma nyie Mwanaspoti mnawaandika, nasi tunabaki kushangaa na kujiuliza hii timu ngoja tuone ligi yao ikianza,” anasema.


JUMA ABDUL AFUNGUKA

Beki mahiri, Juma Abdul aliyeamua kubadili upepo baada ya kushindwa kuafikiana na Yanga na kutimkia Zambia, anasema kambi upande wake ni popote kwa kuwa soka ndio kazi aliyoichagua.

“Maisha popote, muhimu kama mchezaji unaangalia maslahi yakoje. Imani yangu kubwa ni kuhakikisha timu inapanda Ligi Kuu. Kwa kushirikiana na wenzangu naamini tutaweza (kupanda Ligi Kuu),” anasema.


MSIKIE TAMBWE

Amisi Tambwe anasema hana shaka na timu yoyote ile kuitumikia kwani anatambua na kuthamini kazi anayoifanya, huku akikiri kuifahamu vyema Ligi Kuu Bara kutokana na muda ambao amecheza soka hapa nchini.

“Mimi Tanzania ni nyumbani kwetu, pia najisikia furaha sana kurejea tena nikiwa timu nyingine, ndio maisha, nashukuru sana nina watu na changamoto ya viwanja naijua,” anasema.


MUHIBU KAPANIA USIPIME

Katibu wa timu hiyo, Muhibu Kanu anasema hawasajili kwa bahati mbaya, lakini wanaangalia malengo na mahitaji kwa ajili ya kuanza mapambano.

“Kila mchezaji ambaye anasajiliwa anahitajika na ili tuweze kufikia lengo letu ni lazima tufanye usajili mzuri ambao utaleta ushindani zaidi kwa timu nyingine ili tuweze kupanda,” anasema Tambwe.

“Tunajua kupanda Ligi Kuu sio mchezo, lakini tukimaliza usajili na kuweka hadharani kikosi chetu ndio mtaona nini tunakifanya.”

Timu hiyo tayari imeanza maandalizi ya msimu ujao na sasa inafanya mazoezi yake katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.