Don Carlo anavyoanza kukolea ngoma za Kibrazili
Muktasari:
- Na hicho ndicho anachojaribu kukifanya kocha Carlo Ancelotti. Mtaliano huyo, ambaye ni kocha wa timu ya taifa ya Brazil, umri wake wa sasa ni miaka 66, lakini hilo halikuwa kikwazo kwake na kujichanganya katika moja ya matamasha ya kiutamaduni huko Brazil.
BAHIA, BRAZIL: UZEE mwisho vijijini, ndivyo wanavyodai watoto wa mjini.
Na hicho ndicho anachojaribu kukifanya kocha Carlo Ancelotti. Mtaliano huyo, ambaye ni kocha wa timu ya taifa ya Brazil, umri wake wa sasa ni miaka 66, lakini hilo halikuwa kikwazo kwake na kujichanganya katika moja ya matamasha ya kiutamaduni huko Brazil.
Picha adimu za Ancelotti akifurahia sherehe hizo za Brazil zilisambaa kutoka kwenye mitandao. Ancelotti aliamua kusahau kwa muda ishu za ukocha na kufundisha soka na kwenda kuburudika kwenye tamasha hilo. Tamasha hilo si kitu unachoweza kukiona kila siku.
Kocha huyo wa zamani wa Real Madrid alionekana akifurahia tamasha hilo maarufu kama Salvador, ambapo alihudhuria ikiwa ni siku ya pili katika sherehe zilizofanyika katika miji ya Brazil.
Picha hizo zilimwonyesha Mtaliano huyo ambaye kawaida ni mtulivu akiwa na tabasamu, amepumzika, na akiwa ameingia kikamilifu katika midundo, rangi na muziki wa moja ya sherehe kubwa za barabarani duniani. Mwimbaji Leo Santana, aliyekuwa akitumbuiza karibu, alipita eneo la watu maarufu ambalo alikuwa ameketi Ancelotti. Mwimbaji Santana alimwambia Ancelotti ombi lake hadharani, alipomwambia: “Mweke Neymar kwenye timu ya taifa, kwa upendo wa Mungu!”
Katika sherehe hizo, kuna muda Ancelotti alionekana akiwa amekumbatiwa na wanawake watatu. Ancelotti anaonekana kuwa anafurahia maisha yake nchini Brazil baada ya kuonekana akishiriki sherehe hizo maarufu.
Picha za Ancelotti zilikuwa maarufu mitandao na kupata komenti mbalimbali, ambapo mtu mmoja aliandika kwenye mtandao wa X, aliposema: “Don Carlo Ancelotti anafurahia maisha,” akifuatiwa na emoji za kucheka.
Mwingine alicheka na kuandika: “Sasa tunajua kwanini alikwenda Brazil.”
Baadhi walipendekeza kuwa huenda asiondoke nchini humo kutokana na hali ya sherehe ya kufurahisha, licha ya kuhusishwa na nafasi ya kocha wa Manchester United. Ripoti za karibuni, zinadai Ancelotti yupo kwenye mipango ya kusaini dili jipya la kuendelea kuinoa Brazil.
Mwingine aliongeza: “Bro hatajiwi Brazil kamwe.”
Na mwingine amesema: “Siku ya Wapendanao ya Carlo Ancelotti inaenda vizuri kabisa.”
Wengine walicheka: “Ancelotti amekuwa Hugh Hefner lini?”
Na mwingine aliandika: “Sidhani kama ataondoka kwenda Ulaya tena.”
Wakati huo wa furaha ulivutia mashabiki, Ancelotti alihudhuria akiwa na mke wake, mrembo Mariann Barrena McClay.
Ancelotti, ambaye ni mmoja wa makocha waliofanikiwa zaidi katika historia baada ya kushinda zaidi ya vikombe 30 anaonekana kuwa na furaha Brazil licha ya uvumi kuhusu hatima yake ya karibu. Lakini, ripoti ya The Athletic inapendekeza kuwa Ancelotti amekaribia kusaini mkataba wa kuendelea kuinoa Selecao hadi 2030.