Dickson Job ‘Big Brain Defender’ akili sio kimo
Muktasari:
- Job amekuwa panga pangua kikosi cha kwanza cha Stars na Yanga, lakini anasema haikuwa rahisi kufuzu Afcon 2025, ila atatumia michuano hiyo kujitangaza na kujiweka sokoni. Mwanaspoti limepiga naye stori kadhaa.
DICKSON Job ni jina la beki kisiki wa Yanga na ‘Taifa Stars ambaye amekuwa bora eneo analocheza na ana ndoto ya kutumia fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon)2025 na Ligi ya Mabingwa Afrika kutumiza ndoto yake.
Job amekuwa panga pangua kikosi cha kwanza cha Stars na Yanga, lakini anasema haikuwa rahisi kufuzu Afcon 2025, ila atatumia michuano hiyo kujitangaza na kujiweka sokoni. Mwanaspoti limepiga naye stori kadhaa.
AFCON, LIGI YA MABINGWA KUMUUZA
Job akiwa sehemu ya kikosi cha Stars na ameipambani Yanga kutinga hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa baada ya miaka 25, anasema: “Ni michuano mikubwa tunakutana na wachezaji wa aina mbambali wenye uwezo mkubwa, na ni sehemu sahihi kwetu pia kuonyesha uwezo ili kuweza kujiuza kwenye mataifa mbalimbali.
“Naamini kujituma kwangu na kujitoa hakuna kinachoshindikana inaweza kuwa njia sahihi ya kutoka nilipo na kwenda nyingine. Kuhusu ni nchi gani natamani kucheza nikipata nafasi ya kutoka Yanga siwezi kusema ni wapi ila natamani kucheza nchi yoyote ambayo itakidhi mahitaji yangu.”
AKILI SIO KIMO
Mengi yamekuwa yanazungumzwa juu ya kimo cha nahodha huyo msaidizi wa Yanga na nafasi ya beki wa kati anayocheza, lakini mwenyewe anasema hajawahi kuumizwa na kauli hiyo na wala haijampunguzia kasi ya kupambana.
“Kama kimo kingekuwa ni kipimo cha uchezaji basi mimi sina cha ziada zaidi ya akili ambayo naitumia sasa kwenye uchezaji wangu, kuna wachezaji warefu lakini hawana kipaji cha kufanya vizuri naamini katika mbinu na akili,” anasema.
FAINALI SHIRIKISHO BAB’KUBWA
Job amecheza mechi nyingi akiwa Yanga, lakini akiutaja mchezo wa fainali Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger kwenye uwanja wa Stade du Juillet.
“Mechi yangu bora ni siku tumecheza fainali ya Stade du Juillet hii siku sikutarajia kukutana na mashabiki ambao wanashangilia mwanzo mwisho. Ilikuwa siku ngumu na bora kwangu kwa sababu nilicheza fainali licha ya kukosa taji lakini nimeingia kwenye rekodi ya kuvaa medali ya CAF,” anasema.
YEYE NA MAPENZI TU
Achana na mapenzi yake kwenye mchezo wa soka ambao amefanikiwa kuweka rekodi akicheza, lakini ni mpenzi wa nyimbo za mapenzi.
Beki huyo ambaye ni nahodha msaidizi wa Yanga anataja wasanii ambao amekuwa akiwasikiliza mara kwa mara na nyimbo zao zimetawala kwenye simu yake kuwa ni Mbwana Yusuph ‘Mbosso’, Rajab Abdul ‘Harmonize’, Omary Mwanga ‘Marioo’ na Naseeb Abdul ‘Diamond’. “Ukisema nikutajie nyimbo ninazosikiliza mara kwa mara sitaweza kuzitaja kwa uharaka ila wasanii ninaowasikiliza muda mwingi ni hao niliowataja kwenye simu yangu nyimbo zao zipo za kutosha.”
KUTUPIA PAMBA KAWAIDA
Ukitaja mastaa wanaocheza Ligi Kuu ambao wanapiga pamba kali huwezi kusita kutaja jina la Job na unapomuuliza ni mwanamitindo gani anamvalisha.
“Sina mwanamitindo yeyote huwa navaa mwenyewe na hakuna mtu ananichagulia. Nikifungua kabati natoa nguo na nikivaa ndio napata sifa kuwa nimependeza.”