DAVID OUMA; Kocha Mkenya mwenye rekodi zake Bongo
Muktasari:
- Uamuzi huo wa Singida wa kuvunja benchi la ufundi ulifikiwa ikiwa ni muda mfupi tangu timu hiyo ichapwe mabao 2-0 na TRA United, katika mechi ya Ligi Kuu Bara, iliyopigwa Kwenye Uwanja wa Sheikh Amri, Abeid, jijini, Arusha.
JUMAPILI ya Pasaka kwa maana ya Aprili 5, 2026, ilikuwa ni siku ngumu kwa Singida Black Stars, baada ya uongozi wa timu hiyo kulivunja benchi lote la ufundi, lililokuwa linaongozwa na kocha wa kikosi hicho raia wa Kenya, David Ouma.
Uamuzi huo wa Singida wa kuvunja benchi la ufundi ulifikiwa ikiwa ni muda mfupi tangu timu hiyo ichapwe mabao 2-0 na TRA United, katika mechi ya Ligi Kuu Bara, iliyopigwa Kwenye Uwanja wa Sheikh Amri, Abeid, jijini, Arusha.
Ouma aliyetangazwa rasmi kushika wadhifa huo, Januari 5, 2026, akichukua nafasi ya Miguel Gamondi aliyejiunga na timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars', aliondolewa na aliyekuwa meneja mkuu wa kikosi hicho, Othmen Najjar, raia wa Tunisia.
Licha ya Singida kuvunja benchi la ufundi, ila, Ouma ameweka rekodi za kuvutia kwa nafasi mbalimbali alizowahi kushika Tanzania na timu alizofundisha, akihudumu kocha mkuu na wakati mwingine akiwa ni msaidizi kama Mwanaspoti linavyoelezea.
AIPELEKA COASTAL MICHUANO YA CAF
Kabla ya kujiunga na Singida Black Stars, ila Ouma aliwahi kuifundisha pia Coastal Union 'Wagosi wa Kaya', na kocha huyo aliandika rekodi ya kipekee, ambayo itaendelea kukumbukwa sana na mashabiki na wadau wengi wa soka wa kikosi hicho.
Ouma alijiunga na Coastal Union, Novemba 9, 2023, akichukua nafasi ya aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi hicho na Mkurugenzi wa Programu za vijana, Mkongomani Mwinyi Zahera, aliyeondoka kikosini na kujiunga na Namungo maarufu 'Wauaji wa Kusini'.
Msimu wa 2023-2024, Ouma, aliiwezesha timu hiyo kumaliza nafasi ya nne katika Ligi Kuu na pointi 43, baada ya kushinda mechi 11, sare 10 na kupoteza tisa, jambo lililoiwezesha kufuzu kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Hatua hiyo ilikuwa ni mafanikio makubwa kwa kikosi hicho cha 'Wagosi wa Kaya', kwani kilifuzu michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza, tangu mara ya mwisho kiliposhiriki na kuishia raundi ya kwanza mwaka 1989.
Katika michuano ya mwaka 1989, Coastal ilitolewa na Costa do Sol ya Msumbiji kwa jumla ya mabao 5-2, ikifungwa nyumbani mabao 3-2 na kupigwa 2-0, ugenini na tangu hapo haikushiriki tena ikiichukua miaka 25, kucheza kwa msimu wa 2023-2024.
Hata hivyo, Ouma aliachana rasmi na kikosi hicho Agosti 24, 2024, ikiwa ni muda mfupi tu tangu timu hiyo ichapwe mabao 3-0 na Bravos do Maquis ya Angola, katika mechi ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Kichapo hicho kiliifanya timu hiyo kuongozwa na Kocha Msaidizi, Joseph Lazaro, katika mechi ya marudiano, jijini, Dar es Salaam na ilishindwa kutamba nyumbani na kulazimishwa suluhu (0-0) hivyo, kutolewa kwa jumla ya mabao 3-0.
REKODI YA SINGIDA BLACK STARS
Kwa msimu wa 2025-2026, Ouma aliiongoza Singida katika mechi 17 za Ligi Kuu na kati ya hizo alishinda saba, akitoka sare nne na kupoteza sita, akiiacha ikiwa nafasi ya sita na pointi 25, huku timu hiyo ikifunga mabao 19 na kuruhusu 19.
Mbali na Ligi Kuu, Ouma aliweka pia rekodi mpya ya kuiongoza timu hiyo kufuzu Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza msimu wa 2025-2026, baada ya kikosi hicho kumaliza nafasi ya nne kwa msimu wa 2024-2025 na pointi 57.
Katika Ligi Kuu msimu wa 2024-2025, Singida ilimaliza nafasi ya nne na pointi 57, baada ya timu hiyo kushinda mechi 17, sare sita na kupoteza saba, ikiweka rekodi ya kufuzu Michuano ya CAF kwa mara ya kwanza kwenye historia ya kikosi hicho.
Licha ya kufuzu michuano hiyo baada ya kumaliza nafasi ya nne kwa msimu wa 2024-2025, ila Ouma aliweka rekodi nyingine mpya, baada ya kukiongoza kikosi hicho kufika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza.
Katika Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika ambayo timu hiyo ilishiriki kwa mara ya kwanza msimu wa 2025-2026, Ouma aliiongoza hadi hatua ya makundi na kumaliza nafasi ya nne ya msimamo wa kundi C, baada ya kukusanya pointi tano.
Kwenye kundi C, Stellenbosch FC ya Afrika ya Kusini ilimaliza ya tatu na pointi tano kama za Singida, huku CR Belouizdad ya Algeria ikiongoza na pointi zake 15, ikifuatiwa na AS Otoho ya Congo Brazzaville, iliyomaliza ya pili na pointi tisa.
TAJI MOJA LA KAGAME
Tangu ameanza kufundisha timu za Tanzania, Ouma amechukua taji moja tu la Kombe la Cecafa Kagame akiwa na Singida, baada ya kuifunga Al-Hilal Omdurman ya Sudan mabao 2-1 katika mechi ya fainali iliyopigwa, Septemba 15, 2025.
Fainali hiyo iliyopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, jijini, Dar es Salaam, iliifanya Singida kuandika rekodi hiyo mpya, kwani kabla ya hapo kikosi hicho kilikuwa hakijawahi kutwaa ubingwa huo.
Singida iliandika rekodi mpya ya kutwaa taji hilo ikiwa chini ya aliyekuwa Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi, huku Ouma akiwa msaidizi wake.
REKODI ZA KWAO KENYA
Licha ya kufanya mambo makubwa akiwa na timu mbalimbali za Tanzania kuanzia Coastal Union na Singida, Ouma ameweka pia rekodi za kuvutia na za kukumbukwa katika soka la kwao Kenya, alilolitawala kwa kipindi cha zaidi ya miaka yake 21.
Kocha huyo Mkenya anasifiwa na kukumbukwa kwa kuiongoza timu ya taifa ya soka ya wanawake ya Kenya, Harambee Starlets, kufuzu kwa mara ya kwanza kushiriki rasmi Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) mwaka 2016.
Timu hiyo iliandika rekodi hiyo kwa faida ya bao la ugenini, baada ya kikosi hicho kutoka sare ya jumla ya mabao 3-3, dhidi ya Algeria.
Katika fainali hizo zilizofanyika Cameroon, kuanzia Novemba 19 hadi Desemba 3, 2016 na Nigeria kutwaa ubingwa baada ya kuwafunga wenyeji, Ouma aliiongoza timu hiyo kushika ya nne kundi B, bila ya kuvuna pointi yoyote.
Kenya ilichapwa mechi zote na kuziacha Nigeria iliyoichapa Cameroon bao 1-0, katika mechi ya fainali kuongoza kundi B na pointi saba sawa na Ghana iliyokuwa ya pili ila zikitofautiana kwa mabao tu, huku Mali ikimaliza ya tatu na pointi tatu.
Pia, alikuwa na mafanikio makubwa akiwa na Sofapaka FC, akiiwezesha kushinda ubingwa wa ndani wa GOtv Shield mwaka 2014, kisha, baadaye aliteuliwa rasmi kuhudumu katika kikosi hicho akiwa ni Mkurugenzi wa Michezo wa klabu hiyo mwaka 2023.
Ouma aliyetawala soka la Kenya kwa zaidi ya miaka 21, ana leseni ya UEFA, CAF A na uzoefu kutoka kituo cha michezo cha Ajax Amsterdam cha Uholanzi, akifundisha pia timu ya taifa ya Kenya 'Harambee Stars' chini ya Bobby Williams mwaka 2015.