Mastraika wamtibua kocha Singida Black Stars
Muktasari:
- Katika mechi hiyo iliyochezwa Kwenye Uwanja wa Airtel, Singida, mabao ya Azam yalifungwa na Lusajo Mwaikenda, dakika ya 49 na Feisal Salum ‘Fei Toto’ dakika ya 64, huku la kufutia machozi la Singida likifungwa na Ayoub Lyanga, dakika ya 71.
KIPIGO cha mabao 2-1, ilichokipata Singida Black Stars juzi katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC, kimemfanya kocha wa kikosi hicho, Mkenya David Ouma, kudai washambuliaji ndio waliomuangusha.
Katika mechi hiyo iliyochezwa Kwenye Uwanja wa Airtel, Singida, mabao ya Azam yalifungwa na Lusajo Mwaikenda, dakika ya 49 na Feisal Salum ‘Fei Toto’ dakika ya 64, huku la kufutia machozi la Singida likifungwa na Ayoub Lyanga, dakika ya 71.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ouma, amesema timu hiyo ilitengeneza nafasi nyingi za kufunga, japo, umakini mdogo wa kuweza kuzimalizia kwa safu ya ushambuliaji kulisababisha kupoteza mechi, jambo ambalo anaendelea kulifanyia kazi kwa uharaka.
“Tulikuwa na uwezo wa kuimaliza mechi mapema kutokana na nafasi nyingi za kufunga tulizozitengeneza, wenzetu walionyesha ukomavu katika kufanya uamuzi wa haraka na kupata mabao yaliyotupa kazi kubwa ya ziada ili kuyarejesha,” amesema Ouma.
Akizungumzia kiwango cha timu hiyo hasa kwa mechi kubwa, Ouma amesema kinachosababisha kupoteza ni umakini wa eneo lote la ushambuliaji, ingawa, malengo makubwa ni kuhakikisha anaendelea kukipigania kikosi hicho, kimalize nafasi nne za juu. “Mwenendo wetu sio mzuri kwa sababu tunapoteza pointi nyingi dhidi ya wapinzani wetu wakubwa, bado tuna mechi 14, ambazo tunahitaji kupambana zaidi ili tufikie malengo yetu tuliyojiwekea ya kumaliza nafasi nne za juu mwishoni mwa msimu huu.”
Katika mechi 16 ilizocheza timu hiyo hadi sasa, imeshinda saba tu, sare nne na kupoteza mitano, ikiwa nafasi ya sita na pointi 25, ambapo safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho imefunga mabao 19, huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 17.
Kauli ya Ouma inatokana na mwenendo usioridhisha wa washambuliaji wa kikosi hicho, ambapo, Mkenya Elvis Rupia aliyefunga mabao 10, ya Ligi Kuu akionyesha kiwango bora msimu uliopita wa 2024-2025, msimu huu wa 2025-2026, amefunga mawili tu.
Kwa upande wa mshambuliaji, Joseph Guede, aliyewahi kutamba na Yanga kisha kujiunga na Singida aliyoachana nayo Januari 23, 2025 na kutua Al-Wehdat SC ya Jordan kabla ya kurejea tena Januari 2026, hadi sasa amefunga bao moja la Ligi Kuu.
Winga, Mossi Nduwumwe, aliyejiunga na kikosi hicho Januari 2026, akitokea Flambeau du Centre FC ya kwao Burundi, ndiye anayeongoza kwa kufunga mabao mengi, akiwa nayo matatu ya Ligi Kuu Bara, sawa na beki wa kushoto, Mghana Ibrahim Imoro.