Prime
Dabi ya Zenji Simba 4, Yanga 2
ILE siku iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu na mashabiki na wapenzi wa soka kuanzia Bara hadi Zanzibar kunakopigwa Dabi, imefika wakati Simba na Yanga zitashuka uwanjani kuumana katika pambano la kwanza la Ligi Kuu Bara kwa msimu huu na la kwanza visiwani humo kwa ujumla.
Zile tambo za timu ipi ina kikosi na kocha bora zitahitimishwa baada ya dakika ya pambano hilo litakalochezeshwa na mwamuzi Nassoro Mw inchui kutoka Tanga na wasaidizi Kassim Mpanga (Dar), Hamdani Said (Mtwara) na Ramadhan Kayoko wa Dar atakayekuwa mezani.
Hili ni pambano la 115 kwa timu hizo katika Ligi ya Bara tangu 1965, lakini likiwa ni la 11 kwa kila mmoja kwa msimu huu wa Ligi inayoongozwa na Yanga ilikusanya pointi 28 kwa kushinda mechi tisa na sare moja, huku Simba ikiwa ya tatu na pointi 23, ikishinda saba, sare mbili na kipigo kimoja. Pia pambano la leo litakuwa ni la saba kwa timu hizo kukutana Zanzibar na hadi sasa hakuna aliye na uhakika wa matokeo ya mtanange huo, lakini hap0 chini ni matokeo ya mechi sita za awali kwa timu hizo visiwani humo na Simba ikiongoza kwa kushinda mara nne dhidi ya mbili za watani wao.
JANUARI 1975
Hili ndilo lililokuwa pambano la kwanza kwa Simba na Yanga kukutana visiwani ikiwa ni katika fainali za Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (sasa Kagame Cup) ambapo michuano hiyo ilifanikia Zanzibar na Yanga kuibuka wa ushindi wa mabao 2-0.
Fainali za mwaka huo zilishirikisha klabu sita tu, Simba, Gor Mahia ya Kenya na Jeshi ya Zanzibar zilizokuwa Kundi A, huku Mufurila Wanderers ya Zambia, Express ya Uganda na Yanga zikipangwa Kundi B. Simba na Gor Mahia ndizo zilizofuzu nusu fainali kutoka kundi A na kuungana na Yanga na Mufulira.
Simba ilitinga fainali kwa kuifunga Mufurila kwa mabao 2-0 na Yanga kuinyoa K’Ogalo kwa bao 1-0 na watani wakakutana katika fainali iliyopigwa Januari na Yanga kushinda 2-0 kwa mabao Gibson Sembuli na Sunday Manara ‘Computer’.
JANUARI 1992
Miaka 17 baadaye timu hizo zilikutana tena tena visiwani humo katika fainali za michuano hiyo ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati 1992 ambayo ilishirikisha klabu saba zikiwamo Bata Bullets ya Malawi, Simba, Al Hilal ya Sudan na Jamhuri ya Zanzibar zilizokuwa Kundi B, huku Yanga ikipangwa KUndi A na Small Simba ya Zanzibar na Rivertex ya Kenya.
Yanga na Small Simba zilivuka kwenda nusu fainali kwa Kundi A, wakati Simba nAl Hilal zilipenya Kundi B na katika hatua hiyo, Simba iliinyoa Small Simba kwa bao 1-0 na Yanga kuicharaza Al Hilal kwa penalti 10-9 baada ya dakika za kawaida kumalizika kwa suluhu.
Katika mechi ya fainali, dakika 120 zilimalizika kwa sare ya ba0 1-1 na Simba kushinda kwa penalti 5-4 licha ya kila timu kupiga mikwaju nane, Simba ikishinda kupitia kwa George Masatu, Hamza Maneno, Fikiri Magosso, Issa Kihange na George Lucs ‘Gaza’, huku Twaha Hamidu ‘Noriega’, Kassongo Athuman na Damian Kimti wakikosa.
Penalti za Yanga katika fainali hizo ziliwekwa kimiani na Said Mwaibambe ‘Zimbwe’, Issa Athuman, Sanifu Lazaro ‘Tingisha’ na Hamis Thobias Gaga ‘Gagarino’ , huku Said Mwamba ‘Kizota’, Salum Kabunda ‘Ninja’, Abubakar Salum ‘Sure Boy’ na David Mwakalebela wakikosa.
OKTOBA 27, 1992
Miezi kama tisa tu tangu Simba kupata ushindi wa penalti katika fainali za Klabu Bingwa Cecafa, Jumanne ya Oktoba 27, mwaka huo huo timu hizo zilikutana tena, ila safari hii ikiwa ni katika mechi ya Ligi Kuu ya Muungano ambao ndio iliyokuwa ikitumika kutoa Mwakilishi wa Tanzania katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika).
Kama ilivyokuwa Januari, Simba tena ilishinda kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na Damian Kimti, ambaye alikuwa miongoni mwa wachezaji waliokosa penalti katika mechi ya Cecafa na kupeleka kilio Jangwani ambao walitoka pia kupasuka katika Ligi ya Bara msimu huo kwa mbao 2-0. Awali Yanga ilishinda katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Bara kwa bao 1-0 lililotokana na shuki kali la mbali la beki Kenneth Mkapa dakika ya 10 lililodumu hadi dakikaa ya mechi hiyo ya kusisimua.
JANUARI 12, 2011
Pambano la nne kwa timu hizo za Simba na Yanga kukutana Zanzibar ilikuwa ni fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi 2011 iliyopigwa Januari 12, siku ya kilele cha maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar na kama kawaida, Wekundu wa Msimbazi waliibuka kidedea.
Katika mechi hiyo iliyokuwa ya kwanza kwa vigogo hivyo kukutana katika michuano hiyo ya Kombe la Mapinduzi, mabao ya ushindi wa Simba yaliwekwa kimiani na washambuliaji, Mussa Hassan ‘Mgosi’ dakika ya 33 na Shijja Mkina dakika ya 71, huku Yanga ikichezea asimilia kubwa ya kikosi cha wachezaji vijana.
JANUARI 10, 2017
Dabi ya Kariakoo ya tano kupigwa visiwani ilipigwa tena Januari 10, 2017 ikiwa ni mechi ya nusu fainali ya michuano a Kombe la Mapinduzi 2017, ambapo Simba iliendelea ubabe wake mbele ya vijana wa Jangwani kwa kuifunga tena kwa penalti 4-2 baada ya dakika 90 kuisha kwa suluhu.
Ikafuata hatua ya kupigiana penalti na Simba kushinda kupitia mikwaju ya nahodha Jonas Mkude, kipa Daniel Agyei, Mzamiru Yassin na Javier Besala Bokungu, huku Method Mwanjali ndiye pekee aliyekosa. Penalti za Yanga zilifungwa Simon msuva na Thabani Kamusoko, huku zile za Haji Mwinyi Mngwali na kipa Deo Munishi ‘Dida’ zikiokolewa na kipa wa Simba na kuvusha timu hiyo kwenda fainali ilipovaana na Azam FC na kupoteza kwa bao 1-0 la shuti kali la mwana ukome la Himidi Mao ‘Ninja’ dakika 13 na kudumu hadi pambano lilipomalizika Azam ikibeba ubingwa wa tatu.
JANUARI 13, 2021
Hili ndilo lililokuwa pambano la mwisho kwa watani wa jadi hao wa soka nchini kukutana visiwani Zanzibar, likiwa ni la fainali za Kombe la Mapinduzi 2021 ambapo safari hii, Yanga ilijitutumua na kupata ushindi mbele ya Mnyama.
Yanga ilishinda na kubeba lililokuwa taji lao la pili la michuano tangu ilipotwaa mara ya mwaka 2007 kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya dakika 90 kushuhudiwa matokeo yakiwa ni suluhu (0-0).
Yanga ilipata penalti zake kuputia Tuisila Kisinda ‘TK Master’, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Zawadi Mauya na Saido Ntibazonkiza, huku Mukoko Tonombe akipoteza mbele ya kipa Beno Kakolanya aliyeipangua, huku Simba ikifunga kupitia Francis Kahata, Chris Mugalu na Gadiel Michael.
Penalti za Meddie Kagere iligonga mwamba wa juu la lango wakati ile ya nahodha Joash Onyango iliokolewa na kipa Faruk Shikhalo na kuipa Yanga taji la tatu la Mapinduzi tangu 2007.
Je mechi ya leo ikiwa ni ya kwanza ya Ligi ya Bara kwa watani nani ataibuka na ushindi? Tusubiri!