Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mobetto anavyomkaribisha Alikiba Dabi ya Kariakoo

KIBA Pict


KWA mara nyingine tena, Yanga na Simba zinaenda kukipiga pale New Amaan Complex, Zanzibar, ila awamu hii ni katika mchezo wa Ligi Kuu Bara ambao una maana kubwa kwa Alikiba na Hamisa Mobetto.


Siku zote dabi hiyo ya Kariakoo imekuwa ikiteka hisia za mashabiki wengi wa soka kutoka ndani na hadi nje ya nchi, na ndivyo ilivyo kwa mastaa hao wa muziki, filamu na mitindo.


Katika mchezo huo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu 2025/26, Yanga ndiye timu mwenyeji, hivyo alitumia haki yake kikanuni kuhamishia mchezo huo Zanzibar, eneo lenye historia pia kwa Alikiba na Hamisa.

Mastaa hao wenye nguvu kubwa ya ushawishi Bongo upande wa burudani, wana simulizi zinazofanana linapokuja suala la ushabiki kwa timu za Simba na Yanga, ambazo ndizo zinaunda dabi ya Kariakoo.

Alikiba, mwanzilishi wa Kings Music, kwa sasa ni shabiki wa Simba ambao wanakwenda kutupa karata katika dabi hiyo wakiwa tayari wameachwa nyuma kwa alama tano na Yanga katika msimamo wa ligi.

KIBA 01

Kwa upande wake, Hamisa, mwanzilishi wa Mobetto Styles, yeye yupo upande wa Yanga ambao kwa sasa wana rekodi nzuri dhidi ya Simba, wakishinda michezo yote sita ya dabi katika misimu ya karibuni.

Hivyo, katika dabi hii huko visiwani, tunaweza kusema Hamisa ndiye mwenyeji wa Alikiba, mshindi wa tuzo ya MTV Europe Music Awards (EMAs) 2016 kama Msanii Bora Afrika.

Kubwa zaidi, dabi hiyo inawakumbusha miaka mitano iliyopita ambapo walikutana Zanzibar na kufanya kazi ambayo ilikuwa na matokeo mazuri katika ukuaji wa shughuli zao za sanaa.

KIBA 06

Ni pale Hamisa alipotokea katika video ya wimbo wa Alikiba, Dodo (2020), ambao umetayarishwa na Yogo Beats, huku video yake iliyoteka mazungumzo mtandaoni ikisimamiwa na kampuni ya Rockshot.

Hata hivyo, Alikiba katika moja ya mahojiano yake alisema hakujua kama Hamisa atatokea kwenye video hiyo; ni jambo lililopangwa na uongozi wa Kings Music, hivyo ilikuwa kama sapraizi kwake kukutana na Hamisa Zanzibar.

Video ya wimbo huo ulioandikwa na Alikiba na Tommy Flavour, mwimbaji wa zamani wa Kings Music, katika mtandao wa YouTube tayari imeshatazamwa (views) zaidi ya mara milioni 25.

KIBA 05

Hadi kufikia sasa, Dodo (2020) inashikilia nafasi ya nne katika orodha ya nyimbo za Alikiba zilizofanya vizuri zaidi YouTube, ikiwa imetanguliwa na nyimbo kama Mahaba (2023), Mwana (2014) na Utu (2022).

Kingine cha kufurahishwa ni kwamba Alikiba ndiye msanii wa mwisho kwa Hamisa kufanya naye kazi upande huo; yaani tangu kichupa cha ‘Dodo’ kiachiwe, mrembo huyo hajaonekana tena katika video ya msanii mwingine.

Uamuzi huo wa Hamisa umekuja baada ya hapo awali kufanya kazi na waimbaji wengine kama Abdukiba, Barnaba, Quick Rocka na Diamond Platnumz, mwanzilishi wa WCB Wasafi.

KIBA 04

Kwa mujibu wa Hamisa, ili aweze kutokea kwenye video ya msanii yeyote ni lazima yeye ndiye awe mhusika mkuu (main character), kitu ambacho kimefanyika pia katika video yake na Alikiba iliyofanyika Zanzibar.

Hivyo, Dabi ya Kariakoo inayochezwa visiwani humo wikiendi hii ni wazi kuwa inawakumbusha mradi huo, ingawa kila mmoja analiombea chama lake ushindi.

Alikiba anatamani kuiona Simba ikishinda ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kushinda ubingwa baada ya kukosa taji hilo kwa misimu minne mfululizo.

KIBA 03

Na kwa Hamisa angependa Yanga iendeleze rekodi ya ushindi katika dabi na kutetea ubingwa wake, hatua itakayofanya kuzidi kung’arisha rekodi yao ya kutwaa mataji mengi zaidi ya ligi, ambapo hadi sasa wanayo 31.

Hata hivyo, ikumbukwe Alikiba na Hamisa ni kama wamebadilishana kuzishabikia timu hizi za Kariakoo, kitu ambacho kimeonekana pia kwa wasanii wengine, ila kila mmoja ana sababu yake binafsi ya kufanya hivyo.

Ikumbukwe awali Alikiba alijipambanua kama shabiki wa Yanga, ila mshindani wake kimuziki, Diamond, alipohamia katika timu hiyo, ndipo naye akaondoka na kuhamia Simba alipopokelewa vizuri.

KIBA 02

Kwa Hamisa, hakuna asiyejua jinsi alivyokuwa mstari wa mbele katika zile shughuli kubwa za Simba, ila uhusiano wake na aliyekuwa mchezaji wa Yanga, Aziz Ki, ambaye sasa ni mume wake, ndio ulimuondoa Msimbazi.

Mnamo Agosti 2024, ndipo Hamisa alihamia rasmi Yanga; ni katika kilele cha Wiki ya Mwananchi ambapo Aziz Ki alitumia jukwaa hilo kumvisha Hamisa jezi ya timu hiyo, ikiwa ni ishara ya kumkaribisha kama shabiki.