Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Cyprian Kipenye bado anatembea na majina mawili Simba

KIPENYE Pict

Muktasari:

  • Nyota huyo aliyepitia mikasa mbalimbali hadi kufikia hapo alipo, alijiunga na Namungo msimu huu baada ya kuachana na Songea United inayoshiriki Ligi ya Championship, ambapo amezungumzia mengi kuhusu safari yake nzima ya soka ilivyokuwa, akibaki na majina ya watu wawili akilini mwaka waliozibeba ndoto zake katika soka.

KATIKA kila safari ya mafanikio ya mtu yeyote nyuma yake kuna majuto na changamoto nyingi anazopitia hadi kufika nchi ya ahadi, na hivyo ndivyo ilivyokuwa pia kwa kiungo mshambuliaji wa kikosi cha ‘Wauaji wa Kusini’, Namungo FC, Cyprian Kipenye.

Nyota huyo aliyepitia mikasa mbalimbali hadi kufikia hapo alipo, alijiunga na Namungo msimu huu baada ya kuachana na Songea United inayoshiriki Ligi ya Championship, ambapo amezungumzia mengi kuhusu safari yake nzima ya soka ilivyokuwa, akibaki na majina ya watu wawili akilini mwaka waliozibeba ndoto zake katika soka.

KIPE 01

KIONDO AMUIBUA

Nyota huyo anasema safari yake ya soka ilianzia katika kikosi cha vijana cha Simba B, chini ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Nico Kiondo, ikiwa ni siku chache tu tangu amalize masomo ya kidato cha nne kipindi hicho akitoka Mkoa wa Katavi.

“Mwaka 2018, nilipomaliza masomo yangu nilienda Dar es Salaam kutafuta nafasi ya kucheza mpira, nakumbuka ilikuwa kwenye Uwanja wa Kinesi pale Shekilango, ndipo Kocha, Nico Kiondo akavutiwa na kipaji changu na safari ikaanzia hapo,” anasema.

Kipenye anasema moja ya jambo kubwa ambalo Kocha Kiondo alimsihi ni kutuliza akili kwa sababu atampa nafasi ya kujiunga na kikosi cha Simba B, hivyo baada ya hapo msimu wa 2018-2019, akajiunga na kucheza katika timu hiyo kwa miezi minne tu.


KIPE 02

SVEN AMPA SHAVU SIMBA

Nyota huyo anasema baada ya kucheza kwa miezi minne katika timu ya vijana ndipo aliyekuwa kocha wa kikosi hicho raia wa Ubelgiji, Sven Vandenbroeck akampandisha Simba ya wakubwa kutokana na kuvutiwa na kipaji alichokuwa anakionyesha.

“Nakumbuka Simba ilikuwa inacheza na Yanga na mechi ikaisha kwa sare ya bao 1-1, baada ya hapo Meneja Patrick Rweyemamu alinifuata na kuniuliza kama niko vizuri, nikamwambia ndio, kisha akaniambia niende kambi ya timu ya wakubwa,” anasema.

Anasema baada ya kwenda kambini katika kikosi hicho, Rweyemamu alimwambia atakuwa ni miongoni mwa wachezaji watakaoenda Zanzibar kwa ajili ya michuano ya Kombe la Mapinduzi, jambo ambalo lilimfanya ashindwe kulala kwa furaha aliyokuwa nao.

“Baada ya kufika Zanzibar nikapata nafasi ya kuongea vizuri na Kocha, Sven na alichoniambia kuanzia leo wewe ni mchezaji wa timu ya wakubwa, kiukweli ni mtu ambaye sitokaa nikamsahau katika maisha yangu kwa sababu alinisaidia sana,” anasema.


KIPE 08

KILICHOMUONDOA SIMBA

Nyota huyo anasema maisha yake Simba yalikuwa mazuri kwa sababu alipendwa na wachezaji na watu wote, jambo ambalo lilikuwa linampa nguvu sana ya kupambana, japo aliomba kuondoka mwenyewe kwa lengo la kutafuta changamoto sehemu mpya.

“Mimi niliomba viongozi mwenyewe ili niondoke nikatafute sehemu nyingine itakayonifanya nizidi kuonyesha kipaji changu, nashukuru walikubaliana nami na kunitakia kila la heri niendako, kiukweli nilijiona fahari kuishi na watu wenye utu.”


SHABIKI WA SAMATTA, AZIZ KI

Kipenye anasema wachezaji wanaomvutia ni nyota wa Tanzania na Klabu za Fenerbahce ya Uturuki, Aston Villa ya England, PAOK ya Ugiriki na sasa Le Havre AC ya Ufaransa, Mbwana Samatta na Stephane Aziz KI wa Wydad Casablanca kutoka Morocco.

“Nampenda sana Aziz KI na hata alivyokuwa Yanga nilikuwa namfuatilia kwa sababu anacheza nafasi ambayo na mimi naicheza, Kwa Samatta ni kioo kwetu vijana wengi hasa wa Kitanzania wenye malengo ya kufika mbali, naamini inawezekana,” anasema.


MWENDA MSUMBUFU

Anasema licha ya kucheza na mabeki mbalimbali, ila miongoni mwa watu wanaomsumbua kila anapokutana nao ni beki wa Yanga, Israel Mwenda, japo hajutii kwa sababu inampa changamoto nzuri zinazomfanya kumkuza ili azidi kupambana na asibweteke.

“Jamaa ni msumbufu sana ingawa nafurahia ninapokutana na changamoto kutoka kwa mtu yeyote, hii kwangu inanifanya nizidi kufikia na kuongeza juhudi kwa kila ninachokifanya ili niwe bora, maana kufanikiwa ni lazima pia uyashinde majaribu.”

KIPE 06

ANGEKUWA MSANII

Kipenye anasema kama asingekuwa mchezaji wa mpira leo, basi angekuwa ni msanii au dansa kwa sababu ilikuwa ni kazi yake kipindi hicho yupo kwao Katavi hivyo, kwa sasa anajivunia nafasi aliyonayo kutokana na kumuunganisha na watu mbalimbali.

“Siwezi kujutia hapa nilipo leo kwa sababu nilikuwa na mipango yangu ila, Mwenyezi Mungu akanionyeshea sehemu nyingine bora zaidi kwangu, kiukweli najivunia na ndoto yangu kubwa ni kuwasaidia pia vijana wenzangu kufika mbali,” anasema.


KIPE 05

ASAJILIWA KWA SH2 MILIONI

Nyota huyo anasema moja ya kiasi kidogo cha fedha alichowahi kupewa wakati anasajiliwa ilikuwa ni Sh2.5 milioni, kipindi hicho akiichezea Biashara United ya mkoani Musoma, iliyokuwa inashiriki Ligi ya Championship, kabla ya kushuka daraja.

“Msimu wa 2023-2024, nilisajiliwa na Biashara United na ilikuwa kiasi hicho cha fedha, sikuwa na jinsi kwa sababu wakati huo nilikosa timu nyingine, hivyo niliona ni bora nijiunge nao ili iwe nafasi kwangu ya kujitafuta tena upya,” anasema.


MECHI ASIYOISAHAU

Anasema miongoni mwa mechi ambayo hatokaa akaisahau katika maisha yake ni ya ‘Play-Off’, kusaka tiketi ya kucheza Ligi Kuu Bara, ambapo Biashara United ilikuwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi kucheza na Tabora United sasa TRA United.

“Ni mechi ambayo sitoisahau kwa sababu ilikuwa na matukio mengi ya kustaajabisha, gari letu lilipigwa mawe na kuvunjwa hadi vioo, ilikuwa ni zaidi ya vita kwa mashabiki wa timu zote na sisi wachezaji tulicheza kwa kuhofia usalama wetu.”

Katika mechi hiyo iliyokuwa ya marudiano, TRA United zamani Tabora United ilishinda kwa mabao 2-0, Juni 16, 2024, hivyo, kujihakikishia kubakia Ligi Kuu kwa jumla ya mabao 2-1, baada ya pambano la kwanza kuchapwa ugenini 1-0, Juni 12, 2024.

KIPE 04

BAO BORA KWAKE

Anasema licha ya kufunga mabao mbalimbali hadi sasa, ila miongoni mwa bao bora ambalo hatolisahau ni lile alilolifunga msimu uliopita wa 2024-2025, kipindi akiichezea Songea United ilipokutana na Mbeya Kwanza katika Ligi ya Championship.

“Mechi hiyo tulishinda mabao 2-1, kwenye Uwanja wa Majimaji Songea, moja ya kitu nilichopenda nilifunga bao hilo nikiwa umbali wa mita 25, tena mbele ya aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro, kiukweli litabakia moyoni.”


KILA MECHI FAINALI

Kipenye anasema Ligi ya Championship ni ngumu sana kuliko Ligi Kuu Bara kwa sababu kila mechi huwa ni fainali kwani timu mbili za juu ndio zinazopata nafasi ya kupanda daraja moja kwa moja, jambo ambalo linaloongeza mvuto na ushindani zaidi.

“Ligi Kuu timu nyingi zinapambana kubakia kama hazitoweza kushindania ubingwa, jambo ambalo kwa Championship huwa ni tofauti sana kwa sababu unapambana ili upande juu, hali ya namna hiyo huongeza ugumu wa kila mechi mnayocheza,” anasema. 


KIPE 03

CHAMPIONSHIP YAMKOMAZA

Anasema kucheza Ligi ya Championship ilikuwa ni njia nzuri kwake ya kupambana ili kurudi katika ubora wake, kwa sababu baada ya hapo amejifunza mambo mengi ambayo leo hii anajivunia kutokana na uvumilivu mkubwa aliokuwa nao tangu mwanzoni.

“Unapokuwa timu kubwa alafu ghafla ukashuka mashabiki wanaona kama umepotea, kiukweli baada ya kucheza Championship mimi niliamini ni njia bora ya kunirudisha tena katika ramani ya soka, jambo ambalo namshukuru Mwenyezi Mungu amenisaidia.”

Kipenye anasema moja ya malengo yake makubwa ni kuona siku moja anakuwa mchezaji mkubwa ndani na nje ya nchi, huku jambo lingine kubwa analotamani kulifanya ni kuwasaidia pia vijana wengine wanaocheza mpira wa miguu ili watimize ndoto zao.

“Natambua vijana jinsi ambavyo tunapitia changamoto nyingi sana hadi kufikia malengo yetu kwa sababu ni hali ambayo nami pia nimeshakutana nayo, natamani kuona nikisaidia wenzangu ili niweke kumbukumbu nzuri ambazo zitaishi maishani mwangu.”