Clara, straika wa Yanga anayeiota England

MOJA kati ya utani mkubwa kwa watu wa kabila la Wahehe ni kuambiwa eti wanakula Mbwa, na imekuwa hivyo kwa miaka mingi, japo wenyewe wamekuwa wakikanusha kuwa hawafanyi jambo kama hilo.

Kadhalika wamekuwa wakitaniwa kuwa na hasira kiasi ukiwazingua kidogo tu, hawakawii kujiua, lakini kwa nyota wa timu ya taifa ya wanawake anayekipiga Yanga Princess, Clara Luvanga anajibu utani huo kulipa heshima kabila hilo kwa kuupiga mwingi uwanjani.

Clara, anasema stori na utani dhidi ya Wahehe ambalo ni kabila lake ni mambo ya kudumisha utani kwa makabila ya Watanzania na hakuna kitu kama hicho katika maisha ya sasa, huku akisema kuleta heshima kwake ndio maana anafunga sana.

Ndio, katika kikosi cha timu ya taifa ya wanawake U17, Serengeti Girls akiwa ndiye kinara eneo la ushambuliaji, mwanadada huyo anafunga sana akiwa kwenye kiwango bora kabisa, akiwasha moto kuanzia Ligi Kuu ya Wanawake (WPL).

Kabla ya mechi ya marudiano ya raundi ya tatu kuwania tiketi ya Kombe la Dunia 2022 kwa timu za Afrika iliyopigwa jana usiku visiwani Zanzibar kwa timu hiyo ya Tanzania dhidi ya Burundi, Clara ndiye aliyekuwa kinara wa mabao akifunga saba.

Katika WPL, pia amefunga mabao 13 akiwa ndani ya Nne Bora ya wafungaji, licha ya kutocheza mechi nyingi kutokana na jukumu la kuipigania taifa kwenda katika fainali za Kombe la Dunia zitakazopigwa mwishoni mwa mwaka huu huko India.

Mwanaspoti imebahatika kufanya mahojiano na straika huyu, aliyefunga bao pekee lililoizamisha Simba Queens katika mechi ya dabi katika Ligi Kuu ya Wanawake, akivunja mwiko na unyonge wa timu yake mbele ya watetezi hao wa ligi hiyo.

Moja kati ya mambo ambayo yanazungumzwa sana ni aina ya muonekano ambao staa huyu amekuwa nao, watu wengi wamekuwa wakisema au kumdhania kuwa ni mwanaume.


MSIKIE MWENYEWE

Clara anasema; “Jambo hilo la kufananishwa na wanaume, linaloniumiza zaidi katika maisha yangu ya soka kwani, mimi ni msichana na nina mpango wa kuja kuolewa hapo baadae nakuwa na familia, hivyo maneno haya yananichoma sana.”

Mbali ya changamoto hiyo ya kuambiwa hivyo, Clara anasema changamoto nyingine kubwa aliyowahi kukutana nayo kwenye maisha yake ya soka ni hali ngumu ya maisha wakati akiichezea Mapinduzi Queens kabla ya kutua Jangwani.

“Maisha yalikuwa magumu sana pale kuna kipindi hata chakula nacho ilikuwa tabu kupatikana, ila nashukuru kipaji cha soka kimelainisha mambo, namshukuru sana Mungu,” anasema Clara.


ALIKOPITA

Akizungumzia alikotoka Clara anasema alianza maisha yake ya soka kwenye timu za mtaani kabla hajajiunga na Mapinduzi Queens ambayo kwa wakati huo ilikuwa ikishiriki kwenye Ligi Daraja la Kwanza na alicheza hapo hadi akafanikiwa kuipandisha timu Ligi Kuu na baada ya kucheza kwa msimu mmoja ndio akajiunga na Yanga Princess ambako anacheza hadi sasa.


USAJILI YANGA WAMPA NYUMBA

Kama ambavyo watu wengi wakipata pesa huwa wanawaza kufanya vitu ambayo wanaona ni sahihi kwao, kwa Clara naye ilikuwa hivyo hivyo, anasema pesa nyingi zaidi kuwahi kuipata kwenye soka ilikuwa ni wakati anatoka Mapinduzi na kujiunga na Yanga, alipewa pesa ya usajili Shilingi 5 Milioni tano ambazo aliamua kuzitumia kwa kujenga nyumba huko kwao Iringa alikozaliwa.


NDOTO ZAKE

Ingawa imekuwa ngumu sana kwa wachezaji wakike kutoka Afrika kucheza soka, nchini England, lakini kwa Luvanga hiyo ndio ndoto yake kubwa kwenye maisha yake ya soka na anatamani kufika huko kutokana na ukubwa wa soka la wanawake nchini humo kwenye nyanja zote.

“Nchi ambayo natamani sana kufika na kucheza soka ni England,” anasema Clara ambaye pia kwenye upande wa chakula ambacho anapendelea zaidi kula ni ugali na mboga za majani.


ASIPOFUNGA ANAUMWA

Kwa staa huyu jambo limekuwa likimuumiza na kumfanya akose usingizi au akose hamu ya kula kabisa ni kitendo cha kucheza mechi bila kufunga.

“Furaha yangu mimi ni kufunga ninapocheza mechi, hizo ndio huwa nyakati nzuri kwenye maisha ya ngu ya soka kwa sababu nikicheza mechi na nisipofunga huwa nakosa amani ya moyo.”


NJE YA SOKA

Wachezaji wengi huwa na ndoto nyingine nje ya soka na hiyo ipo hivyo kwa mrembo huyu wa Kihehe ambaye yeye anasema kuwa anapenda sana kujiandaa na maisha baada ya soka, hivyo kipaumbele chake ni kuwekeza kwenye biashara mbali mbali.

“Kama nisingekuwa mchezaji mpira najiona kabisa ningekuwa mfanya biashara kwa sababu ndio kitu kingine ninachopenda kufanya.”