Chipo aanze na hili Mtibwa Sugar
Muktasari:
- Kwa kumteua Chipo, kijiwe kinafahamu Mtibwa Sugar imekwepa adhabu nzito iliyokuwa inainyemelea timu hiyo kutoka kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB).
JUZI Mtibwa Sugar ilimtambulisha rasmi Kocha Yusuf Chipo kutoka Kenya kuwa kocha Mkuu kwa msimu huu.
Kwa kumteua Chipo, kijiwe kinafahamu Mtibwa Sugar imekwepa adhabu nzito iliyokuwa inainyemelea timu hiyo kutoka kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB).
Adhabu hiyo ambayo ingeikumba Mtibwa Sugar kwa mujibu wa kanuni ni ya kushushwa daraja kama kanuni 47:19 ya Ligi Kuu msimu huu inavyofafanua.
"Timu yoyote ya Ligi Kuu itakayoanza msimu mpya na kucheza mchezo wa ligi bila kuwa na kocha mwenye ujuzi kwa kanuni ya 77: (1,2,3) itatozwa faini ya Shilingi milioni tano (5,000,000) kwa kila mchezo kwa michezo hadi sita (6) ya Ligi Kuu.
“Endapo bado itashindwa kutimiza sharti hili la kuwa na kocha anayehitajika kikanuni, itaondolewa kwenye Ligi Kuu na kushushwa daraja,” inafafanua kanuni hiyo.
Kwa maana hiyo, Mtibwa Sugar imeshakwepa kiunzi cha kwanza lakini sasa mtihani mkubwa upo kwa Kocha Chipo kuwapa kile wanachokitegemea ambacho hapana shaka ni kufanya vizuri katika ligi na mashindano mengine.
Katika kulitimiza hilo, hapa kijiweni tunamshauri Chipo aanze zaidi na kuiboresha safu yake ya ushambuliaji ili iweze matokeo mazuri ambayo imeyapata katik mechi moja tu kati ya tano ilizocheza msimu huu.
Kwa sisi ambao tumefanikiwa kutazama mechi hizo za Mtibwa Sugar msimu huu, tumeiona ikicheza vizuri kuanzia nyuma hadi katikati lakini mpira unapofika mbele, mabao hayaonekani.
Chipo tayari anapo pa kuanzia, hivyo tunategemea mbinu za kusaka mabao ndio zitaanza kwani safu ya ulinzi inajitahidi kwa kiasi kikubwa.