Chama lako linafunga kipindi gani?
Muktasari:
- Kila timu imekuwa na ubora wa kufunga mabao ambapo zipo hatari kufunga kipindi cha kwanza na zingine kile cha pili huku zipo pia ambazo vipindi vyote zenyewe ni fresh tu zinatupia kambani
LIGI Kuu Bara ilisimama kupisha mechi za kalenda ya Shirikisho la Kandanda la Kimataifa (Fifa), kila timu ikijiuliza juu ya ilivyoanza mechi za kwanza msimu huu, lakini kuna mambo flani ya kuangalia kuhusu ubora.
Kila timu imekuwa na ubora wa kufunga mabao ambapo zipo hatari kufunga kipindi cha kwanza na zingine kile cha pili huku zipo pia ambazo vipindi vyote zenyewe ni fresh tu zinatupia kambani
YANGA KIPINDI CHA PILI
Yanga ambayo ndio vinara wa Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi 10 wakishinda tatu na sare moja, mabao yao mengi wameyatengeneza kipindi cha pili wakifunga sita huku kipindi cha kwanza wakifunga matatu pekee.
Mabao mawili ya kipindi cha pili dhidi ya Pamba ikishinda 3-0, moja dhidi ya Mtibwa Sugar ilipopata ushindi wa mabao 2-0 na matatu ilipoishinda KMC 4-1, mabingwa watetezi wakionyesha ubora wa kufunga mabao mengi kipindi cha pili.
SIMBA KIPINDI CHA PILI
Simba ambayo ipo nafasi ya pili kwenye msimamo ni hatari kipindi cha pili ambapo kwenye mechi tatu mpaka sasa imefunga mabao manne ndani ya dakika 45 za pili huku kipindi cha kwanza ikifunga mabao mawili pekee.
Mabao mawili ambayo Simba iliyafunga kipindi cha kwanza ni kwenye mchezo wake wa kwanza wa ligi msimu huu dhidi ya Fountain Gate ikishinda 3-1 lakini ikaenda kutengeneza ushindi mzuri kipindi cha pili kwenye mechi dhidi ya Namungo iliposhinda 3-0 kisha JKT Tanzania ilipofunga mabao mawili kipindi hicho ikipata ushindi wa mabao 2-1.
MBEYA KIPINDI CHA KWANZA
Takwimu zinaonyesha Mbeya City mabao yake mengi imeyafunga kipindi cha kwanza ikifunga matatu huku kipindi cha pili ikifunga mawili pekee.
Mbeya City ambayo imeshapoteza mechi mbili msimu huu ndani ya mechi sita ilizocheza, ilifunga mabao mawili kipindi cha kwanza iliposhinda 3-0 dhidi ya KMC, kisha ikafunga moja kwenye sare ya mabao 2-2 dhidi ya JKT Tanzania huku mabao ya kipindi cha pili ikiyafunga dhidi ya Fountain Gate iliposhinda 0-1 ugenini na bao la kufutia machozi ililolipata ikipoteza 2-1 dhidi ya watani wake Tanzania Prisons.
DODOMA JIJI CHA PILI
Dodoma Jiji nao ni wale wa kipindi cha pili ambapo kwenye mabao matano iliyofunga, matatu yametengenezwa kipindi cha pili huku mawili yakipatkana kile cha kwanza.
Mabao ya kipindi cha pili yalifungwa ilipotoka sare ya 2-2 dhidi ya Tabora United ambayo sasa ni TRA United, ikafunga pia bao moja kila kipindi iliposhinda 2-0 dhidi ya Coastal Union huku mabao ya kipindi cha kwanza ikiyafunga kwa Pamba iliposhinda 1-0 na lile dhidi ya Coastal Union.
MASHUJAA CHA KWANZA
Mashujaa ni wazee wa kipindi cha kwanza ndicho ambacho kimetengeneza mabao mengi wakifunga matatu huku kile cha kwanza wakipata bao moja pekee.
Iko hivi, mabao yake ya kipindi cha kwanza imeyafunga iliposhinda 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar na dhidi ya Namungo kisha lile la kufutia machozi ilipolala mbele ya Pamba Jiji huku bao lake la kipindi cha pili ikilifunga kwenye sare dhidi ya JKT Tanzania ya bao 1-1.
SINGIDA BS CHA KWANZA
Ukikutana na Singida Black Stars, basi chunga sana kipindui cha kwanza kwani msimu huu mabao yake matatu yote kwenye mechi zake tatu yamefungwa kipindi cha kwanza ikiwa haina bao kipindi cha pili.
Singida ilifunga mabao hayo kwenye mechi mbili za ushindi dhidi ya KMC na Mashujaa FC huku bao lingine ikilifunga kwenye sare ya bao 1-1 dhidi ya Pamba Jiji.
JKT TANZANIA JISHIKE CHA PILI
Wanajeshi wa JKT Tanzania ni hatari zaidi kipindi cha pili ambapo imefunga mabao yake saba kipindi hicho ikiwaimefunga bao moja pekee kipindi cha kwanza.
JKT ambayo imeshinda mchezo mmoja pekee dhidi ya Coastal Union hapo ndipo ilifunga bao kila kipindi ikipata ikishinda 2-1 ambapo ikafunga mabao mengine kwenye mechi za sare dhidi ya Mashujaa,Azam na Namungo zilizomalizika kwa sare ya (1-1),huku ile ya Mbeya City ikiisha kwa mabao 2-2.
FOUNTAIN GATE KIPINDI CHA PILI
Fountain Gate ambao baada ya kuanza mechi tatu za kwanza bila ushindi wala kufunga bao lolote nao wameangukia kwenye kundi ambalo linafunga mabao yake kipindi cha pili ikifunga mawili kati ya mabao yake matatu.
Fountain ambayo ilianza kupata bao kkwenye mchezo wake wa nne ilifunga bao lake kwanza kipindi cha ikishinda 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji na ule dhidi KMC uliomalizika kwa matokeo kama hayo kisha bao lao pekee la kipindi cha kwanza ni lile ililolifunga ikipata sare ya bao 1-1 dhidi ya Coastal Union.
TANZANIA PRISONS KIPINDI CHA PILI
Tanzania Prisons nao ni wazee wa dakika 45 za pili ambapo kwenye mabao yake matatu iliyoyafunga ndani ya mechi nne, mawili yamefungwa kipindi cha pili huku moja likifungwa kipindi cha kwanza.
Prisons ambayo ilianza ligi kwa kupoteza mechi zake mbili za kwanza pia ikimaliza mechi hizo bila kufunga bao, ilifunga mabao yake mawili kwenye dabi dhidi ya Mbeya City iliposhinda 2-1 huku bao pekee la kipindi cha kwanza ni lile walipoichapa KMC kwa bao 1-0.
PAMBA JIJI WAZEE KOTEKOTE
Pamba Jiji hawatabirikim kwanza kwenye mechi zake sita ilizocheza imefanikiwa kufunga mabao kwenye mechi tatu pekee ambapo imefungas jumla ya mabao manne, kila kipindi ikifunga mabao mawili.
Pamba ilifunga bao lake la kwanza msimu huu kwenye sare ya bao kila kipindi ikitengeneza ushindi wao pekee wa mabao 2-1 dhidi ya Mashujaa kisha sare dhidi ya Namungo ikipata bao lake kipindi cha kwanza lakini ile ya dhidi ya Singida ikifunga bao lake kipindi cha pili.
NAMUNGO CHA PILI
Namungo ukikutana nao kuwa makini kipindi cha pili ambacho mpaka sasa kimewatengenezea mabao manne huku kile cha kwanza wakipata moja pekee.
Mabao ya kipindi cha pili iliyapata ilipokutana na Pamba Jiji, lingine ikifunga kwenye sare kama hiyo dhidi ya Azam huku moja ikilipata iliposhinda kwa bao 1-0 mbele ya Tanzania Prisons ilhali bao pekee la kipindi cha kwanza ikilifunga kwenye sare dhidi ya JKT Tanzania.
AZAM CHA KWANZA
Matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC ni hatari kipindi cha kwanza ambapo kwenye mechi tatu wamefunga mabao matatu ndani ya kipindi hicho, huku moja pekee wakilifunga kipindi cha pili.
Azam ilipata sare mbili dhidi ya JKT Tanzania na Namungo mabao yake yote yalifungwa kipindi cha kwanza kisha wenyeji wake kurudisha huku ushindi pekee mpaka sasa iliposhinda 2-0 dhidi ya Mbeya City, ikifunga bao moja kila kipindi.
MTIBWA SUGAR KOTE
Mtibwa Sugar ambayo imerejea Ligi Kuu Bara msimu huu kwenye mechi tano ilizocheza imefanikiwa kufunga mabao mawili ilipopata ushindi pekee mpaka sasa wa mabao 2-0 dhidi ya Fountain Gate huku kila kipindi ikitengeneza bao moja.
COASTAL UNION KIPINDI CHA KWANZA
Ikiwa imeshinda mchezo mmoja mpaka sasa licha ya kucheza mechi tano, Coastal Union kikosi chake kimetengeneza mabao matatu pekee huku mawili kikiyafuga kipindi cha kwanza na moja kile cha pili.
Coastal ilifunga bao la kwanza ikipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons kisha ikapata sare mbili za bao 1-1 dhidi ya JKT ikifunga bao kipindi cha kwanza na ile na Fountain Gate bao lake likifungwa kipindi cha pili.
TRA UNITED CHA PILI
TRA United bado haijajipata ushindi wowote msimu huu ikitoka sare mechi tatu ilizocheza, lakini sare pekee iliyoipa mabao ni ile ya 2-2 dhidi ya Dodoma Jiji huku mabao hayo yakipatikana kipindi cha pili.
KMC HAISOMEKI
KMC iko chini mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kucheza mechi sita za kwanza ikishinda moja pekee na kupoteza tano, lakini imefunga mabao mawili tu msimu huu tangu ulipoanza Septemba 17, mwaka huu.
Mabao hayo mawili yana sura mbili ambapo bao la kwanza ni lile lililoipa ushindi dhidi ya Dodoma Jiji likipatikana kipindi cha pili na lingine ni lile ililopata ikipigwa mabao 4-1 na Yanga likifungwa kipindi cha kwanza.