Chelsea watashinda Ligi Kuu England
Muktasari:
Kama kawaida, ligi hiyo ni ngumu kutabirika. Pia, ikumbukwe kwamba dirisha la uhamisho bado halijafungwa.
MSOMAJI, Ligi Kuu England inaanza wiki hii. Wakati kama huu mwaka mmoja uliopita, niliandika makala katika gazeti hili nilipotabiri kwamba Man City itakuwa mabingwa katika ligi hiyo.
Kama kawaida, ligi hiyo ni ngumu kutabirika. Pia, ikumbukwe kwamba dirisha la uhamisho bado halijafungwa.
Lakini, kutokana na vikosi vya timu za ligi huyo vilivyo sasa, nimejaribu kutabiri tena mshindi wa msimu huu.
Natabiri kwamba Chelsea watatwaa ubingwa. Ni kwa kuwa timu hiyo imefanya usajili bora kulinganisha na timu nyingine zote.
Msimu uliopita Mourinho alidai kutoka mwanzo wa ligi kwamba Chelsea hawawezi kushinda ligi bila mshambuliaji wa maana.
Katika dirisha hili la uhamisho, Chelsea wamemsajili nyota na mshambuliaji wa Atletico Madrid, Diego Costa. Pia, Chelsea hawakuweza kufunga magoli mengi msimu uliopita wakati Oscar alikuwa katika hali mbaya kimpira.
Hata hivyo, sasa Chelsea pia wamemsajili Cesc Fabregas kutoka Barcelona. Washabiki wa Arsenal na Barcelona wanajua kwamba mchezaji huyu ni fundi wa mpira na bila shaka Fabregas atatengeneza nafasi nyingi za kufunga magoli. Kama haitoshi, Chelsea wamemsajili Felipe Luiz kutoka Atletico Madrid, na kwa hiyo wameboresha nafasi ya beki wa kushoto.
Timu nyingine ambayo imesajili vizuri ni Arsenal. Lakini, naamini Arsenal hawatakuwa na nafasi ya kushinda ligi kama hawatasajili kiungo wa kati. Msimu uliopita Arteta alikuwa chaguo la kwanza kwa Arsene Wenger katika nafasi hii. Lakini, mchezaji huyu alikuwa kiungo wa mbele alipochezea Everton na hana uwezo mkubwa wa kukaba.
Pia Arsenal wamemuuza Vermaelen kwenda Barcelona. Ingawa beki huyu alikuwa chaguo la tatu kwa Wenger, Arsenal wanahitaji kikosi kikubwa chenye wachezaji wazuri katika benchi la ufundi pia.
Nafikiri Man City ni timu ambayo itawapa Chelsea upinzani mkubwa. Ni kweli kwamba timu hiyo ilifungwa Jumapili na Arsenal, lakini, bado wana kikosi kizuri sana.
Man City ni mabingwa na msimu uliopita walikuwa na kikosi bora na ndio maana hawajasajili wachezaji wengi katika dirisha hili la uhamisho. Lakini, Man City kama Barcelona, wanahitaji kusajili beki mpya.
Msimu uliopita Kompany na Nastacis wote walikuwa katika hali mbaya kimpira. Demichellis ambaye ni beki mwenye umri wa miaka 33 alikuwa chaguo la kwanza kwa kocha wa Man City, Manuel Pellegrini.
Kuna pengo katika nafasi ya ukabaji katika Man City. Pellegrini atahitaji kuziba pengo hili kama timu yake itahitaji kuwa na uwezo wa kushinda ligi.
Kama haya yasipofanyika katika kikosi hicho, nina uhakika kabisa timu hiyo itakuwa imeamua kutoa mwanya kwa Chelsea kufanya kile ambacho ni wazi kocha Jose Mourinho atakuwa anataka kukifanya.
Haya, Arsenal imeshachukua Ngao ya Jamii, sasa tusubiria kuanza kuona vumbi kamili la ligi kuanzia wikiendi hii.