Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Injinia Hersi Saidi na Yanga ya juzi, jana na leo

Muktasari:

  • Mwaka 1974, baba yake Haji Manara, Sunday Manara akiwa katika ubora wake aliwaongoza Yanga kuwachapa Simba mabao 2-1 katika Uwanja wa Nyamagana. Bonge la mechi. Manara alikuwa katika ubora wake hasa.

AZAM waliziona nyavu za Digui Diarra mara tatu na kupata ushindi wao mtamu wakati wakiwa pungufu. Ilikuwa ni hadithi ya kusisimua juzi katika Uwanja wa CCM Kirumba ambao Yanga wamekuwa wakipata matokeo mazuri katika mechi kubwa.

Mwaka 1974, baba yake Haji Manara, Sunday Manara akiwa katika ubora wake aliwaongoza Yanga kuwachapa Simba mabao 2-1 katika Uwanja wa Nyamagana. Bonge la mechi. Manara alikuwa katika ubora wake hasa.

Baada ya hapo kuna mechi ngumu za Yanga zilichezwa CCM Kirumba hapo hapo Mwanza. Kuna ile mechi ambayo Yanga waliondoka uwanjani na ushindi wa bao 1-0. Jerry Tegete alimfunga Juma Kaseja kama ambavyo Lionel Messi amekuwa akiwafunga makipa wengi bora duniani.

Aliubetua mpira kwa umaridadi mkubwa wakati akitazamana na Kaseja. Ni kama vile ambavyo Messi na wachezaji wengine wanafanya. Yanga wakaondoka Kirumba wakiwa wanashingilia.

Baada ya miaka kadhaa Yanga walirudi tena Kirumba kucheza na Simba katika mechi muhimu na Fei Toto alipiga shuti la mbali la kushtukiza lililomshinda Aishi Manula. Yanga waliondoka wakifurahi. Mwanza ni kama nyumbani kwa Yanga kasoro juzi.

Juzi wameondoka vichwa chini. Moja kati ya mechi muhimu ambayo itakumbukwa. Hawakucheza na Simba. Walicheza na Azam katika mechi ambayo walipaswa kushinda na kwenda kucheza na Simba katika fainali.

Wasisahau Azam ni timu kubwa siku hizi, kwa hiyo mechi ya juzi ni miongoni mwa mechi ambazo Yanga wamecheza Kirumba na wamepoteza, tena kwa aibu. Tunaiweka katika kumbukumbu zetu. Sawa, Azam sio Simba lakini mechi hii nayo tunaiweka kibindoni kama mechi muhimu ambayo Yanga ilipoteza Kirumba.

Yoro Diaby alipewa kadi nyekundu halali kabisa wakati alipomzuia Prince Dube kwenda kufunga bao.

Kwa sisi ambao tunabakia na risiti tunampongeza mwamuzi kwa kuchukua maamuzi sahihi. Sio tu alikuwa amependelea kitu kwa sababu Yanga ni timu kubwa. Hapana. Ahmed Arajiga aliwahi kuchukua maamuzi kama haya dhidi ya Yanga.

Iliwahi kutokea Ibrahim Bacca alimfanyia faulo Nassor Saadun pale Chamazi katika pambano la ligi kuu na kwa kuwa alikuwa mwisho basi Arajiga alitoa kadi nyekundu kwa Bacca. Ni hadithi ya muosha huoshwa.

Baada ya hapo mechi iliendelea na Azam ilifunga mabao mawili dhidi ya Diarra. Na sasa Azam watakutana na Simba katika pambano la fainali la michuano hii ya FA.

Kwanza kabisa ukweli ni kuwa mambo hufika mwisho. Yanga wametawala sana katika michuano hii pamoja na kombe la ligi. Wamefika mwisho.

Hata hivyo, mwisho wao unaacha maswali pia kwa mtu anayeitwa Injinia Hersi Said na genge lake ambalo limekuwa likiipa Yanga furaha katika miaka ya karibuni. Hersi aliichukua timu kutoka kwa Mshindo Msolwa na akaigeuza tishio.

Mpira hauna kificho. Ni Hersi na wenzake kupitia pesa za Ghalib Said Mohamed ndizo ambazo ziliipeleka Yanga juu. Kuanzia kuachana na kina Yikpe Gnamien hadi kuwapata watu kama kina Fiston Mayele, Hersi na wenzake waliitoa timu mbali.

Timu ambayo iliwachapa watani wao mara tano mfululizo. Timu ambayo imetwaa mataji manne ya ligi kuu yetu wandewa mara nne mfululizo. Timu ambayo ilifika fainali za Kombe la Shirikisho na kupoteza kwa mbinde dhidi ya USM Alger.

Ni timu ambayo ilikuwa inashinda mabao mengi kwa kadri inavyojisikia wakati ule ikiwa Chamazi. Kocha alikuwa Manuel Gamondi. Yanga walifanya mambo mengi kadri walivyojisikia. Hatukujua lini ungeweza kuwa mwisho wa utawala wa Yanga.

Lakini baada ya hapo wakaanza kushuka taratibu. Hatukuona tena Hersi na genge lake wakisajili wachezaji wa maana ambao wangekuwa katika viwango vya kina Fiston Mayelle, Aziz Ki, Pacome Zouzoua, Djigui Diarra na wengine.

Kila tulipopiga kelele Yanga walikuwa wanashuka chini tulikuwa tunajibiwa tuna chuki na timu. Ni kelele kama hizi tuliwahi kuzipiga wakati Simba wanashuka chini baada ya utawala ule wa Clatous Chota Chama, Luis Miquisonne, Meddie Kagere na wengineo lakini tukaambiwa GSM anagawa bahasha kwa waandishi ili waisifie Yanga na kuiponda Simba.

Na sasa muda umeongea. Yanga nao wameshuka chini. Ukiweza kuongea utaambiwa bado wanaongoza ligi lakini katika mpira wetu huu ni rahisi kwa timu dhaifu kuongoza ligi. Kama kuna wadhaifu wengine wanashindwa kumtoa kileleni unaweza kudhani anayeongoza ligi ni timu imara kumbe siyo.

Yanga walianza kushuka taratibu. Kuanzia ule ukali wa kutembeza tano tano nyingi pale Chamazi hadi leo kushindwa kuifunga Azam iliyopungua kwa dakika nyingi sio kitu cha kawaida sana. Subiri, sio kwamba ilishindwa kuifunga lakini Azam ilipata mabao mawili ikiwa pungufu.

Miaka miwili nyuma Azam wangekiona chamoto kwa kupungua uwanjani kwa muda mrefu lakini juzi walikuwa wanafurahia soka tu.

Usingeweza kufikiria kilichotokea kama kingetokea miaka miwili nyuma lakini ni kweli kimetokea na tunaoijua Yanga hatushangazwi sana.

Na huu ni muda wa Injinia Hersi na genge lake kurudi katika ramani.

Ni rahisi kuwa namba moja lakini kitu kigumu ni kuendelea kuwa namba moja. Hersi ana mtihani huu. Aliichukua timu ikiwa chini, akaipeleka juu, na sasa anaishuhudia timu ikishuka. Ni kitu kipya kwake ambacho anapaswa kujifunza.

Hawa viongozi ni kama makocha, ni kama wachezaji, ni kama wanadamu wengine maishani. Tunafundishwa kuwa na mwendelezo wa ubora (consistency) katika kazi zetu na maisha yetu kwa jumla.

Nataka kuona Hersi na wenzake wanaichukuliaje changamoto hii kama somo.

Kule kwa watani zao kuna wakongwe wengi ambao licha ya mapungufu yao lakini wamejifunza kuhimili milima na mabonde. Nataka kujua kama akina Hersi wapo tayari kwa hili.

Changamoto nyingine ambayo watakutana nayo katika mtihani huu ni namna ambavyo mashabiki wengine na wanachama wataanza kuwa wapinzani ndani ya timu yao. Kifupi fungate linaweza kufika mwisho na ghafla sura za wanachama zikabadilika.

Wanachama wetu wanapenda maisha mazuri tu. Wanapenda kutawala kila kitu, kila siku. Mambo yakianza Kwenda kombo unaweza kukuta wanakuwa wanakuwa wapinzani wakubwa wa timu yao.