Championship kumenoga, kuna vita nzito

Muktasari:
- Wakati raundi hizo zikibakia, Mwanaspoti linakuletea tathimini ya kinachoendelea na kile kinachotarajiwa kutokea mwisho wa msimu huu, kutokana na ushindani unaoendelea kuonyeshwa na kila timu inayopambana ili kujitengenezea heshima yake.
VITA ni nzito! Ndivyo unavyoweza kusema kuhusu Ligi ya Championship baada ya kubakisha michezo mitano tu kwa kila timu kuhitimisha msimu huu, huku vita kubwa ikitanda maeneo yote, hususani ile ya kupanda Ligi Kuu msimu ujao wa 2025-2026.
Wakati raundi hizo zikibakia, Mwanaspoti linakuletea tathimini ya kinachoendelea na kile kinachotarajiwa kutokea mwisho wa msimu huu, kutokana na ushindani unaoendelea kuonyeshwa na kila timu inayopambana ili kujitengenezea heshima yake.
‘TOP FOUR’ HAIKAMATIKI
Utamu upo eneo hili ambapo timu mbili zitakazomaliza nafasi ya kwanza na ya pili zitapanda Ligi Kuu Bara msimu ujao moja kwa moja, huku zitakazomaliza ya tatu na nne zikipambana kucheza ‘Play-Off’, na hadi sasa ushindani umekuwa ni mkubwa.
Mtibwa Sugar iliyoshuka daraja msimu uliopita, ndio timu yenye nafasi zaidi ya kupanda moja kwa moja kutokana na pointi zake 60, ilizonazo na mwenendo wake hadi sasa, huku vita ikibakia pia kwa Mbeya City, Stand United na Geita Gold.

Mbeya City kabla ya mchezo wake wa juzi dhidi ya Stand United, timu hizo zilikuwa nafasi ya pili na ya tatu zikiwa na pointi 52, zikitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa, huku Geita Gold ikiwa ya nne baada ya kukusanya pointi 51.
Baada ya kushuka msimu wa 2022-2023, Mbeya City inapambana kwa ajili ya kurejea tena Ligi Kuu msimu ujao kama ilivyo pia kwa ‘Chama la Wana’, Stand United ya Shinyanga inayosota kusaka tiketi hiyo, tangu iliposhuka daraja msimu wa 2018-2019.
Geita Gold iliyoshuka msimu uliopita sawa na Mtibwa Sugar, inapambana pia kurejea tena msimu ujao Ligi Kuu Bara jambo linaloongeza mvuto wa kiushindani kwa miamba hiyo, hivyo kuifanya michezo mitano iliyobakia kuvuta taswira ya kipekee.
Mbali na miamba hiyo inayopambania nafasi nne za juu, TMA FC ya jijini Arusha inafuatia ikiwa nafasi ya tano na pointi zake 47, ikifuatiwa na Mbeya Kwanza inayopambana kurejea tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka daraja msimu wa 2021-2022.
VITA YA KUSHUKA DARAJA
Ukiachana na vita ya kusaka nafasi ya kupanda Ligi Kuu Bara msimu ujao, shughuli nyingine ni ya kupata timu mbili ambazo zitashuka daraja moja kwa moja, ambapo hadi sasa upepo sio mzuri kwa ‘Wanajeshi wa Mpakani’, Biashara United ya Musoma.
Hali ya timu hiyo ilianza kuonekana tangu mwanzoni baada ya kuandamwa na ukata ulioifanya kushindwa kufika katika mchezo wa ugenini dhidi ya Mbeya City uliotakiwa kuchezwa Desemba 3, 2024, hivyo kukatwa pointi 15 na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB).

Ili ijinasue na janga la kushuka daraja, Biashara inabidi ishinde michezo yote sita iliyobakia ili kufikisha pointi 25, ingawa itategemea pia na matokeo ya wapinzani wake, hali inayoonyesha wazi kikosi hicho kiko kwenye hatari ya kushuka daraja.
Biashara United iliyoshuka daraja msimu wa 2021-2022, ina pointi saba tu katika michezo 24, iliyocheza ikiburuza mkiani, huku mbali na timu hiyo nyingine zilizokuwa katika hatari ni maafande wa Transit Camp iliyopo nafasi ya 15 na pointi 11.
African Sport haipo pia sehemu nzuri kwani pointi zake 14 zinaweza kufikiwa na timu nyingine, sambamba na Cosmopolitan iliyopo nafasi ya 13 na pointi 16, jambo linalozidi kuongeza ushindani kwa miamba hiyo na kusubiria kile kitakachojiri.
HAUSUNG, GUNNERS WAGENI WAPYA
Wakati zikisubiriwa timu mbili zitakazoshuka moja kwa moja kwenda kucheza First League msimu ujao, tayari wageni wapya watakaochukua nafasi hizo wameshapatikana ambao ni Hausung ya Njombe na Gunners ya mkoani Dodoma zilizokata tiketi hiyo.

Hausung imekuwa timu ya kwanza kupanda kutoka kundi A, ikikusanya pointi 25, baada ya kushinda michezo saba, sare minne na kupoteza mitatu, huku Gunners kutoka kundi B, ikiwa na pointi zake 35, kufuatia kushinda 11, sare miwili na kupoteza mmoja.
Kilichobaki kwa timu hizo zitacheza mchezo wa kutafuta Bingwa wa First League kwa msimu wa 2024-2025 ambapo kinara kundi A Hausung ya Njombe, itakutana na Gunners ya Dodoma kutoka kundi B, sambamba na michezo mingine ya mtoano (‘Play-Off’).
HAT-TRICK NNE
Msimu huu umekuwa mgumu ingawa hadi sasa zimefungwa ‘hat-trick’ nne, akianza mshambuliaji wa Mbeya City, Faraji Kilaza Mazoea, katika mchezo kati ya timu hiyo dhidi ya Maafande wa Polisi Tanzania, walioshinda mabao 4-0, Desemba 13, 2024.
Andrew Simchimba wa Geita Gold akafunga pia wakati timu hiyo iliposhinda mabao 4-0, dhidi ya Transit Camp, Februari 10, 2025, huku Oscar Tarimo wa Mbeya Kwanza akifunga pia katika ushindi wa 5-0, mbele ya Biashara United, Februari 23, 2025.

Nyota mwingine ni William Thobias wa Mbeya City aliyefunga pia wakati kikosi hicho kinachopambana kurejea tena Ligi Kuu Bara msimu ujao, kilipoichapa Kiluvya United mabao 4-0, mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya, Machi 17, 2025.
Kwa msimu uliopita, zilifungwa ‘hat-trick’ tano huku nyota wa zamani wa Biashara United, Mganda Boban Zirintusa akifunga mbili, wakati Kika Salum (Pan Africans), Abdulaziz Shahame (TMA FC) na Oscar Mwajanga aliyekuwa Mbeya Kwanza wakifunga moja.
VITA YA UFUNGAJI
Sehemu nyingine yenye mvuto ni katika vita ya ufungaji bora ambapo anayeongoza hadi sasa ni nyota wa Geita Gold, Andrew Simchimba mwenye mabao 17, akimpindua nyota wa Mtibwa Sugar, Raizin Hafidh aliyekuwa anaoongoza muda mrefu akiwa na 16.

Wanaofuatia ni Abdulaziz Shahame wa TMA FC ya jijini Arusha mwenye mabao 15, Naku James (Mbuni) akifunga 11, huku Yusuph Mhilu (Geita Gold), Boniphace Maganga (Mbeya Kwanza) na William Thobias wa Mbeya City wakifunga manane kila mmoja wao.
MAKOCHA WAWILI TU
Ni timu mbili tu ambazo hazijabadilisha benchi la ufundi, ikiwa haina tofauti kubwa sana na Ligi Kuu waliobakia watatu ambapo kwa Championship, makocha waliokuwepo tangu mwanzoni ni Leonard Budeba (Mbuni FC) na Kessy Abdallah wa African Sports.
Kiluvya United iliyopanda Ligi ya msimu huu, inaongoza kwa kufundishwa na makocha wengi hadi sasa ambao wanafika watatu, sawa na Cosmopolitan na Transit Camp, huku nyingine zote zilizosalia tofauti na hizo mbili zikifundishwa na wawili pekee.
MTIBWA NA REKODI YA KIBABE
Ushindi wa mabao 3-1, ilioupata Mtibwa Sugar dhidi ya TMA FC Machi 28, 2025, umeifanya timu hiyo kuweka rekodi ya kibabe kwani tangu msimu umeanza, haijawahi kupoteza au kutoka sare mchezo wowote iliocheza kwenye uwanja wake wa nyumbani.

Mtibwa iliyoshuka daraja msimu uliopita, imecheza michezo 13, kwenye Uwanja wa Manungu Complex kati ya 25 na kati ya hiyo, imeshinda yote, huku safu ya ushambuliaji ikifunga jumla ya mabao 34 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tano.