Championship inarudi na utamu wake

LIGI ya Championship msimu wa 2022/2023, inaanza rasmi Septemba 17 mwaka huu huku ikitabiriwa kuongezeka kwa ushindani mkubwa kama ilivyokuwa msimu uliopita.

Mwanaspoti linakuletea uchambuzi wa kina juu ya ligi hiyo iliyoteka hisia za mashabiki wengi wa soka nchini kutokana na msisimko uliopo.


VITA YA UFUNGAJI

Hii ni sehemu ambayo italeta mvuto mkubwa kwa sababu ya ubora wa nyota wengi wanaopatikana huku baada ya msimu uliopita mshambuliaji wa JKT Tanzania, Edward Songo kuibuka kinara wa mabao 16 sambamba na kushinda tuzo ya mchezaji bora wa ligi hiyo.

Songo anayetazamiwa kuendeleza moto wake ila atapata ushindani kutoka kwa Danny Mrwanda aliyejiunga na Fountain Gate msimu huu akitokea Ken Gold na wakati akikitumikia kikosi hicho alimaliza wa tatu kwenye ufungaji akifunga mabao 13.

Mastaa wengine watakaoangaliwa ni, Abdiud Mtambuku, Mohamed Haji wanaochezea (Mashujaa) na Peter Mapunda aliyejiunga na Pamba akitokea Mbeya City.


BIASHARA UNITED, MBEYA KWANZA MTEGONI

Timu za Biashara United (Mara) na Mbeya Kwanza (Mbeya) zina shughuli pevu ya kuhakikisha zinapambana ili zirejee tena kwenye Ligi Kuu Bara baada ya msimu uliopita kushuka kutokana na kutokuwa na matokeo mazuri yaliyoshindwa kuwanasua.

Biashara ambayo ilivunja benchi la ufundi, viongozi huku wachezaji wao wakitimkia timu mbalimbali za ligi kuu ilimaliza ya 15 na pointi 28 wakati Mbeya Kwanza ilimaliza ya 16, pointi 25 pia ikikabiliwa na changamoto ya kuondokewa na mastaa wake.


UDHAMINI CHANGAMOTO

Licha ya ubora wa ligi hii ila changamoto kubwa imekuwa kwenye upatikanaji wa mdhamini kama ilivyokuwa kwa timu za Ligi Kuu Bara.

Msimu uliopita klabu mbalimbali zilionekana kuandamwa na kadhia hiyo japo Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo aliweka wazi wapo kwenye mazungumzo na baadhi ya wadhamini kwa ajili ya kuwekeza na kama jambo hilo litafanikiwa litaongeza ushindani.


MECHI ZA KUZITAZAMA

Katika ligi ya msimu huu zipo mechi ambazo hupaswi kuzikosa kutokana na ubora wa timu na vikosi vyote pia uhasama baina yao kulingana na maeneo wanayotoka.

Miongoni mwa mechi hizo ni, Fountain Gate v Biashara United (Septemba 17, 2022), JKT Tanzania v Biashara United (Septemba 24, 2022), Copco v Gwambina, Mbeya Kwanza v JKT Tanzania (Oktoba 8, 2022), Gwambina v Pamba, Mbeya Kwanza v Ken Gold (Oktoba 15, 2022), JKT Tanzania v Fountain Gate (Oktoba 16, 2022), Kitayosce v Mbeya Kwanza (Oktoba 29, 2022).

JKT Tanzania v Green Warriors (Oktoba 30, 2022), Ken Gold v Mbuni (Novemba 5, 2020), Transit Camp v JKT Tanzania (Novemba 11, 2022), Mbeya Kwanza v Mbuni (Novemba 12, 2022), JKT Tanzania v Kitayosce (Disemba 3, 2022), Kitayosce v Fountain Gate (Disemba 17, 2022), JKT Tanzania v Pamba, Transit Camp v Green Warriors na Biashara United v Mbeya Kwanza (Disemba 24, 2022).

Biashara United v Fountain Gate (Januari 21, 2023), Biashara United v JKT Tanzania (Februari 4, 2023), Pamba v Copco (Februari 12, 2023), JKT Tanzania v Mbeya Kwanza (Februari 18, 2023), Gwambina v Copco (Februari 19, 2023), Fountain Gate v JKT Tanzania, Ken Gold v Mbeya Kwanza (Februari 25, 2023), Pamba v Gwambina (Februari 26, 2023) na Green Warriors v JKT Tanzania (Machi 11, 2023).

Kitayosce v Biashara United, JKT Tanzania v Transit Camp (Machi 25, 2023), Kitayosce v JKT Tanzania (Aprili 22, 2023), Pamba v JKT Tanzania, Mbeya Kwanza v Biashara United (Mei 6, 2023) na mchezo wa Pamba v Fountain Gate (Mei 13, 2023).


MACHINJIONI NI HAPA

Mara nyingi katika ligi hii timu zimekuwa zikitumia uwanja wa nyumbani kama ‘Machinjioni’ kwa ajili ya kujipatia pointi tatu muhimu. Zifuatazo ni jumla ya timu zote 16 zinazoshiriki kwenye ligi hii na viwanja vitakavyotumika kwa msimu huu.

Mashujaa (Lake Tanganyika, Kigoma), Kitayosce (Ali Hassan Mwinyi, Tabora), African Sports (Mkwakwani, Tanga), Mbuni FC (Sheikh Amri Abeid, Arusha), Fountain Gate (CCM Gairo, Morogoro), JKT Tanzania (Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam) na Gwambina (Gwambina Complex, Mwanza).

Pamba na Copco (Nyamagana, Mwanza), Transit Camp na Pan Africans (Uhuru, Dar es Salaam), Green Warriors (Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam), Ndanda (Nangwanda Sijaona, Mtwara), Biashara United (Karume, Mara), Mbeya Kwanza (Mabatini, Pwani) na KenGold (Sokoine, Mbeya).