Banda: Simba SC wananitaka

Sunday June 20 2021
banda pic
By Eliya Solomon
By Olipa Assa

MWANASPOTI limefanya exclusive na beki huru Abdi Banda kujua ukimya wake unatawaliwa na nini baada ya kuachana na Baroka ya Afrika Kusini aliyoichezea tangu mwaka 2017-19.

Banda anafunguka mambo mengi, ikiwemo tetesi zilizokuwa zimeenea za kugombana na aliyekuwa kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike pia namna alivyoweza kuyafikia malengo yake ambayo alijipangia akiwa mtoto.

Banda alikwenda kucheza Afrika Kusini akitokea Simba aliyojiunga nayo msimu wa 2014-17, iliyomsajili kutoka Coastal Union ya Tanga, anasimulia mambo mbalimbali kama ifuatavyo.


ISHU YAKE YA USAJILI SIMBA

Banda anasema waajiri wake wa zamani ni miongoni mwa klabu ambazo zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili kwa kuongea na wakala wake ambaye ni raia wa Uingereza anaishi huko Bondeni, Afrika Kusini, “Amenigusia kwamba walimpigia simu.

Advertisement

“Baada ya kunieleza kila kitu kilivyokuwa kwenye mazungumzo, aliniuliza unasemaje kwenye hilo? nilimwambia tuendelee kuwasikilia maana haikuwa klabu pekee ambayo imeonyesha nia ya kutaka kunisajili,” anasema beki huyo.

Vipi kama watafika dau? Banda anasema maisha ya mpira yana mwisho hivyo hatakuwa na chaguo jingine zaidi ya kuchangamkia ofa yao, “Tunacheza mpira ikiwa ni sehemu ya utafutaji, ndio maana ikitokea ofa huwa zinawekwa mezani halafu unafanyika mchanganuo ndio uamuzi wa mwisho unafanyika,”

“Naweza kurudi nyumbani na kucheza soka ikiwa kutakuwa na maslahi makubwa zaidi ya huko nje ambako ndio shabaha yangu kubwa,” anasema.


HAIKUWA RAHISI KUONDOKA SIMBA

Wakati wa mashindano ya COSAFA, 2017 nchini Afrika Kusini ndio kipindi ambacho Banda alifanya uamuzi wa kujiunga na Baroka FC, ilikuwaje? Banda anasema iliwezekana kukamilika kwa uhamisho wake huo kutokana na malengo aliyojiwekea.

“Nakumbuka Mo alitaka niongeze mkataba lakini ilibidi nimzungushe kwa sababu nilikuwa na mipango yangu mingine, msimu huo ulikuwa mzuri kwangu licha ya kwanza maisha yangu ndani ya Simba mwanzoni yalikuwa na changamoto nyingi.

“Kipindi ambacho Mo alitaka niongeze mkataba ilikuwa kabla ya COSAFA, nilikuwa nikimkwepa kwa kumwambia ajenti wangu hayupo hivyo nisingeweza kuongeza mkataba mwenyewe, ni kweli hakuwepo lakini tulikuwa na makubaliano ya kwamba nisiongeze mkataba kwa sababu kulikuwa na dili nyingine kubwa sana Afrika Kusini.

“Sikuondoka kwa ubaya nadhani viongozi wanatambua maisha ya mpira yalivyo nikiwa Afrika Kusini kwenye mashindano ya COSAFA, nilionana na ajenti wangu tukiwa hotelini sehemu ambayo alinielekeza na nikasaini mkataba wangu wa kwanza wa kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, ilikuwa ni furaha kubwa sana kwangu,” anasema.


MAISHA YAKE SAUZI

Mwaka wa kwanza (2017) aliojiunga na Baroka FC haukuwa mrahisi kwake, anaeleza aliutumia kuyazoea mazingira kama hali ya hewa ya baridi kali, vyakula na staili yao ya maisha ya kutokusaidiana tofauti na Tanzania watu wanavyoishi kijamaa.

“Afrika Kusini hawana kusaidiana, kila mtu na maisha yake iwe unaumwa unatakiwa kwenda mwenyewe hospitali bila kutegemea kuna mtu atakuja kukuona kama tulivyozoea hapa kwetu, hivyo mwaka wa kwanza ulikuwa mgumu ila sikukata tamaa;

Anaongeza kuwa, “Kwa kuwa nilikuwa na malengo yangu na nilijua kitu kilichonipeleka Afrika Kusini nilikubaliana na mazingira halisi ya nchi ile, kisha nikaendelea na majukumu yangu ya kufanya kazi,” anasema.


WASAUZI WALIVYO

Banda hashangazwi na maisha anayoishi winga wa Simba, Benard Morrison ambaye alikaa muda mrefu Afrika Kusini kwamba maisha yao hayana kufuatanafuatana, ili mradi tu anaonyesha uwezo wa hali ya juu uwanjani inakuwa imetosha.

Anasema wachezaji wa nchi hiyo, hawapendi maisha ya kambini kwasababu wanaona wanabanwa na kushindwa kupata muda wa kufanya starehe.

“Tanzania wachezaji wanajifichaficha kunywa pombe, Afrika Kusini mchezaji analewa mbele ya makocha na mabosi wake ili mradi tu awe anaonyesha kiwango cha juu uwanjani, ndio maana hawapendelei maisha ya kukaa kambini;”

Anaendelea kusimulia kwamba “Nilipewa kitambaa cha unahodha kwasababu nilikuwa najituma kwa bidii katika mazoezi na waliona sina aina yao ya maisha ya kulewa na kupenda starehe kama wao, hivyo walikuwa wananifurahia kuniona naisaidia sana timu,” anasema.


ISHU YAKE NA AMUNIKE

Wakati akiichezea Baroka FC kabla ya kwenda Highland Park, iliripotiwa kuwepo kwa tofauti baina ya Banda na aliyekuwa kocha wa timu ya taifa la Tanzania ‘Taifa Stars’ na ilikuwa kipindi cha maandalizi ya mchezo wa kuwania nafasi ya kwenda kwenye fainali zilizopita za Afcon Misri dhidi ya Lesotho.

“Watu walizusha tu, kiukweli kabisa sikuwa na tatizo lolote na kocha, kuna watu walizusha maneno, ilikuwa hivi, wakati tukiwa kwenye maandalizi nilishauri tufanye mazoezi muda ambao niliona unafaa kutokana na kufahamu kwangu hali ya hewa ya Afrika Kusini.

“Kitendo hicho kilibebwa na kiongozi mmoja ambaye nadhani hakunielewa nini nililenga na ikaonekana kwamba najiona kuwa mkubwa kitu ambacho hakikuwa sawa, nilijisikia vibaya kwa yaliyokuwa yakiendelea lakini niliweka maslahi ya taifa mbele na nilikuwa mstari wa mbele kuwasapoti wenzangu na mwishowe tulienda Misri,” anasema.


KILICHOMRUDISHA TANZANIA

“Nilirudi Tanzania kuweka sawa mambo yangu huku nikisubiri dirisha la usajili Afrika Kusini lifunguliwe, naweza kurejea Sauzi siku yoyote lakini kilichosababisha nirudi ni kwa sababu timu ambayo nilikuwa nikiichezea Highland Park iliuzwa,” anasema.


MKEWE ACHOMBEZA

Kama mlidhani Banda na mkewe Zabibu Kiba, wametengana, basi habari hii inakuhusu. Wawili hao ndio kwanza penzi lao liko moto, huku wakiendelea kumlea binti yao Naifaty.

Zabibu, ambaye ni dada wa supastaa wa Bongofleva, Ali Kiba, anasimulia jinsi ambavyo anamsaidia mume wake kuwa mchezaji wa kuigwa katika kuonyesha kiwango cha hali ya juu na anatamani aendelee kusaka timu za kucheza nje ya nchi kama atapata fursa.

“Mfano kipindi hiki ambacho alikuwa nyumbani kutokana na kusumbuliwa na majeraha, alikuwa anapata mawazo mengi, nilikuwa najitahidi kumjenga na kwamba atarejea tena kufanya kazi zake, ikumbukwe kwamba soka ndio ajira yake.”

Anaongeza kuwa, “Kuna wakati alikuwa anakosa amani kabisa, nilikuwa nambembeleza kwa maneno mazuri, nilijiepusha kufanya vitu vya kumkera ambavyo vingekuwa vinamuweka kwenye mudi mbaya.”

Anaulizwa je mwanao unapenda afanye kazi gani akikua? Anajibu kwamba anatamani mtoto wao aje asome isipokuwa hawezi kumchagulia kazi na kwamba angekuwa mwanaume angecheza soka kama baba yake.

Advertisement