Balaa zito Azam, sasa ni full sayansi mazoezini

Wednesday August 03 2022
azam pic
By Mwandishi Wetu

WIKI ya pili ya kambi ya Azam FC hapa El Gouna Misri imekuwa tofauti kidogo na ya kwanza. Wiki ya kwanza ilitawaliwa na mazoezi ya kujenga mwili na pumzi ambapo mwanzoni kulikuwa na vipindi vitatu na baadaye kupungua hadi viwili, lakini muda wa mazoezi ukiongezeka kutoka saa moja na nusu hadi saa mbili kila kipindi.

Wiki ya pili nayo ina mambo yake. Ina vipindi vitatu vya mazoezi, lakini viwili vya uwanjani na kimoja cha darasani. Zaidi ya ongezeko la kipindi cha darasani, wiki hii pia imeshuhudia matumizi ya sayansi yakiongezeka zaidi mazoezini.


ASUBUHI

Kuanzia saa mbili hadi saa nne, timu hufanya mazoezi ya uwanjani ambayo yamegawanyika sehemu tatu. Nusu saa ya kwanza ni kujenga pumzi kwa kukimbia na kutumia mpira kucheza rondo (hangaisha bwege) na michezo mingine ya mipira. Nusu saa ya pili huwa ni mazoezi ya mbinu kwenye nusu uwanja au zaidi ya hapo kutokana na nafasi za wachezaji husika.

Saa moja la mwisho ni mechi ya wenyewe kwa wenyewe ili kuzitumia zile mbinu na kuongeza pumzi, lakini pia kutoa mazingira halisi ya mechi.

Advertisement


MCHANA

Huu ni muda wa mazoezi ya kujenga misuli ‘gym’ ambapo kila mchezaji anatakiwa kufikia malengo aliyowekewa na mtaalamu wa sayansi ya michezo, Nyasha Charandula. Kila mmoja hutakiwa kufanya kitu fulani mara zisizopungua 15 kwa kuzingatia uzito wa mtu husika.

Kwa mfano kunyanyua chuma cha mkononi (mara 15), kunyanyua chuma cha mguuni (mara 15) kunyanyua chuma cha begani (mara 15) hivyohivyo kwenye kila zoezi.

Nyasha ambaye ni mtaalamu wa sayansi ya michezo kutoka Zimbabwe akihudumu hadi kwenye timu ya taifa ya nchi hiyo, anasema hadi sasa wachezaji wamevuka kiwango walichopanga hapo awali kufikia muda huu. “Hii ina maana kwamba timu yetu msimu huu itakuwa bora kwenye stamina na utimamu wa mwili,” anasema Nyasha ambaye pia ni mhadhiri wa vyuo vikuu vya Bulawayo Zimbabwe na Gaborone nchini Botswasa wa sayansi ya michezo.


USIKU

Kunakuwa na kipindi cha darasani kinachotumika kufanya uchambuzi wa mazoezi ya asubuhi ya mbinu na ufundi ya uwanjani. Video ambayo hurekodiwa kwa kamera za kisasa za Vevo (kuhusu kamera hizi ambazo Yusuf Bakhresa amezileta kutoka Ujerumani tutajadili katika matoleo yajayo), huchambuliwa kwa kuangalia mwitikio wa mchezaji mmojammoja mazoezini.

Hapa huangaliwa kujituma, kufuata maelekezo, mikimbio na kucheza kwa nafasi. Siku ya kwanza ya darasa hili, Jumamosi ya Julai 30, wachezaji wengi walinaswa wakifanya vitu ambavyo walimu hawavitaki au vilivyo nje ya maelekezo.

Kwa mfano kunogewa na mchezo kiasi cha kusahau kucheza kwa nafasi au kufanya mikimbio mingi lakini isiyofaidisha timu na kadhalika. Zoezi hili huanza saa mbili usiku baada ya chakula cha usiku hadi saa nne usiku.

Baada ya hapo siku inakuwa imeisha watu wanaenda kulala. Hii imesaidia sana kuongeza uelewa wa wachezaji kuhusu mchezo kwani baada ya siku ya kwanza tangu kuanza darasa hili kumekuwa na mabadiliko makubwa ya uchezaji uwanjani.

Kocha Moallin anasema wiki hii yote ya pili kazi itakuwa hiyo na hadi kufikia mwisho kutakuwa na mabadiliko makubwa.


WA STARS, KIMATAIFA KUNOGESHA KAMBI

Wachezaji watatu kutoka timu ya taifa ‘Taifa Stars’ na wawili wa kimataifa ambao walikuwa hajawaungana na timu watajumuika na wenzao kesho, Agosti 3, mwaka huu. Sabuni ya taifa, Abdul Hamis ‘Sopu’, Lusajo Mwaikenda na Pascal Msindo ambao walikuwa kwenye timu ya taifa iliyokuwa katika kibarua cha kuwania kufuzu Chan wataungana na Rodgers Kola na Daniel Amoah waliochelewa kambi kwa sababu za kifamilia.

Awali, kocha mkuu, Abdihamid Moallin hakupanga kuwajumuisha wale wa Stars, lakini sasa amebadili mawazo na kuagiza waje kuungana na wenzao. “Najua kwamba siku zitakuwa chache kwao kuweza kupata kile ambacho wenzao wamekipata huku Misri. Na hiyo ndiyo sababu ya awali kutaka wasije huku ili waungane na wenzao kule kule nyumbani,” anasema kocha.

“Lakini nimeshauriana na wenzangu na kuona kuna faida kubwa kwao kuwa huku. Ukiacha tu mambo ya kiufundi, lakini huku pia wachezaji wanatengeneza umoja, hivyo uwepo wao utawafanya wajuane mapema na wachezaji wapya kuifanya timu yote kuwa familia.”

Rodgers Kola na Daniel Amoah walichelewa kuripoti kwa sababu za kifamilia na sasa wako tayari kuungana na wenzao. Walipotoka nchini kwao walikwenda moja kwa moja Chamazi na ambako wanasubiri hiyo tarehe ifike ili waje hapa.

Advertisement