Azam wanatawanya ubingwa Bara

LIGI Kuu Tanzania Bara inafikia tamati mwanzoni mwa mwezi ujao baada ya kudumu kwa karibia mwaka mzima.

Kulikuwa na vuta nikuvute msimu huu na mwanzoni kabisa baada ya mchezo mmoja Simba waliongoza ligi, lakini baadaye ikawa nadra sana kwao kukaa kileleni mwa msimamo.

Huu ulionekana kuwa msimu wa Yanga, asilimia kubwa walitawala wao huku wakionyesha kuanzia mwanzoni kuwa wanatarajiwa kutwaa ubingwa na ndicho kilichotokea kwani kabla ya michezo miwili walishatwaa ubingwa huo kwa mara ya pili mfululizo.

Yanga wametwaa ubingwa huo wakiwa na pointi 74, huku Simba wakiwa na 67 ikiwa imebaki michezo miwili ni dhahiri kuwa hawawezi kuwafikia tena, lakini kumbuka kuwa baada ya hivyo bado Yanga wana nafasi ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga wana nafasi ya kutwaa ubingwa wa Kombe la ASFC na awali walishatwaa Ngao ya Jamii.

Hii inaonyesha kuwa Yanga wana nafasi ya kuchukua makombe yote makubwa ambayo itayawania, ya hapa nyumbani na moja la nje ya nchi.

Lakini jambo moja la kushtua ni kuona Yanga wanafunga mziki kwenye Uwanja wa Chamazi ambao unatumiwa na Azam FC, DJ wao anasimama na kuwaimbisha mashabiki wao wakati wanamaliza mchezo wao dhidi ya Dodoma Jiji na kupata ushindi wa mabao 4-2 ambao ulionyesha kuwa wameshatwaa ubingwa na hakuna kizuizi tena.

Hii ilikuwa picha mara mbili, moja ya Yanga kuwaonyesha Azam kuwa wanatakiwa kuchukua ubingwa misimu ijayo ili wafurahi namna hiyo, lakini nyingine ikionyesha kuwa Yanga wanatakiwa kuwa na uwanja wao ili washangilie kwa uhuru zaidi.

Stori kubwa ipo kwa upande wa Azam na walistahili kusikiliza midundo ya Dj wa Yanga wakiwa vyumbani kwao na wengine labda wangetuma watu wamweleze apunguze sauti wanataka kulala kwa kuwa silaha zilizowapa Yanga ubingwa waliziuza wenyewe.

Tazama mafanikio ya Yanga nsimu huu, wakati wanakwenda kuchukua ubingwa, nyuma yao yupo Mudathir Yahya, Salum Abubakary Sure Boy na Farid Musa.

Wakati Yanga wakiwa hawana Feisal Salum Fei Toto, walimpata Mudathir akiwa ameshaachana na Azam na yupo kwao Zanzibar akifanya mazoezi na KMKM bila presha yoyote.

Simba ilikuwa timu ya kwanza kumtaka Muda, lakini baadaye Yanga waligeuka na kuchukua fomu na kumsajili kiungo huyo, huyu ndiye aliyefunga bao lililodhihirisha kuwa Yanga ni mabingwa pale kwenye Uwanja wa Chamazi.

Baada ya kufunga bao hilo, Mudathir alikwea jukwaani pale Chamazi kuwaonyesha kuwa amechukulia ubingwa kwenye uwanja ambao awali palikuwa nyumbani kwake, hii ni picha ya pili kwa Azam FC, naamini alitaka pia kuwaonyesha kuwa hapa kulikuwa kwangu mkanikataa, sasa nimerudi hapa na kuwa mfalme.

Lakini ukiutazama pia mchezo huo kwenye Uwanja wa Chamazi, ambao mabosi wa timu ya Azam walikuwa jukwaani, Farid Musa ambaye ni zao lingine la Azam alikimbia pia pembeni kushangilia moja ya mabao mazuri aliyofunga kwenye mchezo huo.

Hii inaonyesha kuwa Azam wamehusika kwenye sehemu kubwa zaidi ya ubingwa wa Yanga msimu huu, ukiachana na hilo rejea miaka minne mfululizo ya mafanikio ya Simba, halafu jaribu kuwakumbuka Azam FC walikuwa wapi.

Wakati Simba wanafanikiwa kutwaa ubingwa miaka minne mfululizo kwenye Ligi Kuu Bara na kufanya mambo makubwa kwenye soka la Afrika, wakubwa waliokuwa wanawapa mafanikio ni wale ambao wanatokea Azam FC.

Kipa bora kwa miaka mitatu kwenye Ligi Kuu Bara, Aishi Manula ambaye alionekana kuwa bora sana akiwa na Azam FC aliondoka bila wengi kutarajia na kutua Simba ambapo hadi sasa ameshatwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne bila kuwa na kizuizi, lakini pia ameshaweka rekodi yake kwenye michuano ya Caf, Kombe la Shirikisho na Kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mbali na Manula rekodi zinaonyesha kuwa mshambuliaji wa Simba John Bocco ndiye alikuwa na mafanikio pia makubwa kwenye chati ya ufungaji bora kwa kipindi chote tangu amejiunga na Simba akitokea Azam FC bila wengi kutarajia.

Bocco ambaye tangu amekuwa na Simba ameshatwaa tuzo ya ufungaji bora, hata msimu huu ambao hajapata nafasi kubwa ya kucheza kuliko wachezaji wengi wa Ligi Kuu Bara anaonekana kuwazidi wachezaji wengi wa Azam kwenye chati akiwa na mabao tisa kwenye ligi hiyo.

Lakini wakati unajiuliza kuhusu jambo hilo, jaribu kumtazama kwa makini beki mahiri wa Simba, Shomary Kapombe, unakumbuka kuwa pia alitoka Azam na kwenda Simba na sasa kwenye miaka zaidi ya mitano anawika na kuingia kwenye chati mbalimbali?

Swali kubwa ambalo unaweza kujiuliza kwa wengi ni kama Azam wanatawanya ubingwa Tanzania Bara.

Wana jicho zuri la kutambua wachezaji wazuri, lakini baada ya kuwaweka kwao wamekuwa wanashindwa kuwatumia kupata ubingwa, jaribu kujiuliza kama Azam wangewatumia wachezaji wao kwa kipindi cha miaka minne kilichopita wangekosa ubingwa leo.

Jiulize uwe na kikosi kina John Bocco, Aishi Manula, Farid Mussa, Mudathir Yahaya, shomary Kapombe, changanya na hawa waliopo Azam kwa sasa wageweza kukosa ubingwa msimu mmoja lakini unaofuata wangetwaa.

Tetesi za usajili kwa sasa zinawataja wachezaji wa Azam kwenda timu mbalimbali, nafikiri umakini unatakiwa wasije wakatawanya ubingwa tena msimu ujao.