Azam hii ilitisha sana

NI miaka nane sasa tangu matajiri wa jiji la Dar es Salam, Azam FC watwae taji la Ligi Kuu Bara msimu wa mwaka 2013/14 na kuweka rekodi ya kucheza mechi 38 bila kupoteza.

Azam chini ya kocha Joseph Omog aliyechukua mikoba ya Stewart Hall katikati ya msimu walitwaa taji hilo na rekodi hiyo ambayo haijavunjwa hadi sasa kwani bado hawajabahatika kutwaa taji jingine la Ligi.

Mwanaspoti linakuletea kikosi kilichoweka rekodi hiyo ambayo haijavunjwa hadi sasa ambayo nyota wake wote wameondoka kikosini. Kuondoka kwa wengi kati yao kulichangiwa na mipango ya klabu ya kupunguza bajeti.


AISHI MANULA

Alikuwa ndiye kipa namba moja wa timu hiyo akiiongoza kuweka rekodi hiyo ambayo haijavunjwa na makocha wengi waliopita ndani ya Azam FC ambayo imetwaa taji moja pekee tangu imepanda daraja msimu wa 2018/19. Yupo Simba kwa msimu wa tano sasa na kuendeleza ubora wake akiwa kipa namba moja Msimbazi.


ERASTO NYONI

Miongoni mwa wachezaji wenye vipaji vya asili, Erasto alikuwa panga pangua kwenye kikosi cha kwanza cha Azam FC. Uwezo wake wa kucheza nafasi mbalimbali uwanjani umemfanya kuwavutia makocha wote wanaofanya kazi naye.

Akiwa na umri wa miaka 33 sasa, kiungo huyu bado thamani yake iko juu klabuni Simba. ambako yuko na mastaa wengine wa zamani wa Azam, Manula, John Bocco, Gadiel Michael, Pascal Wawa na Shomary Kapombe.


GADIEL MICHAEL

Ni beki ambaye aliondoka Azam msimu wa 2016/17 na kujiunga na Yanga tofauti na nyota wengi wa timu hiyo ambao wengi wao walijiunga na Simba mara baada ya kumaliza mkataba wao na Azam na kufanikiwa kujizolea mafanikio makubwa wakiwa ndani ya Simba kwa kutwaa mataji mengi.

Alidumu Yanga misimu miwili tu mara baada ya kumaliza mkataba wake aliamua kujiunga na Simba ambayo anaitumikia hadi sasa japo si kwa mafanikio kutokana na kukosa namba ya kudumu kikosini kama ilivyo kwa mastaa wengine waliotoka Azam FC.


SAID MORAD

Beki wa zamani wa Simba na Ashanti, Juni 29, 2016 alithibitisha mwenyewe kupewa barua na uongozi wa timu yake ya zamani Azam FC kwa madai kwamba hawana mpango wa kumuongeza mkataba na kumuengua kikosini hivi sasa yupo Kagera Sugar.


AGGREY MORRIS

Nahodha wa Azam aliyesimamishwa kwa muda usiojulikana kutokana na utovu wa nidhamu kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Oktoba 6, 2021 imesema kwamba wachezaji hao wameonyesha utovu wa nidhamu kwa meneja wa timu, wachezaji wenzao, benchi la ufundi na viongozi wa kabu kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.

Mkongwe huyo ambaye kwasasa yupo visiwani Zanzibar ni miongoni mwa nyota watatu pekee ambao walibaki kwenye kikosi cha timu hiyo ambao mikataba yao inamalizika mwisho wa msimu na dirisha dogo wanaruhusiwa kuzungumza na timu yoyote kwa mujibu wa sheria za soka.


MICHAEL BALOU

Novemba 2016 ndio uongozi wa timu hiyo ulithibitisha kuachana na mchezaji huyo baada ya mkataba wake kumalizika kuwa hawatakuwa naye tena kutokana na kocha kutokuwa na mahitaji naye.


HIMID MAO

Kiungo ambaye anacheza nje ya Tanzania ni miongoni mwa nyota waliopambana kuhakikisha timu yao haipotezi mchezo hata mmoja kwenye msimu wao wa kwanza kutwaa taji akiwa ndani ya Azam FC.

Aliondoka ndani ya timu hiyo mwaka 2017 baada ya uongozi wake kufikia makubaliano ya kibiashara na Bidvest ya Afrika Kusini kwa ajili ya kunasa huduma ya kiungo huyo na huo ulikuwa mwanzo wa kujaribu changamoto nyingine nje na sasa anakipiga Ghazel El Mahalla ya Misri.


SALUM ABUBAKARI

Ndiye mchezaji aliyecheza misimu mingi ndani ya Azam akiipandisha timu na ni miongoni mwa nyota waliosalia kikosini hadi msimu huu waliposimamishwa sambamba na wenzake wawili.

Mkataba wa Sure Boy unamalizika mwisho wa msimu huu huku dirisha dogo anaruhusiwa kuzungumza na timu yoyote kwani atakuwa amebakiza miezi sita.


GAUDENCE MWAIKIMBA

Mwaikimba alitemwa sambamba na Amri Kiemba 2015 baada ya mikataba yao kumalizika na uongozi kutowaongeza mikataba mipya. Mwaikimba kwasasa yupo Boma FC inayoshiriki Ligi ya Championship ameendeleza makali yake akiwa huko pamoja na kucheza soka muda mrefu.


JOHN BOCCO

Ni mshambuliaji aliyecheza kwa mafanikio makubwa ndani ya Azam FC kwani ni miongoni mwa nyota waliocheza misimu mingi kwenye timu hiyo lakini aliondoka bila heshima yoyote. Bocco yupo Simba na amekuwa katika kiwango bora kwa kipindi alichodumu ndani ya Wekundu hao akiisaidia timu kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara nne mfululizo. Msimu uliopita alimaliza akiwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu akifunga mabao 16 na pia alishinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu.

‘Captain Fantastic’ Bocco amefunga zaidi ya mabao 100 Ligi Kuu Bara.


KIPRE TCHETCHE

Ndiye aliyeibuka mchezaji bora wa msimu huo kutokana na namna alivyoweza kuisaidia timu yake kufanikiwa kutwaa taji la ligi ikiwa ni sambamba na kuwa mchezaji mwenye mabao mengi ndani ya timu.

Aliondoka Azam FC akiwa ameweka historia ya kutwaa taji bila kupoteza huku akijiondoa mwenyewe kikosini baada ya kupata ofa nje ya nchi akitimkia Kedah Darul, Malaysia.


WACHEZAJI WA AKIBA

Mwadini Ally aliondoka Azam na kurudi visiwani Zanzibar, David Mwantika (DTB), Jabir Aziz (JKT Tanzania), Brian Umony, Kelvin Friday (Biashara United), Mudathir Yahya (Azam) na Khamis Mcha (Dodoma Jiji).