Azam FC, Singida Black Stars zilivyoruka kiunzi CAF
Muktasari:
- Azam iliyopo kundi B, imepata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Nairobi United katika mechi ya tatu iliyopigwa kwenye Uwanja wa Nyayo, jijini Nairobi, Kenya na kufikisha pointi tatu baada ya mechi mbili za kwanza kupoteza dhidi ya AS Maniema (2-0) na Wydad (1-0).
UKIZIONDOA Simba na Yanga zenye rekodi ya kufanya vizuri katika Kombe la Shirikisho Afrika hadi kucheza fainali, hakukuwa na timu nyingine ya Tanzania iliyowahi kupata ushindi hatua ya makundi ya michuano hiyo hadi Azam na Singida Black Stars zilipofanya kweli Jumapili iliyopita Januari 25, 2026.
Azam iliyopo kundi B, imepata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Nairobi United katika mechi ya tatu iliyopigwa kwenye Uwanja wa Nyayo, jijini Nairobi, Kenya na kufikisha pointi tatu baada ya mechi mbili za kwanza kupoteza dhidi ya AS Maniema (2-0) na Wydad (1-0).
Kwa upande wa Singida Black Stars, bao la Elvis Rupia, liliipa ushindi wa 1-0 dhidi ya AS Otohô, mechi ya kundi C ikipigwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar. Ushindi huo umeifanya Singida kufikisha pointi nne sawa na CR Belouizdad huku ikikamata nafasi ya tatu baada ya mechi tatu.
Mbali na hilo, Azam imekuwa timu ya kwanza kutoka Tanzania kupata ushindi ugenini hatua ya makundi katika michuano ya CAF msimu huu baada ya zote kushuka dimbani mara tatu.
Azam katika mechi tatu ilizocheza, ugenini ilifungwa 2-0 na AS Maniema, ikaja nyumbani kuchapwa 1-0 na Wydad, kisha imeshinda ugenini dhidi ya Nairobi United (2-1).
Kwa upande wa Singida, ilianza ugenini kufungwa 2-0 na CR Belouizdad, ikatoka sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya Stellenbosch na kushinda nyumbani 1-0 dhidi ya AS Otohô.
Yanga inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa kundi B, ilianza na ushindi wa bao 1-0 nyumbani dhidi ya AS FAR Rabat, ikaenda ugenini kuambulia suluhu (0-0) dhidi ya JS Kabylie, kisha ikafungwa ugenini 2-0 na Al Ahly.
Kwa Tanzania, Simba ndiyo timu pekee haijapata pointi yoyote hatua ya makundi msimu huu ikipoteza mechi zote za Ligi ya Mabingwa Afrika ikipangwa kundi D.
Simba ilianza kuchapwa 1-0 nyumbani dhidi ya Petro Atletico, ikaenda kwa Stade Malien kufungwa 2-1, kisha ikaifuata Esperance na kupokea kichapo cha 1-0.
REKODI MPYA
Rekodi zinaonyesha, ukiziweka kando Simba na Yanga, timu nyingine ya Tanzania iliyowahi kucheza hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika ni Namungo iliyofanya hivyo msimu wa 2020–2021.
Katika msimu huo, Namungo ilimaliza mkiani mwa kundi D bila ya pointi kutokana na kutopata ushindi wala sare, ikipokea vichapo mechi zote sita. Pia ikaondoka bila bao, huku yenyewe ikaruhusu mabao tisa.
Baada ya kupita takribani misimu minne, imeshuhudiwa timu nyingine mbali na Simba na Yanga zimetinga makundi na kuruka kiunzi ilichokikwaa Namungo iliposhindwa kukusanya pointi, pia kushindwa kufunga bao.
Singida Black Stars na Azam zimetinga makundi kwa mara ya kwanza, zimefanikiwa kufunga mabao na kupata ushindi hadi sasa zikiwa na matumaini ya kufanya vizuri zaidi.
Singida Black Stars hii ni mara ya kwanza inashiriki michuano ya kimataifa na imeweka rekodi ambayo haijawahi kuwekwa na timu yoyote ya Tanzania iliyoshiriki kwa mara ya kwanza na kufuzu makundi CAF. Upande wa Azam, imepigania nafasi hiyo kwa takribani miaka 10, hatimaye msimu huu imetoboa na kufuzu makundi.
ZILIZOWAHI KUCHEZA SHIRIKISHO
Katika msimu wa 2018-2019, Mtibwa Sugar ilipata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuwa bingwa wa Kombe la FA 2017-2018.
Mtibwa ilianzia hatua ya awali kwa kucheza dhidi ya Northern Dynamo ya Seychelles, mechi ya kwanza ikashinda 4-0, marudiano ikashinda 1-0 na kufuzu hatua ya pili kwa jumla ya mabao 5-0.
Hatua ya pili ikakutana na KCCA ya Uganda, mechi ya kwanza Mtibwa ikafungwa 3–0, marudiano ikalala 2-1 na kutupwa nje ya mashindano kwa jumla ya mabao 5-1. Safari yao ikaishia hatua ya pili.
Msimu wa 2019-2020 ilikuwa zamu ya KMC ambayo yenyewe iliishia hatua ya awali ikianza na matokeo 0-0 ugenini dhidi ya AS Kigali kutoka Rwanda, nyumbani ikaja kufungwa 2-1, ikaondoshwa kwa jumla ya mabao 2-1.
Namungo ikaja kuvunja mwiko wa kuishia hatua za mwanzoni baada ya msimu wa 2020–2021 kutoboa hadi kutinga makundi.
Hatua ya awali, Namungo iliichapa Al Rabita ya Sudan Kusini mabao 3–0, hakukuwa na mechi ya marudiano baada ya wapinzani hao kujitoa.
Namungo ikafuzu hatua ya kwanza na kuiondosha El Hilal ya Sudan kwa jumla ya mabao 5–3. Mechi ya kwanza Namungo ilishinda 2-0, marudiano ikawa sare ya 3-3.
Katika mtoano kuwania kufuzu makundi, Namungo ikaiondosha 1º de Agosto ya Angola kwa jumla ya mabao 7-5. Mechi ya kwanza Namungo ilishinda 6-2, marudiano ikachapwa 3-1.
Hatua ya makundi pumzi ikakata, matokeo yalikuwa hivi; Raja CA 1–0 Namungo, Namungo 0–2 Pyramids, Namungo 0–1 Nkana, Nkana 1–0 Namungo, Namungo 0–3 Raja CA na Pyramids 1–0 Namungo.
Ikashuhudiwa msimu wa 2021–2022, Biashara United nayo ikishiriki Kombe la Shirikisho. Hatua ya awali iliondosha FC Dikhil ya Djibouti kwa jumla ya mabao 3-0. Mechi ya kwanza ilishinda 1-0, marudiano ikashinda 2–0.
Hatua ya pili ilikabiliana na Al Ahli Tripoli ya Libya. Mechi ya kwanza nyumbani Biashara United ilishinda 2-0, hata hivyo, ikashindwa kusafiri kwenda Libya kurudiana na wapinzani wake, ikaondoshwa mashindanoni. Safari ikaishia hapo.
Geita Gold ilishiriki Kombe la Shirikisho msimu wa 2022-2023 na kuishia hatua ya awali ikiondoshwa kwa kanuni ya bao la ugenini baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya 2-2 dhidi ya Hilal Alsahil ya Sudan. Mechi ya kwanza Hilal Alsahil ilishinda 1–0, marudiano Geita Gold ikashinda 2–1. Kutokana na nyumbani kuruhusu bao moja huku yenyewe ikishindwa kufunga ugenini, Geita Gold ikatolewa mashindanoni.
Msimu wa 2023-2024, ilikuwa zamu ya Singida Fountain Gate ambayo sasa hivi inaitwa Fountain Gate, nayo ilishiriki Kombe la Shirikisho Afrika na kuishia hatua ya pili.
Hatua ya awali, Singida Fountain Gate iliitoa JKU ya Zanzibar kwa jumla ya mabao 4–3, ikianza na ushindi wa 4–1, kisha ikafungwa 2–0.
Baada ya hapo ikakutana na mziki wa Modern Future na kutupwa nje ya mashindano kwa jumla ya mabao 4-2. Singida Fountain Gate ilianza na ushindi wa bao 1–0 nyumbani, ikaenda Misri kufungwa 4–1.
Coastal Union ilishiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2024-2025 na kuishia hatua ya awali ikifungwa jumla ya mabao 3-0 na Bravos do Maquis ya Angola. Mechi ya kwanza ugenini ilichapwa 3–0, nyumbani matokeo yakawa 0-0.
USHIRIKI WA AZAM CAF
Azam ilikuwa inazishuhudia timu nyingine zikitinga makundi tena zikitumia uwanja wao wa Azam Complex, lakini sasa baada ya miaka 21 tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo, ikabadilisha heshima yake kwa kukata tiketi hiyo ya kwenda hatua ya juu baada ya zile mechi za mtoano.
Huu ukiwa ni msimu wake wa 11 kushiriki tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo mwaka 2004, Azam ilikwama mara 10 kutinga makundi ya michuano ya CAF, msimu huu ikatoboa.
Azam iliyoanza kushiriki michuano ya CAF mwaka 2013, ilikuwa haijawahi kucheza makundi na mara mbili imeshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2015 na 2024-2025, zote imeishia hatua ya awali.
Kwa upande wa Kombe la Shirikisho Afrika kabla ya msimu huu kufuzu makundi, huko nyuma imewahi kujitahidi na kufika hatua ya pili. Haikuvuka zaidi ya hapo.
Rekodi zinaonyesha katika Kombe la Shirikisho Afrika, Azam mara ya kwanza ilishiriki mwaka 2013 na kuishia hatua ya kwanza, kisha 2014 (hatua ya awali), 2016 (hatua ya pili), 2017 (hatua ya kwanza), 2019–2020 (hatua ya kwanza), 2021–2022 (hatua ya pili), 2022-2023 (hatua ya pili), 2023-2024 (hatua ya kwanza).
Safari hii imeweka rekodi mpya ya kufuzu makundi chini ya Kocha Florent Ibenge baada ya kuiondosha KMKM kwa jumla ya mabao 9-0 wakati wa mechi ya mwisho. Ilianza kwa ushindi wa mabao 2-0 ugenini, kisha nyumbani ikashinda 7-0.
Kabla ya hapo, mechi ya awali iliitoa El Merreikh Bentiu ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 4-0. Azam ilishinda 2-0 ugenini na nyumbani.
Ilichofanya Azam msimu huu kwa kushinda ugenini mechi ya makundi katika Kombe la Shirikisho Afrika, ni rekodi mpya kwani hata Yanga ilipofuzu hatua hiyo kwa mara ya kwanza katika michuano hiyo mwaka 2016, mechi tatu zote za ugenini ilipoteza dhidi ya MO Béjaïa (1-0), Medeama (3–1) na TP Mazembe (3–1). Ilimaliza mkiani na pointi nne, ikishinda moja nyumbani dhidi ya MO Béjaïa (1-0), pia sare ya nyumbani 1-1 dhidi ya Medeama.
Yanga pia mara ya pili kucheza makundi Kombe la Shirikisho Afrika ilikuwa mwaka 2018, ikamaliza tena mkiani na pointi nne, huku ikipoteza mechi zote tatu za ugenini.
Katika mechi za ugenini, Yanga ilifungwa 4-0 na USM Alger, ikachapwa tena 4-0 na Gor Mahia, kisha ikalala 1-0 mbele ya Rayon Sports. Kwa mechi za nyumbani, ilitoka 0-0 na Rayon Sports, ikafungwa 3-2 na Gor Mahia, ikaja kuifunga USM Alger 2-1.
KUNDI B
P W D L GF GA Pts
1.Wydad 3 3 0 0 5 0 9
2.Maniema 3 2 0 1 3 1 6
3.Azam 3 1 0 2 2 4 3
4.Nairobi Utd 3 0 0 3 1 6 0
KUNDI C
P W D L GF GA Pts
1.Belouizdad 3 2 0 1 5 4 6
2.Stellenbosch 3 1 1 1 2 3 4
3.Singida BS 3 1 1 1 2 3 4
4.AS Otohô 3 1 0 2 4 3 3