Athari za tabianchi zinavyotesa mashabiki, wachezaji
Muktasari:
- Mabadiliko ya tabianchi yamesababisha kuahirishwa kwa baadhi ya mechi, au kusimama kwa muda kutokana na hali mbaya ya hewa. Wakati mwingine kuhamishwa kabisa uwanja hali inayofanya timu kuingia gharama zingine za maandalizi tofauto na awali.
KATIKA sehemu ya kwanza ya makala haya ya athari za tabianchi katika viwanja vya soka tuliona jinsi hali ilivyo na namna wamiliki wanavyoendelea kupambana kukabiliana na mabadiliko hayo. Leo tunaangalia mateso wanayopata mashabiki na timu husika. Twende pamoja...
Meneja wa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Manyara, Jackson Mwendwa anazungumzia gharama za kukabiliana na madiliko ya tabiachi akisema kwa miaka ya hivi karibuni zimeongezeka kutokana na hadhi ya ligi ya Tanzania. “Ni zaidi ya mara tatu au nne ya gharama za kawaida ambazo mwanzo zilikuwa zikitumika,” anasema.
Shaaban Rajabu ambaye aliwahi kuwa meneja bora wa Uwanja wa Lake Tanganyika uliopo Kigoma, anasema anajivunia mafanikio ya kuuweka kwenye viwango vya juu.
“Changamoto ya Kigoma ni hali ya hewa yenye unyevu mwingi na uhaba wa vifaa vya kisasa. Hata hivyo, kupitia juhudi binafsi na msaada wa Mashujaa FC, tulihakikisha uwanja unabaki kuwa salama,” anasema Rajabu.
Meneja wa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Manyara, Jackson Mwendwa anasema: “Ni ngumu sana kutunza uwanja kuhakikisha unakuwa bora muda wote sanasana nyasi kuwa katika uhalisia wake.
“Inachukua muda, nguvu kubwa pamoja na gharama. Siwezi kusema gharama ni kiasi gani lakini ni fedha nyingi sana zinatumika kwa ajili ya kuandaa uwanja au kutengeneza kuwa bora.
“Hapo lazima mnunue mbolea, kuna kumwagilia maji, kuna kununua petroli zinazosaidia kuendesha mashine ya kukata majani.
“Hapa tuna kisima, kipindi cha jua kali tunamwagilia uwanja mara mbili, asubuhi na usiku, huo ndio muda tunaoutumia kuumwagilia uwanja.
“Kipindi cha mvua ni rahisi kwa sababu huwa inanyesha, lakini inapokuwa nyingi unakuta kuna athari zinatokea kwa sababu hata kwenye mazao mvua zikiwa nyingi tatizo.”
Juni 2025, Mwendwa alitunukiwa Tuzo ya Meneja Bora wa Uwanja kwa mwezi huo inayotolewa na Kamati ya Tuzo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), hata hivyo, mwenyewe amesisitiza hayupo kwa ajili ya kutaka sifa za kushinda tuzo, bali anafanya kazi yake ili mpira uchezwe sehemu inayostahili.
“Sisi tumejipanga si tu katika kuchukua tuzo, bali kuhakikisha uwanja wetu unakuwa bora na kusifika Tanzania na nje ya nchi. Lengo ni kuhakikisha uwanja unakuwa bora muda wote.
“Ukiangalia msimu uliopita viwanja vingi vilifungiwa lakini uwanja wetu uliendelea kubaki imara licha ya kutumika na timu nyingi ambazo zilifungiwa viwanja vyao zikaja hapa. Tumejipanga kuhakikisha unakuwa bora muda wote,” anasema Mwendwa.
KWA MASHABIKI
Mashabiki wa mpira wa miguu pia wanakumbwa na athari za mabadiliko ya tabianchi. Hali mbaya ya hewa kama vile mvua kubwa au joto kali huathiri mahudhurio yao viwanjani, na hivyo kupunguza mapato ya klabu kutokana na tiketi na bidhaa mbalimbali.
Shabiki mmoja ambaye amekuwa mhudhuriaji mzuri wa mechi za Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025, Ally Salum, anasema kuna baadhi ya viwanja akienda anakutana na changamoto inayomfanya kutofuatilia mchezo kwa utulivu na wakati mwingine huamua kuangalia kwenye runinga.
“Mfano Uwanja wa KMC Complex au Jenerali Isamuhyo, kipindi cha jua na mvua mashabiki tunaloa, angalau Azam Complex kuna jukwaa limewekea cha kujikinga ingawa sio kote.
“Huwa tunafurahia zaidi pale Benjamin Mkapa kwani sehemu kubwa ya uwanja ina kivuli japo wakati wa jua kali kuna upande utachomwa hadi ushangae na mvua ikinyesha ile ya upepo unaloa kabisa,” anasema.
Mashabiki wanapopungua viwanjani kutokana na hali mbaya ya hewa ikiwemo mvua kubwa au joto kali mapato viwanjani hupungua.
TIMU NAZO
Mabadiliko ya tabianchi yamesababisha kuahirishwa kwa baadhi ya mechi, au kusimama kwa muda kutokana na hali mbaya ya hewa. Wakati mwingine kuhamishwa kabisa uwanja hali inayofanya timu kuingia gharama zingine za maandalizi tofauto na awali.
Mvua kubwa husababisha mafuriko katika viwanja, na joto kali hufanya mazingira ya kuchezea kuwa hatarishi kwa wachezaji.
Mfano wa karibuni ni michuano ya Kombe la Dunia la Klabu iliyofanyika Marekani, kutokana na hali mbaya ya hewa kwa baadhi ya maeneo nchini humo, kuna mechi zililazimika kusimama kwa muda zaidi ya nusu saa hadi saa moja kisha kuendelea.
Katika msimu wa 2024-2025, Simba ililazimika kuutumia Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Zanzibar kwa mechi zs nyumbani za Kombe la Shirikisho Afrika hatua ya nusu fainali na fainali.
Hiyo ilisababishwa na mvua iliyonyesha wakati wa mchezo wake wa robo fainali dhidi ya Al Masry sehemu ya kuchezea kujaa maji na kuharibika hali iliyofanya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuufungia hadi utakaporekebishwa.
Kutokana na hilo, Simba inaamini ilishindwa kufikia malengo ya kuwa bingwa wa michuano hiyo kutokana na kucheza uwanja tofauti na iliouzoea.
Aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Kagera Sugar, Thabit Kandoro anasema: “Mechi za saa 8:00 mchana kiuhalisia ngumu hasa kwa timu zinazosafiri umbali mrefu wachezaji wanakosa muda wa kupumzika, hivyo miili yao inakuwa haifunguki ni kama inapunguza ufanisi wao.
“Mfano mechi ambayo tulitoka Bukoba kwenda kucheza Mbeya dhidi ya Prisons tulitumia gharama kubwa wachezaji kuwa sawa lakini mwili wa binadamu kama haupo sawa haudanganyi, ingawa walijitahidi kwa kadri wawezavyo, naamini Bodi ya Ligi Kuu Tanzania ina watu makini italifanyia kazi jambo hilo, ingawa nisisitize halihusiani na kukosa matokeo mazuri.”
ITAENDELEA KESHO
Makala hii imedhaminiwa na Bill & Melinda Gates Foundation. Kwa maoni tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917