ASEC walitisha, Manula balaa

WAWAKILISHI pekee kutoka Afrika Mashariki na Kati kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Simba baada ya kupoteza ugenini nchini Benin dhidi ya Asec Mimosas kwa mabao 3-0, mechi ya mwisho watakayocheza Dar washindwe wenyewe.
Mechi ya mwisho Simba itacheza nyumbani Aprili 3, Uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya USGN na hakuna wanachohitaji zaidi ya ushindi ili kusonga kwenye hatua ya robo fainali.
Kwa nini Simba washindwe wenyewe kwenda robo fainali? Mechi kati ya USGN waliokuwa nyumbani juzi pia walitoka sare ya mabao 2-2 na RS Berkane ambao nao mchezo wa mwisho watacheza nyumbani kwao Morocco na Asec Mimosas.
Kutokana na matokeo hayo kundi linasomeka kuwa Asec ndio vinara wakiwa na pointi tisa na mechi ya mwisho watacheza ugenini dhidi ya Berkane waliopo nafasi ya pili na pointi saba, huku Simba wakiwa nafasi ya tatu na pointi saba watamaliza na USGN wa nne na pointi zao tano.
Simba wakishinda watakuwa wametinga robo fainali moja kwa moja baada ya kufikisha pointi kumi, huku wakisikilizia matokeo ya Berkane na Asec watamalizika vipi na mmoja kati yao ndiye ataungana nao robo fainali.
Kama Simba watashindwa kupata ushindi kwa kufungwa na USGN watakuwa wameondolewa katika mashindano hayo na kama wakitoka sare wataiweka nafasi ya kusonga mbele hatarini kwani Berkane na Asec wanaweza kufuzu wenyewe.
Katika mechi ya nyumbani Simba wanahitaji kucheza kwa nidhamu kubwa ili kupata ushindi pamoja na wachezaji wao kutopata kadi nyingi za njano kama ilivyokuwa katika michezo iliyopita ukiwamo huu wa Asec Mimosas waliopata nne.
Wachezaji wa Simba kama watapa kadi za njano nyingi maana yake wanaweza kushinda na kusonga hatua ya robo fainali, lakini wakajikuta wakishindwa kucheza mechi ya kwanza hatua hiyo kutokana na kizuizi h-icho cha kadi za njano mfululizo.
Simba wana faida ya kushinda mechi hiyo ya nyumbani kutokana na baadhi ya sababu zikiwemo mwendelezo mzuri wa matokeo wakiwa kwenye ardhi ya Tanzania, kwani mechi mbili kwenye hatua hiyo zote wameshinda, ila wanakutana na timu waliyotoka nayo sare ya bao 1-1 mchezo wa kwanza ugenini, Niger.
Pamoja na hayo, lakini nini kiliiua Simba juzi?
KUSHINDWA KUKABA
Katika mechi hiyo, Asec walipata bao la kuongoza dakika 16 baada ya kazi nzuri ya winga, Anicet Oura aliyempiga chenga Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na kupiga pasi ya chini kwa Aubin Kramo aliyefunga.
Wakati Oura anampiga chenga Tshabalala na kupiga krosi kwa mfungaji ndani ya boksi la Simba kulikuwa na wachezaji saba walioshindwa kukaba kwa usahihi.
Wachezaji hao kila mmoja alikuwa anaangalia mpira unapotoka na kuacha kumkaba Kramo aliyekuwa kwenye eneo la hatari zaidi na kupata urahisi wa kufunga bao na sio katika mazingira magumu licha ya kuwa ndani ya eneo la hatari la Simba.
Bao la pili la Mimosas dakika 25 mfungaji Stephane Aziz Ki alipokea pasi huku nyuma yake akiwapo Jonas Mkude lakini pamoja na kulipa mgongo goli aligeuka na kupiga shuti lililomshinda, Aishi Manula. Bao hilo mbali ya kazi nzuri ya mfungaji, pia kulikuwa na kosa alilofanya Mkude kushindwa kumkaba kikamilifu Aziz aliyegeuka na kufunga.
MANULA MOTO
Manula aliruhusu mabao matatu mchezoni, lakini ndani ya dakika 90 anastahili pongezi kwa kuwa mchezaji bora kutokana na kiwango alichoonyesha katika mchezo huo walioshambuliwa mara kwa mara.
Manula aliokoa mabao ya wazi manne ya Asec waliokuwa na uwezo wa kufunga na pengine kama sio ubora wake, basi timu hiyo ilikuwa inaweza kufungwa zaidi ya mabao matatu.
Katika kuonyesha kuwa Manula ni kipa wa daraja la juu Afrika katika mechi hiyo alipangua mikwaju miwili ya penati ambayo nayo ilikuwa ni nafasi ya Asec kuandika mabao na mchezo huo kumalizika na idadi kubwa ya mabao.
Manula ameendelea kuwa katika kiwango bora kwenye mashindano hayo kwa kutimiza majukumu vizuri kuokoa mashambulizi ya maana - yaani yale ya wazi na kama si ubora wake Simba wangefungwa mengi.
MABADILIKO SIMBA
Kabla ya kuanza kipindi cha pili, Simba walifanya mabadiliko ya wachezaji watatu kwa awamu moja. Walitolewa Kibu Denis, Mzamiru Yassin na Rally Bwalya nafasi zao kuingizwa Benard Morrison, Taddeo Lwanga na Pater Banda.
Mabadiliko hayo yalikuwa na faida kwa Simba ndani ya dakika kumi za mwanzo ambazo walishambulia zaidi langoni mwa Asec tofauti na kipindi cha kwanza ikiwemo kukosa nafasi za kufunga mabao.
Baada ya kufungwa bao la tatu, kocha Pablo Franco alifanya mabadiliko mengine ya kupunguza Mkude na kumuingiza straika, Chriss Mugalu ili kuongeza nguvu katika kushambulia na kutafuta walau bao ugenini.
Katika dakika ya 74, alitoka Inonga na kuingia mchezaji wa zamani wa Asec, Pascal Wawa ili kwenda kuimarisha eneo la ulinzi la Simba wasiruhusu mabao zaidi ya yale waliyokuwa wamefungwa.
KROSI ZAWATESA
Simba wameendelea kuteseka kwa kufungwa mabao yanayotokana na mipira ya krosi kwa msimu wa tano katika mashindano ya kimataifa na kwenye mashindano ya ndani - Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho ASFC na mengineyo.
Katika mazoezi ya Simba wiki hii kabla ya kuifuata Asec, Mwanaspoti lilishuhudia kocha Pablo akitoa mbinu mbalimbali za kuzuia mipira ya kushambuliwa kupitia krosi na muda mwingi mabeki wake walifanya vizuri katika kuokoa. Hata hivyo, katika mechi ya juzi na Asec ilikuwa kama ugonjwa wa muda mrefu ambao umekosa tiba ya kuutibu.
Simba walifungwa bao na Konate kwa kichwa baada ya kutumia upungufu wa mabeki kushindwa kuokoa mpira ya krosi.
PABLO HUYU HAPA
Kocha wa Simba, Pablo anasema katika mashindano hayo kila timu imekuwa ikifanya vizuri na kutokana na hilo aliwapongeza wapinzani wao, Asec kwa kucheza vizuri nyumbani na kufanikiwa kupata ushindi uliowabeba kwenye msimamo wa kundi D.
Hata hivyo, kocha huyo anasema ukiangalia msimamo wa kundi uilivyo kila timu inaweza kufuzu robo fainali ya michuano hiyo, lakini wao pekee wana faida ya kupata pointi moja ugenini dhidi ya USGN ambao watacheza nao katika mchezo wa mwisho utakaopigwa jijini Dar es Salaam. “Kama wapinzani wetu walivyotumia vizuri viwanja vya nyumbani kwao naamini nasi kwa upande wetu tuna dakika 90 za mwisho ngumu nyum bani, lakini naamini tunakwenda kushinda (mchezo wa mwiho) na kusonga hatua ya robo fainali,” anasema Pablo.
Nini maoni yako? Tuandikie; 0658-376417