ARTHUR ASHE: Mkali wa tenisi aliyeacha simulizi ya kusikitisha

Muktasari:
- Hatimaye mwanzoni mwa miaka ya 1960 alichomoza mchezaji mwenye asili ya Afrika Mmarekani, Arthur Ashe na hii leo mtu anayezungumzia tenisi duniani hatakuwa mkweli kama ataliweka jina lake pembeni.
HADI leo nyota wengi wanaotamba katika mchezo wa tenisi duniani wana asili ya watu weupe kutoka Marekani na Ulaya, ukiachilia mbali Wamarekani wenye asili ya Afrika, Serena na Venus Williams, waliong’ara miaka michache iliyopita.
Kwa muda mrefu imekuwa ni nadra kuona nyota wa mchezo huu kutoka Afrika, Asia au Arabuni na hata ikitokea kuona wachezaji wa asili ya Kiafrika waking’ara katika mchezo huu, huwa hawana viwango vikubwa kulinganisha na wenzao.
Serena na Venus William kwa zaidi ya miaka 10 walikuwa maarufu, lakini hadi mwishoni mwa miaka ya 1950 mchezo huu hakuna mchezaji wa asili ya Afrika aliyetamba.

Hatimaye mwanzoni mwa miaka ya 1960 alichomoza mchezaji mwenye asili ya Afrika Mmarekani, Arthur Ashe na hii leo mtu anayezungumzia tenisi duniani hatakuwa mkweli kama ataliweka jina lake pembeni.
Arthur Ashe, aliwapatia heshima Wamarekani wenye asili ya Afrika kwa kufungua ukurasa mpya katika historia ya tenisi.
Alicheza kwa kujiamini na kuiangusha miamba iliyoonekana haitikisiki wakati ule licha ya kupata matatizo ya kiafya, ikiwa pamoja na kupasuliwa moyo mara mbili na matibabu ya ubongo.
Arthur Ashe alipendwa na wazee na vijana na kifo chake Februari 6, 1993 akiwa na miaka 50, kilichotokana na kudungwa sindano iliyomuambukiza virusi vya Ukimwi wakati anapata matibabu kiliusikitisha ulimwengu.
Atakumbukwa kwa mchezo mzuri, msimamo usiotetereka wa kupigania haki za wanyonge na bahati mbaya iliyomkuta wakati maradhi ya ukimwi yakiwa ndio kwanza yamechomoza.
Alikuwa mstari wa mbele katika kampeni dhidi ya ubaguzi wa rangi na alishiriki katika maandamano na kulala barabarani na watu masikini wakati yeye akiwa tajiri.
Wakati akiwa hana huruma alipokabiliana na wapinzani katika mashindano, alionekana tofauti nje ya kiwanja. Alikuwa mtu mwenye maneno ya busara, hekima, maarifa na mafunzo na zaidi ni kwamba hakuringia utajiri na umaarufu wake.

Aliwahi kusema; “Kama lazima binaadamu anataka kuringa, basi afanye hivyo sio kwa cheo chake, fedha au nguvu zake za mwili, bali namna anavyothamini utu na kuheshimu wenzake. Ukiona mtu anaonyesha dharau kwa wengine ujue anayo matatizo ya akili na anahitaji msaada.”
Yeye ni mtu pekee kwa wakati ule mwenye asili ya Afrika kushinda mashindano ya Wimbledon na ya wazi ya Marekani na Australia.
Alizaliwa Richmond, Virginia Julai 10, 1943 na alikuwa na urefu wa sentimita 185 (futi 6 na inchi 1) na uzito wa kilo 73 (Ratili 160). Fedha alizopata kama zawadi kutokana na tenisi zilikuwa dola za Kimarekani 2,584,909.
Alipenda tenisi na mpira wa kikapu tangu utotoni na kutumia muda mwingi kusikiliza muziki na kukaa na mama yake, Matties, aliyefariki dunia ghafla kwa ugonjwa wa moyo wakati akiwa na miaka 6. Kama njia moja ya kujiliwaza aliongeza muda kucheza tenisi.
Alipata umaarufu 1963 alipochaguliwa timu ya Marekani kushiriki mashindano ya Kombe la Davis. Alikuwa mtu wa kwanza mwenye asili ya Afrika kujiunga na timu ya Marekani katika mashindano hayo na ilipofika 1969 Ashe alichomoza kuwa mchezaji bora wa tenisi.
Katika mwaka 1968 aliisaidia Marekani kunyakua Kombe la Davis na mwaka mmoja baadae, yaani 1969 alikataliwa ruhusu ya kuingia Afrika Kusini na serikali ya makaburu, hivyo kutoweza kushiriki mashindano ya wazi kwa sababu ya rangi yake.
Pamoja na kuleta mabadiliko makubwa katika tenisi duniani alisaidia kuuamsha ulimwengu juu ya ubaguzi wa rangi uliokuwapo Afrika Kusini. Aliwahi kuueleza ubaguzi kama uchafu ambao harufu yake mbaya ilimtibua hata mtoto aliyekuwa tumboni mwa mama yake.
Aliwaambia makaburu hawataweza kuwazuia Waafrika kujikomboa na ipo siku watajilaumu kwa vitendo vyao vya ubaguzi na hili sasa tunalishuhudia.
Alikamatwa Januari 11, 1985 kwa kuandamana kupinga ubaguzi mbele ya ofisi ya Ubalozi wa Afrika Kusini, jijini Washington DC. Alikamatwa tena Septemba 9, 1992, nje ya Ikulu ya Marekani alipokuwa akipinga unyanyasaji wa wakimbizi kutoka Haiti.
Harakati zake za kupinga ubaguzi zilimpunguzia muda wa mazoezi na akawa hang’ari hadi 1975 aliponyakuwa ushindi wa Wimbledon kwa kumshinda Jimmy Connors wa Sweden aliyepewa nafasi ya kufaulu. Aliueleza ushindi wake kama ushindi wa watu wanaobaguliwa.
Ashe alifunga ndoa na Jeanne Moutoussamy, mpiga picha wa michezo Februari 20, mwaka 1977 na kung’ara katika karibu kila mashindano ya kimataifa hadi alipofanyiwa upasuaji wa moyo na kustaafu 1980.
Baada ya kustaafu aliliandikia habari za michezo gazeti la Times na alikuwa mtangazaji wa kituo cha ABC.
Katika mwaka 1983 alifanyiwa upasuaji wa pili wa moyo. Kwa mshtuko mkubwa Ashe aliarifiwa mwaka 1988 kugundulika kuwa anaishi na virusi vya UKIMWI alivyopata alipofanyiwa upasuaji wa pili wa moyo.
Yeye na mkewe walilifanya suala hili kuwa la faragha hadi Aprili, 1992 pale gazeti la USA Today (Marekani Leo) lilipotaka kuchapisha habari kwamba anaishi na virusi vya UKIMWI ndipo alipojitokeza hadharani kutangaza habari hizo.
Hapo alitoa nukuu iliyowatoa machozi watu wengi duniani kote aliposema:
“If I were to say ‘God, why me?’ about the bad things, then I should have said ‘God, why me?’ about the good things that happened in my life” (Kama nataka niseme Mola kwa nini mimi kwa mabaya yaliyonipata, basi pia nilipaswa niseme hivyo kwa mazuri niliyopata katika maisha yangu).
Katika mwaka wa mwisho wa maisha yake alitumia muda mwingi kuwaeleza watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI duniani wasikate tamaa na wasiambukize watu wengine. Vile vile aliandika habari za maisha yake, kazi aliyoimaliza wiki moja kabla ya kifo chake.

Miezi miwili kabla ya kifo chake Februari 6, 1993 alianzisha Taasisi ya Afya ya Arthur Ashe inayoshughulikia usalama kwa kinamama wajawazito.
Kwa kuheshimu mchango wake katika tenisi, serikali ya Marekani ilitoa stempu za Arthur Ashe mwaka 2005 na viwanja vingi vya michezo nchini Marekani vimepewa jina lake.
Dunia inamkumbuka Ashe kwa mchezo wake maridadi, harakati zake za kupigania wanyonge, kupinga ubaguzi na kauli za busara zilizotoka mdomoni mwake.
Zifuatazo ni baadhi ya nukuu zake maarufu zinaozidi 100.
• Kutokana na tunachokipata ndio tunaweza kuishi; lakini ni kile tunachotoa ndio kinachofanya maisha.
• Anza hapo ulipo. Tumia ulichonacho na usitamani cha mwenzako. Fanya unaloweza na usijitwishe mzigo usioweza kuubeba.
• Mfanikio Ni sehemu ya safari na sio mwisho wa safari. Unayoyafanya ni muhimu zaidi kuliko matokeo
• Furahia unaposhinda, lakini usikubali kusononeka unaposhindwa.
• Sitaki nikumbukwe kwa mafanikio yangu ya tenisi. Naomba nikumbukwe kwa nilivyotumia mchezo wa tenisi kupambana na madhila na kudai haki za wanyonge.
• Mtu mwerevu hufanya uamuzi pole pole, lakini huheshimu uamuzi yake.
• Sitaki uwezo au mafanikio yangu yahusishwe na kabila au asili yangu. Nataka yote yahusishwe na binaadamu wenzangu.
• Lazima tuheshimu nguvu ya elimu na lazima tuheshimu sheria zilizojengeka kwa misingi ya haki. Lazima tupende nafsi zetu, wazee wetu na watoto wetu, wake zetu na waume zetu.
• Mapenzi ni ghali kwa sababu bei yake halisi haijulikani.