Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aregash - Aziz Ki wa Yanga Princess

Agash Pict

Muktasari:

  • Kiungo huyo alitambulishwa Yanga katika dirisha dogo akifananishwa na staa wa timu hiyo kwa wanaume, Aziz KI ambaye alikuwa mfungaji bora na MVP wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita.

KAMA kuna usajili uliofanikiwa mpaka sasa kwa Yanga Princess, basi ni ule wa kiungo mshambuliaji, Aregash Kalsa kutokea C.B.E ya Ethiopia.

Kiungo huyo alitambulishwa Yanga katika dirisha dogo akifananishwa na staa wa timu hiyo kwa wanaume, Aziz KI ambaye alikuwa mfungaji bora na MVP wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita.

Aregash sio kwa kubahatisha baadhi ya mashabiki kumfananisha na mwamba wa Burkina Faso, kwani mrembo huyo ni fundi haswa akitumia mguu wa dhahabu (kushoto).

Katika mechi yake ya kwanza kucheza akiwa na Yanga Princess dhidi ya Bunda Queens mchezaji huyo alifunga bao na kumuinua Aziz KI ambaye alikuwa uwanjani akishuhudia mchezo huo.

Baada ya kumalizika kwa mechi Aziz alimfuata na kumpongeza akamuelekeza baadhi ya vitu ambavyo akiviongeza atakuwa bora zaidi.

Kitendo hicho kilionyesha ni namna gani Aziz anavutiwa na kiungo huyo ambaye pia ana uwezo wa kucheza winga zote mbili na pia mshambuliaji wa kati.

Mwanadada huyo ambaye mbali na kusakata kabumbu, pia anapendelea masuala ya urembo hasa mitindo ni Muethiopia wa pili kuichezea Yanga baada ya Ariet Udong ambaye naye huu ni msimu wake wa kwanza kucheza Tanzania.


AG 05

MRITHI WA PRECIOUS

Msimu uliopita wakati Yanga inampa mkono wa kwaheri Precious Christopher ambaye baadaye alitimkia Simba Queens, iliwaumiza baadhi ya mashabiki wa timu hiyo.

Hilo lilitokana na ubora wa Mnigeria huyo ambaye alicheza Yanga kwa misimu miwili kuanzia 2022/23 na 2023/24 na kukonga mioyo ya mashabiki wa Jangwani.

Precious ni fundi akitumia mguu wa kushoto na uwezo wa kupiga mashuti ya mbali na hata kufunga penalti za kiufundi vilivyowavutia mabingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Bara na kuamua kumvuta Unyamani.

Kitendo cha kuachana na Precious ambaye ilidaiwa Simba iliweka pesa ndefu kumshawishi akiwa mchezaji huru kiliwaumiza sio tu viongozi, bali hata mashabiki wa Yanga kwani alikuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi.

Msimu uliofuata Yanga ilisafiri hadi Ethiopia kuweka kambi na kuangalia uwezekano wa kuleta mrithi wa Precious ili kuziba pengo lake.

AG 02

Hata hivyo, ilipishana wakati viongozi wanakwenda nchini humo C.B.E ilikuwa bize kwenye michuano ya Cecafa ili kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika.

Bahati nzuri ni kwamba nyota huyo alikuwa kwenye kikosi hicho kilichocheza mechi zote hadi kuchukua ubingwa, ndipo Yanga ikajiridhisha na kiwango cha kiungo huyo aliyekuwa matakwa ya kocha Edna Lema.

Hadi sasa amecheza mechi dhidi ya Bunda Queens na Alliance Queens akifunga bao moja na assisti moja.

Kutokana na kiwango bora alichoonyesha kwenye mechi mbili za ligi huenda akawa mbadala sahihi wa Precious ambaye pia anatumia mguu wa dhahabu.


AG 04

PACHA YA HATARI

Kama ataendelea kuonyesha kiwango bora kwenye mechi zilizosalia za ligi anaweza kuwa msaada mkubwa kwenye kikosi hicho ambacho kilikuwa na changamoto ya namba 10.

Mbali na kuwa na uwezo wa kufunga ni mzuri pia  kupiga pasi sahihi kwa washambuliaji, ambao hadi sasa kwenye tano bora ya wapachikaji mabao Yanga hakuna.

AG 01

Uwezo wa nyota huyo unaweza kuwa na manufaa kwa washambuliaji wa Yanga, Ariet Udong na Jeaninne Mukandasyenga kama kiungo huyo atakuwa na muunganiko nao mzuri.

Lakini, faida zaidi itakuwa kwa Ariet, mshambuliaji ambaye ana nguvu, akili na kasi ambayo kama atakuwa nyuma yake inaweza kuwa balaa lingine.

Kwa sasa Ariet anapitia changamoto ya jeraha la kiwiko cha mguu na nafasi yake imechukuliwa na Jeaninne aliyetambulishwa Jangwani hivi karibuni na tayari kafunga mabao mawili akiwa nyuma ya Aregash.


AG 03

KIMATAIFA

Aregash ana medali mbili za michuano ya kimataifa na ubingwa wa Shirikisho la Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kati ya 2023/24 na 2024/25.

Ikumbukwe C.B.E ndio timu iliyocheza fainali nyingi za Cecafa kwa wanawake ili kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika.

Tangu mashindano hayo yaanzishwe 2021 timu hiyo  imecheza fainali tatu kati ya nne ikichukua ubingwa mara moja msimu huu.

Msimu wa kwanza ilitolewa na Vihiga Queens, ilhali uliofuatia ikaishia hatua za awali na ule wa 2022/23 ilitolewa kwa penalti 5-4 na JKT Queens, huku msimu uliopita iliichapa Kenya Police bao 1-0.

Akiwa miongoni mwa nyota walioisaidia C.B.E kuchukua ubingwa msimu uliopita, bahati haikuwa upande wake hakucheza Ligi ya Mabingwa baada ya kusajiliwa na Yanga.