Anavyopatikana bingwa wa gofu kwa klabu
YANAPOFANYIKA mashindano ya gofu ya klabu, kisheria kila klabu inatakiwa kutoa wachezaji wanane, kisha watakuwa wanacheza wawili wawili, pointi zitakazopatikana zinatoa ubingwa.
Kila klabu itakuwa inategemea uwezo wa wachezaji wake, hivyo watakaokuwa wamepiga mipira michache, ndio watanyakua taji la mashindano.
Mfano katika wachezaji wanane, sita wakafanya vizuri, huku klabu nyingine watatu pekee ndio wakapiga mipira michache katika kiwanja namba 11, basi hawatakuwa na haja ya kumaliza viwanja 18, tayari wanakuwa wametoka kwenye mashindano.
Mfano mzuri ni mashindano ya CRDB-Inter Club, yaliyomalizika mwanzoni mwa mwezi Machi, yakizikutanisha klabu za Dar es Salaam Gymkhana, Morogoro na Lugalo wenyeji na bingwa alikuwa Dar Gymkhana, ambao waliwashinda wapinzani wao kiwanja namba 11.
INAVYOKUWA
Mchezaji aliyecheza vizuri ndiye anayeweza kumbeba mchezaji mwenzake, mwenye nafasi hiyo ya kumbeba ni mchezaji anayecheza handcup ya juu.
Katika kutafuta ‘stroke’ zake alizocheza unachukua neti 90 unatoa 20 ambayo ni handcup yake unapata neti 70.
Kwa matokeo hayo, mchezaji mwenye handcup 20 atakuwa amepata neti 70 katika mchezo huo, endapo mchezaji anayecheza naye ana handcup 0 ili amfikie mwenzake anatakiwa acheze na afikie 70, ingawa mwenye handcup za chini akicheza vizuri anaweza akambeba pia mwenye handcup nyingi.
Baada ya kumaliza kucheza viwanja 18 itatafutwa ‘Stroke’ zake utachukua neti yake aliyopata katika mchezo huo na baadaye unatoa handcup zake ndipo anaweza akapata neti aliyocheza katika mchezo huo.
DAR GYMKHANA USHINDI WAO
Klabu ya Dar Gymkhana ndio mabingwa wa mashindano ya CRDB-Inter Club, baada kushinda katika michezo mingi waliyocheza.
Pia kuna wachezaji wa klabu nyingine ambao walionyesha kiwango kizuri, pamoja na kwamba hawakuzisaidia klabu zao kunyakua taji hilo, lakini walipewa zawadi mbalimbali za pesa na vikombe.
Pia mchezo huo unazingatia unadhifu na kupendeza. Kwa upande wa wanawake aliochukua zawadi hiyo ni Joyce Ndyetabura ambaye ni mweka hazina wa TLGU na kwa upande wa wanaume alikuwa ni Jitine Lavingia kutoka Dar Gymkhana.
Mashindano yalikuwepo miaka mingi iliopita, kabla ya kusimama na kuanza mwaka jana na Lugalo ndio walikuwa mabingwa na mwaka huu wamevuliwa na Dar Gymkhana.
Kwa upande wa Kanda ya Kaskazini inayohusisha klabu za TPC, Moshi Gymkhana na Arusha Gymkhana mashindano yanaitwa Northern Zone Championship na yamekuwa ni ya wazi kwa klabu yoyote inayotaka kushiriki, pia yanafanyika kutokana na ukaribu wa klabu hizo.
Pia kwa Ukanda wa Juu Kaskazini yanaitwa Northen Highland na yanafanyika katika klabu ya Mufundi, nayo ni ya wazi kwa klabu zinazotaka kushiriki.
SAYORE-MWENYEKITI
Mwenyekiti wa Klabu ya Dar es Salaam Gymkhana, Lesser Sayore anasema “Tuliwashangaza wengi ikiwemo klabu ya Lugalo yenye wachezaji wenye uwezo mkubwa, kwani wachezaji wao wanashiriki mashindano mengi, tofauti na sisi, hivyo hatukutarajiwa kuchukua taji hilo.”
Anasema kwa kuwa mashindano ni endelevu, wanajipanga kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye mashindano yatakayofuata.
“Tunahitaji kuweka rekodi ya mataji kwenye klabu yetu ya Gymkhana na hilo linawezekana, kikubwa ni kupanga mikakati na kujiandaa ipasavyo,” anasema.
Rais wa Chama cha Gofu Tanzania (TGU), Gilman Kasiga aliipongeza Dar Gymkhana kwa kuonyesha ushindani, akizitaka klabu nyingine kujipanga, ili mashindano mengine zifanye vizuri.
“Kama mwaka huu mashindano haya yameandaliwa na Lugalo, natarajia klabu zingine ziandae, ili kuendelea kuibua ushindani na vipaji vikubwa,” anasema.
Imeandikwa na Brown Msyani, Olipa Assa na Nevumba Abubakar