Prime
Alianzisha Kamusoko, Aucho akaendeleza, kwaheri Dokta!
HAPA karibuni maisha yalibadilika Jangwani. Hatukutazamia sana. Zamani Yanga walikuwa watu wa mbio kweli kweli. Tangu enzi za mababu zetu. Haishangazi kuona walitoa mawinga wengi walioteleza nchi hii.
Mpira wa Yanga tuliufahamu. Ndiyo maana waliwatoa kina Abubakar Salum 'Sure Boy', Justin Mtekele, Sanifu Lazaro ‘Tingisha’, Edibily Lunyamila na wengineo. Miaka ya karibuni wakawatoa kina Mrisho Ngassa, Shamte Ally na Simon Msuva.
Yanga walikuwa watu wa ‘peleka mbele tukimbizane’. Hapa karibuni ghafla akatokea mtu mmoja aliyeitwa Thaban Scara Kamusoko. Fundi wa mpira. Akaanzisha kitu kilichoitwa ‘kampa kampa tena’. Nipe pasi nikupe halafu nipe nikupe nyingine.
Mbio za Yanga zikatoweka katika akili ya Kamusoko. Mashabiki wa Yanga wakaanza kuufurahia mpira ambao miaka mingi ulikuwa unachezwa na watani zao Simba. Haishangazi Simba walikuwa wanatoa viungo wengi maridadi wakati Yanga walikuwa wanatoa mawinga wengi wazuri na wenye kasi.
Baada ya miaka michache tangu Kamusoko aondoke akaja Khalid Aucho ‘Dokta’. Huyu ndiye alikuwa msingi wa Yanga hii imara. Ndiye aliyekuwa anaituliza Yanga kwa umaridadi mkubwa katikati. Ndiye aliyekuwa anaamuru Yanga icheze vipi kadri pambano lilivyokuwa linasonga mbele.
Mbele ya ukuta wa kina Ibrahim Bacca, Bakari Nondo na Dickson Job kazi ya Aucho ilikuwa kwanza kuulinda ukuta. Sijui ni vipi baada ya kumsikia Aucho kwa muda mrefu tangu wakati ule anacheza Gor Mahia amewezaje kutunza nguvu zake.
Umri wake umesogea. Na labda tunaweza kusema amedanganya miaka. Lakini Aucho ana nguvu nyingi mwilini ambazo vijana wengi wa kileo hawana. Alikuwa anajua sana kuziba nafasi nyingi ambazo mpira wa adui ungepita.
Vile vile alikuwa anajua kugongana sana uwanjani kiasi kwamba kupewa kadi ya njano halikuwa jambo la kushangaza sana. Kwa umri wake na kwa namna ambavyo nimemsikia kwa muda mrefu akicheza soka nilitegemea kuona vijana wengi wa Ligi Kuu wakimuumbua katika suala la umri.
Hata hivyo, katika suala la kugongana na ubabe wa hapa na pale, hakuna siku Aucho alionekana mnyonge au alionekana kuwa umri umemtupa mkono. Kuanzia mechi za ndani hadi zile za nje Aucho alionekana kuwa yule yule tu.
Lakini kubwa ni baada ya kugongana na kuupata mpira angeweza kucheza mpira rahisi. Viungo wetu wengi wanapenda kutembea na mpira bila ya sababu. Aucho alijaribu kuturudisha nyuma katika zama za Kamusoko. Kucheza mpira rahisi.
Tunamkumba Xavi Hernandez kwa kuifundisha dunia namna ya kucheza mpira rahisi. Wachezaji wa Barcelona chini ya Pep Guardiola walimgeuza kuwa ukuta. Wanaugonga mpira kwake kisha unarudi wanauchukua wanaendelea na mambo yao.
Aucho alikuwa anafanya mambo rahisi katika timu. Hali ya hewa ikitulia ndiyo alikuwa anachungulia pasi muhimu zaidi kwenda mbele. Hiki ndicho kilichowafanya Yanga wawe wanaonekana kukosa utulivu wakati Aucho akiwa hayupo uwanjani.
Wiki iliyopita Aucho ameandika waraka wa kuagana na Yanga. Nadhani hadi sasa hivi mashabiki watakuwa wanakuna vichwa ni namna gani wanaweza kuziba pengo la Aucho.
Ni kweli mashabiki wengi wa Yanga wanaamini katika akili ya Injinia Hersi Saidi na rafiki zake wanaiongoza Yanga sasa hivi, lakini hawana uhakika sana kama watampata Aucho mwingine.
Amesajiliwa kiungo Balla Moussa Conte kutoka CS Sfaxien ya Tunisia. Hakuna mchezaji mbaya anayetoka Afrika Magharibi kwenda kule Kaskazini. Anaweza kuwa mchezaji mzuri, lakini je ataweza kuituliza Yanga kama Kamusoko au Aucho.
Mpira wa kisasa unatuambia kuna viungo wa aina mbili. Kuna wale ambao ni wakabaji wazuri. Zamani tuliwaita ‘defensive midfielder’ na tuliwapenda sana. Kina Javier Mascherano, Patrick Vieira, Antonio Conte na wengineo wengi.
Lakini dunia la kileo katika mchezo wa kisasa tuna viungo watulizaji timu. Kina Sergio Busquets, Michael Carrick na wengineo. Hawa wanafahamika zaidi kama ‘holding midfielders’. Kina Aucho wameituliza sana Yanga kwa staili hii ya mchezo. Staili ya pasi nyingi za hapa na pale.
Conte anaweza kuwa mzuri, lakini asicheze kama Aucho wakati ana mpira. Viungo huwa wanatofautiana kwa kiasi kikubwa. Wote wana uzuri wao lakini wakati mwingine huwa wanaamuru staili nzima ya uchezaji ya timu.
Na sasa baada ya Aucho kuaga kuna mambo mawili ya kutafakari. Vijana wetu wamejifunza nini kutoka kwake.
Kama nilivyosema hapo awali nimemsikia Aucho kwa miaka mingi. Anautunzaje mwili wake ndani na nje ya uwanja ni jambo la kujiuliza.
Nawafahamu vijana wengi wa Kitanzania waliomkuta Aucho uwanjani na wamemwacha kama walivyo. Wengine walikuwa katika timu yake na walishindwa kumpora namba licha ya mashabiki kuamini Aucho alikuwa amepitwa na wakati.
Jambo jingine la kutafakari ni kama mipango ya Injinia na wenzake itaendelea kufanikiwa linapokuja katika suala la kubadilisha wachezaji katika nafasi yake. Ilianzia pale Yanga walipoanza kubadilika.
Wakawachukua Mukoko Tonombe na Gift Mauya wakafanya vizuri katika eneo la kiungo.
Baadaye wakaja Yannick Bangala na Khalid Aucho. Mukoko na Gift wakapotea. Baadaye Yannick akaondolewa akaingia Mudathir Yahya na timu bado ikaonekana iko vizuri tu. Akaongezwa Duke Abuya na timu ikaimarika zaidi.
Sasa Aucho ameondoka huku Conte akiingia. Ataendelea kuimarisha sehemu ya kiungo au maisha yatabadilika. Wakati mwingine usajili ni kamari kama ilivyo kamari nyingine. Kitu ambacho Yanga wataweza kujivunia ni kama mambo yakiharibika bado wanao Duke Abuya na Mudathir.
Kwa sasa tunachoweza kusema ni kwaheri kwa Aucho. Kama akibakia katika ligi yetu basi bado ataweza kuendelea kuibariki kwa kipaji maridadi. Kama akiondoka basi tutamkumbuka sana. Ni aina ya wachezaji ambao wameacha alama katika soka letu.