AJE YOYOTE

Tuesday April 06 2021
YOYOTE PIC 1
By Thobias Sebastian

SIMBA wana jambo lao. Wababe hao wa Tanzania wametinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuigagadua AS Vita ya DR Congo mabao 4-1, huku wakiupiga mpira mwingi na kuwapagawisha mashabiki wao waliotamba, “kwa pira lile, tupangiwe timu yoyote tunaipasua.”

Achana na ushindi huo mnono ulioifanya Simba kujihakikishia kumaliza kama kinara wa Kundi A mbele ya Al Ahly, lakini gumzo kubwa ni aina ya mabao waliyofunga nyota kwake kwenye mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

YOYOTE PIC2

Katika mchezo huo uliokamilisha jumla ya siku 2,967 kwa Simba kutowahi kupoteza mchezo ikiwa nyumbani tangu walipofungwa bao 1-0 na Recreativo do Libolo ya Angola mwaka 2013, Luis Miquissone kinara wa mabao kwa sasa wa hatua ya makundi, akifunga matatu na kuasisti mawili, alifunga bao tamu la shuti kali la mwana ukome, kabla ya Clatous Chama naye kujibu mapigo.

Larry Bwalya naye alikwamisha bao akitokea benchi likiwa tamu vile vile na Chama kufunga bao tamu zaidi kwa kuwagaragaza mabeki wa Vita na kuihakikisha Simba kutinga robo fainali ikisaka rekodi yao ya kucheza nusu fainali iliyoiweka 1974 katika michuano hiyo enzi ikiitwa Klabu Bingwa.

SIMBA PIC
Advertisement

Kwa mafanikio hayo, Simba imefuzu mara ya pili ndani ya miaka mitatu kwenye hatua hiyo ya robo fainali ikiwa na Al Ahly, kwani mara ya kwanza ilikuwa 2018-2019 na kukwamia kwa TP Mazembe ya DR Congo ambayo msimu huu imekwama kabisa kufuzu hatua hiyo.

Simba sasa inaenda kukamilisha tu ratiba yao ya makundi Ijumaa hii itakapovaana na Al Ahly ambayo nayo imefuzu baada ya sare ya kibabe ugenini dhidi ya Al Merreikh iliyopo mkiani na alama zao mbili tu baada ya kucheza mechi tano kama wapinzani wenzake wa kundi hilo.

Licha ya ushindi huo wa 4-1, lakini Simba ilipaswa kushinda zaidi ya bao hizo kwani nyota wake, Chriss Mugalu alipoteza nafasi nne za wazi, mbali na Bernard Morrison, Luis Miquissone na Clatous Chama ambao kama wangetulia wangeita timu yao ushindi mnono zaidi.

AS Vita nao walipata nafasi tatu zilizowakuta washambuliaji wao, Ducapel Muloko dakika 26, Fiston Kalala dakika 15, ambao wote walipiga mashuti yaliyolenga lango ila ubora wa Aishi Manula uliinusuru timu kufungwa bao, japo dakika ya 32 aliruhusu moja kupitia Zemanga Soze ambaye naye alipiga shuti la mbali.

Bao hilo lilichafua rekodi ya Manula katika mechi za makundi kwani alikuwa hajaruhusu bao katika mechi nne za awali, lakini pia likiwa ni la pili kwenye mechi tisa za michuano hiyo msimu huu baada ya lile la awali alililofungwa na FC Platinum katika mechi ya raundi ya awali ugenini mjini Harare. Simba imefunga mabao 14 katika mechi hizo tisa msimu huu).

Mwanaspoti linakuletea mabao yote manne ya Simba kwenye mchezo huo dhidi ya AS Vita na namna inavyofanya mashabiki wao kuamini timu yao ikipangiwa klabu yoyote kwenye hatua hiyo ya robo fainali lazima itatoboa tu kutinga nusu fainali kwani msimu huu wamepania kujenga heshima.


BAO LA LUIS

Baada ya Simba kukosa nafasi nyingi za kufunga mabao, katika dakika ya 30 walipata bao la kuongoza kupitia kwa Luis Miquissone aliyefunga bao lake la tatu katika hatua ya makundi.

Bao hilo lilitokana na umahiri wa Bernard Morrison ‘BM3’ aliyeanza kikosi cha kwanza katika mechi hiyo na aliyesumbua sana kwa kasi na chenga zake za maudhi, ambapo alichukua mpira akiwa nje ya boksi pembeni akawapiga chenga mabeki wa Vita na kuingia ndani ya boksi la timu hiyo.

New Content Item (1)

Mara alipoingia kwenye boksi, Morrison alipiga pasi ya mwisho ya chinichini kwa Luis ambaye hakutaka kuremba zaidi ya kufumua shuti kali lililowashinda mabeki watatu wa Vita pamoja na kipa wao, Omossala Medjo.

Wakati Miquissone anafunga bao hilo kwa shuti kali mbele yake walikuwepo, mabeki Michael Mbambu, Ebunga Simba na nahodha, Ousmane Ouattara ambaye kwa mujibu wa mtandao wa (Transfers Markerts) thamani ya kumpata mchezaji huyo si chini ya Sh680 milioni.


BAO LA PILI

Licha ya As Vita kurejesha bao la Luis ndani ya dakika mbili tu, lakini sekunde chache kabla ya mapumziko, Clatous Chama aliwashtukiza wageni kwa kufunga bao la pili.

Chama alifunga bao hilo kutokana na mpira wa Morrison ulimgonga Ouattara na kumkuta Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ aliyekuwa akiwania na Makabi Glody na mpira ukaenda kukumkuta kiungo huyo fundi wa mpira ambaye hakuwa na ajizi zaidi ya kuukwamisha wavuni.

Kabla ya kufunga Chama alimpiga tobo Glody aliyekuwa akimjia kwa kasi kisha kupiga shuti kali la chini lililokwenda kumpita tobo pia nahodha wa Vita, Ouattara na mpira kuzama nyavuni, huku kipa wa timu hiyo akiwa hana la kufanya, licha ya kuurukia lakini akashindwa kuufikia.


SHUTI LA BWALYA

Kocha wa Simba, Didier Gomes alifanya mabadiliko mawili katika dakika 60, kwa kuwatoa Morrison na Mugalu kisha nafasi zao kuchukua, Larry Bwalya na Meddie Kagere.

Mabadiliko hayo yalionekana kuwa na faida kwa Simba, kwani ilimchukua dakika tano tu, Bwalya kufunga bao la tatu katika mchezo huo kwa shuti kali akipokea pasi kutoka kwa Chama ambaye alikuwa amemtengea nje ya boksi.

New Content Item (1)

Bao hilo ambalo lilifungwa dakika 65, kiungo mkabaji wa Vita, Papy Kabamba Tshishimbi aliyeingia kipindi cha pili alishindwa kumkaba vizuri Chama ambaye alimtengea mfungaji mpira nje ya boksi na Bwalya kupiga shuti kali kama anaua nyoka.

Wakati Bwalya anapiga shuti hilo kulikuwa na mchezaji mmoja nyuma wa AS Vita lakini wakati mpira huo aliopiga unakwenda langoni ulimpita tena tobo nahodha, Ouattara ambaye alishindwa kuuzuia.CHAMA BALAA!

Chama kuna wakati anaonekana kama mzembe fulani kwa kucheza soka la taratibu sana na kama hana uamuzi wa haraka, lakini balaa lake si la kitoto, kwani wapinzani wake wamekuwa wakiaibika sana mbele yake.

Kiungo huyo Mzambia aliwaburudisha mashabiki wa Simba walioruhusiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa kukaa kwa mpango maalum dhidi ya Covid 19 akifunga bao la nne lililokuwa la pili kwake katika mechi hiyo na kuzima ndoto zozote za AS Vita na benchi lao.

New Content Item (1)

Bao hilo lilikuwa tamu zaidi kuliko mengine matatu ya Simba, kwani Chama baada ya kupokea pasi kutoka kwa Luis alipiga chenga za kutishia kama anapiga mpira na kuwafanya mabeki wa Vita kujikuta wakigaragara chini akiwamo Mbambu.

Beki huyo alipotishwa na Chama, alikwenda chini na kupiga goti moja kwa mguu wake wa kushoto huku wa kulia ukihangaika kuokoa mpira ambao hata kipa, Medjo ulimshinda akibaki amesimama na kuutazama ukiingia kambani.


WASIKIE HAWA

Baada ya mechi kumalizika kocha wa Simba, Didier Gomes aliwapongeza wachezaji wake kwa kutekeleza yote aliyokuwa akiwaelekeza mazoezini huku akifurahia ushindi huo mnono, ingawa aliamini walipaswa kutokana na mabao mengi zaidi.

Gomes anasema kuifunga timu kubwa Afrika kama AS Vita mabao 4-1, tena wakitawala mpira katika maeneo mengi si jambo dogo na ni ushahidi kwamba kuna kazi kubwa iliyofanyika nyuma, huku akisisitiza huu ni muda wa kila ambaye anahusika na Simba kusherehekea baada ya timu kufuzu robo fainali.

“Kama wachezaji wangu wangekuwa makini katika mechi hii tulikuwa na uwezo wa kufunga zaidi ya mabao hayo manne kwani mbali ya kutawala mpira tulitengeneza nafasi nyingi za kufunga ambazo tulipoteza, lakini katika mpira hilo linaweza kutokea, sasa tunaangalia lililopo mbele yetu,” alisema Gomes na kuongeza;

“Kikubwa ambacho tulikuwa tumepanga ni kufuzu na kuongoza kundi na yote tumefanikiwa. tunaenda kucheza mechi ya mwisho ugenini na baada ya hapo tutaanza maandalizi ya kutosha ya mchezo wa robo fainali.”

Advertisement