Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ahoua kaondoka, mashabiki hawajui walie au wacheke

HISIA Pict


JEAN Charles Ahoua ameondoka zake Simba na tayari ameanza mazoezi na timu yake mpya ya CD Belouzidad ya Algeria. Juzi wakati Simba walipopata faulo mara mbili nje ga boksi la Esparance ya Tunisia kule Tunis kuna shabiki alimkumbuka Ahoua. Aliamini kama Ahoua angekuwepo na akapiga wangeweza kupata bao.


Hata hivyo kuna baadhi ya mashabiki waliamua kusonya. Kwamba Ahoua hakuwa na jipya. Shabiki mmoja akadai kwamba hauwezi kuendelea kuwa na mchezaji ambaye anakuwa hatari katika mipira ya kutenga peke yake. Mwingine akadaiwa kwamba Ahoua hakuwa na vitu vitu ambavyo namba kumi anapaswa kuwa navyo.

HISI 01

Hivi ndivyo ambavyo Ahoua amewachanganya mashabiki wa Simba. Tangu ujio wake hadi kuondoka kwake kuna watu hawajawahi kumuelewa Ahoua. Ameondoka zake na mashabiki wa Simba hawajui kama wanapaswa kulia au kucheka. Katika mitandao na mitaani hausikii kama mashabiki wa Simba wamesononeka kuondoka kwa Ahoua. Ni tofauti na wakati ule Jose Luis Miquissone alipoenda Al Ahly au Clatous Chotta Chama alipoenda Berkane.

Ahoua ni mfano halisi wa namna ambavyo namba na hali halisi huwa zinawachanganya mashabiki wa mpira. Kuna wachambuzi ambao wanaangalia namba zaidi lakini mashabiki wa Tanzania kuna kitu wanataka kukiona nje ya namba. Wanataka mchezaji ambaye anaumiliki mchezo kwa dakika zote alizopo uwanjani. Wanataka mchezaji ambaye ananyumbulika, anapiga chenga maridadi, anapiga pasi maridadi au kufunga mabao maridadi.

HISI 02

Bahati mbaya Ahoua hakuwa mchezaji wa namna hiyo. Wengi walidhani angeweza kuwa mrithi sahihi wa Chama lakini kwa macho ya mashabiki hakuwa chaguo sahihi. Kinachoshangaza ni kwamba ukichukua siku ambazo alivaa jezi ya Simba na ukichukua siku hizo hizo kwa Chama unaweza kukuta Ahoua ana mabao mengi kuliko Chama.

Mashabiki wetu hawaangalii hilo. Wanamtaka mchezaji kama Pacome Zouzoua. Muda wowote anageuka kwa madaha na kufanya kitu kinachokuacha mdomo wazi. Wanamtaka mchezaji kama Fei Toto. Mzenji anaweza kupiga pasi kushoto huku akiangalia kulia. Wanamataka mchezaji kama Chama alivyokuwa anacheza katika ubora wake.

Wanataka mchezaji ambaye ana vitu vingi mguuni na ambaye moja kwa moja anakwenda kuwa mhimili wa timu katika ujenzi wa mashambulizi lakini kuitawala mechi kiasi cha wapinzani kutumia muda mwingi kumkaba kuliko yeye kuwakaba wapinzani. Aina ya wachezaji kama akina Zinedine Zidane au Ronaldinho.

HISI 03

Wachezaji wa aina hii wamependwa Tanzania tangu enzi za kina Sunday Manara, Nico Njohole, Hamis Gaga na wengineo. Miaka ya karibuni pia wamepita akina Ramadhan Chombo ‘Redondo’ Shaban Kisiga ‘Marlone’, Haruna Moshi ‘Boban’, Waziri Mahadhi ‘Mendieta’ na wengineo wengi. Hatukuwatazama sana wachezaji hawa kwa namba zao. Tuliwatazama kwa mateso waliyokuwa wanayatoa kwa wapinzani.

Labda wakati ule wanacheza mpira wa kuhesabu sana namba haukuwepo tofauti na sasa. Labda kwa sasa tungehitaji pia kujua namba zao lakini kuna nchi wanaangalia mambo tofauti na ndio maana Ahoua aliondoka kwao Ivory Coast akiwa MVP. Nadhani walimuhukumu zaidi katika namba zake tofauti na sisi tunavyouangalia mpira. Hata wazungu wapo bize na namba kuliko kuangalia kanzu za akina Jay Jay Okocha. Mpira umebadilika.

Na hata Waarabu waliomchukua Ahoua inaonekana wameangalia zaidi namba zake kuliko mbwembwe nyingine uwanjani. Ni hizi namba ndizo ambazo zimewafanya mashabiki wa Simba wasijue kama wanapaswa kulia au kucheka kufuatia kuondoka kwa Ahoua. Hata hivyo ninachofahamu ni kwamba nyuma yake Ahoua amewaachia madeni baadhi ya wachezaji walioingia Simba katika dirisha dogo.

HISI 04

Wa kwanza ni Clatous Chama. Akiwa na umri wa miaka 34 ataweza kuwateka tena mashabiki wa Simba katika kiwango kile kile ambacho aliwateka awali kiasi kwamba kuziba pengo lake kilionekana kitu kigumu? Chama sio kazima sana kama Ahoua, lakini anapaswa kuitendea haki namba 10 yake kwa kuzalisha mabao zaidi. Kama Ahoua alikuwa na mabao mengi basi walau Chama anapaswa kuwa na pasi za mwisho (assist) nyingi kuwakumbusha Wanasimba namna namba 10 inavyotendewa haki.

Wengine ambao wana deni kwa Ahoua ni washambuliaji wa timu hiyo. Mpira wa kisasa umewageuza viungo wengi kuwa wafungaji zaidi kuliko washambuliaji lakini kazi namba moja ya washambuliaji ni kufunga. Washambuliaji kama akina Jonathan Sowah na Suleiman Mwalimu wakiendelea na mwendo huu huu nadhani kuna kundi la mashabiki wa Simba wanaweza kumkumbuka Ahoua.

Mwisho wa siku pamoja na kuwa hakuwahi kuwa kipenzi cha mashabiki wa Simba lakini ndiye amekuwa mfungaji wao bora tangu alipowasili nchini akitokea Abidjan. Washambuliaji wamewaruhusu yeye, Aziz Ki na Fei Toto kuwa wafungaji bora ingawa ni viungo.

HISI 05

Kuhusu Ahoua na timu yake mpya? Nina wasiwasi kama atadumu sana pale Algeria. Inawezekana ana namba nzuri lakini Waarabu wanavutiwa zaidi na wachezaji wa aina mbili. Kwanza ni viungo wa chini wanaoweza kufanya kazi chafu ya kukaba. Viungo kama akina Damaro Camara. Unapewa kazi ya kuzunguka mbele ya walinzi kama vichaa kisha ukipata mpira unawapa mafundi wa mbele yako.

Haishangazi kuona Himid Mao alidumu muda mrefu pale katika soka la Misri. Alikuwa anabadilisha vilabu tu kwa sababu Waarabu wanapenda mchezaji wa aina yake. Ndio maana pia Alou Dieng wa Mali amekuwa akidumu kwa muda mrefu pale Al Ahly. Kukaba sana na kupasia kwa mafundi ni kazi ya kitumwa ambayo wachezaji wengi wa kiarabu hawapendi kuifanya. Wanawaachia watu weusi.

Aina nyingine ambayo Waarabu wanaipenda kutoka kwetu ni washambuliaji wanaojua kusukumana na kufunga kule mbele. Ni kama anachofanya Fiston Mayele kule Pyramids. Hizo nafasi kwa miaka mingi wamekuwa wakipewa watu weusi. Akina John Utaka walikuwa wanafanya kazi hizo kwa miaka mingi kule Uarabuni. Ngumu sana kwa timu ya Waarabu kukosa kiungo mweusi na mshambuliaji mweusi.

Nafasi kama hii ya Ahoua ni ngumu kwetu. Sijashangaa kusikia Aziz Ki ameshindwa pale Waydad na ameuzwa kwenda Libya. Sijashangaa wakati ule Chama aliposhindwa kule Berkane. Wachezaji wa aina hiyo wanao wengi. Ilifika mahala pale Berkane Tuisila Kisinda alikuwa anacheza dakika nyingi kuliko Chama.

Simuoni sana Ahoua akitoboa sana kwa Waarabu. Kitu kikubwa kingine ambacho kinaweza kuwa kinambeba ni taifa lake. Ivory Coast. Wenzetu wakiona mchezaji ana namba nzuri na anatoka Ivory Coast, Nigeria, Cameroon, Senegal au Mali inakuwa rahisi kuaminika moja kwa moja tofauti na mchezaji kutoka Tanzania. Simon Msuva na Mbwana Samatta ndio ambao wana uwezo wa kulazimisha.