AFCON 2025: Mwisho wa siku kila mtu ana kwao
Muktasari:
- Wachezaji wenye asili ya Afrika ambao ni raia wa mataifa ya Ulaya wameonekana viwanjani wakifurahia mchezo mzuri wa nyumbani kwao kwa asili.
FAINALI za 35 za mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 kusaka taifa bingwa Afrika zinazoendelea huko Morocco zimeleta hisia nyingine kabisa ya uasili.
Wachezaji wenye asili ya Afrika ambao ni raia wa mataifa ya Ulaya wameonekana viwanjani wakifurahia mchezo mzuri wa nyumbani kwao kwa asili.
Sahau kuhusu wachezaji kama Brahim Diaz ambao walizaliwa Ulaya na kuchagua kutumikia mataifa yao ya asili Afrika, kuna wengine ambao walichagua kuzitumikia nchi za Ulaya, lakini bado hisia za Uafrika zinatembea kwenye mishipa yao ya damu.
KYLIAN MBAPPE
Mzaliwa wa Ufaransa kutoka kwa wazazi wenye asili ya Afrika. Mama ana asili ya Algeria na baba asili ya Cameroon.
Nyota huyo wa Real Madrid aliyechagua kuiwakilisha nchi yake ya kuzaliwa Ufaransa ni jina kubwa zaidi lilioonekana kwenye viwanja vya AFCON 2025.
Kwanza ilikuwa katika mechi ya Morocco na Mali, Ijumaa ya Desemba 26. 2025. Ilikuwa kwenye Dimba la Prince Moulay Abdellah mjini Rabat ambapo alialikwa na rafiki yake wa karibu, Achiraf Hakimi ambaye ni nahodha wa Morocco.
Halafu akaonekana katika mechi ya Cameroon dhidi ya Ivory Coast iliyofanyika Jumapili ya Desemba 28, 2025 kwenye Uwanja wa Marrakech, Ouahat Sidi Brahim.
Hapa Mbappe alikuwa akiishahudia nchi ya asili ya baba yake, Cameroon. Na hakuwa peke yake mjini Rabat, bali alikuwa na familia nzima akiwamo mdogo wake, Ethan na wazazi wao.
JULES KOUNDE
Nyota wa Ufaransa na klabu ya Barcelona ya Hispania, Jules Kounde naye ni mmoja wa wana Afrika waliokuja kushuhudia sherehe kubwa zaidi ya soka barani humu.
Kounde ana asili ya Benin anakotoka baba yake mzazi. Japo nchi ya asili yake si sehemu ya AFCON ya mwaka huu, lakini kama mwana wa Afrika akaamua kujumuika na Waafrika wenzake kufurahia mchezo mzuri.
Alionekana mjini Marrakech, Morocco, akishuhudia mchezo wa Ivory Coast na Cameroon.
AURELIEN TCHOUAMENI
Mfaransa mwingine wa Afrika anayeng’ara na timu ya Real Madrid, Aurelien Tchouameni,ni nyota mwingine mwenye asili ya Afrika aliyerudi nyumbani kuibariki AFCON.
Tchouameni mwenye asili ya Cameroon naye alionekana mjini Marrakech akishuhudia mechi ya Ivory Coast na Cameroon.
Zaidi tu ya kuwa Afrika ni bara la kuzaliwa wazazi wake, lakini mwenyewe anajivunia sana bara hili na amekuwa akirudi nyumbani mara kwa mara ikiwemo kwenye hizi fainali za AFCON. Mechi aliyoishuhudia ilikuwa ya taifa lake, Cameroon dhidi ya Ivory Coast.
ZINEDINE ZIDANE
Mfaransa mwenye asili ya Algeria, Zinedine Zidane ‘Zizzou’ alikuwepo kwenye Dimba la Moulay Hassan mjini Rabat kushuhudia mechi ya Algeria na Sudan.
Zaidi ya kuwa Algeria ndio nchi ya asili yake, lakini pia ana mwanawe ambaye alikuwa uwanjani siku hiyo akizilinda nyavu za Algeria.
Mtoto huyo, Luca Zidane, ambaye ni mzaliwa wa Ufaransa kama baba yake aliamua kurudi nchi ya asili ya baba yake kuiwakilisha.
Zidane kama baba akaja kushuhudia mchezo huo uliomalizika kwa ushindi wa 3-0 wa Algeria.
NYUMBANI NI NYUMBANI
Zaidi ya hawa waliokuja kushuhudia kuna wale wengine walioamua kuujua uhondo wa ngoma kwa kuingia na kucheza.
Hawa ni wachezaji waliozaliwa nje ya Afrika, lakini wakaamua kurudi Afrika, ardhi ya asili yao.
Asilimia 30 ya wachezaji wote wa AFCON wamezaliwa nje ya Afrika hasa Ulaya.
Wachezaji wote wa Comoro wamezaliwa Ulaya kasoro mmoja.
Algeria, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DR Congo) na Guinea ya Ikweta zimejaa wachezaji waliozaliwa Ulaya.
Nusu ya kikosi cha Senegal ni wachezaji waliozaliwa Ulaya.
Kwa ujumla, kati ya wachezaji wote 664 wanaoshiriki AFCON ya Morocco, 191 wamezaliwa Ulaya.
Wenyeji Morocco wana wachezaji waliozaliwa Ubelgiji, Ufaransa, Uholanzi na Hispania.
Wachezaji 16 wa Algeria wamelizaliwa Ufaransa, lakini wanao waliozaliwa Ujerumani, Ubelgiji na Uholanzi.
Guinea ya Ikweta ina wachezaji 19 waliozaliwa Hispania katika kikosi chake cha mastaa 28.
Tanzania ina wachezaji wawili waliozaliwa nje ya Tanzania. Hawa ni Tarryn Allarakhia na Haji Mnoga waliozaliwa Uingereza.
FAIDA YA MABADILIKO YA SHERIA
Mataifa yote yaliyojaza wachezaji wenye asili ya nchi zao, lakini wamezaliwa Ulaya wamefaidika kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya sheria yaliyofanywa na Shirikisho la Kandanda la Kimataifa (FIFA).
Wachezaji hawa katika umri mdogo walizichezea timu za taifa za nchi walizozaliwa, lakini baadaye ukubwani wakarudi nyumbani katika asili yao.
Hii inarahisishwa na mabadiliko ambayo FIFA waliyafanya miaka 20 iliyopita yaliyoruhusu wachezaji wa aina hii kubadilisha uraia.
Ni nchi tatu tu kwenye AFCON hizi ndizo hazina wachezaji waliozaliwa nje ya nchi zao. Nchi hizo ni Botswana, Misri na Afrika Kusini.