A TO Z siku 10 za Magnet Hispania

Tuesday May 10 2022
Magnet pPIC
By Eliya Solomon

YALE makinda 10 ya Kitanzania ambayo yalienda Vigo, Hispania kwa ajili ya mafunzo na majaribio yamerejea nyumbani, Tanzania huku yakiacha gumzo nchini humo kwenye klabu ya Celta Vigo inayoshiriki La Liga.

 Makinda hao wanatoka kwenye kituo cha kulea na kuendelea vipaji cha Magnet Youth Sports Academy na waliondoka nchini Aprili 19 huku wakiagwa na Naibu Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Saidi Yakubu aliyemwakilisha Waziri, Mohamed Mchengerwa.

Kabla ya kukwea pipa ‘ndege’ na kwenda Ulaya, wachezaji hao wa Kitanzania ambao kwa majina ni Abdu Mandeke, Avner Mrina, Patrick Greenton, Joseph Jr Michael ,Lenox Mgitu, Troy Makoi, Aaron Mrina, Ahmed Pipino-Diego, Samuel Shilla na Ethan Mnyavanu walipata nafasi ya kukutana na rais wa nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.

Kama ambavyo anafahamika ni mtu wa michezo basi, Kikwete aliwapa moyo wachezaji hao waliokuwa na viongozi wawili, Mwenyekiti wa kituo, Tuntufye Mwambusi aka Tuntu na Mkurugenzi wa Ufundi -Wane Mkisi na kuwaeleza wanatakiwa kuitumia vyema nafasi hiyo.

Nini kilijiri huko Hispania na kipi kitafuata baada ya kurejea kwao nchini? Majibu anayo Mwenyekiti, Tuntu ambaye tumefanya naye mahojiano ya kina na kueleza kila kitu ikiwemo vile ambavyo walikuwana na kupiga stori na nyota wa Celta Vigo, Iago Aspas.


Advertisement

KONEKISHENI NA CELTA VIGO

Akiwa miongoni mwa waanzilishi wa kituo hicho kwa lengo la kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto ambayo inawakabili vijana wengi wa Kitanzania ambao wanakosa misingi mizuri ya soka angali wakiwa madogo, Tuntu alisema haikuwa rahisi kupata ukaribu ‘Konekisheni’ na Celta Vigo.

Wigo wake wa kuwa na marafiki hapa nyumbani na nje ulimsaidia kwenye hili kwani mmoja wa marafiki zake alikuwa akifahamiana na Celta Vigo hivyo baada ya kuona juhudi zake aliamua kumuunganisha nao na ndipo mawasiliano yalipoanza.

“Tulianza kwa kufanya vikao kwa njia ya mtandao, walitaka kunisikia na kuona je tunaweza kuongea lugha moja kuhusu kile tunachoamini katika mpira wa miguu, walitaka kujua zaidi kuhusu Magnet, niliwaeleza na kwa bahati nzuri walivutiwa na maono, mipango na mitazamo yetu kuhusu kituo.”

“Hatukuishia hapo, waliendelea kuhoji zaidi na walipotosheka wakanialika pale Celta Vigo katika mji wa Vigo, huo ulikuwa mwaka 2019.Kwenda pale ilikuwa ni hatua muhimu sana kwani tukiweza kufanya mazungumzo ya kina, nikahudhuria programu za vijana kwa siku tano, wakifanya presentation ya philosophy yao na kunikutanisha na Mkurugenzi wa Academy na mahusiano wa kimataifa wa Celta Vigo ambaye naye alifurahi sana kwani hawajawahi kuwa na mahusiano Afrika.

“Baada ya makubaliano ya awali walisema wanahitaji kuja Tanzania ili kujiridhisha kama kunaukweli wowote ili tuwe na mahusiano ya karibu ambayo yatakuwa na matokeo chanya kwenye soka la vijana,” anasema na kuongeza.

“Kama ambavyo waliniahidi walikuja Tanzania na tulifanya kliniki ya mpira hapa Dar na kufanya camp Arusha. Program zote mbili ziliendeshwa na kocha wa celta Vigo wakishirikiana na wa kwetu na wakaona vile ambavyo tunaendesha programu zetu na viwango vya watoto wetu.Kiukweli walivutiwa sana na sisi na kutoa maksi zaidi ya 90, waliporejea Hispania ndio wakatufungulia sasa milango ya mahusiano,” anasema.


CORONA ILICHELEWESHA

Tuntu anasema janga la virusi vya corona kwa kiasi kikubwa lilichelewesha safari yao kwani walitakiwa kwenda mapema Hispania hata hivyo walijipa muda wa kujiandaa.

“Ilikuwa ngumu kwenda Hispania kipindi kile ambacho janga la virusi vya corona lilikuwa limechachamaa, mawasiliano baina yetu na Celta Vigo yaliendelea na ilitubidi kusubiri hadi muda sahihi utapofika na kweli ukafika na tukasafiri,” anasema.


MAMBO YALIVYOKUWA HISPANIA

Makocha wa akademi ya Celta Vigo, ambao walikuwa wanasimamia programu hizo za mazoezi asubuhi na jioni, walifurahishwa na viwango vya mchezaji mmoja mmoja hivyo walitaka kuona katika mbinu (tactical) vile ambavyo wanaweza kushindana na wale wa akademi yao.

Kocha Borja na wengine wawili ndio waliongoza programu ya mazoezi kwa siku kadhaa, Tuntu anasema kocha huyo aliwaeleza,

“Magnet Academy mnafanya kazi Nzuri. Najua jioni itakuwa ngumu kidogo kwani wachezaji wetu wamekaa muda mrefu pamoja lakini nina imani watafanya vizuri.” Kocha akaendelea kusema naona tofauti ndogo kwa ujuzi (individual skills ) ukifananisha na wachezaji wa akademi hiyo. Hichi kitu kiliwafanya makocha wa klabu hiyo kushangaa.

Mkurugenzi wa Ufundi wa Magnet ambaye pia ni Mkufunzi wa Shirikisho anasema “kuna vitu vidogo vidogo sana ambavyo ni vya kimbinu sana lakini kwenye misingi ya mpira vijana wetu walifanya vizuri.”


KUKUTANA NA IAGO ASPAS

Wakiwa ndani ya programu zao, Tuntu anasema walipata nafasi ya kukutana na mshambuliaji hatari wa Celta Vigo, Aspas mwenye mabao 17 nyuma ya Karim Benzema ambaye anaongoza orodha ya wafumania nyavu wa La Liga akiwa na mabao 26.

“Alikuwa akimleta kijana wake mazoezini, nilishangazwa sana na tukio lile maana licha ya ukubwa wa jina lake lakini anaheshimu sana taaluma ya watu wengine, alielezwa kuhusu ujio wetu pale na tukapata nafasi ya kuongea naye,” anasema na kuongeza.

“Ni mtu poa sana kwangu ilikuwa ni mara ya pili kukutana naye maana hata katika mkutano wa kwanza (2019) pale Celta Vigo na kwa bahati nzuri nilienda kukutana na hadi nyota wengine wa timu hiyo, kilikuwa kipindi ambacho tunaimarisha mahusiano,” anasema.


CHAKULA CHA MCHANA NA BALOZI

Makinda hao wakiongozwa na Mwenyekiti, Mkurugenzi wa Ufundi na baadhi ya wazazi waliweza kukutana na Balozi wa Tanzania katika nchi za Ufaransa, Uhispania na Ureno, Samwel Shelukindo na kula chakula cha pamoja jijini Madrid. “Ilikuwa ni siku nzuri sana kwani tulipata nafasi ya kuongea mawili matatu na balozi wetu pamoja na Watanzania wengine waishio nchini humo,” anasema.

Balozi Shelukindo ambaye pia anahistoria nzuri katika mpira wa miguu kwa kucheza akiwa timu ya jeshi na wizarani alifurahishwa sana na uwakilishi wa vijana hao wa Magnet na kuahidi ushirikiano na kituo hicho kwa maslahi mapana ya taifa.


WAITAZAMA CELTA VIGO

Aprili 20, Tuntu anasema walipata nafasi ya kwenda uwanja wa Celta Vigo, Abanca-Balaidos na kushuhudia mchezo wa La Liga kati ya wenyeji wao dhidi ya Getafe.

“Haikuwa siku nzuri kwa Celta Vigo maana tulishuhudia wakifungwa nyumbani mabao 2-0, lakini tulijifunza mambo mengi kwenye ule mchezo,” anasema.


RIPOTI KUTUMWA

Tuntu anasema baada ya kurejea nyumbani Celta Vigo itatuma ripoti ya mchezaji mmoja mmoja kwa lengo la kuimarisha zaidi vijana hao na kujua mwendelezo, hata hivyo huo sio mwisho wa mahusiano yao maana kuna mipango mizuri katika hili na kwa wachezaji wengine.


MAFUNZO YA MAKOCHA

“Tunaimani kubwa na mahusiano yetu na Celta Vigo kuwa yatakuwa na matokeo chanya sio kwa wachezaji tu maana tumekubaliana nao watakuwa na mafunzo maalumu na makocha wetu kwa lengo la kutuinua zaidi na kuielewa na kuitumia philosophi yao njia itakayorahisisha kwa vijana wetu kuweza kuingia kwa urahisi katika mpira wa Hispania na mpira wa kimataifa. Eneo hili ni muhimu,” anasema.


UJIO WA CELTA VIGO (2022)

Tuntu anasema tutawaona coaches wa Celta Vigo Academy wakija hapa nchini mwezi wa Saba ambapo wachezaji wengi kutoka Magnet watapata nafasi katika kliniki ya mpira itafanyika Dar na Arusha.

Kwa nini Arusha? Tuntu anasema, “Hali ya hewa na mazingira yanafanya Arusha kuwa sehemu nzuri kwetu wote Magnet na makocha wa Celta Vigo na Pia sisi Magnet tunategemea kufungua kituo huu mwezi wa tano katika jiji la Arusha.”

Advertisement