Simba, Namungo msiwadharau wapinzani

Thursday December 03 2020
simba pic

TIMU zetu nne kutoka Tanzania Bara na Visiwani wikiendi hii zina kibarua kigumu cha kuhakikisha wanasonga mbele kwenye michuano ya kimataifa iliyo chini ya CAF.

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Zanzibar, Mlandege FC wao inaiwakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Namungo FC na KVZ zenyewe zipo kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo timu hizi mbili sasa zitacheza kwenye viwanja vyao vya nyumbani.

Tukianza na Simba ambao walicheza mechi ya kwanza ugenini katika jiji la Jos, Nigeria kwa kuifunga Plateau United bao 1-0 lililofungwa na Clatous Chama raia wa Zambia watacheza mechi ya marudiano keshokutwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Waliocheza na Simba sio wabaya, wana uwezo wa kushinda mchezo huo hasa idadi ya bao ambalo walishinda Simba ugenini ambalo linawapa nguvu wapinzani wao kwamba huenda wakapambana kushinda mechi hiyo kwa zaidi ya bao moja.

Hata wapinzani wakishinda bao moja, bado uwiano wa mabao itakuwa ni 1-1 ambapo watalazimika kuingia kwenye penati ambazo hazina mwenyewe katika kuziokoa, hivyo Simba wanapaswa kuchunga zaidi mechi hiyo ya marudiano na sio kujiamini na kujisahau kwa madai ya kuwa nyumbani.

Advertisement

Ingawa Simba inafanya vizuri mechi zake za nyumbani lakini huu ni mpira ambapo kila mmoja anakuwa na mbinu zake katika kuhakikisha anapata ushindi, mbinu sio za nje ya uwanja tu bali hata ndani ya uwanja wanaweza kuzidiwa na kufunga.

Wachezaji wa Simba wanapaswa kuwa makini mno katika uchezaji wao, kuwa na nidhamu ya mchezo ambayo haitapelekea kupewa adhabu ambazo zitawapa faida wapinzani wao.

Kwa upande wa Mlandege FC ambayo inakwenda kucheza ugenini nchini Tunisia, wanaondoka leo Jumamosi pamoja na kwamba walipigwa bao 5-0 nyumbani wana matumaini ya kushinda mechi ya marudiano watakapoivaa Club Sportif Sfaxien.

Hata hivyo, Mlandege watakutana na wakati mgumu kwa Waarabu hao kutokana na uwezo wao wa kucheza ambapo wapinzani wana faida ya vitu viwili, maumbo ya miili yao pamoja na kucheza uwanja wa nyumbani. Vitu hivyo viwili ndivyo vilivyowaponza Mlandege wakiwa nyumbani, walishindwa kuutumia vyema uwanja wa Amaan na kukubali kufungwa mabao mengi huku mabao ya wapinzani wao yakifungwa kwa kichwa kutokana na maumbo yao kuwa marefu.

Mlandege wana mtihani mkubwa na mzito ili kuufuzu hatua inayofuata, idadi ya mabao yaliyofungwa awali ni kubwa mno kiasi kwamba kocha na wachezaji wao wanapaswa kujitoa hasa kuhakikisha wanashinda zaidi ya mabao hayo au kuyafikia ili waingie kwenye matatu, jambo ambalo huenda ni la kufikirika zaidi.

Namungo FC wana faida mbili kubwa na washindwe wao kuzitumia, mechi ya kwanza walicheza nyumbani na kushinda bao 3-0 dhidi ya Al Rabita ya Sudan Kusini.

Namungo walipaswa kwenda kucheza mechi ya marudiano nchini Sudan lakini kutokana na hali ya usalama kutokuwa nzuri nchini humo mechi hiyo itachezwa hapa hapa Dar es Salaam uwanja wa Azam Complex.

Hiyo ni faida kubwa kwa Namungo labda kama watafanya uzembe kwa kushindwa kujitoa kupambania ushindi wao maana ni kama wanacheza nyumbani kama ilivyokuwa mechi ya awali.

KVZ itakuwa uwanja wa nyumbani wa Amaan keshokutwa Jumamosi kurudiana na Alamal SC Atbara ambapo mechi ya awali waliyocheza ugenini KVZ walipigwa bao 1-0.

Kwa vile wanacheza nyumbani basi wana kila sababu ya kuhakikisha wanashinda mechi hiyo, kwa kurudisha na kuongeza bao ili wasonge mbele, KVZ hawakuondoka kinyonge kwenda Sudan, walijiandaa basi hata sasa watajiandaa kushinda mechi hiyo ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Advertisement