Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Lamine Yamal anapatikanaje Simba, Yanga!

Yamal Pict
Yamal Pict

Muktasari:

  • Miaka 17 tayari ameshatwaa taji la Euro. Miaka 17 dunia inamuimba. Huku kwetu ndio maana tunadanganya miaka. Hauwezi kumpeleka mtoto mwenye umri wa miaka 17 akaimba wimbo wa taifa tayari kwa ajili ya kuliwakilisha taifa.

KWAMBA kuna uwezekano wa mtoto wa Kitanzania katika umri wa miaka 17 akafanya mambo kama ya Lamine Yamal? Ni jambo gumu kufikirika. Amezaliwa Julai 2007 na tayari ni staa wa soka duniani kote. Kwetu sisi ni ngumu kumpata Lamine Yamal.

Miaka 17 tayari ameshatwaa taji la Euro. Miaka 17 dunia inamuimba. Huku kwetu ndio maana tunadanganya miaka. Hauwezi kumpeleka mtoto mwenye umri wa miaka 17 akaimba wimbo wa taifa tayari kwa ajili ya kuliwakilisha taifa.

Mtoto mwenye umri wa 17 hatujui yuko wapi. katika umri wa miaka sita tu Barcelona walikuwa wamemuona Lamine katika klabu ya utotoni wakamchukua na kumpeleka La Masia. Simba na Yanga wanamjua mtoto mwenye miaka sita mwenye kipaji alipo? Wana uchunguzi wa watoto wenye vipaji wa umri huo?

Na hata wakimuona watampeleka wapi?. Sisi mchezaji ana kipaji ana miaka 17 na bado hatujamuona. Lini tunaweza kumuandaa kwa mabadiliko ya mwili na akili? Lamine Yamal amefanyiwa mabadiliko makubwa ya mwili na akili kuweza kushindana.

Y 03
Y 03

Halikuwa jambo la kipaji peke yake. kulikuwa na suala la kuubadilisha mwili wake kiushindani. Hapa ndio kuna suala la chakula na aina fulani ya mazoezi. Lamine wa Tanzania anaishi katika umaskini uliopitiliza kiasi kwamba ni vigumu kwao kuwa na milo mitatu.

Soka ni mchezo wa watu maskini. Ni ngumu kumpata mchezaji wa maana pale Masaki. sio kwamba hakuna wachezaji, baba zao wamechagua watoto waende shule za kimataifa kwa ajili ya kuwaandaa kwa kazi nyingine. Sio soka.

Hawa ndio watoto ambao walau wangeweza kutusaidia katika suala la lishe na huduma bora kutoka katika familia. Hata hivyo wazazi wao wengi wanaamini kwamba itakuwa ni kujihatarisha kama watachagua kazi ya soka. Huku kwa watoto maskini Mwananyamala na Temeke ndipo wanasoka huwa wanatokea lakini makuzi yao yanakuwa yamezingirwa na hali ngumu. Hali ambayo inadumaza mwili na akili.

Klabu pia haiwezi kumuhudumia kwa ada ya shule wala chakula cha nyumbani. Tupo bize na kusaka wachezaji ambao wataweza kutupa ushindi leo katika uwanja wa taifa. Akili yetu kubwa ni kwa wachezaji waliopo Bunju na Kigamboni.

Y 01
Y 01

Ni ngumu kwa Lamine wa Tanzania kuwa katika programu maalumu ya kukuza mwili wake na akili yake. kuwa tayari katika ushindani wa hali ya juu ndani ya miaka 17 tu.  kwa wenzetu ni jambo linalowezekana kwa sababu wanaandaa wachezaji tangu wakiwa na miaka sita.

Zaidi ya kila kitu ni kwamba wenzetu wana mechi nyingi za vijana ambazo zinamfanya mchezaji kuwa tayari kisoka katika umri mdogo. Kuna Ligi za watoto, halafu kuna Ligi za vijana. Hapa katika Ligi za vijana kuna ligi za ndani na Ligi za nje.

Vijana wa Ulaya chini ya umri wa miaka 17 wameshazurura sana kucheza Ligi za Ulaya na nyinginezo. Wanapata ushindani wa maana kila wikiendi kiasi kwamba wanapopandishwa kikosi cha wakubwa, huku misuli yao ikiwa imeongezeka, linakuwa jambo rahisi kwao kwenda sambamba.

Huku kwetu wachezaji wetu wanajilea wenyewe. Wana safari ndefu. Viwanja ni vibovu. Lishe ni duni. Walimu hawana utaalamu wa kutosha. Klabu hazina programu za uhakika za kumkuza kijana. Itafute timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17.

Y 02
Y 02

Kuna wachezaji wanaotoka katika timu za Ligi Kuu? Hapana. TFF inapambana kusaidiana na Academy mbalimbali kwa ajili ya kuwapata vijana hao.

Wenzetu wakiita timu za vijana chini ya umri wa miaka 17 utasikia wachezaji wametoka Marseille, PSG, Inter Milan, Manchester United na kwingineko. Sisi TFF ikiita vijana chini ya umri wa miaka 17 utasikia wachezaji wanatoka Kwimba Academy, Newala Academy pamoja na Academy yao wenyewe TFF.

Safari ya Lamine Yamal wa Tanzania ni ngumu na yenye misukosuko mingi. Sio Tanzania pekee, bali nchi nyingi za watu weusi safari ya Lamine Yamal wetu inakuwa ngumu. Haishangazi kuona wachezaji wengi wa Kiafrika wamedanganya umri.

Mchezaji anakuwa tayari kupambana akiwa na umri wa miaka 25. Wakati huo atalazimika kudanganya ana umri wa miaka 19. Na hapo bado anakuwa hajakomaa kisawasawa na huwa tunamuita kinda. Ukikunjua historia ya maisha yake haifanani na miaka 19. Lakini Yamal katika umri wa miaka 17 historia yake haijapindapinda. Ni kwa sababu ameandaliwa vema.

Sababu nyingine kubwa ambayo inatufanya tusimuandae Yamal wetu ni kutoamini kwamba tunaweza kufanya biashara katika soka. Klabu kibao zinaandaa wachezaji tangu wakiwa dogo lengo kubwa sio tu kwamba wakaitumikie timu ya kwanza, bali pia kuwauza kwa pesa nyingi ambazo zitaendeleza bajeti nyingine za klabu.

Kuna vitalu vingi ambavyo vimesababisha klabu kama Ajax Amsterdam, Porto, Benfica, na wengineo wengi kuendelea kuwa imara kipesa. Zinazalisha vijana wengi wenye vipaji na katika hesabu rahisi ni kwamba gharama ya kuwaandaa ni kubwa lakini hata hivyo ukiuza vijana wawili kwa pauni 15 milioni tu unaendelea kuhudumia vijana wengi. Ni biashara kama zilivyo biashara nyingine.