KIJIWE CHA SALIM SAID SALIM: Scolari kocha anayeamini anachokiamini
UNAWEZA ukawa mwanafunzi anayefanya vibaya darasani, lakini ukaja kuwa mwalimu mzuri. Sio kawaida, ila inatokea, watu wanafanikiwa kwa sababu yako, ulivyowafundisha darasani licha ya kuwa hukuwa unafanya vizuri kipindi unasoma.
Ni sawa na kwenye soka, wapo makocha ambao wanatajwa hawakuwa na soka zuri enzi wanacheza, lakini kwenye ukocha wamezifanya timu nyingi kubeba mataji. Kazi zao zinaheshimika.
Luiz Felipe Scolari, ni mmoja wa makocha ambao hawakucheza soka zuri. “Ondoa huo mguu wa mbao,” ni kauli za kebehi alizozipata kila alipoingia kucheza nafasi yake ya beki.
Kocha huyu raia wa Brazil na Italia, kwa sasa ni ana miaka 71 na ameendelea kuwa mmoja wa makocha bora na wanaopendwa zaidi duniani.
Kebehi ya ‘Ondoa huo mguu wa mbao’ ilitokana na kushindwa kumiliki vyema mpira na kila alipoupata alibutua mbele na si kuuchezea.
Hata hivyo, kumbukumbu za Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) zinaonyesha Scolari aliyeanza kufundisha soka mwaka 1982, ndiye kocha aliyefundisha timu nyingi zaidi, za klabu na timu za taifa zikiwamo Brazil na Ureno.
Ameweka rekodi ya kufundisha timu nyingi kubwa kuliko makocha 20 (nyingine zaidi ya mara moja) kutoka mataifa ya Ulaya, Uarabuni, Asia, China na Amerika ya Kusini bila kujali hali zao za uchumi.
Kocha huyo ambaye wazazi wake wana asili ya Ureno, alizaliwa Novemba 9, 1948 katika Mji mdogo wa Passo Fundo, Brazil na alichezea klabu za madaraja ya chini kuanzia mwaka 1966 hadi 1981.
Alianza kufundisha soka 1982 na klabu yake ya kwanza ilikuwa CSA ya Brazil na baadae timu nyingine ndogondogo hadi 1985 alipoajiriwa na Al-Shabab ya Saudi Arabia.
Baada ya muda mfupi alirudi Brazil kuifundisha klabu ya Gremio iliyokuwa katika hali mbaya na kuiwezesha kutwaa ubingwa wa Jimbo la Faucho 1987.
Kuanzia hapo alikwenda Kuwait kujiunga na Al Qadisiya kwa mkataba wa miaka miwli na kutwaa Kombe la Mfalme mwaka 1989.
Kutokana na mafanikio hayo, alichaguliwa kuwa kocha wa muda wa nchi hiyo na kuiwezesha kutwaa kombe la Nchi za Ghuba’.
Hata hivyo, ilimlazimu kuondoka Kuwait baada ya majeshi ya Rais wa Iraq, Saddam Hussein kuivamia nchi hiyo.
Alirudi Brazil na kuajiriwa na klabu ya Criciuma na kuipa kombe la Copa do Brasil kabla ya kutimkia Afrika Kaskazini, nchini Misri na kuifundisha Al Ahly.
Hata hivyo, muda mfupi baada ya kumalizika kwa vita vya Ghuba, Scolari alirejea Kuwait na kujiunga tena na Al Qadisiya, kabla ya kurejea Brazil na kuifundisha klabu ya Palmeiras na kubeba makombe matatu yakiwemo, Copa do Brasil, Mercosur na Copa Libertadores na kuifikisha fainali ya Kombe la Mabingwa wa Mabara mwaka 1999, licha ya kufungwa na Manchester United.
Kutokana na kuifikisha Palmeiras fainali, alichaguliwa kuwa kocha bora wa Bara la Amerika ya Kusini mwaka huo.
Moja ya sifa yake kubwa ni kutokukaa na timu muda mrefu na aliwahi kukataa mkataba wa miaka miwili na kusaini mmoja na klabu ya Crizeiro ya Brazil mwaka 2000.
“Nikiwa mwalimu hupenda kuzunguka kama pia au anavyofanya mchezaji kiwanjani. Haya ndio maradhi yangu na naomba wanaonipenda na wanaonichukia wanivumilie,” akikaririwa maneno hayo kutokana na kutodumu kwake na timu kwa muda mrefu.
Juni 2001, Scolari alikabidhiwa timu ya taifa ya Brazil iliyokuwa imebakisha michezo mitano ikiwa katika hatari ya kutokufuzu kucheza Fainali za Kombe la Dunia na ingekuwa ni mara ya kwanza kushindwa kufanya hivyo.
Hata hivyo, licha ya kufungwa bao 1-0 na Uruguay katika mchezo wake wa kwanza, alifanikiwa kuifikisha fainali na kufuzu Kombe la Dunia zilizofanyika Korea Kusini na Japan mwaka 2002.
Kazi ilikuwa kwenye kuita kikosi cha Brazil na alimwacha mshambuliaji kinara wa timu hiyo, Romario licha ya shinikizo kutoka kwa wadau mbalimbali wa soka.
Hata hivyo, hakujali presha ya wadau na mashabiki wa Brazil ambao walikuwa wanasubiri waone atafanya nini bila uwepo wa Romario.
Katika fainali hizo Brazil ilizifunga Uturuki, China, Costa Rica, Ubelgiji, England na Uturuki kwa mara ya pili kisha, kisha kufika fainali dhidi ya Ujerumani na kutwaa ngombe la Dunia, huku nyota wake Ronaldo De Lima akiibuka shujaa Brazil ikishi9nda mabao 2-0 na kubeba taji la tano.
Mwaka 2003, magazeti yaliuliza hatma ya kocha huyo baada ya kuachana na Brazil, wapi atakwenda kwani hakuwa anatulia na timu moja. Hatimaye aliibukia timu ya taifa ya Ureno na kukaa nayo kwa muda mrefu hadi 2008 alipojiuzulu baada ya kufungwa mabao 3-2 na Ujerumani katika mzunguko wa pili wa Kombe la Ulaya.
Mafanikio akiwa na Ureno ni kuifikisha fainali za Kombe la Ulaya mwaka 2004 na ilifungwa na Ugiriki 1-0 katika fainali.
Baada ya kuondoka Ureno mwaka 2008, haikuchukua muda akaajiriwa kuifundisha klabu ya Chelsea ya Ligi Kuu England Julai 1, 2008 na kuwa kocha wa kwanza kushinda Kombe la Dunia na kuifundisha klabu inayoshiriki Ligi Kuu England na awali ilikuwa akaifundishe Manchester City ila alikataa.
Scolari alitimuliwa Chelsea mwaka mmoja baadaye (Februari 2009) kutokana na matokeo mabovu na alinukuliwa akisema.
“Nimekutana na wababe wenzangu. Mimi sikai kwa muda mrefu na Chelsea nayo ni hivyo hivyo. Wamenifukuza kabla sijawakimbia.”
Juni 2009, Scolari aliingia mkataba wa miezi 18 na klabu bingwa ya Uzbekistan, Bunyodkor wenye thamani ya Dola 13 milioni kwa mwaka, ingawa aliachana na klabu hiyo Mei, 2010 baada ya kushindwa kuingia fainali za Kombe la Mabingwa la Bara la Asia.
Alipotimulia alisema, “Wamefanya vyema kunitimua kwa sababu watanipa nafasi ya kumshughulikia mtoto wangu kusoma badala ya kushughulikia watoto wa wenzangu kucheza soka.”
Haikumchukua muda mrefu kwani aliporudi Brazil alijiunga tena kuifundisha Palmeiras Juni, 2010, kwa mkataba wa miaka miwili na kuiwezesha kubeba kombe la Copa do Brasil, hata hivyo, aliachana nayo baada ya matokeo mabaya Septemba 2012.
Baada ya kukaa kwa miezi miwili bila ya imu, Scolari alichaguliwa kocha wa Brazil Novemba 28, 2012 kutokana na umahiri wake.
Hata hivyo, ni kocha mwenye hasira na hapendi kuingiliwa na viongozi na huwa hachukui muda kuachana na timu, huku kuna wakati huwaambia viongozi wanaomwingilia majukumu yake waingie uwanjani wafundishe wao.
Tabia yake ya kutopenda kuingiliwa inapendwa na wachezaji ambao husema ni watoto wake na anataka aachiliwe mwenyewe awalee.
Hata hivyo, licha ya kustaafu miaka mitatu iliyopita, ila ghafla mwaka jana alirudi uwanjani kuifundisha Atletico Minieiro ya Brazil kwa mkataba unaomalizika mwishoni mwa mwaka huu.