Ambundo: Si mchezo Yanga kuna vita nzito

Friday October 15 2021
ambundo pic
By Thomas Ng'itu

WINGA Dickson Ambundo wa Yanga ni miongoni mwa wachezaji wenye uwezo wa kucheza pande zote mbili kushoto na kulia uwanjani na kufanya umuhimu wao uonekane.

Ambundo ambaye amesajiliwa msimu huu akitokea Dodoma Jiji alikoonyesha ubora na kuwafanya mashabiki wa soka nchini kuvutiwa naye kisha Yanga wakampa mkataba wa miaka miwili.

Winga huyo ana kazi ya kufanya kwenye kikosi hicho kutokana na kuwania namba na nyota kama Yacouba Songne, Farid Mussa, Jesus Moloko, Yusuph Athuman na Deus Kaseke.

Mwanaspoti lilifanya mahojiano na winga huyo ambaye kwa sasa anasumbuliwa na majeraha ya mkono aliyoyapata kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya DTB.


KUPIGANIA NAMBA

Advertisement

Katika kikosi cha Yanga kumeonyesha kuna vita kubwa ya namba inayomfanya kocha Nassredine Nabi awe na wigo mpana wa kupanga kikosi.

Ambundo anaweka wazi kuwa kuna changamoto ya namba, lakini mpaka anajiunga na Yanga alikuwa ameshajiandaa kwenda kupigania.

“Changamoto ni kubwa ukiangalia kila mchezaji anahitaji kucheza. Kama mchezaji inatakiwa kupambana kuhakikisha napata nafasi na hata nikikosa, basi nitakapopewa nionyeshe (uwezo),” anasema.

“Nadhani inatakiwa kutuliza akili na kukubaliana kitakachotokea, maana mpira unachezwa wazi.”


TOFAUTI KENYA, TANZANIA

Ambundo ni miongoni mwa wachezaji waliocheza soka la kulipwa nje ya nchi, akiwahi kutumikia kikosi cha Gor Mahia ya Ligi Kuu Kenya iliyoshiriki pia Ligi ya Mabingwa Afrika.

Anasema kuna tofauti kubwa ya ligi ya Tanzania na Kenya kutokana na mechi nyingi nchini kuonyeshwa kwenye runinga tofauti na Kenya.

“Hapa mechi zote zinaonyeshwa tofauti na Kenya kwa sababu kule utaona chache. Wachezaji tunahitaji tuwe na video ili zikusaidie. Kuna watu wanataka kukuona, basi unawatumia na kiufupi sisi tuna Ligi bora,” anasema Ambundo.


ANAVYOLIISHI SOKA

Wachezaji wengi nchini wanapata maisha kupitia soka na hilo lipo wazi kutokana na namna ambavyo wadhamini wanamiminika na kuzifanya timu kuwa na pesa kuwalipa mishahara na usajili.

Ambundo ambaye amepita katika timu za Mbao, Alliance, Gor Mahia na Dodoma Jiji anasema ni miongoni mwa wachezaji ambao wamenufaika kupata pesa zinazoendesha maisha yake. “Kwa kiasi chake imenilipa ukiangalia mpaka sasa familia inapata ugali, nashukuru Mungu,” anasema.


YANGA NI NJIA TU

Wachezaji wengi wa soka nchini wana ndoto ya kutoka na kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, lakini kwa upande wa Ambundo alicheza nje kisha akarejea tena nyumbani.

Ambundo anasema licha ya kwamba amerejea nchini bado hajakata tamaa ya kucheza soka la kulipwa nje kwani anaamini kabisa uwezo huo bado anao.

“Yanga kwangu ni njia ya mafanikio. Naamini nipo sehemu sahihi ya kunifanya kufika eneo ambalo nalitaka,” anasema mchezaji huyo.

Ambundo ni miongoni mwa wachezaji waliotoka nje na kurejea nchini kama walivyo kina Elias Maguri, Salum Chuku, Abdi Banda na wengineo.

Advertisement