SIMULIZI YA HADITHI: Machozi ya mshumaa -1
Muktasari:
- “Kwa kweli mi’ sikufahamu ni wazi umetuma ujumbe ‘wrong number’ inaonyesha kabisa ulikuwa na matatizo mazito na mpenzi wako. Lakini nashukuru Mungu umeweza kuachana na mawazo...
KARIBUNI... Hakuna anayejali maumivu ya mshumaa unaomwaga machozi ambayo huwafurahisha watu kwa kusambaza mwanga unaoangaza pande zote bila kujua kila chozi linalodondoka huwa lina maumivu makali yanayochangia mauti yake. Watu wengi wamekuwa wahanga wa mapenzi ambao kila kukicha macho yao yamekuwa yakidondosha machozi huku wakiwa na maumivu makali mioyoni mwao baada ya kuumizwa na mapenzi. Wengi walioteketea kwa kushindwa kuvumilia machozi kupelekea kupotea kwenye sura ya dunia na kubakia na simulizi kama mshumaa ulioteketea kwa kuwamulikia watu, lakini hakuna anayejali maumivu yake. Kama kuna mtu angesikia kilio cha mshumaa hakika asingefurahia mwanga wake, bali angeuhurumia kwa maumivu unayosikia kutoa mwanga huku ukiteketea. Kila mtu aliye ndani ya uhusiano atakiri mapenzi ukiyakosea yanaumiza, yanatesa na yanaua. Lakini waliopata bahati ya kupenda panapopendeka huiona pepo kabla ya kifo. Ndani ya riwaya hii kuna maumivu makali yenye kutoa machozi kama mshumaa ambayo yatakufanya uheshimu machozi ya mshumaa na hutakubali kufurahia mwanga wake, bali kuutunza mshumaa wako ili usimwage machozi na kukufanya ufurahie mwanga bila kudondosha machozi. Ili kuisikia sauti ya mshumaa na thamani ya machozi yake naomba unipe muda wako ili upate kitu kitachokufanya uyaheshimu machozi ya mpenzi wako...TWENDE PAMOJA
KUTOKANA na Abby kurudi kutoka katika mihangaiko yake ya kutwa nzima akiwa amechoka sana, baada ya kuoga kwa kuwa alikuwa amekwisha kula kabisa alijitupa kitandani na usingizi mzito kumchukua. Alilala kama mfu, hata simu yake ilipopigwa mara nyingi hakuisikia. Alishtuka siku ya pili alfajiri aliposhika simu yake alishtuka kukuta kuna ‘missing calls’ zaidi ya ishirini zote za namba moja. Pia kulikuwa na ujumbe mfupi zaidi ya tano wote wa namba moja ambayo ilikuwa ngeni kwake.
Kabla ya kupiga simu alisoma kwanza ujumbe uliotumwa kwake: Wa kwanza ulisomeka: Mpenzi nakupenda sana sijawahi kumpenda mwanaume chini ya jua hata kama hunitaki pokea simu zangu naomba unisikilize hata sekunde moja kisha nipo radhi na uamuzi wako.
Ujumbe wa pili: Mpenzi ni kweli umeamua kunizika ningali hai. Uamuzi wako umekuwa wa ghafla sana. Ulichofanya sawa na kuupasua moyo wangu kwa kisu butu bila ganzi, ukimya wako ni hukumu yangu ya kifo mimi ni marehemu mtarajiwa.
Ujumbe wa tatu ulisomeka: Najua umeamua, ila nakuomba usiache kuhudhulia mazishi yangu.
Ujumbe wa nne ulisema: Nakufa nikiwa nakupenda sana sitapenda mwanaume yeyote chini ya jua mpaka nafufuliwa.
Abby baada ya kusoma ujumbe wote alijikuta akichanganyikiwa na kuamua kupiga simu japokuwa namba ilikuwa ngeni. Pia hata ujumbe ule ulikuwa mgeni kwake. Baada ya kupiga simu iliita kwa muda na kupokewa upande wa pili.
“Haloo.”
“Ooh! Afadhali,” Abby alishusha pumzi ndefu baada ya kupokewa upande wa pili na kuamini mwenye simu mpaka anapokea, basi Mungu mkubwa amesitisha kujitoa uhai wake. Aliamini ile ilikuwa kutingisha kiberiti kwa mpenzi wake, lakini hakuwa na lengo la kujiua. Pamoja na kuwaza vile bado hakumjua aliyetuma ujumbe ule ambao aliamini ulikuwa umekwenda kwake kimakosa.
“Afadhali ya nini?” upande wa pili uliuliza.
“Dah! Nashukuru Mungu kubadili mawazo mabaya ya kujiua.”
“Kujiua? Wewe ni nani?” sauti ya upande wa pili iliuliza kwa mshtuko.
“Kwa kweli mi’ sikufahamu ni wazi umetuma ujumbe ‘wrong number’ inaonyesha kabisa ulikuwa na matatizo mazito na mpenzi wako. Lakini nashukuru Mungu umeweza kuachana na mawazo mabaya.”
“Ha! Kumbe ndivyo ilivyokuwa, kumbe alitumia simu yangu bila kujua.”
“Mungu wangu. Sasa huyo shoga yako yupo wapi?”
“Ni kweli jana alitimiza dhamira yake ya kuutoa uhai wake.”
“Jamaniii! Mbona kuna wanaume wana roho mbaya, unawezaje kumwacha mpenzi wako atoe roho yake kwa ajili yako, makosa yanasameheka ndiyo maana penseli imewekewa ufutio kwa vile wanajua kuna kukosea na kusahihisha.”
“Kaka wee! Dunia yote ingekuwa na wanaume kama wewe ingegeuka pepo ya dunia.”
“Kwani msiba upo wapi, kama ni karibu nije nizike.”
“Jambo la kushukuru tulimuwahi kabla hajajidhuru zaidi, kwa sasa tupo hospitali na sasa anaendelea vizuri.”
“Ooh! Afadhali. Asante Mungu kumuokoa mja wako, mpo mkoa gani?”
“Mwanza.”
“Ooh, Hata mimi nipo Mwanza mpo hospitali gani nije nimuone?”
“Tupo Aga Khan.”
“Ngoja nije nimuone kama angekufa ningeumia sana japo simjui ila ujumbe wake umeniumiza sana.”
“Sawa.”
Baada ya kukata simu Abby alishusha pumzi ndefu na kumshukuru tena Mungu kuyaokoa maisha ya msichana aliyeamini hana hatia. Alikwenda kuoga kisha alibadili nguo na kutoka kuwahi hospitali. Alipitia super market kununua vitu vya mgonjwa japokuwa alikuwa hamjui.
Alikodi teksi moja kwa moja hadi hospitali ya Aga Khan. Baada ya kuteremka kwenye teksi alipiga simu na kuelekezwa kuwa atamkuta mwenyeji wake nje ya wadi ya wanawake. Alielekea upande wa wadi ya wanawake na kumkuta binti mrembo ambaye alimchanulia tabasamu pana baada ya kuamini ndiye mgeni wake.
“Karibu, mgeni wetu?” Sheila alimkaribisha Abby.
“Ndiyo, asante.. Vipi mgonjwa?”
“Hajambo kiasi, twende ukamuone,” Sheila alisema huku akipokea mfuko wa vitu vilivyoletwa na kumuachia maua ambayo alijua wa kumpa ni yeye mwenyewe. Mlango ulifunguliwa na kuingia ndani kilikuwa chumba cha mtu mmoja.
Walimkuta mgonjwa amepitiwa usingizi macho ya Abby yalimuona binti mrembo amejilaza kitandani na kujiuliza unawezaje kukubali ua kama lile la kupamba dunia liondoke hivihivi. Sheila alimsogelea na kumtikisa kidogo. Zawadi alifumbua macho na kukutana na mwanaume mgeni mbele yake.
Bila kusema neno alimtazama kwa muda huku akiilazimisha akili yake kumtambua aliyekuwa amesimama pembeni ya kitanda akiwa na maua mkononi, bila kupata jibu ni nani. Alitamani yule aliyesimama na maua angekuwa mpenzi wake Jimmy, basi angepiga kelele ya furaha.
“Pole,” Abby alimpa pole Zawadi ambaye bado alikuwa njia panda.
“Asante,” alijibu kwa sauti ya chini yenye kusikika huku akijiinua na kukaa kitako.
Abby alimpa maua Zawadi ambaye aliyapokea huku akishukuru.
“Asante kaka yangu,” Zawadi alishukuru huku akiwa bado anamtazama yule kaka mtanashati tena maridadi.
“Mrembo thamani ya mtu si kwa mtu mmoja, bali dunia nzima.” Abby alimsemesha Zawadi kwa sauti adimu ambayo inaweza kuzimisha dunia inayowaka moto.
“Ni kweli lakini moyo una nafasi moja ya upendo pia hakuna mzani sawa wa upendo.”
“Ni kweli kabisa, lakini mbegu ya upendo humea kwenye udogo wenye rutuba ya mapenzi kamwe hauoti kwenye jiwe.”
Kauli ile ilimfanya Zawadi amkazie macho yake makubwa kidogo yule mwanaume ambaye alikuwa hamjui na kuuliza kwa sauti ya juu kidogo.
“Unamaanisha nini?”
“Kabla sijakujibu nilitaka kujua kwa nini binti mrembo kama wewe kuchukua uamuzi mzito kama huu?”
“Siamini hata kama nitakueleza kila kitu unaweza kutatua tatizo langu. Siku zote kila aliae hushika kichwa chake na maumivu ya moyo hayana wa kuyapokea zaidi ya wewe mwenyewe.”
“Kwa kauli yako ni sawa lakini inasambaa na kuwaumiza wapendwa wao, unafikiri wangapi wangeumia kwa uamuzi wako wakati aliyesababisha hajui maumivu yako anaendelea na starehe zake wala hagongwi na mshipa wa kichwa.”
“Mmh! Kwanza kabla ya yote nataka kujua wewe ni nani mbona sijawahi kukuona kabla?”
Zawadi alitaka kumjua alitaka kumjua mwanaume aliyesimama pembeni yake mwenye maneno aliyoyatamani kuyasikia kwa kipenzi chake Jimmy, Abby alimweleza kilichosababisha yeye kuwa pale.
“Pamoja sikujui lakini niliumia sana kutokana na jumbe zako kuonesha umeumizwa sana. Ningeumia zaidi kama ungepoteza maisha kwa ajili ya mapenzi ya mtu asiyejua thamani ya upendo wako kwake. Wapenzi wengi hawathamini upendo wa watu wanaowapenda sawa na kufurahia mwanga wa mshumaa kwa kutothamini machozi yake ambayo huwa maumivu ya kuteketea kwake.”
“Ooh! My God, Pole kwa usumbufu niliokusababishia, nina imani haina maana pia sioni muhimu wa kumuhadithia kila mmoja kwa vile kila nikimaliza maumivu yanaanza upya. Nimeapa sitalizungumzia tena bali namuachia Mungu,” Zawadi alisema kwa sauti ya chini lakini tamu kama kinubi cha Mtume Sauli.
“Mrembo hujui ni kwa nini ujumbe ule umekuja kwangu, siku zote Mungu ana mkusudio yake. Siku zote kuyaifadhi maumivu moyoni ni sawa na kutengeneza sumu sawa na damu chafu itengenezayo jipu. Nifanye kama ndugu yako tubadlishane mawazo ili kuiondoa sumu moyoni mwako ili uitambue thamani yako chini ya jua.”