SIMULIZI YA HADITHI: Jana dume -6

Muktasari:

  • Nikakumbuka ile methali ya Kiswahili isemayo “Hamadi kibindoni, silaha ni iliyo mkononi.” Nikajiambia kwa wakati ule Smith ndiye aliyekuwa mkononi na ndiye ambaye ningeweza kumtumia.

Yule mzungu ameniahidi kuwa naweza kuvipata vyote kama nitakubali kuwa naye. Sikuona kama kulikuwa na kikwazo cha kuwa naye. Mwanaume ambaye tuliahidiana kuja kuoana hakuwa amenichumbia na inawezekana akapata msichana mwingine na akabadili mawazo yake. Mwanaume si wa kumtegemea sana.

Nikakumbuka ile methali ya Kiswahili isemayo “Hamadi kibindoni, silaha ni iliyo mkononi.” Nikajiambia kwa wakati ule Smith ndiye aliyekuwa mkononi na ndiye ambaye ningeweza kumtumia.

Baada ya kuwaza kwa dakika kadhaa nilinyanyuka na mkoba wangu uliokuwa na Dola 4,000 yaani sawa na Shilingi milioni kumi na laki tatu na upuuzi na kuingia nao chumbani. Nilizifungia zile pesa kwenye kabati. Wakati nataka kubadili nguo nilizokuwa nimevaa, simu yangu ikaita.

Nilipoitazama nikaona namba ya Dachi, nikaipokea.

“Hello Mr Dachi…!”

“Ndio ninatoka hapa hotelini.” Dachi akaniambia kwenye simu.

“Mimi niko nyumbani, nimepumzika kidogo.

“Nilidhani unanifikiri mimi.”

“Wewe nimeshakufikiria.”

“Kwa hiyo umeshapanga utakuja lini nyumbani kwangu?’

“Nitakuja kesho.”

“Nitafurahi sana kukuona. Utakuja saa ngapi?”

Saa moja usiku.”

“Ukitaka kuja unifahamishe.”

“Nitakupigia simu.”

“Sawa.”

                                        *****

Asubuhi ya siku iliyofuata nilipotoka nyumbani nilikwenda benki nikaweka shilingi milioni saba katika akaunti yangu. Shilingi milioni tatu nilibaki nazo mkobani mwangu.

Nilipotoka benki nilizunguka katika maduka mbalimbali nikajifanyia shopping ya Shilingi milioni mbili. Baada ya kununua kila kitu nilichohitaji nilikodi teksi iliyonirudisha nyumbani Sinza.

Niliingia chumbani mwangu nikazijaribu nguo nilizonunua pamoja na viatu. Nikaona zilikuwa sawa. Nilichukua wigi ambalo nililinunua kwa shilingi laki tatu nikaenda saluni kupachikwa wigi hilo.

Nilipotoka saluni nilikwenda kumtembelea dada nyumbani kwake. Baada ya kusalimiana naye aliniambia.

“Umependeza leo!”

“Kwa sababu ya hili wigi?” Nikamuuliza.

“Nalijua bei yake, bila laki tatu hulitoi dukani.”

“Ni kama hivyo, nimepata mchumba wa kizungu ndiye anayenipendezesha.”

“Usiniambie!”

Nikamdokeza dada kuhusu uhusiano wangu na yule mzungu.

“Awe na nia kweli ya kukuoa, asikudanganye akakuchezea kisha akaja kukuacha.” Dada akaniambia.

“Atanichezea mimi, atajichezea mwenyewe! Mi shida yangu nimle tu kwa sababu nimeona pesa yake iko nje nje.”

“Kama ni kumla umle taratibu. Kama una pupa kama hivyo utajikuta unaliwa wewe!”

“Kwanza yule mtu mwenyewe naona kama ana nia njema na mimi, sijui lakini. Bado naendelea kumchunguza.”

Niliendelea kuzungumza na dada hadi jua lilipokuchwa nikaondoka kurudi nyumbani kujiandaa kwenda kwa mzungu wangu.

Baada ya kuvaa nguo nilizopenda nitoke nazo nikampigia simu kumjulisha kuwa ninakwenda kwake. Akaniambia kwamba ananisubiri.

Nakumbuka ilikuwa saa kumi na mbili na nusu nilipotoka nyumbani. Nilikodi teksi iliyonipeleka katika hoteli ya Lux ambayo mzungu huyo alikuwa amepanga chumba.

Nilipofika nilimpigia tena simu, akaniambia alikuwa chumba namba 35. Nikaenda. Kilikuwa ghorofa ya kwanza. Nilipomaliza kupanda ngazi nilianza kukitafuta chumba namba 35. Nikakiona. Nikaenda kubisha mlango.

Kitu kilichonishangaza ni kuwa licha ya kubisha mlango kwa sekunde kadhaa sikupata jibu. Nikaujaribu mlango ambao ulifunguka, nikaingia ndani. Dachi mwenyewe hakuwemo chumbani ila niliona sauti yake kwenye kitanda. Sikujua alikuwa ametoka au yuko bafuni.

Nikajaribu kufungua mlango wa bafuni. Nilichokiona kwenye macho yangu kilinipasua moyo na kunifanya niache mdomo wazi kwa mshituko.

Nilimuona Dachi amesimama akioga. Alikuwa mtupu kama alivyozaliwa. Kwa vile alielekea upande uliokuwa na mlango wa bafu nilimuona wazi wazi.

Kitu cha kwanza kilichonistaabisha ni ule weupe uliokuwa kwenye ngozi yake, haukuwa weupe wa kawaida na haukuwa weupe niliozoea kumuona nao ninapokutana naye. Ulikuwa weupe uliopitiliza! Isitoshe ngozi yake iliota manyoya marefu kama ngozi ya mnyama. Manyoya hayo yalimuota mwili mzima kwenye miguu, kwenye mikono, kwenye shingo na kwenye kifua na tumbo ndio kulikuwa na msitu kabisa!

Yalikuwa manyoya meupe kama yaliyopakwa rangi. Kwa vile manyoya hayo yalikuwa yameingia maji yalikuwa yamelala kwenye ngozi na kuonekana kama ya nyani mzee aliyenyeshewa na mvua.

Kioja hakikuwa hicho tu, macho yake ndiyo yaliyotisha zaidi. Yalikuwa kama ya paka mwitu yakiwa na mboni zilizounda mstari mwembamba wa kijivu halafu yalitoa nuru kali kama yalikuwa yanawaka.

Bado. Kucha zake za miguu na mikono zilikuwa ndefu kama kucha za kubandika. Yaani hazikuwa tofauti na mnyama.

Niliogopa. Nikajiambia, kumbe huyu mzungu yuko hivi! Huyu ni jini si binaadamu!

Nikaufunga ule mlango haraka. Nilikimbilia kwenye mlango wa chumbani nikaufungua na kutoka mbio!

Nilishuka ngazi mbili mbili hadi nikafika chini. Nikatoka nje ya ile hoteli huku nikishukuru Mungu kuwa nimenusurika.

“Yule jini angenifyonza damu leo!” Nikajiambia.

Macho yangu yalikuwa yakiangaza huku na huku kutafuta teksi.

Kwa vile nilikuwa natetemeka kwa hofu mpaka makalio yangu yalikuwa yanacheza. Magoti nayo yalikuwa yakininyong’onyea, yaani nisingeweza tena kutembea kwa miguu. Ningeanguka tu.

Nikaiona teksi. Lakini wakati naifuata nilisikia nikiitwa nyuma yangu.

“Enjo!”

Nilipogeuka nyuma nikamuona yule mzungu amenifuata nje ya hoteli akiwa amevaa suti yake, sasa akionekana wa kawaida tu.

“Enjo hebu simama, unakwenda wapi sasa?” Dachi akaniuliza.

Nilijuta kugeuka nyuma. Kwa kweli sasa nilikuwa namuogopa yule mzungu. Nikageuza uso wangu haraka kuelekea mbele. Nilikuwa nimeshaifikia ile teksi. Dereva alishanifungulia mlango wa nyuma.

“Ingia twende!” Akaniambia.

Nikajipakia huku nikitetemeka. Mwili ulikuwa umeishiwa nguvu kabisa.

Wakati nafunga mlango nilimuona Dachi naye akifuata teksi.

“Nikupeleke wapi?” Dereva wa teksi niliyojipakia akaniuliza.

“Nipeleke Sinza.”

Teksi ikaondoka.

Nilipomtazama tena yule mzungu kwenye kioo nilimuona akipanda teksi.

“Anakwenda wapi?” Nikajiuliza hofu.

Baada ya muda kidogo niligundua kuwa alikuwa ananifuata mimi. Teksi aliyopanda ilikuwa nyuma ya ile teksi niliyopakiwa.

“Mama yangu…leo nimekwisha!” Nikajiambia na kutoa simu yangu.

Nikampigia dada huku jicho langu likiwa kwenye teksi aliyopanda Dachi.

Dada akapokea simu.

“Dada kumbe yule mzungu niliyekuelezea mchana ni jini, nimemfuata hapa hoteli nikamuona bafuni anaoga lakini ana umbile la kijini. Nimemkimbia kwa teksi lakini ananifuata nyuma kwa teksi nyingine. Mwambie shemeji anifuate haraka…” Nilimwambia dada kwa sauti ya mtu aliyepatwa na hofu kiasi cha kukaribia kulia.

Tayari dada akawa amepatwa na wasiwasi. Akaniuliza tulikuwa barabara gani. Nikamwambia.

“Mumzungushe zungushe tunawafuata.” Dada akaniambia na kukata simu.

Nikafungua pochi yangu na kutoa noti tatu za shilingi elfu kumi kumi nikampa yule dereva.

“Shika hii pesa, nataka uichenge hii teksi iliyo nyuma yetu kabla hatujakwebda Sinza.” Nikamwammbia dereva huyo kisha nikamuuliza.

“Utaweza?”

Dereva aliitazama teksi hiyo kwenye kioo akaniambia.

“Kazi ndogo tu.”

Alitia gea. Teksi ikafyatuka na kuanza mbio. Alikata kona kadhaa kuikwepa teksi hiyo lakini baada ya muda kidogo tukaiona tena nyuma yetu. Tumbo lilikuwa likiniunguruma kwa kijua siku ile ulikuwa ndio mwisho wangu. Haja kubwa ilikuwa karibu kunitoka. Nilikuwa nimelikaza tumbo nisiadhirike.

“Huyu jamaa hachengeki.” Dereva wa teksi akaniambia.

“Sasa tutafanyaje?” Nikamuuliza kwa hamaki.

“Tufanye nini? Unajua mimi sijakuelewa.”

“Nilitaka tuikwepe hii teksi!”

Hapo hapo dada akanipigia simu. Nikakimbilia kupokea ile simu. Dada akataka kujua tuko katika barabara gani. Nikamtajia.

Baada ya muda kidogo nikaona gari la shemeji limetokeza mbele yetu. Lilitaka kutupita nikatoa mkono kwenye dirisha na kulipungia huku nikipiga kelele.

“Shemeji! Shemeji!”

Gari hilo likasimama pembeni mwa barabara.

“Dereva rudi nyuma ulifuate lile gari.” Nikamwambia dereva wa teksi huku nikijisikia ahueni kuliona gari hilo.

Dereva wa teksi akapunguza mwendo na kukata kona. Akalifuata gari hilo la shemeji lililokuwa limesimama.

Ile teksi iliyokuwa nyuma yetu ilipita moja kwa moja na kwenda kusimama mbele.

Kabla ya teksi kusimama sawa sawa nilishafungua mlango. Teksi ilisimama ubavuni mwa gari la shemeji. Nikashuka na kufungua mlango wa nyuma wa gari la shemeji nikajipakia haraka haraka.

Nikampungia mkono dereva wa teksi aende zake. Ile teksi ikaondoka. Shilingi elfu thelathini zangu nilizompa nikazisamehe.