Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HADITHI: Bomu Mkononi -23

Muktasari:

Mwanangu alifikia umri wa miaka minne akiwa na majina mawili. Jina la Amani alilopewa na Mustafa na jina Ramadhani alilopewa na Musa. Pia alifikia umri huo akijua kuwa ana baba wawili. Hakuweza kujua wala kuniuliza ni nani baba halisi kwa sababu bado alikuwa hana maarifa.

Sehemu ya 23

“HUYO mtoto alikuwa na tatizo gani?”

“Tumbo linamuuma lakini nimepatiwa dawa na nimeshampa.”

“Hali yake ikoje kwa sasa?”

“Kwa sasa hajambo na amepata usingizi.”

“Nimeambiwa alikuwa analia sana?’

“Jana usiku hatukulala jinsi alivyokuwa analia.”

“Ngoja nakuja.”

“Nilikuwa nataka kumpigia kawahi yeye kupiga,” nikamwambia dada wa kazi mara tu nilipomaliza kuzungumza na Mustafa. Nilikuwa nimeketi sebuleni na msichana huyo.

“Amesema alikufuata hospitalini?”

“Amenifuata, sijui amekwenda hospitali gani?’

Dada wa kazi akacheka kabla ya kuniambia.

“Alikuwa na wasiwasi, ameona atoke tu aende hospitali yoyote iliyo karibu.”

Haukupita muda mrefu Mustafa akatokea. Dada wa kazi ndiye aliyekwenda kumfungulia geti. Mustafa akaliingiza gari na kuliegesha.

Alipokuja sebuleni alichutama karibu na mahali nilipomlaza mtoto. Akakifunua chandarua chake.

“Usikifunue utaingiza mbu,” nikamwambia.

Mustafa akakifunika tena na kunitazama.

“Ni tumbo tu au alikuwa na tatizo jingine?” Akaniuliza.

“Tatizo lake lilikuwa ni tumbo tu.”

Mustafa akainuka.

“Kwani unamnywesha maji gani?” Akaniuliza.

“Maji ya chupa. Simpi maji mengine.”

“Sasa tumbo lake limechafuliwa na nini?”

“Sijui.”

Mustafa akakaa karibu yangu. Dada wa akazi akainuka na kuondoka.

“Anapata choo kizuri?” Mustafa akaniuliza.

“Tangu jana choo chake si kizuri.”


“Daktari amesemaje?”

“Amempima tu kisha amempa dawa.”

“Basi muache alale atakuwa amepata nafuu.”

Asubuhi ya siku iliyofuata Mustafa alimkagua mtoto na kumuona alikuwa mzima na mwenye afya njema.

“Amechangamka sana leo,” akaniambia.

“Zile dawa zimemsaidia sana,” na mimi nikasisitiza kuhusu dawa.

Kusema kweli sehemu kubwa ya maisha yangu ya usichana ilitawaliwa na ulaghai, utapeli na uongo huku uso wangu ukiendelea kuonyesha upole na huruma. Kama kuna watu wanafiki, mimi nilikuwa mnafiki namba moja kwani kile kilichokuwamo ndani ya moyo wangu sicho kilichokuwa kinaonekana kwenye uso wangu.

Maisha yaliendelea hivyo huku nikiyafurahia. Ule ulaghai ukawa ndio hulka yangu. Moyo wangu uliondoka woga nikawa ninajiamini hata pale ninaposema uongo.

Sikujua ilikuwaje mpaka nikabadilika kiasi kile. Ikapita miaka minne bila Mustafa wala Musa kujua kuwa nimeolewa na wanaume wawili. Nilikuwa nikiishi na kila mume kwa kupanga zamu. Huyu akisafiri naenda kwa yule.

Wakiwepo wote nabaki kwa Mustafa huku nikiendela kumdanganya Musa kuwa niko kwa shangazi au wakati mwingine nikimuaga safari ya kwenda Tanga ambako ndio nyumbani.

Musa ndiye aliyekuwa akiniamni sana na ndiye niliyemdanganya sana kuliko Mustafa. Mustafa ingawa alizaliwa Bagamoyo lakini alikulia Dar. Alikuwa mtoto wa mjini kinyume cha Musa aliyekulia Handeni na kuja Dar akiwa kijana tayari.

Mwanangu alifikia umri wa miaka minne akiwa na majina mawili. Jina la Amani alilopewa na Mustafa na jina Ramadhani alilopewa na Musa.

Pia alifikia umri huo akijua kuwa ana baba wawili. Hakuweza kujua wala kuniuliza ni nani baba halisi kwa sababu bado alikuwa hana maarifa.

Shangazi yangu naye hakuweza kujua chochote kinachoendelea. Kuna kipindi Mustafa alikuwa amekwenda China, shangazi akaumwa sana.

Nilihamia Ilala kwa ajili ya kumuuguza. Alipoona hapati nafuu akaniambia nimpeleke Tanga kwa ndugu zake. Nikampeleka. Kila nilipopata nafasi nikawa naenda Tanga kumjulia hali.

Kulikuwa na siku moja nilikwenda Ilala nyumbani kwake kwani mara kwa mara nilikuwa nakwenda kwa ajili ya kukagua nyumba yake, wakati natoka nikakutana na Sele, yule mchumba wangu wa kwanza aliyekimbilia Sauzi baada ya maisha kumuwia magumu.

Kama mtakumbuka tulianza mapenzi yetu tangu tulipokuwa shuleni. Alipomaliza kidato cha nne alipata kazi bandarini. Tukapanga kuoana lakini ghafla Sele akafukuzwa kazi kutokana na tabia ya wizi wa mizigo inayoingizwa. Mipango yetu ya kuoana ikafa.

Siku ile aliyokuwa anaondoka kwenda Sauzi aliniahidi kuwa akirudi atakuja kunioa. Siku za mwanzo mwanzo tulikuwa tunawasiliana hatimaye mawasiliano yakakatika. Nikamsahau kabisa.

Siku ile nilipomuona wakati natoka kwa shangazi nilimsahau. Alikuwa amebadilika sana. Alikuwa amenawiri na alikuwa amevaa mavazi ya thamani sana.

Tukasalimiana kisha akaniuliza.

“Mishi ni wewe au nimekuchanganya?”

“Na mimi najiuliza Sele ni wewe au macho yangu yananidanganya?” Nikamwambia.

Sele akacheka.

“Ni mimi. Macho yako hayajakudanganya,” akaniambia.

“Umekuja lini?”

“Yapata wiki moja sasa. Nakutafuta sijakuona.”

Wakati tunazungumza nilikuwa namtazama jinsi alivyovaa.

Alikuwa amevaa miwani ya jua pamoja na chepeo. Kwa vile kilikuwa kipindi cha baridi alivaa jaketi la ngozi la rangi ya kijivu pamoja na suaruali aina jinzi ambayo aina yake sikuwahi kuiona popote.

Chini alivaa viatu fulani ambavyo sikuweza kutambua aina yake. Licha ya mavazi hayo kumuweka tofauti alikuwa amevaa cheni ya dhahabu shingoni. Kwa kweli alipendeza sana.

“Mimi nipo,” nikamwambia huku mawazo yangu yakiwa mbali. Nilikuwa nimevutiwa na jinsi alivyovaa.

“Nilisikia umeolewa?’ Akaniuliza.

Moyo wangu ukashituka.

“Nani alikwambia?”

“Nimesikia tu mitaani.”

“Hapana. Sina mume.”

“Hujaolewa?”

“Niliolewa lakini niliachana na yule mwanaume muda mrefu.”

“Nilikuwa nimekuletea gari Mishi.”

“Umeniletea gari, liko wapi?”

“Halijafika. Nilipakia magari mawili langu na lako. Nadhani baada ya wiki mbili yatakuwa yameshafika.”

“Nitafurahi kulipata hilo gari.”

“Nilisema kama Mishi atakuwa hajaolewa, gari hilo litakuwa lake lakini kama atakuwa ameolewa itakuwa bahati mbaya.”

“Kama nilivyokwambia niliolewa lakini niliachana na huyo mwanaume. Hivi sasa nipo nipo tu.”

“Sasa labda uniambie tukutane wapi na muda gani ili tuweze kuzungumza zaidi.”

Hilo gari aliloniambia Sele lilinitia tamaa sana. Ikabidi nipange muda na mahali pa kukutana naye. Nilihisi pia Sele alikuwa amekuja na pesa za kutosha na kwakuwa alionekana bado alinipenda niliamini ningeweza kumla kadiri nitakavyotaka.

Nikamwambia tukutane kesho yake saa nane mchana katika hoteli moja iliyokuwa pale pale Ilala.

Akachukua namba yangu na mimi nikachukua yake, tukaagana.

Niliporudi nyumbani mawazo yangu yote yalikuwa kwa Sele. Nilikuwa nikilaani kwanini niliharakisha kuolewa na sikuolewa na Sele.

Nilihisi Sele ndiye aliyekuwa na sifa zaidi za kuwa mume wangu kuliko Musa na Mustafa.

Kwanza Sele alikuwa kijana wa mjini aliyezaliwa mtaa wa Pangani wilaya ya Ilala. Yaani tumetoka mbali. Tulijuana na kupendana tangu tulipokuwa shule. Isitoshe Sele alikuwa amerudi kutoka nje ya nchi baada ya kufanikiwa.

Katika wiki ile nilikuwa nikikaa Kimara kwa Musa baada ya Mustafa kuondoka. Alikuwa amekwenda India kwenye biashra zake. Lakini Musa alikuwepo. Kuwepo kwa Musa kusingenizuia kukutana na Sele kwani nilikuwa na uongo mwingi wa kumpa.

Usiku wa siku ile nikamwambia Musa kuwa kesho yake ningekwenda Tanga kumjulia hali shangazi.

Kwa jinsi ambayo sikuitegemea Musa aliniambia.

“Tutakwenda sote.”

“Halafu nyumba na mtoto vitabaki na nani?”

“Ramadhani tutakwenda naye.”

“Si lazima twende sote, acha niende mimi. Kama unataka kwenda kumsalimia mkwe wako tutapanga siku nyingine.”

“Sawa.” Musa akaniambia.

Ndio maana nilimpenda sana. Alikuwa rahisi kukubali wazo langu hata kama ninamdanganya. Uwezo wake wa kuona mbali ulikuwa mdogo sana.

Asubuhi yake nikajipara na kuondoka. Badala ya kuelekea kituo cha mabasi cha Mbezi kupanda basi la kwenda Tanga nikaenda Ilala. Kwa vile ilikuwa mapema sana nilipitisha muda nikiwa nyumbani kwa shangazi.

Ilipofika saa sita nikampigia Sele.

“Sele vipi?” Nikamuuliza mara tu alipopokea simu yangu.

“Poa. Mimi tayari niko hapa hotelini.”

“Umeshafika?”

“Nilifika mapema sana. Nahisi leo tutalala hapa.”

“Usijali.”

“Ndio unakuja au..?”

“Ninakuja, niko hapa Ilala kwa shangazi.”

“Nakusubiri.”

“Sawa.”

Nikaondoka. Kwa vile hoteli niliyokuwa nakwenda haikuwa karibu nilikodi teksi.

Nilipofika, kabla ya kushuka kwenye teksi nilimpigia Sele.

“Nimeshafika,” nikamwambia.

“Uko wapi?”

“Bado niko kwenye teksi, njoo unifuate.”

“Poa. Ninakuja.”

Baada ya sekunde chache tu Sele akatokeza kwenye lango la hoteli. Nilipomuona nilifungua mlango wa teksi nikashuka. Akanifuata kunako teksi. Jinsi nilivyomuona hakuwa timamu. Alikuwa ameanza kulewa.

“Hello baby,” akaniambia huku akinishika mkono.

Inaendelea...