Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

HADITHI: Bomu Mkononi - 20

Muktasari:

  • Binti mrembo cheupe, ambaye ukimwangalia unaweza kusema ni Mwarabu, anawavuruga wanaume kwa kuolewa na mume zaidi ya mmoja. Hili ni bomu mkononi...

TATIZO lililokuwapo ni kuwa nilishamdanganya Mustafa kuwa sikuwa na ndugu yeyote hapa Dar. Hilo ndilo lililonifanya nishindwe kupanga uongo wa kumwambia kwamba ninakwenda kwa ndugu yangu fulani.

Mpaka kulipokucha asubuhi nikawa nimepata uongo lakini sikumwambia kitu asubuhi ile. Baada ya kumtayarishia chai ya asubuhi alikunywa na kuondoka. Hakuniambia alikuwa anakwenda wapi.

Nikasubiri hadi saa nne ndipo nikampigia simu kumuita.

“Una nini?” Akaniuliza.

“Kumetokea tatizo kidogo,” nikamwambia.

“Tatizo gani?”

“Ndio nataka uje nikueleze.”

“Kwani huwezi kunieleza kwenye simu?”

“Kumetokea msiba huko Kimara.”

“Msiba wa nani?”

“Pale nilipokuwa naishi yule mama mwenye nyumba amefariki asubuhi hii nimepigiwa simu.”

“Sasa ulitakaje?’

“Nilitaka kukufahamisha kuwa yule mama ni kama mama yangu, niliishi naye tangu nikiwa msichana mdogo. Amenifanya kama mwanawe na wanawe ni kama ndugu zangu, kwa hiyo nataka kwenda kumzika.”

“Mazishi ni saa ngapi?’

 “Sijajua bado, nitajua huko huko.”

“Nisubiri ninakuja hapo nyumbani.”

“Usichelewe sana.”

Nikahisi Mustafa akifika anaweza kutaka kunipeleka kwa gari wakati hakukuwa na msiba wowote, nikamwambia.

“Au niende tu…?”

“Basi funga nyumba uende, funguo zangu ninazo.”

Nilishukuru aliponiambia hivyo, nikamwambia.

“Sawa.”

Nikakata simu na kujitayarisha kutoka. Nilijitayarisha haraka haraka ili Mustafa asije akarudi na kuniambia atanipeleka kwa gari.

Nilipokuwa tayari nilitoka, nikafunga nyumba na kutafuta teksi iliyonipeleka Kimara kwa mume wangu wa kwanza.

Nilipofika tu nikampigia simu Musa.

“Baby wangu umzima?” Nikajidai kumwambia kwenye simu.

“Mimi ni mzima tu, sijui wewe mke wangu?” Musa akanijibu.

“Mimi pia ni mzima. Mmeshaondoka mpakani?’

“Tumeondoka tangu alfajiri.”

“Mtafika Dar saa ngapi?”

“Kila ilivyo tutaingia usiku.”

“Kwa hiyo nisikuwekee chakula?”

“Usiniwekee.”

“Poa. Safari njema mume wangu.”

“Poa.”

Baada ya kumzuga Musa na kujiona yeye ndiye kidume peke yake nilikata simu.

Hawa wanaume wamezoea kutuchezea sisi wanawake, ngoja na mimi niwachezee. Nikajiambia kimoyomoyo wakati liliponijia wazo kuwa mtindo niliokuwa nikiutumia wa kuwa na waume wawili haukuwa wa kiungwana.

Kwa vile nilikuwa sina kazi ya kufanya nikampigia simu Amina.

Amina alipopokea simu aliniambia haraka.

“Siku hizi umekuwa mswahili shoga yangu.”

“Sio hivyo shoga, ile jana simu yangu iliisha chaji ghafla. Sijui yule fundi alinibadilishia betri yangu!” Nikampiga uongo.

“Mara simu ilikuwa mbovu, mara betri imebadilishwa, siku hizi hueleweki.”

Aaah…niamini shoga. Mbona muda huu nimekupigia?”

“Mimi naona si bure..!”

Aliposema hivyo nilishituka nikajidai kucheka.

“Kwanini unaniambia hivyo?’ Nikamuuliza ili kama amesikia jambo anieleze.

“Naona shoga si bure, iko namna. Hutaki tu kuniambia.”

“Hakuna kitu, kama kipo tungekwishaambizana. Vipi Shabir hajambo?” Nikabadili ile mada ghafla.

“Hajambo.”

“Yupo au amesafiri?”

“Amejaa tele kama pishi ya mchele.”

“Rafiki yake Mustafa naye yupo?”

“Mh! Mustafa walikwishatengana, siku hizi kila mmoja ana biashara yake.”

“Unasema ukweli shoga?”

“Yule jamaa alikuwa mjanja sana, anamtia hasara mwenzake.”

“Anamtia hasara kivipi?”

“Nafikiri alikuwa anamuibia pesa.”

“Sasa utakuja lini nyumbani tuzungumze?”

“Nitakuja.”

“Niambie siku.”

“Naweza kuja hata kesho.”

“Poa. Njoo kesho. Utakuja saaa ngapi?”

“Nitakuja asubuhi.”

Baada ya kuzungumza na Amina nikaiweka simu yangu pembeni na kufikiria kwenda kupika.

Siku ile nilishinda nyumbani. Mlinzi alipokuja jioni nilikutana naye.

“Leo upo?” Akaniuliza.

“Nimerudi tangu asubuhi. Nilikuwa safarini,” nikamdanganya.

Nilidhani angeniuliza nilikwenda wapi lakini hakuniuliza. Nikatoa shilingi elfu kumi na kumpa.

“Asante,” akanishukuru kisha aliniambia.

“Mwenye nyumba naye sijamuona muda mrefu.”

Alikuwa akimaanisha mume wangu.

“Yupo safarini lakini atarudi leo. Unaweza kumuona usiku.”

“Sawa.”

Baada ya hapo nikarudi ndani. Nilimsubiri Musa nilipoona hatokei nikaenda kulala.

Akaja kuniamsha saa saba usiku kwa kunipigia simu. Simu iliita sana mpaka nilipozinduka nikaipokea.

Sikutazama nani aliyekuwa anapiga. Nilikimbilia kuipokea na kuuliza.

“Nani?”

“Mimi Musa, nifungulie mlango.”

“Uko nje?” Nikamuuliza.

“Ndio niko nje.”

“Subiri.”

Nikashuka kitandani na kujifunga khanga kisha nikatoka. Nilikwenda kwenye mlango wa mbele nikaufungua. Musa akaingia.

“Karibu,” nikamwambia huku nikimpokea begi lake.

Tuliingia chumbani. Musa akaenda kuoga. Wakati anaoga nilifungua begi lake na kuchunguza vitu vilivyokuwamo.

Nilikuta nguo zake, chupa tatu za pafyumu na vitu vyake vingine. Nilipopekuapekua zaidi nikakuta kipakiti cha kondomu kilichotiwa kwenye soksi.

“Ha!” Nikashituka.

“Kondomu hizi ni za nini?” Nikajiuliza.

Hapo ndipo nilipopata mawazo kuwa mume wangu naye amekuwa muasharati kama mimi. Niliichukua ile pakiti ya kondomu kisha nikarudisha vile vitu kama nilivyovikuta.

Ingawa hatua yangu ya kuolewa kwa mara ya pili ilikuwa ya kuchukiza zaidi, nilikerwa kuziona zile kondomu. Nilijua kuwa mume wangu alikuwa na wasichana wengi huko vijijini anakopita.

Maisha ya mimi na yeye yalikuwa mfano wa miguu na mikono ya nzi. Nzi anapoisugua mikono na miguu yake, waswahili wana tafsiri zao. Wanasema. “Wewe ukijua hivi na mwenzako anajua vile.”

Lakini nilishukuru kwamba Musa anajua umuhimu wa kutumia kondomu, vinginevyo tungeuana.

Pamoja na kujikaza lakini moyo wangu haukukubali kumuachia, nilimgoja kwa hamu atoke bafuni.

Nilipomuona anatoka tu nikamuonesha ile pakiti yake ya kondomu na kumuuliza.

“Kondomu hizi ni za nini?”

Musa alishituka sana.

Alikitupia macho kile kiboksi cha kondomu kisha akanitazama mimi.

“Kwanini unaniuliza mimi, kwani umezipata wapi?’ Akaniuliza kwa mshangao.

“Nimezipata kwenye begi lako, zilikuwa ndani ya hii soksi,” nikamwambia huku nikimuonyesha ile soksi.

“Si za kwangu.”

Nilipoona amezikana nilimtolea macho.

“Si za kwako ni za nani, kwani begi hili sio lako?”

“Ni za taniboi wangu.”

“Kama ni za taniboi wako zilifikaje kwenye begi lako?”

Nilikuwa namhoji kama vile tuko mahakamani.

“Nadhani alikosea. Mabegi yetu yanafanana. Badala ya kuzitia kwenye begi lake amezitia kwenye begi langu.”

Nikaona mume wangu ananipa hadithi ya kujihami isiyo na kichwa wala miguu. Alinifanya nitoe kicheko cha uongo.

“Mume wangu unanifanya mimi sina akili. Yaani mtu anunue kondomu asiziweke kwenye begi lake aweke kwenye begi lako…”

“Amini ninachokueleza, sikudanganyi. Hizo si kondomu zangu.”

“Mimi nakwambia ni za kwako, wewe si mume mwaminifu.”

Nilipomwambia. “Wewe si mwanaume mwaminifu.” Sauti yangu ilinisuta kwa vile mimi mwenyewe pia sikuwa muaminifu. Lile neno “Mwaminifu” lilififia mdomoni mwangu kama vile niliishiwa na sauti.

“Unanituhumu bure mke wangu, mimi ni mwaminifu sana. Taniboi wangu ndiye aliyefanya uzembe.”

“Mimi naona wewe na taniboi wako lenu ni moja tu.”

“Hapana. Yeye hana mke, mimi simuingilii maisha yake.”

“Sasa kama kondomu hizi si za kwako nipe namba ya taniboi wako nimpigie simu aje achukua kondomu zake.”

Musa akatikisa kichwa.

“Hapana, usimpigie simu.”

“Kwanini?”

“Hawezi kuja huku usiku huu.”

“Basi nitampigia nimuulize tu kama hizi kondomu ni zake?”


“Yanini kumuumbua mtu bure, mke wangu usipende kuingilia maisha ya watu!”

“Mimi nataka kumuuliza kwa sababu kondomu nimezikuta ndani ya begi la mume wangu.”

“Sasa ninakwambia usimuulize, ukimuuliza ni kama unamuaibisha bure. Wewe amini tu kuwa hizo kondomu ni za kwake.”

“Mimi sitaki tubishane lakini nakushukuru sana kwamba umekumbuka kondomu.”

“Kwanini unaniambia hivyo?”

“Nakuambia hivyo kwa sababu umehakikisha usalama wako na wangu. Nyinyi wanaume hamuaminiki. Sasa kama umekumbuka kondomu nakushukuru sana. Endelea hivyo hivyo wala sitakuwa na ugomvi na wewe.”

Inaendelea…