Dili iliyokufa - 35
ILIPOISHIA
Nikawaza nikimtilia kwenye chakula haitafaa kwa sababu chakula hicho tunakula sote. Nikawaza tena labda nimtilie kwenye mchuzi kwa vile kila mmoja anakuwa na bakuli lake la mchuzi. Nikaona kwenye mchuzi itafaa lakini bado kulikuwa na tatizo.
Huwa sitii mchuzi kwenye vibakuli nikiwa jikoni, huutia pale pale mezani wakati yeye anaona. Kama nitaamua kuutia jikoni, atashituka. Atajiuliza leo mchuzi umetiwa jikoni wakati siku zote unatiwa mezani, kulikoni!
Nikaendelea kuumiza kichwa changu kuwaza. Sikutaka nishindwe. Kama kuna watu wanaweza kuwatilia waume zao dawa kwenye vyakula, kwanini mimi nishindwe?
Nikiwa kwenye lindi la mawazo hayo nikasikia mlango wa mbele unabishwa. Nikatoka chumbani na kwenda kufungua mlango. Nikamuona wifi yangu Hamisa, yaani dada yake mume wangu amesimama kando ya mlango.
SASA ENDELEA...
KIDOGO nilishtuka kwani Hamisa hakuwa na kawaida ya kututembelea pale nyumbani.
Kwa vile alikuwa amenizidi umri, nilikuwa nikimwamkia.
“Shikamoo wifi, karibu ndani.”
“Marahaba. Habari ya hapa?” akaniuliza huku akiingia ndani.
“Nzuri wifi, karibu ukae.”
Hamisa akakaa kwenye kochi.
“Mume wako yupo?”
“Yupo kazini, hajarudi bado,” nikamjibu huku nikiketi karibu yake.
“Nimekuja kuwatembelea tu, ninyooshe miguu. Siku nyingi hatujaonana,” akaniambia.
Nikashukuru kujua kwamba alikuwa amekuja kututembelea, tukaendelea na mazungumzo kwa karibu saa mbili. Yalikuwa mazungumzo ya kawaida tu kati ya mtu na wifi yake. Baadaye Hamisa akaniaga na kuondoka.
Nikaingia jikoni na kuanza kupika. Mpaka muda huo nilikuwa bado nawaza kuhusu ile dawa. Nilikuwa sijajua nitafanya nini. Lakini nilijiambia kwamba kama nitashindwa siku ile, nitasubiri siku inayofuata.
Hapo hapo nikapata wazo kwamba nisile chakula pamoja na mume wangu. Yaani nijifanye nilipatwa na njaa mapema, hivyo nikaamua kula kabla ya mume wangu kurudi.
Nilipopata wazo hilo, nikajitilia chakula nikala kabisa ili akija nisile naye.
Lakini mume wangu alipokuja, hakuja peke yake. Alikuwa amefuatana na rafiki yake kipenzi Mohammed Awawi. Huyo jamaa tulikuwa tunamwita kwa kifupi Mudi.
Nikasalimiana na Mudi huku nikijiambia kimoyomoyo kwamba mpango wangu ungeweza kukwama kwa sababu ya yule mgeni ambaye sikumtarajia.
Baya zaidi ni kwamba ile dawa nilikuwa nimeshaitia kwenye mchuzi kwa kujua kwamba mimi mwenyewe sitakula.
Sasa kama wangekula wote, shemeji naye angekula mkojo wangu. Niliogopa asije akanipenda, ikawa balaa!
Kitu cha kwanza alichouliza mume wangu ni chakula. Nikajiambia kwamba kama watakula wote, basi wale tu. Sikuwa na la kufanya. Dawa nilikuwa nimeshaitia kwenye mchuzi.
Mume wangu alikwenda kukaa mezani lakini Mudi akakaa kwenye kochi. Nikajidai kumuuliza.
“Mbona shemeji huendi mezani? Si nawaandalia chakula?”
“Mimi nilishakula, siwezi kuongeza tena,” akaniambia.
Nilishukuru aliponiambia hivyo lakini mume wangu hakukubaliana naye.
“Njoo Mudi, utabaruku kidogo,” akamwambia.
“Hapana, endelea tu. Nimeshiba sana. Siwezi kuongeza. Nitakuja kula siku nyingine. Hapa ni kwangu, sina wasiwasi.”
Nikawaacha wanazungumza, nikaingia jikoni na kutayarisha chakula.
Nilipokwenda kukiweka juu ya meza nikamwambia Mashaka kwamba hata mimi nilikuwa nimeshakula. Alibaki yeye tu.
“Kumbe nakula peke yangu!” akasema huku akijitilia wali kwenye sahani.
Niliketi naye ili nimuone anavyokula mchuzi ule.
Tabia yake mara nyingi kabla ya kuanza kula ilikuwa kuchota mchuzi kwa kijiko kisha kuuonja. Na hivyo ndivyo alivyofanya siku ile. Aliuonja ule mchuzi, kisha nikamwona anakunja uso.
“Mbona mchuzi mchungu sana? Umetia nini?”
Aliponiuliza hivyo nilishtuka.
“Labda ni limao tu,” nikavunga.
“Hapana. Hebu onja.”
Akauchota tena kwenye kijiko na kukielekeza kwangu.
“Hebu onja,” akaniambia.
Hapo sikuwa na ujanja. Chakula nilikuwa nimekipika mwenyewe halafu nikatae kuonja? Isingewezekana.
Nikasogeza mdomo wangu, akaninywesha ule mchuzi kwenye kijiko. Nilitaka nisiumeze, lakini sikuweza kuzungumza, ikabidi niumeze wote. Kweli ulikuwa mchungu kutokana na ile dawa niliyotia. Nilikuwa nimeitia nyingi.
“Mbona ni mzuri tu, mume wangu. Labda ni mdomo wako tu,” nikajidai kumwambia.
“Ni mdomo wangu?”
Akauonja tena. Safari hii hakuusikia sana kutokana na ile ladha ya kwanza kuwa bado kinywani mwake.
“Ni mdomo wako tu, hauna uchungu wowote,” nikamwambia.
“Labda ni mdomo wangu...”
Akajitilia mchuzi kwenye wali na kuanza kula.
Ili asiifikirie ile ladha aliyokuwa ameisikia, nilianza kumsemesha maneno ya kawaida ili aendelee kula. Na kweli alikula chakula chote alichojitilia, na mchuzi akauumaliza licha ya kuwa na uchungu.
Nikafurahi, ingawa na mimi nilikuwa nimeuonja kidogo. Kwa vile yule mganga aliniambia kwamba hata nikila chakula kitakachotiwa dawa hiyo hakitakuwa na tatizo, sikujali sana.
Sasa nikawa nasubiri nione matokeo.
Siku ya pili nilitengeneza juisi kwa ajili ya kumtilia ile dawa. Nikamuwekea kidogo.
Siku ya tatu nikamuwekea tena kwenye juisi. Akainywa kidogo, kisha akaninywesha na mimi. Yalikuwa mapenzi. Sikukataa. Nikainywa.
Dawa ikampata yeye na mimi.
Ile siku ya tatu usiku nikajaribu kumuomba pesa. Nilimuomba shilingi laki mbili.
“Subiri mwisho wa mwezi,” akaniambia na kuongeza,
“Hivi sasa nimebakiwa na hela za chakula tu. Nikizitoa tunaweza kukwama.”
“Sawa, nitasubiri.”
Tangu siku ile ya kwanza nilipoonja ule mchuzi kwenye kijiko, mawazo yangu yakawa kwa yule mganga. Ile siku ya pili niliyokunywa tena ile dawa kwenye juisi, mawazo ndiyo yakazidi. Ajabu ni kwamba mume wangu niliyekuwa nikimpenda alinitoka moyoni mwangu kabisa, na badala yake nikaanza kumpenda yule mganga.
Kila nilipokaa nilikuwa na kiherehere cha kutaka kwenda kwake. Ile siku ya tatu sikuenda, nikaenda siku ya nne.
Nilipofika nilimkuta mganga akimuagua mtu mle chumbani. Wale wanawake ninaowakuta pale uani wakanipa kiti ili nimsubiri. Nikakaa karibu na mlango wa kile chumba.
Baadaye kidogo mlango wa chumba hicho uliokuwa umefungwa ukafunguliwa. Nikamwona yule mganga anatoka akiwa ameshika chetezo cha moto. Jicho langu likaelekea ndani ya chumba hicho, nikamwona aliyekuwa akiaguliwa akiwa mwanamke. Tena alikuwa amevuliwa nguo zake na kuvalishwa kaniki.
Usishangae nikikwambia roho iliniuma nilipomwona mwanamke huyo. Nilihisi kwamba yule mganga angemfanyia kama alivyonifanyia mimi, na mimi sikutaka afanyiwe hivyo kwa sababu ya wivu.
“Oh, kumbe ni wewe?” yule mganga akaniambia aliponiona.
“Ni mimi, shikamoo.”
“Marahaba. Endelea kusubiri. Kuna mteja namshughulikia,” akaniambia, kisha akamwita mmoja wa wale wanawake na kumwambia amtilie makaa ya moto kwenye kile chetezo.
“Nitasubiri tu, hakuna shida,” nikamjibu, lakini moyo ulikuwa bado ukiniuma.
Sikujiuliza kwa nini moyo uniume wakati yule mtu hakuwa mume wangu. Nilijiona niko hivyo tu.
Mganga akarudi kwenye kile chumba. Chetezo kikarudishwa kikiwa na makaa ya moto. Mganga akakichukua, akabana ule mlango ili nisione ndani. Ajabu ni kwamba kitendo hicho pia kiliniumiza moyo wangu. Niliona kama vile mganga huyo alinifungia mlango nisione mambo yake.
Nilikaa pale kwa karibu nusu saa nikifikiria hili na lile. Baada ya muda huo mlango ukafunguliwa. Nikamwona yule mwanamke akitoka. Nikageuza uso wangu pembeni ili nisitazamane naye.
Lakini alinisalimia.
“Habari gani?”
“Nzuri,” nikamjibu huku nikimtazama kwa nyuma. Nilimwona akipandisha nguo yake ya ndani huku akitembea. Nikajua alikuwa amevuliwa kila kitu kama nilivyofanywa mimi.
“Haya, ingia,” sauti ya mganga ikanishitua na kunifanya nisimtazame tena yule mwanamke.
Nikainuka kwenye kiti na kuingia katika kile chumba.
“Karibu ukae,” mganga akaniambia.
Nikakaa kwenye jamvi. Kimoyomoyo nilikuwa najiuliza kwa nini hawa waganga wa kienyeji hawaboreshi mazingira yao wakati wanapata pesa nyingi. Kila siku tunakaa chini tu.
Mganga alikuwa amekaa mbele yangu.
“Haya, niambie, umefanya zile dawa?” mganga huyo akaniuliza.
“Nimefanya.”
“Umemtilia kwenye chakula?”
“Nimemtilia kwa siku tatu kama ulivyoniagiza.”
“Na wewe umekula hicho chakula?”
“Ilibidi nile ile siku ya kwanza. Unajua niliitia kwenye mchuzi. Akaniambia mchuzi ni mchungu, ‘Hebu uonje.’ Nikauonja.”
“Lakini haina madhara hata kama umeuonja.”
“Na siku ya pili nilimtilia kwenye juisi. Akanywa kidogo, kisha akaninywesha na mimi.”