Dili iliyokufa -34
ILIPOISHIA
“Ukija siku hiyo ya tatu ndiyo nitakupa dawa hiyo. Siwezikutoa dawa zote kwa pamoja, zinaweza kumchanganya akili”
“Sasa lini ataanza kubadilika”
“Haitachukua muda. Utaanza kuona mabadiliko kidogo kidogo lakini Siku utakapokuja nikikupa hiyo dawa ya kumtilia kwenye chakula ndio utaona mabadiliko makubwa. Utamuona haondoki nyumbani na kila wakati anataka kuwa na wewe.”
SASA ENDELEA...
“Na nikihitaji pesa pia anipe”
“Si umemuulilia?”
“Ndiyo nimemuulilia.”
“Atakupa pesa unazotaka.”
“Hata kama nitamwambia anipe mshahara wake wote atanipa?”
Nilipomuuliza hivyo mganga akacheka.
“Akitaka kukupa mshahara wake wote, yeye mwenyewe atabaki na nini?”
“Nataka mimi ndiye nipange matumizi yetu.”
“Mtafika huko huko lakini kwa taratibu, usiwe na haraka.”
“Sawa. Sasa mimi naenda.”
“Wewe nenda. Usisahau kuja baada ya siku tatu.”
“Sitasahau, nitakuja. Mimi ndiye mwenye shida.”
Nikamuaga yule mganga na kuondoka. Wakati natoka niliona aibu hata kutazamana na wale wanawake. Niliona kama wanajua nilichofanyiwa. Nikawaaga huku nikitembea harakaharaka.
Nilipotoka nje ya ile nyumba nikaanza tena mwendo wa kurudi barabarani. Ukienda kwa mganga ni kama uliyekwenda kwa daktari. Ukiambiwa vua nguo unavua. Bana pumzi unabana. Fumba macho unafumba. Hakuna kuuliza.
Na kwa mganga wa kienyeji ni hivyo hivyo, lakini wao sasa wamezidisha.
Nilipofika kituoni nilikuta daladala kadhaa zikisubiri abiria. Nikapanda ile iliyokuwa imejaa watu. Nilipoingia mimi wakaingia watu wengine wawili. Daladala ikawa imejaa, ikaondoka hapo hapo.
Niliporudi nyumbani nikampigia simu Mwanaisha na kumwambia kuwa nimerudi.
“Hata mimi nimerudi nyumbani sasa hivi. Nilikuwa nimetoka. Vipi?”
“Amenifanyia.”
“Amekufanyia vipi?”
Sikutaka kumweleza kinaganaga. Niliona aibu.
“Amenipa dawa za kuchoma na dawa nyingine ametaka nijipake mwilini. Lakini baada ya siku tatu ameniambia niende tena.”
“Wewe nenda, baada ya siku tatu utaona matokeo yake.”
“Nitakwenda shoga. Maji ukiyavulia nguo lazima uyaoge.”
“Kwanini unasema hivyo? Kwani amekwambia nini?”
“Nimekwambia hivyo kwa sababu ya hizo safari za nenda rudi.”
“Sasa utafanyaje shoga, wakati hawa waume zetu ili tuishi nao vizuri ni mpaka kwa mzizi.”
“Tena mimi umenizindua wewe. Nilikuwa siyajui kamwe!”
“Ndiyo hivyo. Hapa ni mjini hakuna mashamba. Mashamba ni waume za watu. Ukizubaa tu utaona mume wako anachukuliwa huku wewe mwenyewe unaona. Nyumbani kwake hafiki tena.”
“Ni kweli shoga. Ukimuamsha aliyelala utalala wewe. Huyu bwana ameniamsha. Karibuni nitamlaza yeye.”
“Nitakuja huko kwako baadaye kidogo tupige stori.”
“Sawa shoga, mie nipo.”
Nikakata simu.
Mume wangu aliporudi jioni nilipiga stori naye vizuri nikijifanya sina hasira naye. Nilikuwa namuandaa kwa ajili ya usiku kama alivyoniagiza mganga kwamba ukifika usiku lazima nijichanganye naye, tena kuwe na giza.
Kwa jinsi tabia ya mume wangu ilivyokuwa imebadilika, suala la kuchanganyika naye lilikuwa lazima nililiandae mimi. Yeye hakuwa na habari na mimi kabisa. Akishatoka kwa wasichana zake, shauku ya kuwa na mimi anakuwa ameimaliza huko huko.
Hapa kwangu anakuja kulala tu kama vile mimi ni dada yake.
Siku ile sikumuomba pesa kwani ugomvi wetu mkubwa unakuwa kwenye pesa. Yaani alikuwa mgumu kama jiwe! Pesa zote alikuwa akizimaliza kwa wasichana wake.
Ulipofika usiku tayari nilikuwa nimeshamtia kile kitu ambacho Waarabu wanakiita “shakawa”, yaani ile hamasa kali ya kutamani tendo la ndoa.
Na ndivyo ilivyokuwa. Kawaida yetu tulikuwa hatuzimi taa kwa sababu tulikuwa tumesha zoeana. Lakini usiku huo nilizima taa kama nilivyoagizwa na mganga, na jamaa hakuniuliza chochote.
Mambo yakaenda kama nilivyoyapanga. Baada ya hapo tukalala. Mimi nililala bila kuoga. Nilikuwa nafuata maagizo ya mganga wangu.
Zikapita zile siku tatu. Nikaenda tena kwa yule mganga. Nilipofika sikumkuta. Nikaambiwa alikuwa ameenda kuchimba dawa tangu asubuhi.
Nikapewa kiti nimsubiri. Ilikuwa saa nne. Nikasubiri hadi saa tano ndipo mganga alipotokea. Akanikaribisha kwenye chumba chake cha uganga.
“Umeniletea habari gani?” akaniuliza baada ya kuketi.
“Uliniambia nije baada ya siku tatu, ndiyo nimekuja.”
“Unamuonaje mume wako katika siku hizi tatu?”
“Tunazungumza vizuri lakini bado sijaona mabadiliko.”
“Sawa.”
Mganga akaagiza aletewe makaa ya moto. Moto ulipoletwa aliniambia niketi chini mbele yake. Nilipoketi alizivuta na kuzing’oa nywele zangu tatu zilizokuwa kwenye utosi, akazichanganya na dawa zake na kuzitia kwenye yale makaa ya moto.
Akaninong’onezea maneno ambayo sikuyasikia. Baadaye alichukua kichupa kidogo cheupe akaniambia nikitie mkojo.
“Nenda chooni kanitilie haja ndogo humu,” akaniambia.
Nikatoka na kuwauliza wale wanawake waliokuwa uani.
“Choo kiko wapi?”
Wakanionesha. Nikaingia na kujikamua haja ndogo ambayo niliielekeza kwenye kile kichupa.
Niliporudi chumbani kwa mganga nilikuta na yeye alikuwa ameshika kichupa kama kile ambacho ndani yake kilikuwa na maji ya manjano, akanipa.
Nikakishika. Kichupa hicho kilikuwa kina joto. Nilishuku yale maji yaliyokuwemo ndani yake yalikuwa ni mkojo wake ambao aliutoa mara tu nilipotoka mle chumbani.
“Hii dawa iliyomo katika kichupa hiki nilichokupa ichanganye katika kichupa hiki ulichokitia haja ndogo,” mganga akaniambia.
Nikatia ile dawa katika kile kichupa alichoniambia. Nikajiambia kama ilikuwa dawa, ilikuwa imechanganywa na mkojo wake kwani harufu yake ilisikika waziwazi.
“Sasa nipe,” akaniambia.
Nikampa vile vichupa. Kile kilichokuwa kitupu akakiweka chini. Kile chenye dawa pamoja na haja ndogo akakishika. Akasemea maneno huku akikitia dawa zingine kutoka kwenye tunguri zake.
Baadaye akanipa na kuniambia:
“Utakwenda kumtilia mume wako kwenye chakula asubuhi na jioni.”
“Mmh…!” nikaguna kimoyomoyo.
Nikamlishe mume wangu mkojo? Tena si mkojo wangu peke yangu, tumechanganya na wake!
Nilisita kwanza nikishangaa kabla ya kumuuliza.
“Nikamtilie hiki kichupa kizima?”
“Tia kidogo kidogo kwa siku tatu.”
“Kama kiasi gani?”
“Kadiria tu kiasi cha kijiko kimoja kidogo.”
“Nimtilie kwenye chakula gani?”
“Chakula chochote tu, hasa kwenye mchuzi au chai.”
“Hatajua?”
“Hawezi kujua.”
“Sasa kama hicho chakula tunakula sote itakuwaje?”
“Kwani wewe ukila mkojo wako kuna tatizo gani?”
“Mkojo wangu? Si kuna na wa kwako pia?” nikamwambia lakini kimoyomoyo. Hakunisikia.
“Kama hutaweza kumtilia peke yake, unaweza kutia katika chakula mtakachokula nyote. Baada ya siku tatu tu mume wako atabadilika,” mganga akaniambia baada ya kuona nilikuwa kimya.
“Sasa asubuhi hanywi chai nyumbani. Anakula usiku tu.”
“Mtilie hata huo usiku.”
“Haitakuwa na tatizo?”
“Haitakuwa na tatizo.”
“Kwa hiyo baada ya siku hizo tatu nije tena?”
“Sasa ukija unakuja kunipa matokeo. Mimi ninapofanya kazi ninataka kujua matokeo yake.”
“Sawa. Basi nitakuja baada ya siku tatu.”
Baada ya hapo nikaagana na yule mganga na kuondoka.
Niliporudi nyumbani nikakificha kile kichupa jikoni. Nikaingia chumbani na kujipumzisha kitandani. Hapo nilikuwa nikijiuliza jinsi nitakavyomtilia ile dawa mume wangu wakati tunakula chakula pamoja. Na mimi nilikuwa sitaki kuila ile dawa ingawa mganga aliniambia isingeharibu kitu.
Ningekuwa sijui kama ni mkojo ingekuwa afadhali. Ule ulikuwa ni mkojo, isitoshe mganga naye alikuwa amechanganya na mkojo wake. Kwa vyovyote vile nisingeweza kula.
Nilijua haikuwa vizuri hata kumtilia mume wangu lakini kwa vile nilikuwa nataka kumnyoosha, ningeweza kumtilia kitu chochote ilimradi tu asife. Hata kama ni haja kubwa pia ningemtilia. Potelea mbali.
Nikawaza nikimtilia kwenye chakula haitafaa kwa sababu chakula hicho tunakula sote. Nikawaza tena labda nimtilie kwenye mchuzi kwa vile kila mmoja anakuwa na bakuli lake la mchuzi. Nikaona kwenye mchuzi itafaa lakini bado kulikuwa na tatizo.
Huwa sitii mchuzi kwenye vibakuli nikiwa jikoni, huutia pale pale mezani wakati yeye anaona. Kama nitaamua kuutia jikoni, atashituka. Atajiuliza leo mchuzi umetiwa jikoni wakati siku zote unatiwa mezani, kulikoni!
Nikaendelea kuumiza kichwa changu kuwaza. Sikutaka nishindwe. Kama kuna watu wanaweza kuwatilia waume zao dawa kwenye vyakula, kwanini mimi nishindwe?
Nikiwa kwenye lindi la mawazo hayo nikasikia mlango wa mbele unabishwa. Nikatoka chumbani na kwenda kufungua mlango. Nikamuona wifi yangu Hamisa, yaani dada yake mume wangu, amesimama kando ya mlango.