Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dili iliyokufa - 32

HADITHI 32 Pict

ILIPOISHIA

   “Sasa kwanini anamjali huyo na kunidharau mimi?”

   “Ni mapenzi tu yamezidi kwa mwenzako”

   “Sasa nataka umuondoshe huyo msichana halafu unifanyie dawa huyu mwanaume anipende mimi peke yangu, yaani kila nitakachomwambia anisikilize mimi”

SASA ENDELEA...


“Unakumbuka ulinifanyia dawa kama hiyo. Mpaka leo mume wangu ametulia. Ninachotaka ananipa,” Mwanaisha akamwambia yule mganga.

“Hakuna tatizo. Nitamuondosha huyo msichana na nitakupa dawa. Huyo mume wako hatatamani msichana mwingine tena zaidi yako na atakupenda mpaka kufa.”

Hapo nikapata moyo na kuanza kutabasamu.

“Nifanyie hiyo kazi. Nimkomeshe.”

“Kuna vitu nitavihitaji.”

“Vitu gani?”

“Kwanza nitataka unipatie nyuzi za nguo yake hata kama ni uzi mmoja.”

“Huo utapatikana.”

“Nataka na mchanga wa nyayo zake, yaani pale mahali anapokanyaga uchukue mchanga kidogo uniletee.”

“Hata kama kakanyaga akiwa amevaa kiatu?”

“Hata kama kakanyaga akiwa amevaa kiatu.”

“Nyumbani kwetu kuna sakafu mpaka uani, labda nivizie akitoka nje wakati anaenda kazini.”

“Mvizie akitoka ndipo utazipata kirahisi,” Mwanaisha akaniambia.

“Sawa. Na kingine?”

“Jina lake na la mama yake. Ukiniletea vitu hivyo nitamuweka sawa.”

“Mama yake anaitwa Hawa.”

“Utaniandikia kwenye karatasi siku utakapokuja.”

“Sawa. Wewe mwenyewe utahitaji kiasi gani?”

“Hii kazi ni kubwa, si ndogo, utanipa shilingi laki moja.”

“Itahitajika sasa hivi au...?” nikamuuliza mganga huyo kwa vile kwenye pochi yangu sikuwa na pesa ya kutosha.

“Hiyo pesa utaileta utakapokuja.”

“Nije lini?”

“Utakapopata hivyo vitu nilivyokuagiza.”

“Nitafanya mpango nivipate leo, kesho nitakuja.”

Nikamtazama Mwanaisha kisha nikamuuliza:

“Au unanishauri vipi?”

“Hata kesho unaweza kuja kwani mahali penyewe si umeshapajua?”

“Kwani hutanileta tena?”

“Itategemea nafasi yangu. Kwa kesho huenda nisipate nafasi.”

“Sawa. Nitakuja hata peke yangu. Sidhani kama nitapotea.”

“Nyumbani kwangu hapapotezi. Ukishashuka kwenye daladala unaongoza njia moja kwa moja tu,” mganga akaniambia.

“Nitakuja tu, hakuna tatizo.”

“Kwa leo niachie tu kifungua mkoba.”

Nikamtazama Mwanaisha.

“Kifungua mkoba ndio nini?” nikamuuliza.

“Acha chochote ulichokuwa nacho,” Mwanaisha akaniambia.

Nikafungua pochi yangu na kutoa noti ya shilingi elfu kumi nikampa yule mganga.

“Iweke hapo chini,” mganga akaniambia.

Nikaiweka chini mbele yake.

“Sasa sisi tunakwenda zetu,” nikamwambia.

“Mnaweza kwenda. Kazi yako ni hapo kesho utakapokuja.”

Tuliinuka, tukamuaga yule mganga na kutoka. Tuliwaaga wale wanawake tuliowakuta uani, tukaenda zetu.

“Huyu mganga si mchezo kwa dawa za mapenzi. Atamnyoosha mume wako na wewe utakuja kuniambia,” Mwanaisha akaniambia tukiwa njiani.

“Mimi nataka amnyooshe sawasawa. Na inachukua muda gani?”

“Atakwambia mwenyewe.”

“Kwani wewe ulipomfanyia mume wako ilichukua muda gani?”

“Kama wiki moja tu.”

“Haina shida, hata ichukue wiki mbili, mradi anyooke tu.”

Tuliporudi nyumbani, Mwanaisha akaenda kwake na mimi nikaingia nyumbani kwangu.

Kitu cha kwanza nilichofanya ni kwenda kufungua kabati na kutafuta nguo ya mume wangu ambayo ningeitoa nyuzi. Kulikuwa na suruali yake moja ambayo alikuwa akipenda kuivaa, nikaichukua.

Katika kutafutatafuta, nikashika kwenye pindo la chini la suruali hiyo. Nikaigeuza kwa ndani na kukuta nyuzi zilizosimama. Nikaanza kuzivuta. Nyuzi zenyewe zilikuwa nyembamba na zilikuwa zinakatika.

Hata hivyo, nilipata nyuzi tatu nikazifunga kwenye karatasi kisha nikakiweka kikaratasi hicho kwenye pochi yangu.

Mume wangu aliporudi kutoka kazini, nikapata kazi ya kuvizia nyayo zake. Kila alipokwenda nilikuwa namfuata nyuma. Kwa vile nyumba nzima ilikuwa na sakafu ya marumaru, ilikuwa vigumu kuzipata alama za nyayo zake humo ndani. Nikasubiri atoke nje.

Hakutoka nje hadi saa moja usiku. Aliponiambia kuwa anatoka, hata sikumuuliza anakwenda wapi au atarudi saa ngapi. Nilimuitikia tu. Wakati anatoka nilikuwa nimesimama kwenye mlango nikimtazama.

Alipoivuka baraza ya nyumba yetu akaanza kukanyaga kwenye mchanga kuelekea barabarani. Alama za viatu vyake zikaonekana kwenye mchanga huo.

Alipofika mbali nikatoka na kuuchota ule mchanga wenye alama za viatu vyake. Nikaingia ndani na mchanga huo, ambao niliufunga kwenye kitambaa kisha nikakiweka kwenye pochi yangu. Usiku ule mume wangu alirudi mapema. Ilipofika saa tatu nikamuona anaingia.

Nikamuacha akae kwenye kochi kisha nikamfuata na kumuomba shilingi elfu hamsini ili nichanganyie na zangu nipate laki moja ya kupeleka kwa mganga.

“Unataka elfu hamsini ya nini?” akaniuliza, uso wake akiwa ameukunja.

“Kwani mimi sina shida zangu?”

“Shida gani sasa? Niambie.”

“Mpaka nikwambie shida yangu ndiyo unipe? Kwani mimi si mke wako? Ulitaka anipe pesa nani?”

“Sasa wewe unaleta kesi...”

“Kesi unaitaka mwenyewe. Siku hizi mume wangu nikikuomba pesa una majibu mabaya sana, sijui ni kwanini.”

“Majibu mabaya yapi niliyokujibu au unaanza maneno...!”

“Basi bwana. Naona labda una mwenzangu unayempa. Akufukuzae hakwambii toka.”

Nilipomwambia hivyo niliinuka nikamuacha kwenye kochi. Nikaingia zangu chumbani.

Asubuhi kulipokucha, mume wangu alipotoka kwenda kazini, niliinua godoro. Nilikuwa nikihifadhi pesa zangu chini ya godoro. Nikatoa shilingi laki moja za mganga na kuzitia kwenye pochi yangu kisha nikaliweka godoro vizuri.

Baada ya hapo nikampigia simu Mwanaisha.

“Habari ya asubuhi, shoga?” nikamsalimia.

“Nzuri shoga. Umeamkaje?”

“Nimeamka salama. Ndiyo nataka nitoke niende kule.”

“Vipi, umepata vile vitu ulivyoagizwa?”

“Nimevipata.”

“Basi nenda. Kama nilivyokwambia jana, leo sitapata nafasi ya kukusindikiza. Kuna mahali nataka kwenda.”

“Haina neno. Nilitaka kukufahamisha tu.”

“Sawa.”

Nikakata simu na kujiandaa na safari ya kwenda kwa mganga. Nilipokuwa tayari nilitoka. Nilikwenda stendi nikapanda daladala ya Mwahako. Nilipofika nikaanza kutembea kwa miguu hadi nikafika katika ile nyumba ya mganga.

Niliwakuta wale wanawake wakishughulika na kazi zao. Nikawasalimia kisha nikawauliza:

“Nimemkuta mganga?”

“Mganga yupo, karibu,” mwanamke mmoja akanijibu.

Nikapitiliza hadi katika mlango wa kile chumba cha mganga. Mlango ulikuwa wazi. Nikapiga hodi. Mganga aliponiambia “karibu” nikaingia.

“Shikamoo,” nikamuamkia mganga huyo aliyekuwa akisoma kitabu cha Kiarabu.

“Marahaba. Habari ya huko?” akaniuliza.

“Nzuri.”

“Karibu ukae.”

Nikakaa.

“Vile vitu nilivyokuagiza umevipata?” akaniuliza.

“Nimevipata,” nikamwambia.

Nikafungua pochi yangu na kutoa kile kitambaa kilichokuwa na mchanga pamoja na kipakiti kilichokuwa na nyuzi. Nikampa.

Alikifungua kile kitambaa na kile kipakiti kisha akaviweka chini.

“Sasa mama itabidi uvue nguo zako zote ubaki mtupu!” mganga akaniambia.

Nikashituka.

“Nivue nguo zote mpaka za ndani?” nikamuuliza nikiwa nimemtolea macho ya mshangao.

Mganga hakujali macho yangu. Akanijibu kwa utulivu:

“Ndiyo. Vua mpaka nguo yako ya ndani.”

Kwa vile ni jambo ambalo sikulitarajia, kwanza nilisita, nikawa najiuliza:

“Nivue nguo nibaki mtupu mbele yake?”

“Nikishavua ndiyo itakuwaje?” nikamuuliza.

“Ndiyo uganga wako utakapofanyika.”

“Hata Mwanaisha naye alivua nguo?”

“Usitake kujua mambo ya mwenzako. Wewe jua yako yaliyokuleta hapa. Masharti ya uganga wako ni lazima uvue nguo. Mimi pia nitavua.”

Mama yangu!

“Tutakuwa hatuna nguo sote wawili?”

“Ndiyo.”

“Huyu mganga asije akanibaka!” nikajiambia kimoyomoyo.

Lakini nikaona asingeweza kunifanyia kitu kama hicho kwa kuwa huko uani kulikuwa na watu, pengine mmoja wao alikuwa mke wake. Pia nilijiambia aliyenileta pale alinipa sifa za yule mganga. Labda nikivua nguo ndiyo mafanikio yatakapokuja.

“Maji ukiyavulia nguo, yaoge mama,” mganga akaniambia alipoona nafikirifikiri.

Aliponiambia hivyo alisimama na kusindika mlango. Kidogo ndani ya kile chumba kukawa na giza lakini bado tulikuwa tunaonana. Aliposindika mlango aliifungua shuka yake aliyokuwa amejifunga na kuitupa chini. Sikutaka hata kumtazama. Na mimi nikasimama na kugeuka upande mwingine. Nikaanza kupembua nguo zangu moja baada ya nyingine.

Nilikuwa nimelazimika kufanya kitendo ambacho moyo wangu ulikuwa haukitaki. Lakini moyo huo huo ukaniambia, “Potelea mbali.”