Dili iliyokufa -26
ILIPOISHIA
“Familia yako ilifikaje hapa Tanga?’
“Mimi nilizaliwa Tanga na nilikuwa nikilelewa katika kituo cha watoto yatima kilichoko pale Kwaminchi. Kuna mzungu alikuja kunichukua ili kunilea. Yeye ndiye alinipeleka Zambia nikiwa mdogo sana”
“Yuko wapi huyo mzungu hivi sasa”
Alifariki dunia tangu mwaka jana, ndio nikaamua kurudi Tanga kuitafuta familia yangu”
SASA ENDELEA...
“Ulifika katika hicho kituo cha yatima?”
“Ndiyo, nilifika. Wakanitambua, lakini wakaniambia wao hawaijui familia yangu isipokuwa nihangaike mwenyewe kuitafuta.”
“Uliambiwa ni nani aliyekupeleka katika kituo hicho?”
“Nilipelekwa nikiwa mtoto sana. Mimi mwenyewe sikumbuki. Na sikupata maelezo ya kutosha kwa sababu uongozi wa kile kituo umebadilika; si ule wa zamani.”
Kwa kutaka kuthibitisha maelezo ya yule kijana, Wakwetu alimwambia:
“Tunaweza kwenda pamoja katika hicho kituo?”
“Kwa ajili gani?”
“Kwa ajili ya kujua historia yako na kuweza kukusaidia kuijua familia yako.”
“Sawa, twende.”
Walifika katika kile kituo cha kulelea yatima kilichoko Kwaaminchi. Walikutana na mkuu wa kituo hicho ambaye alimuuliza Masumbuko:
“Wewe si ulikuja juzi hapa kuitafuta familia yako?”
“Ndiye mimi.”
“Umeshaipata?”
“Sijafanikiwa bado.”
“Nilikwambia si rahisi kuipata kwa sababu wewe ulilelewa katika kituo cha yatima na uliletwa ukiwa mtoto....”
“Ngoja niingilie kidogo...” Wakwetu akamkatiza.
“Wewe ni nani?”
“Nitakufahamisha.”
Wakwetu akamueleza mkasa uliomtokea yule kijana na jinsi alivyoweza kumfahamu hospitalini.
Mkuu wa kituo cha yatima akashangaa aliposikia mkasa huo.
“Mimi sina habari kabisa!” alisema.
“Hivi ndiyo anatoka hospitalini.”
“Vijana wa mjini walidhani ana pesa.”
“Sasa lengo langu kubwa ni kujaribu kumsaidia. Nimekuja naye hapa ili tupate kumbukumbu zake, tujue aliletwa mwaka gani, aliletwa na nani na wazazi wake walikuwa kina nani.”
“Mafaili ya vijana wote yanahifadhiwa. Kumbukumbu zao tunakuwa nazo, lakini mafaili ni mengi, na kulipata faili lake ni kazi pevu kwa sababu ni la miaka mingi.”
“Tafadhali ifanye hiyo kazi kwa gharama yoyote. Kama hutakuwa na nafasi, tafuta mtu mwingine akusaidie. Nitamlipa.”
Wakwetu alitoa noti mbili za shilingi elfu kumi kumi akampa.
Mkuu wa kituo cha yatima alipozipokea shilingi elfu ishirini alisema:
“Kuna kijana nitampatia hizi pesa atusaidie. Njoo baada ya saa mbili. Hilo faili litakuwa limeshapatikana.”
Wakwetu alijua kuwa hakukuwa na kijana yeyote ambaye angepewa pesa hizo, bali zilikuwa zake yeye, na faili angelitafuta mwenyewe.
“Sawa. Tutakuja muda huo. Ninaweza kuja peke yangu au nikiwa na huyu kijana?”
“Sawa, hakuna tatizo.”
Wakwetu na Masumbuko wakaondoka.
“Sasa nikurudishe kule gesti?” Wakwetu akamuuliza Masumbuko wakiwa kwenye gari.
“Ndiyo, nirudishe.”
“Hapana. Nitakupeleka mahali penye usalama zaidi.”
“Wapi?”
“Kwenye hoteli kubwa.”
“Nitashukuru sana.”
Wakwetu alimkodishia Masumbuko chumba katika hoteli moja. Halafu alimpatia shilingi laki moja.
“Kaa hapa, nitakuona baadaye.”
“Sawa, mzee.”
Wakwetu alikwenda kazini kwake. Ilipofika saa sita aliondoka na kurudi tena katika kile kituo cha yatima. Alikuta faili la Masumbuko likiwa juu ya meza. Jinsi lilivyokuwa, lilionyesha lilifutwa vumbi dakika chache tu zilizopita.
“Faili lake hili hapa,” mkuu wa kituo hicho alimwambia Wakwetu, kisha akaongeza:
“Lilipatikana ndani sana.”
“Linasemaje?”
“Ngoja nikusomee.”
Mkuu wa kituo hicho alifungua faili hilo na kuanza kumsomea.
“Masumbuko aliletwa katika kituo hiki akiwa na pacha wake miaka kumi na minane iliyopita. Walikuwa na umri wa miaka mitano kila mmoja. Waliletwa na mwanamke mmoja Mwarabu aliyeitwa Kulthumu Mohamed aliyekuwa akiishi maeneo ya Nguvumali.
“Mwanamke huyo alitoa maelezo kwamba watoto hao walikuwa yatima; hawakuwa na baba wala mama.
Yeye aliwachukua wakiwa wachanga kutoka kwa bibi mmoja ambaye hakuwa na uwezo wa kuwalea. Bibi huyo alifariki siku chache baadaye. Mapacha hao walikuwa wajukuu zake. Nadhani wazazi wao walikuwa wamefariki.
“Yule mwanamke aliwalea mpaka walipofikisha umri wa miaka mitano kila mmoja, halafu mume wake alifariki dunia, na yeye akaamua kurudi kwao Uarabuni. Ndipo alipowaleta hapa, nasi tukawapokea.
“Walipoanza masomo ya msingi, Masumbuko alikuja kuchukuliwa na mzungu mmoja ambaye alisema angekwenda kumlea na kumpa elimu. Tangu alipochukuliwa hakuonekana tena mpaka juzi alipokuja na kujitambulisha mwenyewe. Akatuambia kwamba alikuwa Zambia.
“Mwenzake naye alichukuliwa na mchungaji wa kanisa moja akiwa na umri wa miaka saba. Naye hajafika tena hapa.”
Mkuu wa kituo hicho alimaliza na kulifunga faili hilo.
Wakwetu alishusha pumzi ndefu.
“Katika mazingira kama hayo itakuwa vigumu kwa Masumbuko kuipata familia yake,” mkuu wa kituo hicho alimwambia Wakwetu.
Hata hivyo, Wakwetu hakumsikiliza. Alikuwa katika lindi la mawazo. Uso wake ulikuwa umetaharuki.
“Asante sana. Nimefurahi kuisikia historia fupi ya Masumbuko. Nitajitahidi kumsaidia,” alisema baada ya kuzinduka.
Akanyanyuka, akamuaga mkuu wa kituo hicho, kisha akatoka.
Alirudi nyumbani kwake. Alijihisi amepatwa na fadhaa. Mawazo ya mchanganyiko yalikuwa yamekichafua kichwa chake. Hakuzungumza chochote na mke wake. Aliingia chumbani, akaoga na kubadili nguo, kisha akakwenda kuketi sebuleni.
Alipokuwa ameketi huku akichezea simu yake, alikumbuka kitu. Alikumbuka kwamba alisahau kumuuliza yule mkuu wa kituo cha yatima kuhusu mtoto wa pili aliyechukuliwa na mchungaji. Alitaka kujua mtoto huyo alipelekwa wapi na mchungaji huyo alikuwa wa kanisa gani.
Aliona ilikuwa muhimu apate taarifa hizo siku hiyohiyo, akaamua kurudi tena kwenye kile kituo cha yatima. Akamuaga mke wake na kutoka. Sharifa alipomwona Wakwetu akiwa amefadhaika, alishindwa hata kumuuliza anakwenda wapi.
Kwa kuwa aliona angehitaji safari nyingi, Wakwetu alimfuata James ili amuendeshe, ingawa muda wa kazi wa James ulikuwa umekwisha. James akampeleka katika kituo hicho cha yatima. Alipokuwa anasimamisha gari, alimuuliza Wakwetu:
“Mzee, umefuata nini hapa?”
“Nina shughuli kidogo,” Wakwetu akamjibu.
“Unajua hapa ndipo nilipolelewa mimi, na sijafika tena tangu nilipoondoka.”
“Kumbe wewe ulilelewa hapa?” Wakwetu akamuuliza kwa mshangao.
“Nililelewa hapa. Nilikuja kuchukuliwa na Mchungaji Antony James Hiza akanilea yeye. Yeye ndiye aliyenipa jina la James.”
Wakwetu alishtuka. Akajiuliza, isije kuwa huyu ndiye ndugu yake Masumbuko?
“Ulikuwa na pacha wako aliyechukuliwa na mzungu?”
“Niliambiwa hivyo. Umejuaje?”
“Hebu twende ndani.”
Walishuka kwenye gari wakaingia ndani ya kituo hicho. Mkuu wa kituo hicho alikuwa anatoka, wakakutana.
“Nimerudi tena,” Wakwetu akamwambia.
“Una shida gani tena?”
“Ninakuomba turudi ofisini. Kuna maswali mawili matatu nataka kukuuliza.”
Wakaenda ofisini.
Walipoketi, Wakwetu akamuuliza mkuu wa kituo hicho:
“Hivi yule mchungaji aliyemchukua yule mtoto wa pili anaitwa nani?”
Lile faili lilikuwa bado lipo juu ya meza. Mkuu wa kituo hicho akalifungua na kupekua nyaraka zilizokuwa ndani.
“Anaitwa Mchungaji Antony James Hiza,” akamwambia.
Wakwetu akageuza uso na kumtazama James.
“Ulichosema ni kweli,” alimwambia.
“Mzee, unanikumbuka mimi?” James akamuuliza yule mkuu wa kituo cha yatima.
Mkuu wa kituo hicho alimtazama na kumuuliza:
“Kwani wewe ni nani?”
“Mimi ndiye niliyechukuliwa na Mchungaji Antony James Hiza kutoka katika kituo hiki.”
“Unasema kweli?”
“Kweli kabisa.”
Mkuu wa kituo hicho cha yatima alishangaa.
“Umekuwa mkubwa sasa. Ulikuwa wapi?” alimuuliza James.
“Niko hapa hapa Tanga. Nimeajiriwa na mzee Wakwetu.”
Aliposema hivyo, James alielekeza mkono wake kwa Wakwetu.
“Kumbe kijana ni mfanyakazi wako?” mkuu wa kituo cha yatima akamuuliza Wakwetu.
“Ni mfanyakazi wangu, lakini wakati namuajiri sikujua kama alitoka katika kituo hiki. Alinieleza leo.”
“Vizuri sana. Sasa yule mchungaji aliyekuchukua kwa sasa yuko wapi?” mkuu wa kituo cha yatima akamuuliza James.