Dili iliyokufa - 25
ILIPOISHIA
Wakwetu alipatwa na mshangao. Alielezwa jambo ambalo hakulitarajia.
Majaliwa aliendelea:
“Kila mara alikuwa akiniambia hivyo. Mwisho nikaona imefika kikomo. Ndipo nikamuahidi nikutane naye kule gesti.”
Majaliwa aliposita, Sharifa alimsemea:
“Ndipo ukaja kuiba bastola ya baba yako?”
“Ndiyo,” Majaliwa alijibu kwa sauti ya chini.
“Halafu mlipokutana hapo gesti ikawaje?” Sharifa akajifanya anamuuliza.
“Tulikuwa chumbani, akaanza kuni...”
“Kukufanya nini?” Sharifa aliendelea kumuongoza Majaliwa ili kufanikisha uongo wao.
“Alikuwa ananipapasa kama shoga, halafu akaishika suruali yangu ili anivue. Ndipo nilipotoa bastola na kumpiga risasi.”
“Kwanini hukuenda kutoa taarifa polisi ukaamua kumpiga risasi?” Wakwetu alimuuliza, lakini hakuwa na nguvu tena.
“Mimi nilitaka kumtisha tu ili asirudie tena, lakini risasi ilifyatuka kwa bahati mbaya.”.
SASA ENDELEA...
“Bado ulifanya kitendo cha hatari, kwa sababu kama ungekamatwa ungekabiliwa na kesi ya kutaka kuua”
“Ni kweli baba, baada ya kufikiri niliona nilifanya kitendo kibaya na ninaomba msamaha kwenu”
“Unajua hasira mume wangu…” Sharifa akadakia. “Ukiwa na hasira unaweza kufanya jambo baya bila kujua, baadaye ndio unajuta”
“Mimi sikumfiria yule kijana kuwa anaweza kuwa na tabia hiyo. Anaonekana kuwa mpole sana” Wakwetu alisema.
“Huo ni upole wa nje tu, ndani ya moyo wake hujui kulivyo. Vijana wengi wa siku hizi wameharibika. Huwezi hata kuwadhania. Wanataka kumuharibu mwenzao!” Sharifa alipiga chapuo na kulaani.
Akaongeza. “Mimi kwa upande wangu nimekusamehe mwanangu. Kama sababu ya kumpiga risasi huyo kijana ilikuwa ni hiyo, nimekusamehe na naamini baba yako pia atakusamehe”
“Kwa bahati njema ile kesi imekwisha lakini usirudie tena kitendo kama hicho ni cha hatari sana” Wakwetu alisema sasa sauti yake ikionesha huruma.
“Sawa baba, sitarudia tena”
“Bado nakusisitiza kuwa uwe mtu mzuri, ujiepushe na makundi kundi ya vijana wasio na tabia njema. Umenielewa?”
“Nimekuelewa baba”
“Baada ya hapo napenda kukwambia kuwa nimekunjua moyo wangu na nimekusamehe”
“Nakushukuru baba yangu kwa kuonesha mapenzi juu yangu. Nakushukuru pia mama kwa imani yako juu yangu”
Sharifa akatabasamu. Akanyanyuka na kukumbatiana na Majaliwa. Baada ya kumaliza kukumbatiana na mama yake, Majaliwa alimfuata baba yake ambaye alinyanyuka wakakumbatiana.
Baadhi ya wanawake hatari!
Baada ya kukumbatiana na baba yake, Sharifa alimuuliza.
“Umeshakula?”
“Bado sijakula”
“Haya njoo nikuwekee chakula, ule halafu upumzike”
Sharifa alikwenda kumtayarishia chakula Majaliwa kisha akakaa naye mezani. Wakwetu aliwaacha akaingia chumbani.
“Umezungumza vizuri sana” Sharifa alimwambia mwanawe wakati anakula. Sauti yake ilikuwa ya chini.
Majaliwa hakumjibu zaidi ya kutabasamu.
“Zile dawa za yule mganga pia zimefanya kazi kidogo” aliendelea kumueleza.
“Ni kweli. Baba amenikubalia mara moja” Majaliwa alimkubalia.
“Alikuwa hataki kusikia habari zako. Alikuwa mkali kama pilipili. Sikutarajia kama angekukubali kirahisi hivi”
“Ninaamini sasa tutaelewana”
“Mimi nataka muelewane na uwe na heshima ili aone kuwa umejirekebisha”
“Sawa mama”
Majaliwa alipomaliza kula mama yake alimuondolea vyombo.
“Sasa nenda chumbani kwako ukaweke vitu vizuri”
Majaliwa aliondoka kwenye kiti na kuingia chumbani mwake. Baada ya kupeleka vyombo jikoni Sharifa aliingia chumbani kwa mume wake.
“Majaliwa sasa amejirudi” alimwambia Wakwetu huku akiketi kitandani.
Wakwetu alikuwa amejinyoosha kitandani akitafakari.
“Nimemsamehe kosa lake lakini akirudia tena makosa, namfukuza kabisa”
“Hawezi kurudia. Amejirudi isitoshe sababu aliyoitoa inakubalika”
“Majaliwa alipaswa kuja kutuambia sisi kabla ya kuchukua hatua aliyochukua”
“Labda kosa lake ni hilo lakini mimi nalichukulia ni sababu ya utoto tu”
“Kila siku ni utoto, atakua lini sasa!”
Sharifa akabakia kutoa kicheko cha uongo kisha akajilaza pembeni mwa Wakwetu.
*************
Asubuhi iliyofuata Wakwetu alikwenda hospitali ya Bombo kumjulia hali yule kijana aliyepigwa risasi. Usiku uliopita alimfikiria sana. Alimfikiria kwa sababu maneno aliyoelezwa na Majaliwa hayakulingana na muonekano wa kijana huyo.
Kijana huyo alionekana mpole na asiye na itikeli za kimjini tofauti na alivyomueleza Majaliwa kuwa alikuwa akitaka kumfanyia vitendo visivyofaa. Wakwetu hakumuamini Majaliwa moja kwa moja. Nusu alimuamini na nusu hakumuamini.
Asubuhi kulipokucha akaona aende hospitali kumdadisi ili kupata ukweli zaidi. Alipofika alimkuta Masumbuko akiruhusiwa kuondoka hospitali baada ya hali yake kutengemaa.
“Shikamoo baba” alimwamkia Wakwetu huku akiinuka kwenye kitanda alipokuwa ameketi.
“Unajionaje hali yako?” Wakwetu akamuuliza.
“Kwa sasa sijambo”
“Naona ndio umeruhusiwa kuondoka?”
“Nimeruhusiwa na ndio ninaondoka”
“Unaishi wapi?”
Kijana hakujibu.
“Ukitoka hapa unakwenda wapi?” Wakwetu akamuuliza tena.
“Sijajua bado”
Jibu hilo likamtia shaka Wakwetu.
“Kwanini unasema hujajua bado?”
“Mimi ni mgeni hapa Tanga.”
“Twende, nina gari. Nitakusaidia lifti”
Walitoka nje ya hospitali. Wakwetu akampakia Masumbuko kwenye gari lake.
“Wewe hukai Kwaminchi?” Wakwetu alimuuliza kijana huyo mara tu alipoliondoa gari.
Masumbuko akatikisa kichwa.
“Sikai Kwaminchi.”
“Umeniambia ni mgeni hapa Tanga, unatoka wapi?”
“Natoka Zambia”
“Wewe ni mwenyeji wa Zambia?”
“Hapana”
“Ni mwenyeji wa wapi?”
Kijana huyo alinyamaza.
“Sasa ungependa nikupeleke wapi?”
“Nilikuwa nimepanga chumba kwenye gesti moja.”
“Kwa hiyo ungependa nikupeleke huko”
“Ndiyo”
“Hebu niambie ni tukio gani lililokukuta hadi ukalazwa hospitali?”
“Kuna kijana alinipiga risasi”
“Kwanini”
“Sijajua bado”
“Alikupiga risasi ukiwa wapi?”
“Nikiwa hapo gesti”
“Ulimfanya nini”
“Sikumfanya kitu na pia kijana mwenyewe simfahamu”
“Hebu nieleze vizuri, ilikuwaje mpaka akakupiga risasi?’
Masumbuko alinyamaza kidogo. Akaonekana kutafakari kisha akamtazama Wakwetu.
“Ilikuwa kama saa mbili usiku nikiwa pale gesti. Kuna kijana mmoja alikuja chumbani kwangu. Alibisha hodi kisha akaingia ndani. Alipoingia ndani alinisalimia vizuri kisha akaniuliza kama mimi ndiye Masumbuko. Nikamwambia ni mimi”
“Ndiyo…”
“Nilipomjibu hivyo alitia mkono ndani ya shati lake, akatoa bastola aliyokuwa ameipachika kiunoni na kunielekeza nayo. Kwa kweli nilishituka sana. Nikapurukushana naye lakini akawahi kunifyatulia risasi. Basi sikujua tena kilichotokea”
“Ukaja kujikuta upo hospitali?”
“Ndiyo”
“Tuseme alitaka kukuibia pesa zako?’
“Sijui lakini pesa nilizokuwa nazo mfukoni, nilirudishiwa na polisi jana. Pesa zangu hazikuibiwa”
“Sasa huyo aliyekupiga risasi lengo lake lilikuwa nini?”
“Sijajua”
“Je ukimuona unaweza kumjua?”
“Sidhani kama nitaweza kuijua sura yake kikamilifu kwa sababu ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kumuona ila alikuwa mfupi kiasi na mweusi” Hivyo ndivyo alivyokuwa Majaliwa.
“Unaitwa nani?” Wakwetu aliendelea kumuuliza Masumbuko.
“Naitwa Masumbuko”
“Masumbuko uliniambia kuwa unatoka Zambia, ulifuata nini hapa?”
“Hapa nimekuja kuitafuta familia yangu” Masumbuko alimjibu.
“Familia yako iko wapi?”
“Sijajua lakini najua ipo hapa Tanga.”
“Familia yako ilifikaje hapa Tanga?’
“Mimi nilizaliwa Tanga na nilikuwa nikilelewa katika kituo cha watoto yatima kilichoko pale Kwaminchi. Kuna mzungu alikuja kunichukua ili kunilea. Yeye ndiye alinipeleka Zambia nikiwa mdogo sana”
“Yuko wapi huyo mzungu hivi sasa”
Alifariki dunia tangu mwaka jana, ndio nikaamua kurudi Tanga kuitafuta familia yangu”