Dili iliyokufa -24
ILIPOISHIA
“Kweli mama? Kwa hiyo nirudi leo?”
“Subiri kwanza. Nataka niuelewe msimamo wake vizuri”
“Mpaka lini?”
“Nitakwambia”
“Sawa”
Sharifa akakata simu.
Majaliwa alikwenda kwa wakala wa kuweka na kutoa pesa kwenye simu. Akatoa shilingi elfu tisini. Baada ya hapo alikwenda kupanda daladala. Akaenda Machui.
SASA ENDELEA...
Alipoingia nyumbani kwa yule mganga alimpatia shilingi elfu hamsini.
“Mama amenipa nikuletee,” akamwambia.
“Sawa.”
“Haya, naenda.”
“Karibu.”
Majaliwa aliporudi kule gesti, alimpigia simu mama yake na kumwambia kuwa ameshampelekea mganga pesa zake.
“Amekwambia nini?” Sharifa akamuuliza.
“Hakuniambia kitu.”
“Sawa. Sasa umesharudi?”
“Ndiyo, nipo gesti.”
“Haya, tulia. Usizurure ovyo.”
“Sawa, mama.”
Majaliwa akakata simu.
Saa saba mchana, Wakwetu alirudi nyumbani. Neno la kwanza alilomuuliza Sharifa lilikuwa:
“Umempigia Majaliwa?”
“Sijampigia bado.”
“Kwanini? Si nimekwambia umpigie umwambie arudi?”
“Uliniambia, lakini nilibanwa na kazi.”
“Mpigie sasa hivi.”
Sharifa alisita. Hakutaka kuzungumza na Majaliwa mbele ya Wakwetu. Kulikuwa na mambo mengi aliyotaka kumfundisha ili atakapokuja na kuulizwa na baba yake aweze kumjibu.
Lakini hakutaka kuipoteza nafasi aliyoitoa mume wake. Akaingia chumbani na kuchukua simu yake. Laiti Wakwetu angekuwa mbali kidogo, angempigia mwanawe na kumfundisha majibu ya kumpa baba yake. Lakini Wakwetu alikuwa karibu sana. Kwa vyovyote vile asingeweza kumpigia.
Sharifa alitoka na simu, akasimama karibu na mlango na kupiga namba tofauti. Kisha akamwambia mume wake:
“Simu ya Majaliwa haipatikani.”
“Jaribu kumpigia tena.”
Sharifa alirudia kuipiga ile namba ambayo haikuwa sahihi, kisha akatikisa kichwa.
“Haipatikani.”
“Mtoto mwenyewe haeleweki. Kwanini anazima simu?”
“Labda imeishiwa chaji.”
“Basi utajaribu baadaye.”
Sharifa akairudisha simu chumbani. Aliporudi sebuleni, alimuuliza Wakwetu:
“Yule kijana aliyepigwa risasi na Majaliwa anaendeleaje?”
“Sijafika hospitalini tangu juzi, lakini nitakwenda kumuona kesho.”
“Pengine atakuwa amesharuhusiwa.”
“Sidhani. Atakuwa bado yupo.”
“Lakini wewe hutakuwa unahusika naye tena.”
“Sihusiki naye, ila ninataka kumsaidia, na niliwaahidi hivyo madaktari.”
“Utaingia gharama za bure. Ungemuacha tu.”
“Hapana, si vizuri. Pia ninataka kujua alimkosea nini Majaliwa. Ninaamini hakumpiga risasi bure.”
Sharifa akanyamaza kimya.
Wakwetu baada ya kula chakula cha mchana, ambacho pia kiliwekwa dawa na Sharifa, alitoka kwenda kazini kwake. Mara tu alipotoka, Sharifa akampigia simu Majaliwa.
“Sikiliza, Majaliwa. Baba yako alipokuja kula chakula cha mchana aliniambia nikupigie nikwambie urudi nyumbani, lakini nilishindwa kukupigia muda ule kwa sababu kulikuwa na mambo nataka kukufundisha,” akamwambia mwanawe.
“Mambo gani?”
“Utakapokuja akikuuliza ulikuwa wapi, mwambie ulikuwa Kwaminchi kule ulikokuwa umepangisha chumba. Utamwambia uliishi na wale watu kwa sababu mlikuwa mmezoeana. Umeelewa?”
“Ndiyo, nimekuelewa mama.”
“Na akikuuliza kwanini ulimpiga risasi yule kijana aliyelazwa Bombo, mwambie yule ni kijana muhuni ambaye alitaka kukufanyia kitendo cha ulawiti. Muanzie mbali kwamba kila siku yule kijana alikuwa anakutongoza kama mwanamke.”
“Ndiyo.”
“Siku ile ndipo uliahidiana naye mkutane pale gesti, ambapo ulichukua bastola kwa lengo la kutaka kumkomesha. Ukimweleza hivyo, utamaliza kabisa hasira yake, isipokuwa usisahau kumuomba msamaha kwa mara nyingine.”
“Sawa. Nimekuelewa.”
“Sasa ikifika saa kumi na moja, wewe uje hapa nyumbani. Atakuwa amesharudi. Nataka ukija utukute tuko sote.”
“Sawa mama, nitakuja saa kumi na moja.”
“Usisahau nilivyokueleza.”
Sharifa, baada ya kumkumbusha, alikata simu. Alisubiri hadi ilipofika saa kumi, akampigia Wakwetu.
“Nimeshampigia Majaliwa. Amesema atakuja,” alimwambia kwenye simu.
“Sawa,” Wakwetu akamjibu.
“Nadhani itakuwa hatua nzuri ya kumrekebisha.”
“Ni hapo atakapokuja tutaonana naye.”
“Sawa.”
Sharifa akakata simu. Kidogo sasa moyo wake ulikuwa na furaha. Kama alikuwa na wasiwasi, ulihusu Majaliwa kushindwa kujieleza vizuri kwa baba yake. Lakini aliamini kuwa angeweza kujieleza, kwa vile alimsisitizia sana suala hilo.
Saa kumi na nusu, Wakwetu akawasili nyumbani. Alipoketi tu sebuleni akauliza:
“Majaliwa ameshafika?”
“Hajafika bado, lakini nilimpata kwenye simu nikamwambia aje,” Sharifa alimweleza.
“Mbona hajafika?”
“Naamini atafika.”
“Alikwambia yuko wapi?”
“Ameniambia yuko Kwaminchi.”
“Kwaminchi kwa nani?”
“Kule alikokuwa akiishi zamani.”
“Ndiyo aliamua kurudi kule?”
“Si unajua akili za watoto. Alikuwa hana pa kwenda pengine.”
Wakwetu alinyamaza na kunyanyuka. Aliingia chumbani, akabadilisha nguo na kuvaa teitei. Alirudi tena sebuleni. Wakati anaketi, Majaliwa akabisha mlango.
“Karibu,” Sharifa akamwitikia.
Majaliwa akafungua mlango na kuingia.
Aliingia taratibu kama vile alikuwa mgeni wa nyumba hiyo. Aliusukuma mlango kwa upole na kuufunga, kisha akamfuata Wakwetu kwa unyenyekevu na kumuamkia.
“Shikamoo baba.”
“Marahaba.”
Baada ya kuitikiwa, alimfuata mama yake.
“Shikamoo mama.”
“Marahaba mwanangu. Hujambo?”
“Sijambo mama.”
“Karibu, ukae.”
Majaliwa akaketi kwenye kochi karibu na mama yake.
“Majaliwa, ulikuwa wapi?” Wakwetu akamuuliza.
“Nilikuwa Kwaminchi.”
“Kwaminchi kwa nani?”
“Kule nilikokuwa nikiishi zamani.”
“Kwanini uliondoka bila kuaga, na kwanini ulikwenda kukaa Kwaminchi?”
“Kwa sababu nilifanya makosa.”
“Makosa gani?”
“Kwanza niliiba bastola yako, baba, na pili nilichukua gari bila ruhusa yako.”
“Ni kwanini ulifanya hivyo?”
Majaliwa aliinamisha uso wake na kunyamaza kimya.
“Ulipoiba bastola yangu na kuchukua gari langu bila ruhusa, ulikwenda kufanya nini?”
“Kuna kijana nilikwenda kumpiga risasi,” Majaliwa alijibu huku akiangalia chini.
“Hapo ndipo nilipokuwa nataka kufika. Huyo kijana alikufanya nini?”
“Alikuwa ananifanyia vitendo vya kihuni.”
“Vitendo gani?”
Majaliwa akanyamaza kimya. Alikuwa akitafuta ujasiri wa kumweleza vile alivyofundishwa na mama yake. Upande mmoja wa moyo wake ulikuwa tayari kueleza. Alikuwa ameshapanga maneno yote ya kusema. Lakini upande mwingine wa moyo huo huo ulikuwa na woga.
Ule upande uliokuwa na ujasiri ulikuwa ukijaribu kuushinda ule wenye woga ili awe tayari kuzungumza. Kwa sekunde kadhaa alizokaa kimya, alikuwa akikusanya nguvu za kuzungumza.
“Majaliwa, niambie. Huyo kijana alikufanyia vitendo gani vya kihuni hadi ukaamua kwenda kumpiga risasi?” Wakwetu alimuuliza alipoona yuko kimya.
Swali hilo lilimpa Majaliwa ujasiri. Akaanza kueleza.
“Yule kijana alikuwa akiniambia anataka kunigeuza kama mke wake, yaani anifanyie vitendo ambavyo ni kinyume na maumbile.”
Wakwetu alipatwa na mshangao. Alielezwa jambo ambalo hakulitarajia.
Majaliwa aliendelea:
“Kila mara alikuwa akiniambia hivyo. Mwisho nikaona imefika kikomo. Ndipo nikamuahidi nikutane naye kule gesti.”
Majaliwa aliposita, Sharifa alimsemea:
“Ndipo ukaja kuiba bastola ya baba yako?”
“Ndiyo,” Majaliwa alijibu kwa sauti ya chini.
“Halafu mlipokutana hapo gesti ikawaje?” Sharifa akajifanya anamuuliza.
“Tulikuwa chumbani, akaanza kuni...”
“Kukufanya nini?” Sharifa aliendelea kumuongoza Majaliwa ili kufanikisha uongo wao.
“Alikuwa ananipapasa kama shoga, halafu akaishika suruali yangu ili anivue. Ndipo nilipotoa bastola na kumpiga risasi.”
“Kwanini hukuenda kutoa taarifa polisi ukaamua kumpiga risasi?” Wakwetu alimuuliza, lakini hakuwa na nguvu tena.
“Mimi nilitaka kumtisha tu ili asirudie tena, lakini risasi ilifyatuka kwa bahati mbaya.”