Dili iliyokufa -23
ILIPOISHIA
Sharifa akagutuka.
“Nibaki uchi kabisa?”
“Ndio uganga wenyewe mama”
“Mh!” Sharifa akaguna.
“Umesema unataka uwahi kurudi, mbona unasita sita au tuache?’
“Tusiache, nilikuwa nawaza tu”
“Unawaza nini?”
“Kitu chenyewe umeniambia kwa ghafla, sikuwa nimejiandaa”
“Wenzako wengi wamefanikiwa, ukienda kwa daktari kuwa tayari na utakachoambiwa”
“Sawa, ngoja nivue kwa sababu nina shida”
Sharifa alivua gauni akabaki na nguo za ndani.
“Endelea kuvua,” Mganga akamwambia.
SASA ENDELEA...
“NIVUE na chupi?’
“Ndiyo”
“Mh!”
Sharifa aliguna lakini alivua. Akabaki na sidiria tu.
“Nataka nikuchanje katika sehemu zako za siri ili nikutie dawa yangu ambayo itampagawisha mzee” Mganga alimwambia Sharifa akiwa ameshika tunguri mkononi.
“Chanja tu”
“Lala kichalichali”
Sharifa akalala kichalichali huku moyo wake ukiwa na wasiwasi wa kubakwa. Mganga alimchanua miguu akamchanja chale tatu shemu za siri kisha akampaka dawa.
“Sasa inuka uvae nguo zako”
Sharifa akainuka na kuvaa.
“Hakikisha leo usiku mnakutana ndio dawa itashika sawa sawa”
Sharifa alimuelewa akajaribu kucheka ingawa uso wake ulikuwa umefadhaika.
“Sawa” akamjibu.
“Nitakupa dawa ambayo utamtilia kwenye chakula”
“Sawa”
Mganga alimfungia dawa hiyo ya unga unga kwenye karatasi akampa.
“Ukifika nyumbani utapuna visigino vyako kwa kiwembe. Ule unga unga utakaotoka utautia kwenye hii dawa halafu utamtilia kwenye chakula kwa muda wa siku tatu”
“Hicho chakula mimi nisile”
“Ni hiyari yako, ukiamua kula haina madhara”
“Sawa. Na ni wakati gani, asubuhi, mchana au usiku?”
“Ni wakati wowote utakaopata nafasi. Mtilie mara moja kwa siku, kiasi kidogo tu”
Sharifa alikuwa ameshamaliza kuvaa, akakichukua kile kikaratasi kilichofungwa dawa akakitia kwenye pochi yake.
“Unanihakikishia kuwa atabadilika?’
“Sana. Utakuja kuniambia”
“Nitashukuru sana”
Sharifa alitoa shilingi laki moja kutoka kwenye pochi yake akampa mganga.
“Hiyo pesa iliyobaki kama nilivyokwambia nitampa mwanangu akuletee kesho”
“Usisahau tu.”
“Sitasahau, nitampa”
“Sasa mnaweza kwenda zenu”
Sharifa akamuaga yule mganga na kutoka. Mwanawe alikuwa akisubiri kwenye teksi. Na yeye akajipakia. Wakaondoka.
Wakati teksi ikiwa kwenye mwendo Majaliwa alimuuliza mama yake.
“Yaani baba kutoka leo ataondoa kinyongo na mimi?”
Sharifa hakupenda Majaliwa azungumze maneno yale mbele ya yule dereva wa teksi,akajifanya kama hakumsikia.
“Kama siamini vile…” Majaliwa aliendelea.
Sharifa akamtazama kwa macho makali kisha akamfinyia jicho moja.
Majaliwa akamuelewa, akanyamaza kimya.
“Dereva tufikishe kule kule gesti tulikokwenda mwanzo” Sharifa akamwambia dereva wa teksi ambaye alimkubalia kwa kichwa.
Walipofika hapo gesti Sharifa alimwambia Majaliwa ashuke.
“Tutazungumza kwenye simu nikifika nyumbani” akamwambia.
Majaliwa alishuka na kusimama kando ya dirisha.
“Mama si nilikwambia sina hela”
Sharifa akaguna. Alifungua pochi yake na kutoa noti za shilingi elfu ishirini akampa.
“Chukua hizi kwanza”
“Hizo hazitoshi mama” Majaliwa alisema huku akinyoosha mkono kuzipokea.
“Nina pesa ya kulipia teksi tu. Chukua hizo kwanza”
Majaliwa alizitia mfukoni kisha akamwambia mama yake. “Haya baadaye”
Sharifa alipofika nyumbani aliificha ile karatasi ya dawa jikoni. Akaanza kushughulika na kazi nyingine. Akakumbuka kwamba alimuahidi mwanawe kuwa angempigia simu. Akaingia chumbani na kumpigia.
“Kesho kuna pesa nitakutumia kwa simu umpelekee yule mganga, si utapaelewa?” akamuuliza.
“Siwezi kupotea. Na pesa yangu je?” Majaliwa akamuuliza.
“Nitakutumia pamoja hapo kesho”
“Nitaenda kwa teksi au daladala”
“Utaenda kwa daladala, si utakuwa peke yako”
“Sawa”
“Nataka nimpime huyu baba yako leo, kama atabadilika nitakujulisha”
“Nijulishe nijue. Nimechoka kukaa huku. Sipati huduma yoyote”
“Nitakujulisha, basi ni hapo kesho”
“Utanitumia muda gani hizo pesa?”
“Asubuhi”
“Sawa”
Sharifa akakata simu.
Siku ile Sharifa alikuwa katika mkao wa kumchunguza Wakwetu. Akiwa jikoni usiku alichukua kiwembe akapuna visigino vyake vya mguu wa kulia na kushoto kama alivyoambiwa na mganga. Ule unga unga uliotoka aliukinga kwenye karatasi.
Alipopata unga unga wa kutosha aliutia kwenye mchuzi ambao alikuwa ameuandaa kuupeleka mezani. Dakika chache baadaye akawa ameandaa chakula juu ya meza. Alimuita Wakwetu akamuwekea chakula kwenye sahani na yeye akajiwekea cha kwake. Wakaanza kula.
Yeye hakujiwekea mchuzi. Alikula nyama kavu pamoja na mboga mboga. Lakini Wakwetu hakugundua kitu. Baada ya kula aliondoa mwenyewe vyombo akavipeleka jikoni.
Wakati wa kulala Sharifa alitekeleza agizo jingine aliloambiwa na mganga. Ingawa Wakwetu mawazo yake yalikuwa mbali, Sharifa alitumia mbinu za kuyarejesha mawazo ya Wakwetu na wakaweza kushirikiana kikamilifu.
Baada ya hapo Sharifa alishawishi Wakwetu wakaoge ili amchangamshe. Waliporudi ndipo Sharifa alipoanza kusikitika.
“Namkumbuka sana mtoto wetu, nimem miss sana”
“Unamaanisha Majaliwa?”
“Kwani tuna mtoto mwingine zaidi yake?”
“Suala la Majaliwa bado nalifikiria sana”
“Kwani bado hujaamua kumsamehe mwanao?”
“Siamini kama Majaliwa amejirudi”
“Lakini si amekuomba msamaha?”
“Kuniomba msamaha haimaanishi kujirudi. Pengine anataka usalama tu”
“Sikiliza mume wangu, Majaliwa ameshajirudi na amejua kosa lake ndio sababu amekuandikia barua na kukuomba msamaha. Na mimi pia ninamuombea kwako” Wakwetu akanyamaza kimya. Ukimya wa Wakwetu ulimpa dalili Sharifa kuwa Wakwetu ameanza kusalimu amri.
Asubuhi kulipokucha kabla ya Wakwetu kutoka, Sharifa alimuuliza.
“Jana uliniambia bado unalifikiria suala la Majaliwa, umepata jibu gani?”
“Kama mnawasiliana mwambie aje nyumbani” Wakwetu alimjibu hivyo kisha akatoka.
Wakwetu alipotoka Sharifa alifungua kabati akachukua shilingi laki moja. Alimuita Mage akampa zile shilingi laki moja.
“Nenda kwa wakala wa pesa wa kampuni ya simu ninayotumia, niwekee hizi pesa kwenye akaunti yangu”
Mage alipokea zile pesa. Kwa vile mara kwa mara alikuwa akitumwa na Sharifa kumuwekea pesa kwenye akaunti yake ya simu alikuwa ameikariri na kuijua namba yake.
Mage alitoka akaenda kwa wakala aliyekuwa jirani, akaweka shilingi laki moja kwenye akaunti ya simu ya Sharifa kisha akarudi.
“Tayari nimeweka”
“Sawa” Sharifa alimjibu na kuingia chumbani mwake. Aliitazama simu yake na kuona ujumbe ulioonesha kuwa kulikuwa na shilingi laki moja iliyotumwa katika akaunti yake.
Akampigia simu Majaliwa.
“Uko wapi?”akamuuliza mara tu Majaliwa alipopokea simu.
“Niko hapa masikani na vijana wenzangu” Majaliwa akamjibu.
“Sasa nakutumia shilingi laki moja, elfu hamsini utampelekea yule mganga. Zilizobaki utachukua wewe”
“Nauli ya kwendea?”
“Utatoa kwenye hizo pesa zako. Umenielewa?”
“Sawa”
“Nakurushia sasa hivi na wewe uende sasa hivi”
“Sawa” Sharifa alikata simu akamtumia shilingi laki moja Majaliwa. Meseji ikamthibitishia kwamba muamala umefika kwa Majaliwa. Akampigia simu tena.
“Umeziona hizo pesa?” Sharifa alimuuliza.
“Nimeziona”
“Sasa katoe elfu haamsini umpelekee yule mganga”
“Baba amesemaje?”
“Anaelekea elekea kidogo. Ameniambia nikwambie urudi nyumbani”
“Kweli mama? Kwa hiyo nirudi leo?”
“Subiri kwanza. Nataka niuelewe msimamo wake vizuri”
“Mpaka lini?”
“Nitakwambia”
“Sawa”
Sharifa akakata simu.
Majaliwa alikwenda kwa wakala wa kuweka na kutoa pesa kwenye simu. Akatoa shilingi elfu tisini. Baada ya hapo alikwenda kupanda daladala. Akaenda Machui.
Alipoingia nyumbani kwa yule mganga alimpatiaa shilingi elfu hamsini.