Dili iliyokufa - 10
ILIPOISHIA
“Kutoka siku hiyo Sharifa akaajiriwa na Wakwetu. Alitakiwa kuanza kazi siku ile ile. Baada ya kufanya kazi kwa miezi mitatu, Wakwetu alibadili mawazo yake. Siku moja alimwita ofisini kwake na kumwambia:
“Sharifa, nakumbuka kuwa uliniambia mume wako alifariki kwa ajali ya gari.”
“Ndiyo, alifariki kwa ajali ya gari.”
“Kwa nini hujaolewa tena mpaka sasa?”
“Niliamua tu niendelee kuishi peke yangu mpaka nitakapomsahau marehemu mume wangu.”.
SASA ENDELEA...
“JIBU hilo likamchekesha Wakwetu.
“Mpaka sasa bado hujamsahau”
“Hivi sasa nimeshaanza kumsahau”
“Uko tayari kuolewa?”
“Naam, akitokea mume wa kutaka kunioa niko tayari”
Wakwetu alinyamaza kidogo akafikiri kisha alimwambia Sharifa.
“Umenijibu vyema. Nataka nikuoe. Nimeona unafaa kuwa mke wangu”
“Mimi niko tayari” Sharifa alimwambia haraka.
Halafu wote wakacheka. Sasa kilikuwa ni kicheko cha mapenzi.
Kutoka siku ile Wakwetu alianza kufanya taratibu za uchumba huku akimuacha Sharifa aendelee na kazi.
Miezi miwili baadaye Wakwetu na Sharifa wakaoana. Sasa wakawa ni mume na mke na si mfanyakazi na bosi wake. Sharifa sasa akawa na amri na kampuni ya Wakwetu kwani aliachiwa mamlaka ya kuiongoza.
Wakwetu akahisi kwamba alikuwa ametimiza moja ya malengo yake kwa kumuoa Sharifa. Lengo lake jingine amabalo lilikuwa bado kitendawili lilikuwa ni kuwapata watoto wake.
Mara kadhaa alikwenda kwa yule mzee aliyempa simu lakini mzee huyo alimwambia kuwa hakuwa amefanikiwa kupata taarifa zozote kuhusu watoto hao.
Wakwetu alimueleza Sharifa historia yake na kuhusu watoto wake ambao hawakuwa wakijulikana waliko.“Nimeshakamilisha malengo yangu mawili, sasa bado lengo moja ambalo ndilo linalonisumbua kwa sasa” Wakwetu alimwambia mke.
“Ni malengo gani mawili ambayo umeshayakamilisha?” Sharifa akamuuliza.
“Lengo langu la kwanza lilikuwa kuanzisha kampuni. Kampuni nimeshaianzisha. Lengo langu la pili lilikuwa kuoa mke, mke nimeshaoa na ni wewe. Lengo langu la tatu ambalo bado ni kitendawili ni kuwapata watoto wangu”
“Mimi naamini kuwa utawapata kama wapo hapa Dar. Kama hivyo ambavyo unawatafuta, bila shaka na wao wanamtafuta baba yao”
“Nilisikia kwamba hawako hapa Dar, wako Zambia”
“Lakini hizo ni tetesi tu. Na hata kama ni kweli wako Zambia, Zambia sio Meka au Madina, iko siku watarudi nyumbani kwao.”
“Nimefurahi kwa kuona unanipa moyo, nitaendelea kuwatafuta nikiamni maneno yako kwamba hata wao wanaweza kuwa wananitafuta mimi”
Siku zikazidi kupita. Baada ya Wakwetu kukata tamaa ya kuwapata watoto hao, aliona ajitahidi apate angalau watoto wawili kwa Sharifa.
Katika mwaka wa kwanza Sharifa hakupata ujauzito. Walisubiri mwaka wa pili na watatu, vivyo hivyo Sharifa hakupata ujauzito. Wakaanza kwenda kwa madaktari.
Sharifa alichunguzwa na kuonekana na tatizo dogo katika kizazi chake, akapatiwa matibabu na kuahidiwa kuwa akimalliza dawa alizoandikiwa atumie atapata ujauzito.
Sharifa alitumia dawa hizo bila mafanikio. Katika kipindi cha mwaka mmoja alikuwa amemaliza zaidi ya madaktari kumi ambao walikuwa mabingwa wa matumbo ya wanawake.
Kulikuwa na siku Sharifa alikwenda kwa daktari mmoja bila kufuatana na mume wake. Akamuelea daktari huyo kuwa alitumia tembe za kuzuia kushika mamba kwa miaka mingi hivyo anahisi kuwa zimeathiri kizazi chake.
Sharifa baada ya kuchunguzwa kwa kina alifanyiwa matibabu ambayo yalimpa matumaini ya kushika mimba. Siku zikapita bila Sharifa kupata dalili yote ya kupata mimba.
Sharifa aliporudi tena kwa daktari wake aliambiwa huenda tatizo lilikuwa kwa mume wake.
“Yeye alishazaa watoto wawili na mke wake wa kwana ambaye alikufa”
“Unaweza kuwa mzima halafu ukawa mgonjwa. Kuzaa kwake hakumaanishi kuwa hawezi kupata tatizo la kumzuia asizae tena”
“Kwa hiyo tufanyeje”
“Na yeye anatakiwa kufanyiwa uchunguzi. Kama itagundulika tatizo liko kwake ashughulikiwe”
Sharifa alikwenda kumfahamisha mume wake kuwa na yeye alitakiwa kufanyiwa uchunguzi. Wakwetu naye akaenda kufanyiwa uchunguzi. Uchunguzi huo ukaonesha kuwa Wakwetu hakuwa na tatizo.
Wote wawili hawakuwa na matatizo, sasa kwanini walikuwa hawapati mtoto?
Swali hilo lilikuwa likigonga katika vichwa vya wote wawili. Kwa upande wa Wakwetu lilimkumbusha watoto wake ambao alikuwa hawajui walipo. Alijiambia laiti watoto hao wangekuwepo asingekuwa na haja ya kuhangaika kutafuta mtoto kutokana na umri aliokuwa nao.
Lakini kwa upande wa Sharifa tatizo hilo la kutopata mtoto lilikatisha tamaa yake ya kupata utajiri wa Wakwetu. Alijiambia kama angezaa na Wakwetu angekuwa na uhakika wa kumiliki mali za Wakwetu wakati atakapokufa.
Kutokana na umri wake na umri wa Wakwetu Sharifa alikuwa na hakika kwamba Wakwetu ndiye ambaye angetangulia kufa akimuacha yeye akiwa na miaka kadhaa ya kuishi.
Sasa afanye nini? Akajiuliza.
Kwa upande mwingine aliendelea kujiambia, iwapo Wakwetu atawapata watoto wake hao ndio watarithi mali za baba yao na yeye hatapata kitu.
Jambo hilo halikumpendeza, sasa ikambidi afikirie la kufanya.
Siku hiyo alikuwa amekaa sebuleni akiwaza. Kumbukumbu zikaanza kumjia. Alikumbuka jinsi alivyopata mimba akiwa shuleni. Alipata mimba akiwa kidato cha tano jambo lililosababisha afukuzwe shule. Baba yake naye alikasirika akamfukuza nyumbani.
Alilea mimba yake akiwa kwa rafiki yake wa kike hadi akajifungua. Mama yake ndiye aliyekuwa akimtembelea kisirisiri bila baba yake kujua. Ni kutokana na msaada wa mama yake Sharifa aliweza kuilea mimba yake na hatimaye kujifungua salama.
Baba yake alipofariki miaka michache baada ya Sharifa kujifungua mtoto, ndipo alipohamia nyumbani kwao. Mama yake akachukua jukumu tena la kumuendeleza kimasomo na kufanikiwa kusomea uhasibu.
Ingawa alimdanganya Wakwetu kuwa aliwahi kuolewa na kwamba alipunguzwa kazi baada ya shirika alilokuwa akifanya kazi kubinafsishwa, Sharifa hakuwahi kuolewa. Alikuwa akiishi na wanaume kwa muda mfupi na hatimaye kuachana.
Kwa upande wa kazi, hakuwa amepunguzwa kazi bali alihusika na wizi wa fedha na kufunguliwa kesi. Ingawa alishinda kesi ile kwa msaada wa wakili wake, alifukuzwa kazini na ikambidi akae nyumbani kwa muda mrefu.
Sasa mtoto wake alikuwa mkubwa, alikuwa amemzaa miaka ishirini na miwili iliyopita alipopata mimba akiwa shule. Alipokuja Tanga kutoka Arusha alipangisha chumba maeneo ya Kwaminchi akamuagiza mtoto wake aliyeitwa Majaliwa wakawa wanajishughulisha na mradi wa kukaanga chipsi.
Ndipo siku moja Sharifa alipoona lile tangazo la kazi ya uhasibu kwenye gazeti. Akajaribu kuandika barua ya maombi kuona kama atafaniwa. Ndipo alipipigiwa simu na Wakwetu na kuitwa.
Jambo jingine alilomdanganya Wakwetu ni kusema kwamba hakuwa na mtoto na kwamba mimba yake iliharibika baada ya mume aliyemuoa kufariki kwa ajali ya gari.
Hatimaye Sharifa kwa vile alikuwa mrembo na mwenye sifa zote za mwanamke jamali, aliolewa na Wakwetu.
Tangu akiwa mfanyakazi wa Wakwetu hadi kuwa mke wake, Wakwetu hakugundua hata siku moja historia sahihi ya mke wake. Hakugundua kuwa alikuwa na mtoto aliyemuacha Kwaminchi akiwa na mradi wa chipsi.
Mama mtu licha ya kumjulisha mwanawe kuwa anaolewa, alimuonya asifike nyumbani kwake na asijitambulishe kuwa yeye ni mtoto wake.
Wenyewe walikuwa wakiwasiliana kisirisiri kwa simu kama kulikuwa na jambo walilohitaji kuzungumza.
Mara kwa mara Majaliwa alikuwa akimfahamisha mama yake kuwa mradi wao wa chipsi sasa ulikuwa ukididimia na mtaji ulikuwa unakata.
Akiwa amekaa hapo sebuleni akiwaza ndipo Sharifa alipofikiria kumzunguka Wakwetu.
Siku iliyofuata baada ya Wakwetu kuondoka nyumbani kwenda kazini kwake, Sharifa naye alitoka. Alikodi teksi iliyompeleka Kwaminchi kwa mwanawe.
Alimkuta majaliwa akijiandaa kwenda sokoni kununua viazi na mahitaji mengine ya biashara yake.
“Ndio unataka kwenda sokoni?” Mama yake akamuuliza.
“Ndiyo nilikuwa nataka kutoka”
“Hebu kaa kidogo. Kuna kitu ninataka kukueleza”
Majaliwa akakaa na mama yake naye akakaa.
“Sikiliza mwanangu bila kutumia ujanja tutakufa masikini. Yule mume wangu ana watoto wake anawatafuta, sidhani kama atawapata lakini kama atafanikiwa kuwapata ndio watakuwa warithi wake. Sasa mimi nataka nikupachike wewe pale nyumbani ujifanye ni mmoja wa hao watoto wake. Unasemaje utaweza?”
“Endelea kunieleza ili nipate kuelewa jinsi ambavyo tutafanya mpaka aone kuwa mimi ni mtoto wake”