Dili iliyokufa - 9
ILIPOISHIA
Katika nyumba ya jirani na kiwanja hicho Wakwetu alimkuta mzee aliyekuwa ameketi barazani kwenye kiti cha uvivu. Akaenda kumsalimia.
“Shikamoo mzee.”
“Marahaba. Hujambo?”
“Sijambo. Unajisikiaje hali yako mzee wangu?”
“Hali yangu ni nzuri. Karibu.”
“Asante. Mzee wangu naomba kukuuliza.”
“Uliza.”
“Kulikuwa na bibi mmoja aliyekuwa na kiwanja hiki kilichoko jirani yako. Sijui kama unamfahamu?”
“Nani? Bibi Zainab?”
“Ndiye yeye hasa!”
“Yule bibi alishakufa miaka mingi sana.”
“Alikuwa na mjukuu wake msichana mmoja aliyekuwa akiitwa jina hilo hilo. Sijui kama naye unamfahamu?”
“Yule aliwahi kuolewa na kijana mmoja akamkimbia akaenda Afrika Kusini. Hakurudi tena. Alimuacha mwenzake na ujauzito…”.
SASA ENDELEA...
“SASA yuko wapi?”
“Naye pia alikufa. Alizaa kwa operesheni lakini hakuzinduka tena”
Wakwetu akatikisa kichwa kusikitika.
“Na huyo mtoto aliyemzaa alipelekwa wapi, au naye alikufa?”
“Alizaa mapacha wawili wa kiume. Walilelewa na bibi yao. Tulikuwa nao hapa. Lakini mapacha wale hatujui waliishia wapi kwani yule bibi alipokutwa amekufa hakuwa na watoto”
Maelezo hayo yakamgutusha Wakwetu. Kwa upande mmoja yalimfurahisha kujua kuwa mke wake alizaa mapacha wawili wa kiume. Lakini kwa upande mwingine yalimshitua kusikia kuwa mke wake huyo alifariki dunia baada ya kuzaa kwa operesheni na watoto aliozaa hawafahamiki waliko.
Licha ya kutopata uhakika wa kitu alichoelezwa Wakwetu alihisi kuvutika na mazungumzo hayo.
“Sasa tuseme hao watoto aliwapeleka wapi?”
“Haikufahamika. Hadi leo hatujui wale watoto wako wapi”
Mzee akatikisa kichwa kusikitika kabla ya kuongeza.
“Watoto wale walikuwa wakipata mateso sana. Bibi mwenyewe hakuwa na uwezo. Ilibidi watu wengine wamsaidie yule bibi kumpa pesa za kuwanunulia maziwa”
Wakwetu alibaki kimya akiyasikiliza yale maneno kwa majonzi.
Mzee akaendelea kumueleza.
“Tatizo kubwa lilikuwa kwa mume wa Zainab mwenyewe. Tulisikia alikimbilia Afrika Kusini. Ikaja habari hapa kuwa alinyongwa kutokana na kushiriki kwenye vitendo vya ujambazi. Halafu tukapata habari nyingine kuwa alikuwa kwenye meli”
“Mzee wangu nataka nikwambie ukweli. Mimi ndiye niliyekuwa mume wa Zainab” Wakwetu akamwambia mzee huyo.
Mzee huyo aliposikia hivyo alishituka akamkazia macho Wakwetu.
“Wewe ndiye uliyekuwa mume wa yule binti…ndiye uliyekwenda Afrika Kusini… ukapotea kabisa?”
“Ndiye mimi”
“Sasa kwanini ulipotea?”
“Si kupotea.Ni kama mlivyosikia, nilipatwa na mitihani ya kimaisha. Nilipokuwa Afrika Kusini nilikamatwa na kushitakiwa kuwa nilimuua tajiri yangu aliyekuwa ameniajiri kazi nikahukumiwa kunyongwa lakini nilikata rufani ikabainika kuwa nilionewa nikaachiwa huru”
Wakwetu akaendelea kumueleza.
“Ni kweli kuwa baada ya hapo nilipata kazi kwenye meli. Ile meli ilikuwa inafanya safari za Ulaya. Sasa sikupata mawasiliano tena na huku nyumbani”
“Mbona hukurudi tena?”
“Hilo ndilo kosa langu. Nimerudi sasa nikiwa mtu mzima. Zaidi ya miaka ishirini imeshapita”
Mzee akatikisa kichwa.
“Umechelewa sana. Unauliza leo habari ya mke wako na watoto wako? Mke wako alikufa na watoto wako hawajulikani wako wapi na hivi sasa watakuwa watu wazima”
“Miaka ni mingi, watakuwa ni wakubwa lakini ninataka niwajue”
“Endelea kuuliza kwa ndugu na jamaa jamaa zake. Unaweza kugundua mahali waliko”
“Miaka mingi imepita itakuwa ni vigumu kuwapata lakini nitajitahidi. Na wewe mzee wangu jaribu kuniulizia ulizia, nitakuwa ninakuja kwako mara kwa mara unipe taarifa”
“Kwani wewe unaishi wapi kwa sasa?”
“Kwa sasa ninakaa hotelini lakini nina mpango wa kununua nyumba”
“Kama nitasikia habari zao nitakupata wapi?”
“Kwani mzee huna simu?”
“Sina simu mwanangu”
“Nitakununulia simu na nitakuletea kesho ili tuwasiliane”
“Nitakushukuru sana”
Wakwetu alitoa pochi akaifungua na kutoa noti tano za elfu kumi kumi, akampa yule mzee.
“Chukua hizi pesa zitakusaidia, mimi nakwenda zangu”
“Asante sana. Kwanza nakupa pole kwa matatizo yaliyokukuta na pili nakupa pole kwa kufiwa na mke wako na kupotelewa na watoto wako lakini mimi nitajitahidi kukutafutia taarifa za watoto wako”
“Nitakushukuru sana mzee wangu”
“Kumbe hapo kesho utakuja saa ngapi?”
“Niambie wewe nikufuate saa ngapi?”
“Nimekuuliza hivyo kwa sababu umeniambia utanipatia simu na hiyo ndiyo ninayotarajia kufanyia mawasiliano ya kuhusiana na watoto wako”
“Nitakuja saa tano na nitakuletea na hiyo simu”
“Basi wewe njoo hiyo saa tano, pengine nitakuwa nimeshapata taarifa zinazohusu watoto wako”
“Asante mzee wangu.”
“Karibu sana.”
Sasa akiwa kwenye gari lake akirudi katika hoteli aliyopanga chumba baada ya kuachana na mzee aliyekuwa akizungumza naye, Wakwetu alijiambia alikuwa amefanya kosa kubwa kusahau alikotoka baada ya kufika Ulaya.
“Nilisahau kwamba niliacha mke wangu akiwa mjamzito, sasa baada ya kurudi nakuta mke amekufa na watoto hawajulikani waliko” Aliwaza kwa uchungu.
Lakini lililomsikitisha zaidi si kifo cha aliyekuwa mke wake ambacho aliamini kilitokana na kudura ya Mungu bali ni kutojulikana kwa watoto wake.
Alijiambia pengine watoto hao wamekuwa ni watoto wa mitaani wasio na baba wala na mama wakihangaika kutafuta riziki zao. Au pengine wamekuwa vibaka wanaosakana na polisi mchana kutwa.
Matumaini ya kuwapata watoto hao yalikuwa madogo sana hasa kwa vile imepita miaka mingi tangu bibi yao alipofariki dunia.
Alipofika katika hoteli aliyokuwa amepanga chumba aliingia chumbani mwake na kuendelea kutafakari zaidi kuhusu kupotea kwa watoto hao.
Kwa upande mwingine alijiambia kwa vile amefahamishwa kuwa mke wake amefariki ingembidi aoe mke mwingine haraka.
Alikuwa mepanga pia kuanzisha kampuni yake ya kuingiza na kutoa mizigo bandarini. Alifikiria kuanzasha kampuni hiyo tangu alipokuwa Ulaya ambapo alikuwa akiona jinsi shughuli hizo zilivyokuwa zikifanyika alipokuwa melini.
Siku ya pili yake Wakwetu alipotoka hotelini hapo alikwenda katika duka moja la simu akanunu simu moja kwa ajili ya yule mzee aliyemuahidi. Akasajili laini na kumuwekea katika simu hiyo. Ilipofika saa nne na nusu akaamua kumfuata nyumbani kwake.
Alimkuta pale pale barazani alipomkuta jana yake.
“Shikamoo mzee” Wakwetu akamsalimia mzee huyo.
“Marahaba. Habari ya tangu jana?”
“Ni nzuri. Nimekuja tena kama tulivyoahidiana jana” Wakwetu alimwammbia huku akitia mkono kwenye mfuko wa koti lake na kutoa ile simu aliyoinunua pamoja na kifaa chake cha kuchajia.
“Nimekuletea ile simu”
“Oh Nashukuru sana na mimi nimelishughulikia lile suala lako” Mzee alisema huku akipokea ile simu.
“Nimekuwekea laini kabisa” Wakwetu alimwambia huku akimtajia namba ya laini yake.
“Asante sana”
“Nimekuwekea na salio la shilingi elfu tano”
“Kwa hiyo mimi napiga tu?”
“Unapiga tu hadi salio liishe ndio unaweka jingine”
“Asante”
Mzee alimuita msichana mmoja aliyekuwa humo ndani na kumwagiza amtolee kiti Wakwetu.
Wakwetu alipotolewa kiti aliketi na kumuuliza mzee huyo.
“Umesema kuwa umelishughulikia sula langu?”
“Ndio nimelishughulikia. Kuna mwanamke mmoja ambaye alikuwa karibu sana na yule bibi, nilimfuata kumuulizia kuhusu wale watoto akanipa hadithi ndefu”
“Alikupa hadithi gani?”
“Alinimabia kwamba wale watoto walichukuliwa na mwanamke mmoja wa kiarabu ambaye alikwenda kuwalea huko Nguvumali. Inesemekana aliwapeleka shule kusoma lakini yule mwanamke alipokuwa mzee alirudi kwao Oman, sasa haikujulikana wale watoto walikwenda wapi lakini kuna taarifa kwamba watoto hao wako Zambia”
“Wako Zambia kwa nani?”
“Haijulikani wako kwa nani lakini inawezekana wamekwenda kutafuta maisha”
Baada ya kuwaza kidogo Wakwetu alimwambia mzee huyo.
“Ningependa unikutanishe na huyo mwanamke ili aweze kunipa ufafanuzi zaidi”
“Ninaweza kukutanisha naye. Hayuko mbali”
Mzee huyo alinyanyuka kwenye kiti.