Dili iliyokufa - 10
ILIPOISHIA
“Wako Zambia kwa nani?”
“Haijulikani wako kwa nani lakini inawezekana wamekwenda kutafuta maisha”
Baada ya kuwaza kidogo Wakwetu alimwambia mzee huyo.
“Ningependa unikutanishe na huyo mwanamke ili aweze kunipa ufafanuzi zaidi”
“Ninaweza kukutanisha naye. Hayuko mbali”
Mzee huyo alinyanyuka kwenye kiti.
SASA ENDELEA...
“Twende,” akamwambia Wakwetu.
Wakwetu naye alinyanyuka na kuongozana na mzee huyo.
“Nyumba anayoishi huyo mwanamke ni ile pale.”
Mzee alimuonesha nyumba ya tatu kutoka ilipokuwa nyumba yake.
Walipofika katika nyumba hiyo, mzee alipiga hodi na kumwita Mama Tizo.
Mwanamke huyo alipotoka nje, walisalimiana naye kisha mzee alimtambulisha Wakwetu kwa mwanamke huyo.
“Mama mwenyewe niliyekwambia ndiye huyu hapa.”
“Nimefurahi kumuona na kumfahamu.”
Wakwetu akamgeukia mwanamke huyo.
“Najua kwamba hunifahamu. Mimi ndiye mkwe wake marehemu Bi. Zainab aliyekuwa na nyumba yake pale.”
Wakwetu alimwambia mwanamke huyo huku akimuonesha mahali ilipokuwa nyumba ya bibi huyo.
“Ulikuwa mkwe wake kivipi?”
“Pengine nimekosea kueleza, yaani mjukuu wake ambaye pia alifariki na ambaye alikuwa akiitwa jina hilo hilo la Zainab alikuwa mke wangu.”
Mwanamke huyo akagutuka na kumtazama mzee aliyefika na Wakwetu.
“Huyu bwana ndiye uliyenizungumzia habari zake ukaniambia kuwa anawatafuta watoto wake?” akamuuliza.
“Ndiye yeye.”
“Habari za siku kaka yangu?”
“Ni nzuri. Tunashukuru kwamba tuko salama.”
“Ulikuwa wapi?”
“Nilikuwa nje ya nchi kwa miaka mingi.”
“Ulipoondoka ulimuacha mke wako akiwa mjamzito?”
“Ndiyo, nilimuacha akiwa mjamzito. Niliporudi nikapata habari kwa mzee hapa kuwa alizaa kwa upasuaji watoto wawili. Yeye mwenyewe akafariki lakini watoto walinusurika.”
“Ni kweli. Hao watoto walilelewa na bibi yao. Bibi yao alipokufa walichukuliwa na mwanamke mmoja wa Kiarabu. Alikuwa akiishi eneo la Nguvumali.”
“Nimeambiwa na mzee. Sasa kilichonileta hapa ni kutaka kukuuliza utanisaidiaje ili niweze kuwapata watoto hao?” Wakwetu alimuuliza mwanamke huyo.
“Sidhani kama wapo hapa Dar. Kwa mara ya mwisho kupata habari zao ni mwaka jana, nilisikia kwamba wapo Zambia.”
“Wapo Zambia kwa nani?”
“Sasa hapo sikuweza kujua na pia habari zenyewe zilikuwa za kijuujuu tu.”
“Hakuna mtu yeyote ambaye unadhani anafahamu habari za watoto hao?”
Mwanamke huyo akatikisa kichwa.
“Sidhani kama kuna mtu anayefahamu habari zao hapa mtaani kwetu.”
Baada ya kuwaza kwa sekunde chache, Wakwetu alimwambia mwanamke huyo:
“Nashukuru kwa maelezo yako, isipokuwa nakuachia hii kazi. Endelea kunifanyia utafiti. Ukifanikiwa kupata habari zao, naomba umfahamishe huyu mzee. Nimempa namba yangu ya simu.”
“Hakuna tatizo. Nitaendelea kukuulizia kwa watu mbalimbali. Endapo nitapata fununu tu zinazowahusu wao, nitamjulisha mzee.”
Wakwetu alitoa noti mbili za shilingi elfu kumi akampa mwanamke huyo.
“Chukua hizo zitakusaidia kwa leo.”
“Asante. Mungu akubariki.”
Mwanamke huyo alipokea pesa hizo huku akitabasamu.
“Sasa sisi tunaondoka. Naweza kuja kukutembelea siku yoyote.”
Baada ya Wakwetu na mzee huyo kuondoka nyumbani kwa mwanamke huyo, walirudi nyumbani kwa mzee ambapo Wakwetu aliagana naye na kumtaka asisite kumpigia simu endapo atapata habari za watoto wake.
Mzee akamuahidi kuwa hatasita kufanya hivyo. Wakwetu akaondoka.
Mwezi mmoja ukapita bila Wakwetu kupata habari yoyote. Katika mwezi huo, Wakwetu alifanikiwa kununua nyumba iliyokuwa ikinadiwa na dalali wa mahakama katika eneo la Sahare.
Ilikuwa nyumba ya kifahari ingawa haikuwa ya ghorofa. Wakwetu alifanikiwa kuipata baada ya kuwazidi dau wanunuzi wenzake waliokuwa wakiiwania.
Baada ya kuinunua nyumba hiyo, aliipiga rangi na wiki moja baadaye alinunua fanicha za nyumba nzima na kuziingiza ndani.
Siku hiyo hiyo ndiyo aliyoondoka katika chumba cha hoteli na kuhamia katika nyumba yake hiyo.
Kwa vile anapoondoka nyumbani hapo nyumba hubaki tupu, aliamua kuweka mlinzi wa saa ishirini na nne kwa ajili ya kulinda usalama wa nyumba yake.
Wakati huo huo alikuwa akiendelea na mipango yake ya kusajili kampuni ya kuingiza na kutoa mizigo bandarini. Alifanikiwa kupata ofisi katika Barabara ya Ecken. Aliipata kutoka kwa mtu aliyekuwa akihamia Mwanza.
Ilikuwa ofisi kubwa yenye hadhi ambayo Wakwetu aliigawanya sehemu tatu. Sehemu moja ikiwa kwa ajili yake mwenyewe na sehemu zilizobaki kwa ajili ya wafanyakazi wake.
Baada ya kila kitu kuwa tayari, Wakwetu alianza kazi. Alianza na wafanyakazi watatu. Baada ya siku chache aligundua kuwa alikuwa akihitaji kuwa na mhasibu. Akatoa tangazo la kazi ya uhasibu kwenye gazeti.
Siku ile ile lilipotoka tangazo, barua zilianza kumiminika. Aliziacha barua hizo kwa siku tatu kabla ya kuanza kuzifungua na kuzisoma.
Katika barua zote alizopata kulikuwa na moja tu ambayo ilikuwa na muombaji mwanamke, akaona amchague huyo. Kwa vile alikuwa ameweka namba yake ya simu, alimpigia hapo hapo.
“Nazungumza na Sharifa?” Wakwetu aliuliza mara tu simu yake ilipopokelewa.
“Ndiyo. Naitwa Sharifa.”
“Ulituma maombi ya kazi ya uhasibu katika kampuni yetu.”
“Ndiyo nilituma.”
“Tafadhali fika katika ofisi zetu kesho kwa ajili ya usaili.”
“Nikifika niulize nani?”
“Muulize mkurugenzi, mmiliki wa kampuni.”
“Asante, nitafika.”
“Unatakiwa ufike mapema asubuhi.”
“Nitafika mapema.”
Wakwetu akakata simu.
Siku ya pili yake saa moja asubuhi, mwanamke huyo akafika ofisini hapo. Alifika mapema kabla ya mfanyakazi yeyote kufika. Wakwetu alipofika alimkuta mgeni wake akimsubiri.
Alipoingia ofisini kwake na kuketi, mwanamke huyo naye akaingia.
“Shikamoo,” akamwamkia Wakwetu.
“Marahaba. Hujambo?”
“Sijambo.”
“Karibu, keti.”
Mwanamke huyo akakaa kwenye kiti.
Wakwetu akamtupia macho. Mwanamke huyo alikuwa mweupe mwenye mwili uliojaa. Uso wake wa duara ulikuwa na macho makubwa, pua ndefu na midomo ya wastani.
“Naweza kukusaidia?” Wakwetu alimwambia baada ya kutazamana naye.
“Mimi ndiye Sharifa niliyetuma barua ya maombi ya kazi.”
“Karibu sana.”
Wakwetu aliitafuta ile barua yake ya maombi. Alipoiona aliikunjua na kuanza kuisoma tena.
“Umeandika hapa kuwa una umri wa miaka thelathini na mitano.”
“Ndiyo.”
“Wewe ni mwenyeji wa wapi?”
“Mwenyeji wa Arusha.”
“Ulisomea Arusha?”
“Nilisomea Arusha na hapa Tanga.”
“Sawa. Kuna mambo ambayo ninataka kuyajua kutoka kwako. Uliwahi kufanya kazi wapi na wapi?”
“Niliwahi kuajiriwa kazi sehemu moja tu huko Kilimanjaro kwenye shirika moja la umma.”
“Kazi gani?”
“Hiyo hiyo ya uhasibu.”
“Kwa nini uliacha kazi huko?” Wakwetu akamuuliza Sharifa.
“Lile shirika lilibinafsishwa tukajikuta tupo wahasibu wawili. Ikabidi mimi niachishwe kazi.”
“Ni muda gani sasa tangu uachishwe kazi?”
“Ni miaka miwili.”
“Sawa. Swali jingine nililotaka kukuuliza ni kama umeolewa.”
“Sijaolewa bado.”
“Umri huo bado hujaolewa?”
“Niliolewa mara ya kwanza. Mume wangu alifariki kwa ajali ya gari. Sasa tangu afariki sijaolewa tena.”
“Alifariki lini?”
“Nafikiri sasa inafika miaka mitano.”
“Ulipata naye mtoto?”
“Hapana, hatukuwahi kupata mtoto. Aliniacha nikiwa mjamzito. Mimba nayo ikaharibika.”
“Oh! Pole sana.”
“Asante.”
“Nimepokea barua nyingi za maombi ya kazi lakini nimeteua barua yako wewe kwa sababu niliona wewe ndiye mwanamke peke yake uliyejitokeza. Kwa hiyo nimekupa upendeleo.”
“Nashukuru kwa hilo.”
Kutoka siku hiyo Sharifa akaajiriwa na Wakwetu. Alitakiwa kuanza kazi siku ile ile. Baada ya kufanya kazi kwa miezi mitatu, Wakwetu alibadili mawazo yake. Siku moja alimwita ofisini kwake na kumwambia:
“Sharifa, nakumbuka kuwa uliniambia mume wako alifariki kwa ajali ya gari.”
“Ndiyo, alifariki kwa ajali ya gari.”
“Kwa nini hujaolewa tena mpaka sasa?”
“Niliamua tu niendelee kuishi peke yangu mpaka nitakapomsahau marehemu mume wangu.”